"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, April 19, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 59


SWALI 1: Nini maana ya Kipaimara?..Na je! Ni jambo la kimaandiko?
JIBU: Kipaimara ni Neno lenye maana ya “uthibitisho”…Neno hili linatumika katika madhehebu baadhi kama vile Katoliki, Orthodoksi na Anglikana kama kanuni muhimu ya ukristo..Kwamfano Kanisa Katoliki lina kanuni saba za kufuata wanazoziita Sakramenti.

Kwahiyo kipaimara Ni moja wapo ya hizo kanuni saba (sakramenti 7), ni kanuni ya Imani ambapo mtu anapaswa aipitie ili awe AMETHIBIKA MBELE ZA MUNGU. Na kanuni hiyo si nyingine zaidi ya KUWEKEWA MIKONO NA MAASKOFU WA KANISA…

Madhehebu yanayotumia kanuni hii yanasimamia mistari kutoka katika kitabu cha..

Matendo 8: 14 “Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;
15 ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;
16 kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.
17 NDIPO WAKAWEKA MIKONO YAO JUU YAO, NAO WAKAMPOKEA ROHO MTAKATIFU.”

Kwahiyo kinachotokea ni kwamba baada ya mtoto kubatizwa, atapaswa apitia mafunzo fulani yanayohusiana na kipaimara, na akishahitimu, ndipo atakusanyika kanisani na kuwekewa mikono na Askofu, na ndipo Roho Mtakatifu atashuka juu yake kama alivyoshuka juu ya hao wasamaria waliokuwa wamebatizwa tu lakini bado walikuwa hawajashukiwa na Roho Mtakatifu.

Kwahiyo kwa lugha rahisi au nyepesi ni kwamba hao Wasamaria walipokea kipaimara kwanza kwa mikono ya akina Petro na Yohana, ndipo Roho Mtakatifu akashuka juu yao..ikiwa na maana kuwa kama wasingewekewa mikono na Mitume na Bwana Yesu Kristo kamwe wasingepokea kile kipawa cha Roho Mtakatifu.

Kwahiyo Kanisa katoliki na mengine wakaichukulia hiyo kama ni kanuni ya MUHIMU SANA ya kufuata kwa kila mkristo, kwamba ili mtu athibitike kuwa mkristo kweli kweli na ili aweze kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu ni lazima abatizwe kwanza na kisha awekewe mikono na maaskofu wa kanisa, Na akishapitia hizo hatua kikamilifu ndipo anaweza kukubalika kama ni mshirika halali wa kanisa, na zaidi ya yote ni Mkristo..Kabla ya hapo anakuwa hajulikani kama ni mkristo.
Sasa kwa namna ya kibinadamu, hiyo inaweza ikaonekana ni sawa, inaweza ikaonekana ni utaratibu mzuri, au ni kanuni ya kufuata siku zote,..Lakini je! Ni sahihi kulingana na maandiko?.

Kwanza kabisa kabla ya kuelezea kipaimara, tuuzungumzie ubatizo kwa ufupi: ni muhimu kufahamu kuwa watoto wachanga hawabatizwi kulingana na Neno “Imani” lenyewe lilivyo, Ili iwe imani, ni lazima kwanza mtu aamini kitu fulani, sasa watoto wachanga hata kujielewa tu hawajajielewa, sasa wataaminije?..watamwamini vipi Yesu Kristo kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yao, na kwamba amekufa kwa ajili yao, na kwamba wanapaswa watubu kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao, wakati hata fahamu za kujitambua wao wenyewe hazipo ndani yao?
Kwasababu biblia inasema..

Warumi 10: 13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? TENA WAMWAMINIJE YEYE WASIYEMSIKIA? Tena wamsikieje PASIPO MHUBIRI?
15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema”

Kwahiyo Ubatizo wa vichanga sio sahihi kulingana na uhalisia wa mambo yote, haihitaji ufahamu mwingi sana kuelewa jambo hilo. Kumbatiza mtoto mchanga ni sawa na kwenda mtaani na kumchukua mtu asiyemjua Mungu kabisa pasipo kumhubiria, wala kumfundisha chochote na kwenda kumzamisha kwenye maji na kumwambia tayari umebatizwa!...Hiyo ni kazi bure.

Na pili, kuhusu kipaimara, Mitume hawakutoa kanuni Fulani kwamba mtu akitaka kupokea Kipawa cha Roho Mtakatifu ni lazima awekewe mikono na viongozi wao kwanza?..Hapana hawakutoa hiyo formula hata kidogo..Petro Na Yohana waliwawekea mikono wale wasamaria kwa wakati ule tu kwasababu ndio njia waliyoongozwa na Roho waitumie kwa wakati ule tu! Mahali pengine watu walishukiwa na Roho pasipo kuwekewa mikono na mtu yoyote. Kama tu siku ya Pentekoste watu walishukiwa na Roho pasipo kuwekewa mikono na mtu yoyote.

Na pia tunaona huyo huyo Petro alipokwenda nyumbani kwa Kornelio kumhubiria injili yeye na nyumba yake, Roho aliwashukia wale watu wote pasipo hata Mtume Petro kuwawekea mikono..

Matendo 10: 43 “Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.
44 Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.
45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu”.
Unaona hapo? Wakati Petro akiwa anazungumza tu! Roho aliwashukia juu yao, Na sehemu nyingine Petro alipowahubiria watu zaidi ya elfu 3, na walipoamini..aliwaambia namna ya kupokea Roho Mtakatifu pasipo kuwekewa mikono akawaambia.. 
Matendo 2:36 “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.
37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Unaona na hapo? Petro Hakuwaambia watu tubuni mkabatizwe na kisha njooni tuwawekee mikono ndipo mpokee kipawa cha Roho Mtakatifu badala yake maneno hayo yanaonyesha kuwa mtu anaweza kupokea Roho Mtakatifu pasipo hata kuwekewa mikono na mitume. Kwahiyo kuwekewa mikono sio kanuni ya kupokea Roho Mtakatifu, kanuni ya kupokea Roho ni kutubu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu.
Mwingine anaweza akapokea Roho kwa kuwekewa mikono, mwingine anaweza apokee pasipo kuwekewa mikono…Na kwa jinsi Roho atakavyochagua njia ya kushuka juu ya huyo mtu, baada tu ya mtu kutubu na kubatizwa.

Ni sawa na wakina Petro mahali pengine walikuwa wanatumia hata leso zao kuponya wagonjwa, na sehemu nyingine wanataja tu jina la Yesu pasipo kutumia chochote na watu wanafunguliwa..kwahiyo ni njia tu ambayo Roho aliyokuwa anawaongoza kwa wakati husikia ndiyo waliyokuwa wanaitumia..lakini huwezi kuona Petro anatoa kanuni maalumu kuwa sehemu zote watu ili wafunguliwa lazima watumie leso, huwezi kuona jambo hilo..

Tofauti na ilivyo siku hizi za mwisho..Mafuta, chumvi, udongo ndio KANUNI ya kupokea uponyaji, kila tatizo linatatuliwa na maji ya maombezi, kila tatizo linatatuliwa na mafuta ya maombezi na chumvi…Inakuwa ni kanuni, jina la Yesu halitumiki tena…Ni roho hiyo hiyo iliyopo pia katika mifumo ya kipaimara na ubarikio.

Kwahiyo kipaimara ni mfumo wa kimapokea ambao hausimami katika uhalisia wa kibiblia, ambao malengo yake ni kuwafanya watu waamini kuwa kuwekewa mikono na askofu, tayari wamekamilika na ndio tiketi ya kuthibitika mbele za Mungu..ni mfumo ambao unawafanya watu waridhike na kanuni za dini kuliko kanuni za biblia.

Utamwuliza mtu unauhakika wa kwenda mbinguni, atakwambia ndio nimebatizwa na nimepokea kipaimara…lakini mwulize nini maana ya Roho Mtakatifu na matunda yake ni yapi?..atakwambia sijui?, muulize nini maana ya unyakuo atakuambia sijawahi kusikia hata hicho kitu, muulize umeokoka atakwambia dini yangu haifundishi hivyo, mwambie kuwa Tunaishi siku za mwisho atakuambia sijui?..lakini atajisifia kipaimara chake kwa sherehe kubwa aliyoifanya siku hiyo. Utakuta mtu analijua dhehebu lake kuliko anavyoijua biblia.

Kwahiyo kanuni za kipaimara sio kanuni zilizokatibiwa na Mungu bali wanadamu, Mungu hajatoa kanuni maalumu kuwa mtu lazima apitie kipaimara au apakwe mafuta ya maombezi, au atumie chumvi ndipo afunguliwe au akubaliwe na yeye..yote hiyo ni mipango ya ibilisi kuwafanya watu wasitafakari maandiko kwa kina bali wapate njia za mkato za kutatua matatizo yao. Na kujiridhisha katika hizo kama ndio sababu ya kukubaliwa na Mungu, kumbe sio.
 
Ubarikiwe.

SWALI 2: Tukisoma Matendo 19:13 Inasema pale "Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, NAO NI WAPUNGA PEPO....” swali,Naomba kufahamu hawa Wapunga Pepo ni watu wa aina gani ndugu zangu?

JIBU: Tafsiri ya Neno kupunga pepo ni “kufukuza pepo”…hiyo ni lugha iliyotumika katika tafsiri yetu ya Kiswahili inayosimama badala ya kufukuza pepo…Kwahiyo zamani na hata sasa zilikuwepo njia nyingi za kuondoa pepo ndani ya mtu…

Watu wa Mungu wanao uwezo wa kufukuza mapepo kwa kutumia jina la YESU, kadhalika na watu wa shetani wanauwezo wa kufukuza pepo.
Sasa njia wanayotumia watu wa Mungu kufukuza mapepo ni tofauti na njia wanazozitumia wachawi au waganga…
Wakristo wanafukuza pepo na kumfanya yule mtu kuwa huru kabisa kabisa, kwa kutumia jina la Yesu Kristo kwa Imani, mtu huyo anafunguka na kuwa huru..kama mtu alikuwa na pepo fulani lililomletea ugonjwa Fulani labda ugonjwa wa kuumwa tumbo, linapoondolewa kwa jina la Yesu linaondoka moja kwa moja pamoja na ule ugonjwa wake na madhara yake yote.

Lakini waganga wa kienyeji au wachawi wanavyofukuza mapepo ni tofauti kabisa kwao haiwi hivyo..wao hawayafukuzi bali wanaleta mapepo mengine juu ya yule mtu yenye nguvu zaidi ya lile pepo lililopo ndani ya yule mtu, kwahiyo kinachotokea labda yule mtu alikuwa na pepo fulani lililomletea ugonjwa fulani labda wa kuumwa tumbo, Yule mtu anapokwenda kwa mganga(mpunga pepo)… yule mganga anamtumia pepo lingine lenye nguvu kuliko lile la ugonjwa wa tumbo linamwingia labda tuseme pepo la utasa na lile pepo la ugonjwa wa kuuma tumbo nguvu zake zinafunikwa na lile lingine la utasa lililomwingia.

Kwahiyo yule mtu baada ya kuaguliwa na yule mganga anaweza akajisikia unafuu wa kupona tumbo kwa muda…lakini baada ya kipindi fulani anakuja kujigundua tena kapata utasa au ugonjwa mwingine mkubwa zaidi…sasa hiyo hali ya kupunguza pepo hili nguvu kwa kulileta lingine lenye nguvu zaidi ya lile la kwanza ndiyo inayoitwa “kupunga pepo”.

Ni sawa kuleta nyoka ndani ili ale panya wanaokula mahindi yako ghalani, atawapunguza tu na kufurahi kwa muda lakini hawezi kuwamaliza wote, na zaidi ya yote huyo nyoka siku moja atakuletea madhara na wewe…

Kwahiyo waganga hawana uwezo wa kutoa mapepo, wanaongeza pepo juu ya pepo, kwasababu shetani hawezi kujifitini kwenye ufalme wake mwenyewe kama Bwana Yesu alivyosema…

Mathayo 12:26 “Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?”.

 SWALI 3: Wale Watakatifu waliofufuka na Bwana Yesu WALIKUWA WAPI KABLA YA KUFUFUKA kwao je! walikuwa Peponi au ni wapi?.

JIBU: Wafu wote waliokufa kabla ya Kristo kuja duniani walikuwa makaburini, au sehemu za wafu, mahali pengine katika biblia panapaita Kuzimu, Daudi aliomba katika roho akisema "Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu."(Zaburi 16:10)

Aliomba asiende sehemu za wafu iliyo njia ya wote, lakini tunasoma alikufa na akakusanywa na baba zake huko, Lakini kumbe Unabii huo ulikuwa haumuhusu yeye bali Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni yeye pekee nafsi yake haikubaki huko.

Hivyo biblia haielezi kwa mapana walikuwa wanaishije ishije huko..lakini ni mahali ambapo hatuwezi kusema palikuwa ni salama sana, kwa maana shetani naye kwa sehemu Fulani alikuwa anao uwezo wa kuwasiliana na hata watu wenye haki waliokuwa wamekufa zamani, tunalithibitisha jambo hilo kwa Samweli,(1 Samweli 28)…Na hiyo ni kwasababu ya kuasi kwetu ndipo kulipompa shetani baadhi ya funguo za kututawala sisi hata mpaka baada ya kufa kwetu..japo alikuwa hana uwezo wa kuwaondoa mahali walipokuwepo…Lakini Kristo alipokuja na kushinda vyote pale msalabani, ndipo akachukua funguo zote za kuzimu na mauti na sasa wafu wote anawamiliki yeye.

Ufunuo 1: 17 "Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

Hivyo leo hii hakuna mtu au pepo lolote, au shetani anayeweza kuwasiliana na mtu wa aina yoyote yule aliyekufa ile awe mwenye dhambi au asiye na dhambi isipokuwa YESU peke yake..Ukiona mtu anakuambia mzimu wa baba yangu, au bibi yangu umenijia basi ujue kuwa hilo ni PEPO lililojigueza na kuvaa sura ya yule mtu,na wala si yule mtu halisi..Sasa kukaa kwake Bwana kaburini zile siku tatu, kulikuwa ni kushuka kuzimu huko wafu wote walipo ili kuwatenga wale wafu waovu na wema kwa injili aliyokwenda kuwahubiria.

1Petro 3:18 "Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,
19 AMBAYO KWA HIYO ALIWAENDEA ROHO WALIOKAA KIFUNGONI, AKAWAHUBIRI;
20 watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji".

Sasa wale wema ambao waliishi maisha ya haki duniani na ya kumcha Mungu walihamishwa na kupelekwa mahali pa raha zaidi, ambapo panajulikana kama PEPONI/PARADISO (Kule alipomwambia yule mwizi aliyesulibiwa kuwa atakuwepo naye siku hiyo hiyo peponi)…Lakini wale waovu waliosalia walisogezwa mahali pa shida zaidi huko huko kuzimu…. Na katikati yao kukawekwa SHIMO kubwa ili wa kule wasiweze kuja huku na wa huku kwenda kule katika Roho,..Wale wema walipandishwa juu, lakini waovu walizidi kukaa chini na ndio maana yule tajiri katika habari ya Lazaro utamwona akinyanyua macho yake na kumwona Lazaro upande wa pili kule kuzimu.

Luka 16:19 "Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.
20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi,16.21 naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake.
22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.
26 Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.
27 Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,
28 kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.
29 Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.
30 Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.
31 Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu".

Sasa tukirudi kwenye swali wale wafu walikuwa wapi, ndio hapo siku ile Bwana aliyofufuka utawaona wafu watakatifu wakitoka makaburini, na kuhamishiwa Peponi,..Hivyo mtu akifa leo katika haki moja kwa moja anapanda peponi/paradiso akisubiria UFUFUO wa Haki siku ile ya unyakuo..lakini atakayekufa katika dhambi, naye moja kwa moja atateremka Jehanum, kwenye mateso makali akingojea naye kufufuliwa siku ile ya hukumu mbele ya kiti kile cheupe cha Enzi cha Mwanakondoo ahukumiwe kisha atupwe kwenye lile ziwa la moto…..

Hivyo huu ni wakati wa kuweka mambo yetu sawa, yasije yakatukuta kama yale ya yule tajiri, biblia inasema itatufaidia nini tuupate ulimwengu mzima na mwisho wa siku tupate hasara ya nafsi zetu.?. Kiburi cha mwanadamu ni maua leo kipo kesho kinanyauka, ikiwa leo utajikuta haupo tena duniani..Huko uendako utakuwa mgeni wa nani? Huko hakuna nafasi ya pili,....Wokovu unapatikana bure sasa, ukikupita leo kesho utautafuta kwa kilio na kusaga meno na hautauona.. Ni maombi ikiwa maisha yako yapo mbali na Kristo basi leo fanya uamuzi wa kumkabidhi yeye maisha yako na yeye ana upendo na ni mpole na ameahidi kukupokea, na kuwapokea wote wanaomkimbilia yeye.

Ubarikiwe

4 comments: