"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, May 22, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 63


SWALI 1: 1 Samweli1:17-18. Inasema: Daudi akamwomboleza Sauli,na Yonathani, mwanawe,..."(Kama ilivyoandikwa katika KITABU CHA YASHARI').Hicho kitabu cha Yashari ni kipi?

JIBU: Kumbuka Biblia sio kitabu cha kinabii tu kutabiri mambo yajayo peke yake, hapana bali pia ni kitabu kilichorekodi historia ya mambo yaliyopita, Na hiyo yote ni ili kutufundisha na kutuonya sisi kwa mifano iliyo hai ambayo ilishawahi kutokea huko nyuma,tuamini na kugeuka, Hivyo sikuzote ili historia iweze kukubalika kuwa ni kweli ipo wazi kuwa ni lazima iwe imetibitishwa kwa ushahidi zaidi ya mmoja,

Kwa mfano haiwezekani historia ya vita vya Kagera ijulikane na watanzania tu peke yao watu wengine duniani wasiifahamu, yaani tujitangaze duniani kote sisi tulipigana vita na Uganda, lakini hakuna taifa hata moja lililoona hilo na kuthibitisha habari hiyo, kwa namna moja au nyingine zinaweza zikawa ni habari za kuzusha tu, lakini kama jirani zetu wakenya walishuhudia ni kweli, waganda walishuhudia ni kweli tulipigana nao, na Waafrika wote waliokuwepo kipindi kile watashuhudia jinsi walivyoshirikiana na sisi katika vita vile, basi hiyo vita kwa asilimia zote itakuwa ni ya ukweli na ilishawahi kupiganwa na hata kwa vizazi 100 vijavyo havitaweza kukana kwa ushahidi huo.

Vivyo hivyo biblia nayo, ilivyoandika habari, kwa kuwathibitishia watu kuwa hayo yote ni kweli ikiwa kama mtu atatokea hatoamini kilichoandikwa, basi vipo vitabu vingine ambavyo vimerekodi habari za matukio hayo hayo biblia iliyoyarekodi, na mojawapo ndio hichi kitabu cha YASHIRI ambacho tunaona kimeandika maombolezo ya mashujaa na sehemu nyingine matendo makuu yaliyofanywa na mashujaa wa Israeli.

Sasa tafsiri ya hilo Neno Yashiri “NI MTU MWEMA AU MTU MTU WA HAKI”, hili ni Neno la Kiyahudi, hivyo kitabu cha Yashiri ni kitabu cha mtu mwema, au mtu wa haki, na kitabu hichi katika biblia hakijazungumziwa hapa tu tunakisoma pia katika kitabu cha Yoshua :

Yoshua 10: 12 “Ndipo Yoshua akanena na Bwana katika siku hiyo ambayo Bwana aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni.
13 Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao. Hayo, Je! Hayakuandikwa ndani ya kitabu cha YASHARI? Basi jua likasimama kimya katikati ya mbingu, wala halikufanya haraka kuchwa kama muda wa siku nzima”.

Unaona, vipo pia vitabu vingine vinatajwa mbali na hii biblia yetu, ukisoma Hesabu 21:14, utaona kimoja kinaitwa kitabu cha VITA VYA BWANA. Ukisoma pia (1Nyakati 29:29), Utaona kulikuwa na kitabu kinachojulikana kama KITABU CHA TAREHE CHA SAMWELI MWONAJI, kulikuwa na kitabu cha tarehe ya Nathani, nabii, na pia kulikuwa na kitabu cha tarehe ya Gadi, mwonaji; Pia kulikuwa na kitabu cha tarehe cha wafalme wa Yuda, ukisoma (1Wafalme 14:29), utaliona hilo:..

1Wafalme 14:29 “Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?”

Unaona vyote hivyo vilinakili matukio ambayo biblia ilirekodi pia. Lakini sasa hiyo haimaanishi kuwa ni vitabu vilivyovuviwa na Roho Mtakatifu kwamba vitumike kuwa mbadala wa Biblia hapana, Hivyo vipo kuithitisha kuwa Biblia ni kweli na sio biblia kuthibitisha kuwa vitabu hivyo ni kweli.

Halikadhalika leo hii, utasema mimi siiamini kuwa biblia ina habari za ukweli, wala siamini kama YESU alizaliwa na bikiria kwa uweza wa Roho Mtakatifu, wala siamini kama alipaa, hizo ni hadithi za kutunga tu, zilibuniwa tu na watu Fulani Rumi, lakini nataka nikuambie vipo vitabu vingi vya historia na vya kidini mbali na hiyo biblia unayoitilia mashaka na vyote vinathibitisha ujio wa kwanza wa Yesu Kristo kuwa ni yeye pekee ndiye aliyezaliwa na bikiria kadhalika vinathibitisha ujio wake wa pili duniani kuwa atakuja kuuhukumu ulimwengu wote. na mojawapo wa vitabu hivyo ni QURAN!..Sasa sio kwamba Qurani ni kitabu cha kweli cha Mungu hapana, kina mambo mengi sana yasiyo ya ukweli, lakini ndani yake kibebea chembechembe ndogo za ukweli kwamba ni kweli alishawahi kutokea Mtu wa kipekee aliyezaliwa bila dhambi na kuishi duniani anayeitwa YESU, na huyo atarudi tena mara ya Pili.

JE! Mambo yote Yesu aliyoyafanya tangu kuzaliwa kwake mpaka kufa kwake, na kurudi kwake hayakuandikwa katika kitabu cha waislamu Quran?. Ni uthitisho gani tena unahitaji?

Utakwenda wapi uukimbie uso wa Mungu, na ukweli uliopo katika Kristo Yesu?. Tubu leo YESU ndiye Njia kweli na uzima, NA YUPO MLANGONI KURUDI TENA, Hakuna tumaini nje ya yeye. Wala siku ile hakutakuwa na cha kujitetea.

Ubarikiwe.

SWALI 2: 1 Petro 5:14 Biblia inasema …"Salimianeni kwa BUSU LA UPENDO. Amani na iwe kwenu nyote, mlio katika Kristo. ”….Hapo ana maana gani? Mfano Binti mtakatifu akikutana nami anibusu shavuni kisha anisalimu au Mimi nikionana na Mke wako barabarani kwa kuwa ni mtakatifu kama mimi nimbusu kisha nimsalimu SHALOM?..

JIBU: Ukisoma mstari huo kwa makini utaona biblia inasema ‘BUSU LA UPENDO’ Sehemu nyingine biblia inataja kama BUSU TAKATIFU..Unaweza kusoma hiyo katika Warumi..Warumi 16: 16 “Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yawasalimu.”.. Na Pia katika 1Wakorintho16:20 inasema: “Ndugu wote wawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.”…Na mistari mingine utakayoweza kukutana na hilo neno ni 2 Wakorintho 13:11, na 1 Wathesalonike 5: 24…Mistari yote hiyo inathibitisha kuwa kuna kitu kinaitwa Busu Takatifu.

Sasa zamani kipindi cha Bwana wetu Yesu Kristo, na hata kabla ya hapo, kulikuwa na utaratibu wa kubusiana kama ishara ya salamu ya heshima kidogo, salamu ya kubusiana ndio ilikuwa salamu ya msingi kabisa kwa wakati huo, kama sasahivi ilivyo salamu ya kupeana mkono…kwahiyo watu walikuwa wakikutana walikuwa wanabusiana kwa nia ya kuonyesha upendo,shukrani, uthamani wa mtu n.k…Na kumbuka haikuwa busu la mdomo kwa mdomo hapana! Bali busu la mdomo kwa shavu au ubavu wa shavu.

Na sasa tukirudi kwenye biblia inasema kuwa tusalimiane kwa BUSU TAKATIFU, ikiwa na maana kuwa sio Busu la mapenzi, wala sio busu la ubaya kama lile Yuda alilomsaliti nalo Bwana katika..

Mathayo 26: 48 “Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni.
49 Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu”.

Bali busu linalotajwa hapo ni BUSU LA HERI, NA BARAKA na UPENDO..Yaani mtu anambusu ndugu yake katika Kristo kwa nia ya kumtakia heri na Baraka kutoka kwa Mungu, kama mwamini.

Lakini huo ulikuwa ni utamaduni wa zamani za wakati huo, ambapo Busu lilikuwa halina tafsiri nyingi tofauti tofauti kama ilivyo leo…Lakini leo hatuna utaratibu huo wa kubusiana..tuna utaratibu wa kupeana mikono…ambao huo unaweza kubeba maana kubwa zaidi au pengine hata sawa na kubusiana…Leo hii mwanamume akikutana na mwanamume mwenzake na kumbusu mbele za jamii haileti hiyo tafsiri Mtume Paulo aliyokuwa anaizungumzia hapo ya BUSU TAKATIFU, bali inaleta tafsiri nyingine…Ingekuwa ni kwa kipindi cha wakati wake ingeweza kueleweka.. 
Kwa wakati huu Busu takatifu linalokubalika katikati ya kanisa ni Busu kati ya dada na dada, au kati ya mzazi na mtoto na si kati ya kaka na dada ambao si ndugu, au kaka na kaka…Busu kati ya kaka na kaka inaleta tafsiri nyingine na maswali mengi,…

Kwahiyo hapo ni muhimu kutofautisha tu salamu zinazotumika kulingana na nyakati..Mtume Paulo hakusema kuwa hilo ni agizo toka kwa Mungu, kwamba ni lazima kila tukutanapo tusalimiane kwa kubusiana..hapana! kwasababu salamu zinabadilika kulingana na nyakati…angekuwepo katika wakati huu ambao tunapeana mikono au kukumbatiana kama salamu badala ya kubusia, angeshauri tusalimiane kwa kupeana mikono ya Utakatifu, nk.

Kwahiyo ukikutana na mwamini mwanamke, msalimie tu kwa kumpa mkono hiyo ni sawa na kumsalimia kwa busu takatifu haileti tofauti yoyote.
Ubarikiwe.
 
SWALI 3:Je! Kwetu SISI WATAKATIFU mtu akikuambia umuombee anaTATIZO halafu ukimuuliza ni tatizo gani asikuambie tatizo(Anasema hilo ni siri yake moyoni)-Huyo Tumuombee hilo tatizo lake la siri yake moyoni au?? Karibuni wapendwa..
JIBU: Kuna maombi ya kuombeana sisi kwa sisi ambayo hayahitaji mtu kumuhadithia mwingine ili amwombee, kwamfano kumwombea ndugu yako, Mungu amlinde na Yule mwovu, Mungu asimsahau katika ufalme wake, Mungu ampe kuokoa, Mungu ampe afya njema, Mungu amsaidie asimame katika imani asitetereke, Mungu ampe Amani na Upendo, mafanikio n.k..hayo ni maombi ambayo kila siku tunatakiwa tuyatamke kwa ndugu zetu wote wa mwilini na rohoni, Ndio jambo ambalo Mtume Paulo pia alikuwa analifanya:

Wakolosai 1:9 ‘’Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, HATUACHI KUFANYA MAOMBI NA DUA KWA AJILI YENU, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni;
10 mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu;’’

Lakini yapo mahitaji mengine ambayo ni LAZIMA mtu AYANENE kwa faida yake mwenyewe, kama amedhamiria kuhitaji msaada kutoka kwa wengine. Kama mtu anayehitaji kuombewa tatizo Fulani linalomsumbua halafu haweki bayana hitaji hilo, nguvu ya kuombewa itatoka wapi, ni wazi kuwa anajizuilia Baraka zake yeye mwenyewe. Biblia inaposema tuchukuliane mizigo, inamaanisha kuwa tusaidiane kwa kuitambua mizigo ya wenzetu, ukubwa wake, na uzito wake, ili mtu ajue ni jinsi gani kwa sehemu ya neema aliyopewa atamsaidia kuubeba, lakini kama mzigo kauficha mwenyewe ndani yake, wale wengine hata wakimwombea hawataomba ipasavyo, kwasababu hawatajua ukubwa au uzito wa tatizo lenyewe.

Jaribu kufikiria labda mtu ana ugonjwa ambao unamsumbua kwa muda mrefu, halafu hataki kuwaambia watu wanaomwombea kuwa anaumwa yeye anasema niombeeni tu..wale watu kweli wataomba pamoja naye lakini hiyo itaishia pale pale, lakini kama mfano kama angeweka bayana kuwa anasumbuliwa na ugonjwa Fulani(akautaja jina) na ameshahangaika muda mrefu bila matumaini yoyote, sasa kwa kuzungumza tu vile tayari katika roho anauchukua ule mzigo wake na kuwapa wengine, ndio hapo inatokea wale wenzake wanaguswa sana na shida yake, huruma zinawajaa ndani, wanaamua hata kutenga muda wao kufunga na kuomba kwa ajili ya shida yake, wengine wanampa maneno ya faraja ya kimaandiko, wanakuwa karibu naye kila siku, wengine wanaguswa wanamsaidia katika mahitaji machache ya mwilini kama kuna ulazima, na mwisho wa siku Yule mtu uponyaji wake unamfikia kwa haraka zaidi kwasababu walikuwepo wengine kuuchukua mzigo pamoja naye..

Hivyo ni lazima tujue kuwa kuna aina ya mahitaji ambayo mtu anaweza kukuombea bila hata ya kueleza siri ya moyo wako, lakini kuna mahitaji mengine kwa faida yako mwenyewe, unapaswa uwaambie ndugu wengine waaminifu, kumbuka pia sisemi kuwa kila jambo umweleze mtu, hapana, yapo mengine hayapaswi kuwekwa hadharani bali kwa watu uliowathibitisha kuwa ni waaminifu kwa Mungu. Kuna vitu vitu kama ukimwi, kesi za mauaji, n.k. hizo tafuta tu watumishi waaminifu wa Mungu, lakini vitu vingine kama magonjwa ya kawaida, ndoa, migongano, uzinzi n.k. Zungumza kwa ndugu wengine. Lakini usikae na tatizo lako moyoni ikiwa unahitaji kweli kuombewa na wengine.
Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment