"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, April 19, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 60


SWALI 1: Shalom mtumishi wa Mungu; Naomba unisaidie kuelewa haya maandiko katika (matendo 9:3-7, 22:6-9, 26:12-14). Pale Mtume Paulo alipokuwa anatoka Yerusalemu kwenda Dameski kushika wakristo na kukutana na YESU njiani. Kama yanazungumzia habari moja mbona kama yanajichanganya yenyewe?.
JIBU: Mtafaruku mkubwa kwenye vifungu hivyo vitatu ni pale ile sauti ilipotoka mbinguni ikisema na Paulo. Watu wanajiuliza inakuaje sasa sehemu moja biblia inasema wale watu waliisikia sauti ya Yesu iliyosema na Paulo , na sehemu nyingine biblia inasema hawakuisikia?, Ni kwanini iwe hivyo?
Kwamfano Tukisoma Matendo 9:7 inatuambia…. “Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, WAKIISIKIA SAUTI, WASIONE MTU.”

Lakini tukirudi tena kusoma kwenye kitabu hicho hicho cha Matendo ile sura ya 22.9 Paulo anasema…”Na wale waliokuwa pamoja nami WALIIONA ILE NURU, LAKINI HAWAKUISIKIA ILE SAUTI YA YULE ALIYESEMA NAMI”.

Unaona hapo kunaonekana kama kuna mkanganyiko fulani, inaonyesha kama maandiko yanajipinga hivi, huku yanasema wale watu waliisikia sauti, wakati huo huo tena mbeleni kidogo inasema wale watu hawakusikia ile sauti iliyosema naye. Ni kweli kabisa tukisoma kwa juu juu tu tunaweza kuona maandiko yanajipinga lakini kiuhalisia maandiko hayajichanganyi, badala yake ni sisi ndio tunakosa shabaha ya kuyaelewa..uelewa wetu ndio unaojichanganya.

Na ndio maana Mtume Paulo kwa kuyaona mambo kama hayo alikuwa akimsisitiza Timotheo mara kwa mara, akimwambia afanye bidii katika KUSOMA (1Timotheo 4:13)..Sasa Kusoma kunakozungumiziwa hapo sio kusoma kama mtu asomavyo gazeti, halafu basi, hapana bali ni kusoma kwa KUJIFUNZA..yaani Kwa kuchukua muda kutafakari na kuchambua kwa undani maandiko huku ukimwomba Roho Mtakatifu akuongoze kuyaelewa vinginevyo biblia inaweza kubakia kwako kuwa kama kitabu kisichoeleweka daima, na kinachojipinga siku zote.

Sasa tukirudi darasani.

Katika maandiko kumbuka Neno KUSIKIA linamaana kubwa zaidi ya “kusikia” tu peke yake..Kwa mfano Utaona Yesu alipofundisha mifano yake mingi alimalizia na kauli hii “mwenye masikio ya kusikia na asikie.” Unaona hapo Hakumaanisha kuwa watu waliokuwa mahali pale walikuwa viziwi hawasikii alichokuwa anakizungumza, hapana bali alimaanisha “mwenye masikio ya kuelewa na akielewe kile alichokuwa anakimaanisha.”..

Hali kadhalika Mungu anaweza kuzungumza na mtu maneno yanayoeleweka kabisa na kumshushia ujumbe, lakini kwa mtu mwingine ujumbe ule ukamwasilia kama sauti tu ya ajabu, au ngurumo tu, au mlio wa ajabu usioeleweka,..tunalithibitisha hilo kwa Yesu siku ile aliponyanyua kichwa chake juu na kumwomba baba ndipo sauti ilipotoka juu na kusema naye.…,

Yohana 12: 28 "Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.29 Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye.[30 Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu

Unaona hapo? Wale watu waliisikia sauti kabisa, na wengine wakatambua ya kuwa ni Mungu ndiye aliyekuwa anasema naye, lakini Hawakuielewa …ilikuja kwao kama kitu kingine kama ngurumo tu, sauti isiyoeleweka.. “” kwahiyo waliisikia sauti lakini ni sawa na hawajaisikia maana hawajaielewa.

Na ndicho kilichowakuta kundi la watu hawa, walipokuwa wanatoka Yerusalemu kuelekea Dameski, wakiongozwa na kiongozi wao mkuu Sauli (Paulo), waliokwenda kuwakamata Wayahudi wote waliokuwa wakimtangaza Kristo hadharani ili kuwarudisha Yerusalemu waadhibiwe….Ndio katikati ya safari yao walipokutwa na tukio hilo la ajabu, njia mida ya adhuhuri ile nuru kuu kutoka mbinguni ikawaangazia wote, ndipo Yesu akaanza kuzungumza na Sauli kwa lugha ya Kiebrania.

Sasa hapo wale watu waliokuwa na Sauli muda ule waliisikia kweli sauti fulani iliyotoka mbinguni, lakini kwao ilikuja kama sauti isiyoeleweka…kama mlio tu au mngurumo!..

Na ndio hapo sasa tukirudi kwenye vile vifungu kama kile cha kwanza mwandishi anasema..”

Matendo 9:7 …. “Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, WAKIISIKIA SAUTI, WASIONE MTU.”
Unaona, Hapa ni sawa na kusema walisikia ngurumo tu au sauti isiyoeleweka kutoka mbinguni mahali pale, hakukuwa kimya kabisa kulikuwa na sauti fulani mahali pale,.

Sasa Tukirudi kwenye kile kifungu cha pili inatuambia..
Matendo 22.9 …”Na wale waliokuwa pamoja nami WALIIONA ILE NURU, LAKINI HAWAKUISIKIA ILE SAUTI YA YULE ALIYESEMA NAMI”.

Hapo ni sawa na kusema Hawakuelewa, kile walichokisia..Hivyo maandiko yapo sawa, na wala hayajipingi na hata sasa biblia inatumbia Luka 8:18 "Jiangalieni basi jinsi msikiavyo;"..Tunapaswa tuwe makini na kile Mungu anachosema nasi, katika maandiko wakati mwingine tunaweza kujiona tumefika tunaelewa kila kitu, biblia tunaifahamu yote, hakuna hadithi tusioyoijua katika biblia, lakini kumbe hatujaielewa sauti ya Mungu iliyojificha nyumba yake.

Bwana Yesu alisema.. Mathayo 13:14 “Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, KUSIKIA MTASIKIA, WALA HAMTAELEWA; Kutazama mtatazama, wala hamtaona.13.15 Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.”
 
Mungu aturehemu na atujalie kumjua zaidi..

Ubarikiwe.

SWALI 2: Shalom kucheza karata ni sahihi kwa Mtu aliye MKRITO?
JIBU: Kwanza kabisa hebu tujifunze juu ya hili..”Ni kwanini Shule nyingi za bweni karibia zote, zinakataza watoto kuwa na simu au kucheza karata au magemu au kuangalia movie?”..unafikiri ni kwanini?..Jibu ni rahisi ni kwasababu vitu hivyo vinapotumiwa na wanafunzi vinawasababishia kwa namna moja au nyingine kutokuwa na kiasi na matokeo yake inawapelekea kusahau kilichowapeleka shule na mwisho wa siku ni kufeli tu, Kwani ule muda ambao mtoto angepaswa afikirie masomo yake anajikuta anafikiria ile movie aliyoiangalia jana usiku au zile karata alizokuwa anazicheza au atakazozicheza, na mwisho wa siku hiyo inabadilika na kuwa hasara kubwa kwa mwanafunzi, na kwa shule na kwa Taifa kwa ujumla…Sasa kama wanadamu wanauwezo wa kuwa na hekima kama hiyo ya kupambanua hayo mambo yanayofaa na yasiyofaa…unadhani kwa Mungu itakuaje?..Ni dhahiri kuwa itakuwa ni zaidi ya hapo.

Biblia inasema tusiupende ulimwengu 1 Yohana 2:15 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele”.

Unaona? Kwanini biblia inasema tusiipende dunia?..sio kwamba dunia ni mbaya, sio kwamba michezo ni mibaya, wala sio kwamba kustareheka ni kubaya…hapana vitu vyote hivyo sio vibaya kama vikitumiwa ipasavyo…Ubaya ni kwamba tunaishi duniani kwa muda! tupo darasani kwa kipindi kifupi sana, tukiyafuata hayo mambo ya duniani basi tujue kuwa hatutazingatia mambo ya Mungu, na matokeo yake ni kufeli na hivyo kupata hasara ya nafsi zetu. na Mungu wetu hataki tupotee ndio maana anatuambia tukae mbali na mambo hayo ya ulimwengu…

Sisi (watoto wa Mungu) Ni sawa na mwanafunzi walioko shuleni, tena shule za Bweni…Ni wasafiri tu wa hapa duniani, tunatengeneza maisha yetu sasa ili tuwe na maisha bora huko katika umilele unaokuja…Hivyo kama ni starehe, basi tutazifanya sana katika hiyo mbingu mpya na nchi mpya inayotungojea huko mbeleni, kama ni kufurahi, kama ni kuzurura, kama ni kucheza na kujiburudisha kwa jinsi tupendavyo basi tutafanya sana katika hiyo Yerusalemu mpya ambayo Mungu ametuandalia huko mbeleni, ..…lakini sasa katika ulimwengu huu sio wakati wake…Hayo mambo ni ya wakati wa zamani zijazo za wakati wa ulimwengu ujao, ambapo huko kutakuwa hakuna kusoma tena biblia wala kuhubiri, wala kufunga, wala hakutakuwa na majaribu tena, wala maumivu wala kula kwa jasho, wala kujizuia…hayo mambo hayatakuwepo kule, kule itakuwa ni sehemu ya furaha, ya kufanikiwa na ya uhuru usio na kifani. Ndivyo maandiko yanavyosema.

Lakini Wengi wanasema ni ushamba kujinyima raha katika ulimwengu huu, lakini hao hao hawajui kuwa ni ushamba mkubwa zaidi kujinyima raha za umilele unaokuja huko mbeleni…jiulize ukifa leo huko utaenda kuwa mgeni wa nani?. Kumbuka Mwanafunzi mwenye busara ni yule anayezingatia kilichompeleka shuleni..sio ushamba mwanafunzi kujizuia kuangalia movie ili atumie muda wake vizuri katika masomo, wala si ushamba mwanafunzi anapojizuia kuzurura zurura huku na huko na badala yake muda wote unautumia kutafakari masomo ili mitihani aje kufaulu vizuri…anajinyima hivyo vyote kwasababu anajua ni kwa faida yake mwenyewe na ni kwa muda mfupi tu, ..anajua siku akimaliza shule na kufaulu, atayafanya hayo sana na zaidi ya hayo…

Na sisi tunapaswa tuzingatie kwasasa kile kilichotuleta duniani. Sio ushamba kuukataa ulimwengu, sio kila kitu kinachoja mbele yetu tukijaribu tu, vingine vinatupoteza muda, vingine vinatuondoa katika dira ya wokovu, vingine vinaturudisha nyuma… Ni wajibu wetu kuenenda katika hii dunia kwa werevu.

Kwahiyo kwa kuhitimisha, mchezo wa karata haufai kwa mtoto wa Mungu, utacheza karata masaa mawili lakini kushika biblia dakika tano huwezi, utaangalia muvi series hata masaa nane lakini biblia dakika 10 huwezi…huoni kuna roho nyuma ya huo mchezo?..roho inayokufanya kutokuzingatia mambo ya msingi ya Imani. Hiyo ni roho inayokupeleka katika kufeli maisha. Hivyo tuwe makini sana.

Ubarikiwe.

SWALI 3: Ninatamani kwenda kusomea udaktari , lakini nina mashaka labda sio mapenzi ya Mungu kwangu, inanifanya nisiwe na maamuzi ya kueleweka..Naomba ushauri nifanyeje ili nijue masomo Mungu aliyoyakusudia nisomee katika maisha yangu.?

JIBU: Swali hilo linafanana na lile la mtu anayemwomba Mungu mpenzi sahihi wa kuoa/kuolewa katika maisha yake.. Mara nyingi tunatarajia Mungu atufunulie aidha kwa ndoto au maono au unabii au kwa njia nyingine iliyo dhahiri juu ya mpenzi wa kuoa, na hiyo inatufanya tufikiri labda pengine Mungu asipotumia njia kama hizo kabisa basi tumeoa mke/mume asiyesahihi, au tumeingia mahali pasipotupasa.

Lakini kumbuka Mungu kujitambulisha kwetu kama MSHAURI WA AJABU,(Isaya 9:6) ni uthibitisho tosha kuonyesha kuwa Mungu sio dikteta wa mawazo ya mtu. Ikiwa na maana kuwa kama angekuwa hataki wewe uwe na uchaguzi wako binafsi, basi asingejitambulisha kwako kama mshauri badala yake angejiita “kamanda”..Tatizo linakuja ni pale ambapo hatumfanyi Mungu kuwa mshauri wetu, na ndio hapo tunaingia katika maamuzi yasiyo sahihi..

Lakini mtu atajiuliza je! Tunamfanyaje Mungu kuwa mshauri wetu?..Jibu lipo wazi , na mashauri yake yapo wazi kabisa na karibu kila mtu anayafahamu na ameshayasikia, na hayo si mengine zaidi ya MAANDIKO MATAKATIFU.

Hivyo ikiwa tumefikiria kufanya jambo Fulani ambalo tumelipenda, pengine tunataka kuoa au kuolewa na mtu fulani, jambo la kufanya kwanza ni kutuliza akili, pata muda wa kutosha wa kuombea jambo hilo, kisha ukishamaliza hatua hiyo lichukue katika maandiko, uangalie je! Litapinga imani yako au la!..kwa mfano unaweza ukawa umetamani kweli kufanya biashara Fulani ya kuuza vinywaji,lakini ndani yake kuna pombe,..sasa hata kama uliiependa biashara hiyo lakini ushauri wa Mungu unakuambia hapana maandiko hayaruhusu pombe…

Hivyo moja kwa moja unapaswa uache , utafuate kitu kingine.
Inawezekana pia binti umempenda mwanaume mzuri, lakini ni wa imani tofauti, na yeye anataka mfunge ndoa muishi pamoja,..Lakini ushauri wa Mungu unakukataza katika maandiko, kwamba ndoa inapaswa ifungwe katika Bwana tu!, hivyo ikiwa mtu huyo hatataka kuigekia imani ya kweli ya Yesu Kristo, basi unachopaswa kufanya ni kukataa jambo hilo hata kama ulikuwa unampenda kiasi gani.. Hiyo ni kwa faida yako mwenyewe.

Lakini ikitokea sasa umeshavipitisha vyote hivyo kwenye mizani ya ki-Mungu na kuona kuwa hakuna chochote kinachopingana na maandiko na ndani yako umekipenda kweli na unasikia amani kukifanya, kwamfano, unahitaji kwenda kusomea udaktari hapo hakuna ubaya wowote, maadamu tayari ulishatenga muda wa kumwomba Mungu akutangulie basi hiyo inatosha kukupa amani kuwa Mungu ameshakusikia..Hivyo usiogope kwenda kusomea..

Kwasababu biblia inasema.

Mithali 16:1 “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.”

Hivyo hata ikitokea hicho ulichomwomba Mungu kukifanya au kukitenda hakikuwa ni sawasawa na mapenzi yake, kwa kuwa ulishamshirikisha mawazo yako kabla ya kuingia basi yeye mwenyewe atahakikisha anakuepusha nacho, au atakuandalia mazingira mazuri ya kutimiza kusudi lake ndani yake. Kama hajakujibu kwa ndoto au maono vile vile atakuepushia nacho pasipo ndoto wala maono kama sio mpango wake..Mungu wetu hatuweki kwenye mtego kwamba tumwombe akae kimya na aruhusu tufanye jambo fulani kimakosa ili kesho na kesho kutwa aje kutulaumu!..yeye hayupo hivyo wanadamu ndio wapo hivyo..

Kwahiyo Kikubwa tu hakikisha huchukui uamuzi wowote bila kuupeleka kwanza kwenye maombi kwa muda wa kutosha, (sio maombi ya chai, hapana walau tenga kipindi kirefu kidogo, kuonyesha umakini kwamba umekusudia kweli kumkabidhi Mungu njia zako, hata ikiwezekana funga siku kudhaa,) ,Na pili hakiki kama kinaathiri imani yako au kinapingana na maandiko..ikiwa vitu hivyo viwili umevizingatia ipasavyo na hakuna shida basi endelea mbele kufanya unachotaka kufanya kwasababu Mungu atakuwa pamoja na wewe kuyaonyoosha mapito yako. Usisubiri ndoto wala maono.

Mithali 16: 3 Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.

Lakini kama unasubiria maono au ndoto, au malaika akutokee ndipo achukue hatua...nakushauri acha kwasababu unaweza ukavunjika moyo pale ambapo majibu yatakuja usivyotarajia kwa kutokuona chochote, na mwisho wa siku ukajikuta upo njia panda hujui lipi la kufanya.
SWALI 4: Shalom! Luka 23:27 "Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata,na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua vyao na kumwombolezea.Yesu akawageukia,akasema,Enyi binti za Yerus'alemu,msinililie mimi,bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.29"KWA MAANA TAZAMA SIKU ZINAKUJA mtakaposema,HERI WALIOTASA,na MATUMBO YASIYOZAA,na MAZIWA YASIYONYONYESHA. Naomba kufahamu Siku hizo Kwanini hao walisema "Heri waliotasa..heri matumbo yasiyozaa..heri maziwa yasiyonyonyesha??
JIBU: Shalom! Hayo maneno a Bwana Yesu aliyazungumza kabla ya kupandishwa msalabani, Tunaona wale wanawake waliokuwa wanamfuata walimwonea huruma sana na kusikia uchungu mkubwa kwa mateso aliyokuwa anayapitia…lakini Bwana Yesu akawaambia msinililie mimi bali jililieni ninyi nafsi zenu na watoto wenu..

Kwanini alisema vile…Kwasababu aliona kipindi kifupi sana kinachokuja mbeleni…kwamba mambo yaliyompata yeye yatakwenda kuwapata na wao pia, pamoja na watoto wao tena makubwa zaidi ya hayo…ambapo na wao pia watakatwa katwa na wanawake watachichwa kama kuku. Na kama unafuatilia unabii vizuri wa Biblia utakuja kuona kuwa kipindi kifupi tu baadaye AD 70 (yaani miaka 37 baada ya kusulibiwa kwa Bwana)..Jeshi la Rumi lilikuja na kuuzingira mji wa Yerusalemu na kuuchoma moto na kuwaaua watu wengi sana wakiwemo wanawake na watoto …historia inasema zaidi ya watu milioni moja na laki moja waliuawa…Mpaka ikaonekana kuwa ni heri mwanamke aliyetasa ambaye hakuzaa mtoto kuliko Yule aliyezaa na kuona mtoto wake anachichwa kama kuku mbele yake,Yerusalemu kulikuwa na maombolezo makubwa sana, hiyo ni kutimiza unabii alioutoa Bwana juu ya Mji huo katika..

Luka 19: 41 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,
42 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.
43 Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;
44 watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”.

Mathayo 23.37 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!
38 Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa”.

Unaona hapo? Sababu ya Mji kuharibiwa na kufanywa ukiwa?..Ni kwasababu hawakujua saa ya kujiliwa kwao, ni kwasababu Masihi alikuja kwao na wao wakamkataa wakasema anapepo, anakufuru n.k hawakujua kuwa yeye ni mwokozi na ndiye aliyeteuliwa na MUNGU kuwa ukombozi kwa mwanadamu…Na kwasababu hiyo, Bwana akawaambia ule ulinzi na amani vimeondoka kwao siku zinakuja siku watakapoteketezwa na kuangamizwa na kutolewa kutoka katika nchi yao..Ndio maana Bwana akawaambia msinililie mimi, bali jililieni nyinyi na watoto wenu..kwasababu yatakayokuja kutokea mbeleni ni makubwa kuliko haya yangu.

Hiyo ilikuwa ni dhiki au adhabu kwa wayahudi (yaani waisraeli) kwa kumkataa Masihi, na kadhalika itakuja dhiki nyingine iliyo kubwa na isiyo na mfano kwa watu wa dunia nzima, kwa wale wote ambao wanamkataa Kristo sasa na kumsulibisha katika akili zao..Dhiki hiyo itakuwa ni kubwa isiyokuwa na mfano kuliko hiyo iliyowapata wayahudi..Biblia inaeleza hivyo.

Kwahiyo tukiyajua hayo, sio wakati wa kuchezea hatima yetu ya milele, kabla dhiki kuu haijamiminwa duniani tunapaswa wakati huo tuwe tumekwenda na Bwana katika unyakuo. Je! Na wewe una uhakika utakuwepo miongoni mwao watakaomlaki Bwana mawinguni?

Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment