"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, May 19, 2019

BWANA YESU ALIKUWA ANAONYESHA KUWA MUNGU NI MUNGU MWENYE AKILI TIMAMU.


Bwana Yesu mara nyingi alikuwa akiwaaminisha watu kwa mifano,yaani ni jinsi gani Mungu alivyo na akili timamu na alivyo na kumbukumbu nzuri sana katika mambo yake yote, alijaribu kila namna kuwatolea watu ile dhana ya kuwa Mungu ni kiumbe cha ajabu kilicho mbinguni kinahitaji kuabudiwa tu wakati wote, na hakina muda wa kutazama mambo mengine manyonge yawahusuyo wanadamu, nikisema mambo manyonge ninamaanisha mambo yanayozunguka maisha ya mwanadamu ya kila siku, kama vile majukumu, afya, chakula, malazi, matamanio ya maisha bora, raha, sherehe n.k..

Yesu alituhakikishia kuwa Mungu anatuzingatia sana, kwa kutumia mifano mirahisi kabisa iliyo hai ili kutuonyesha sisi ni jinsi gani Mungu alivyo na kumbukumbu ya haraka sana juu ya watu wake na viumbe vyake vyote..Embu chukua muda tafakari huu mfano kama ulivyo, najua unaweza kuwa na tafsiri nyingi unazozifahamu lakini naomba kwa sasa usiongeze chochote utafakari tu kama ulivyo, naamini utajifunza kitu kikubwa sana ndani yake...
Mathayo 6:26 “Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. NINYI JE! SI BORA KUPITA HAO?”.
Nataka nikuambie Mungu hategemei msaada wako wewe ili akutimize mahitaji yako ya rizki, yeye anaweza kufanya hayo yote bila msaada wako na ukaishi vizuri tu,,..Huoni kama hilo linaweza kuwa ni faraja kwako katika kile UNACHOKIFANYA sasahivi, kiwe ni kinakidhi au hakikidhi?, pengine umekata tamaa ya maisha kwa namna moja au nyingine na kuona kama vile Mungu haoni unayopitia, lakini nataka nikumbie kama ndege hawamwongezei chochote na analo jukumu la kuwalisha, wewe hupaswi kuwa na hofu hata kidogo..Kwasababu wewe ni mara nyingi sana zaidi ya wao.

Mfano mwingine ni huu..
Mathayo 6:30 “Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?”.
Nilipokuwa ninautafakari sana huu mstari na kujiuliza ni wapi maua yanamzidi Sulemani kwa kuvikwa vizuri, nikagundua japo kuwa hayajisumbukii kwa chochote yapo pale pale, lakini kumbe rangi za maua huwa hazifubai, lakini mavazi ya Sulemani yalikuwa yanachakaa na kila siku anahitaji yabadilishwe apewe mapya.
Japo Sulemani alikuwa anaoga kila siku lakini aliishia kutoa jasho lakini maua hayana historia ya kuoga lakini yanatoa harufu nzuri miilini mwao, ambazo ndio hizo wanadamu hutumia kujinakshi miili yao na majumba yao na kutengenezea marhamu mbali mbali…Kwa Hapo Sulemani ameachwa mbali sana na maua ya kondoni.

Lakini nataka nikuambie, hata wewe utajiri wako, au mali zako, au UMASKINI wako hauwezi kumsaidia Mungu, kukupendezesha au kukufanya mpya zaidi na kuvutia.. Fahamu tu ukipenda kudumu katika kuutafuta ufalme wake basi, lile Neno “Je! hatazidi sana kuwavika ninyi enyi wa imani haba” litakuwa ni la kwako, iwe ni katika uchache au katika wingi..

Mfano mwingine tena ni huu…
Mathayo 7:11 “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”.
Watoto wetu wakituomba, tuchukulie mfano baiskeli tutafanya juu chini kwenda kuwanunulia…hata kama hakitakuja kwa wakati husika lakini kwa jinsi wanavyoendelea kusumbua tutafanya juu chini tuwanunulie tu hata kwa kukopa au kujichanga…

Sasa kama wewe unaelewa hali ya mwanao, kwanini yeye Mungu wetu wa mbinguni asielewe yako?, mpaka unapaniki na kuogopa na kukosa raha ya maisha kama vile yeye sikio lake ni zito, yupo mbali hakuoni wala hakusikii.. Nataka nikuambie huna haja ya kufunga na kuomba juu ya hilo, Mungu yupo “very sensitive, more than any living creature on Earth or Heaven”..Anao upeo mpana wa kufikiri na kuhisi mambo kuliko wewe unavyodhani, anaweza kuhisi tatizo lako ni lipi kabla hata halijaingia akilini mwako. Biblia inalithibitisha hilo.
Mathayo 6: 7 “Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.
8 Basi msifanane na hao; MAANA BABA YENU ANAJUA MNAYOHITAJI KABLA NINYI HAMJAMWOMBA”.
Unaona?, Anajua hata unalokwenda kumwomba wiki ijayo,,, ashindweje kujua taabu au shida unayopitia sasa hivi, anajua unaumwa na unateseka katika magonjwa na unahitaji kupona, analijua hilo, anafahamu una haja na kuwa na maisha mazuri anajua, anajua unahitaji kuolewa na umri umeshakwenda, anajua unahitaji pesa avae nguo nzuri upendeze, anajua unahitaji uishi katika nyumba yako mwenyewe uwe na uhuru wako binafsi, anajua kwasasa ungependa uwe na usafiri wako,,..anafahamu hayo yote…Lakini unajiulize unakuwaje sasa?

Sasa sikiliza hekima zake zinavyomalizia na kusema..
Mathayo 6:31 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
33 BALI UTAFUTENI KWANZA UFALME WAKE, NA HAKI YAKE; NA HAYO YOTE MTAZIDISHIWA.
34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake”.
Anasema Utafute kwanza ufalme wake…rafiki, tamani kumjua kwanza Mungu maishani mwako, tamani kufahamu hukumu zake na mapenzi yake kwako,..Weka mambo yako ya wokovu wako sawa sasa, uwe unahukika kwamba hata leo ukifa Mbingu ni yako, uwe na uhakika kwanza hata unyakuo ukipita leo usiku wewe utakuwa wa kwanza kuisikia sauti ya Bwana Yesu ikikuita mawinguni…Na kesha hayo mengine mwachie yeye atamalizana nayo.. NA HAYO YOTE MTAZIDISHIWA.

Fahamu kuwa Mungu anazo akili timamu zaidi ya unavyofikiri.

Ubarikiwe sana.

2 comments: