"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, May 22, 2019

CHACHU YA MAFARISAYO NA CHACHU YA HERODE.


Chachu ni nini?. Chachu kwa lugha ya sasa ni HAMIRA, na kwa kawaida ukiitazama hamira unaweza ukadhani ni unga Fulani hivi, lakini kiuhalisia ule si unga bali ni mkusanyiko wa wadudu wenye uhai kwa lugha ya kitaalamu wanaitwa YEAST, hawa wanadudu ndio wanaofanya kazi ya kumengenya ule unga, na kutoa gasi maalumu ambayo ndiyo inaufanya ule unga uumuke. Kwahiyo hamira sio kama chumvi au sukari ambavyo havina uhai ndani yake, Hamira ni kitu chenye uhai kwasababu ni wadudu wale. Na ndio maana ikiwekwa mahali inaweza kubadili maumbile ya kitu na kukifanya kuwa kingine kabisa..
Kwamfano unga wa ngano ukitiwa hamira, ukila kalmati sio sawa na utakavyokula keki, na sio sawa na utakavyokula tambi au maandazi. Yote hii inafanywa na kazi moja ya Hamira (CHACHU). Kubadilisha maumbile.

Na ndio maana Bwana alitumia Neno “chachu” kuonyesha madhara yanayoweza kumtokea mtu asipojihadhari na hayo atakayoonywa.

Tukisoma.
Marko 8:15 inasema “Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode”.
Mathayo 16:12 “Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo”.

Mahali pengine anasema:
Luka12 :1 “Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni UNAFIKI”.

Kwahiyo kumbe chachu anayoisemea alikuwa anamaanisha kuwa ni MAFUNDISHO YA KINAFKI. Ambayo yanaletwa na hayo makundi mawili, kundi la kwanza ni watu wa kidini na kundi la Pili ni wana SIASA.

Na leo kwa neema za Mungu tutaliangalia zaidi hili kundi la PILI. Tunajua makundi yote haya wakati wa BWANA YESU na ule wa mitume yote yalifanyika kuwa maadui wakubwa wa kazi ya Mungu, tunaona wakati tu Bwana Yesu anazaliwa Herode alitaka kumuua lakini mpango wake ukashindikana, baadaye mtoto wake akafanikiwa kumuua Yohana Mbatizaji, na ndio huyo huyo alitaka tena kuja kumuua Yesu, lakini Yesu alimwita Mbweha..halikadhalika mafarisayo na waandishi walikuwa wanamvizia siku zote za huduma yake wamwangamize mpaka baadaye mwishoni wakafanikiwa wote wawili kuungana (yaani Herode na mafarisayo) ili kumuua YESU.

Lakini heri wangekuwa wanafanya vile kwa ujinga, Lakini Bwana alikuwa anasema wanafanya kinafki, ikiwa na maana kuwa wale ambao wangepaswa wawe watenda haki na watunza sheria za Imani na za nchi wao ndio wanaokuwa wa kwanza kutokusimamia haki, kwa nje wanaonekana ni watenda haki na wanasiasa bora lakini kumbe ndani yao ni wanafki…Na kwasababu hiyo basi Yesu akawaonya wanafunzi wake wajitenge na njia zao, kwasababu kama wakiambatana nao, wao pia muda si mrefu wategeuzwa kwa unafki wao na kufanana nao, na mwisho wa siku watajikuta wanamkosea Mungu.

Jambo hilo hilo tunaonywa hata na sasa, TUJIEPUSHA NA WANASIASA, sio kwamba tusionge nao kabisa, au tusile nao au tusialikwe nao hapana…Bali tusikubali CHACHU yao iingie ndani yetu.. Kwasababu hiyo inaweza ukatubalisha maumbile yetu ya kiroho na kuwa watu tofauti kabisa, tofauti na tulivyokuwa hapo mwanzo. Na sisi tutaanza kuwa wanafki, tutaanza kufanana na wao,.na mwisho wa siku tutaangamia.

Hilo ni kosa mojawapo linalofanywa na watumishi wengi wa Mungu sasa, ikiwa Mungu amekupa ujumbe kwa mwanasiasa, basi utoe kulingana na maagizo ya ki-Mungu, na usiwe wakati wa wewe kila jambo la kisiasa upo, kampeni upo, jeshi la polisi upo, bungeni upo, ..n.k..vikao vya kisiasa mtaani kwako upo, mijadala ya kisiasa upo, Hayo ni mambo ambayo kwa nje unaweza ukaona upo sahihi lakini nyuma yake unajiangamiza mwenyewe.

Ukiwa umeamua kuwa mtumishi wa Mungu, na mtumishi wa Mungu siye anayehubiri tu madhabahuni, bali yeyote Yule anayemtumikia Mungu kwa karama aliyopewa (huyo ni mtumishi wa Mungu) weka mbali mambo ya SIASA, tuwache wao na shughuli zao na sisi tuendelee na shuhuli zetu za kutangaza habari za haki, na injili..Na ndivyo tutakavyo fanikiwa kutumika pasipo kujikwaa.
1Wakorintho 5:7 “ Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;
8 basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli”.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment