"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, May 1, 2019

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI, AU KUTOA TALAKA?Shalom Mwana wa Mungu, karibu tuyatafakari maandiko na kujifunza.

Leo kwa Neema za Bwana tutajifunza, ni kwanini Mungu aruhusu katika agano la kale wana wa Israeli waoe mke zaidi ya mmoja. Huu umekuwa ni mjadala mkubwa sana, usio na mwisho miongoni mwa wakristo wengi wasio na ufunuo kamili wa Roho Mtakatifu kuhusu maandiko hayo.

Kwanza kabisa ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hajawahi kumwagiza mtu yoyote mahali popote aoe mke zaidi ya mmoja. Hakuna mahali popote Mungu alishawahi kumpa Mwanadamu hayo maagizo…utaniuliza mbona kwenye kumbu 21:15 na kumbu 25:5 inazungumzia habari ya mtu kuwa na mke zaidi ya mmoja?. Ni kweli habari hizo zinazungumzia kuhusu kuwa na mke zaidi ya mmoja, lakini hiyo bado haimfanyi Mungu kuhalalisha mke zaidi ya mmoja..Nitakuthibitishia hilo leo kwa maandiko.

kulielewa vizuri hili suala, hebu tusome maandiko yafuatayo na kisha tuyatafakari..

Kumbukumbu 17: 14 “Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako ukaimiliki, na kukaa humo; nawe utakaposema, Nitaweka mfalme juu yangu mfano wa mataifa yote yaliyo kando-kando yangu;
15 usiache kumweka yule atakayechaguliwa na Bwana, Mungu wako, awe mfalme juu yako; umweke mmoja katika ndugu zako awe mfalme juu yako; usimtawaze mgeni juu yako, ambaye si ndugu yako.
16 Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri, ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa Bwana amewaambia, Tangu sasa msirudie tena njia ile.
17 Wala asijizidishie wake, ili moyo wake usikengeuke; wala asifanye fedha zake na dhahabu kuwa nyingi mno.
18 Tena na iwe, zamani aketipo juu ya kiti cha ufalme wake, ajiandikie nakala ya torati hii katika chuo, kufuata hicho kilicho mbele ya makuhani Walawi;
19 na awe nayo, asome humo siku zote atakazoishi; ili apate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wake, ayashike maneno yote ya torati hii na amri hizi, kwa kuyafanya;
20 moyo wake usije ukainuliwa juu ya ndugu zake, wala asikengeuke katika maagizo, kwa mkono wa kuume wala wa kushoto; ili apate kuzifanya siku zake kuwa nyingi katika ufalme wake, yeye na wanawe, katikati ya Israeli”.

Sasa ukisoma mistari hiyo kwa makini, utaona kuwa Bwana anawapa maagizo wana wa Israeli jinsi mfalme wao anavyopaswa awe siku watakapokuja kumchagua…utaona Mungu anawaambia, mfalme huyo anapaswa asiwe mtu wa kujiongezea mali nyingi wala asiwe wa kujiongezea wake..

Sasa kwa maagizo hayo haimaanishi kuwa Mungu, tayari ndio kawapa amri ya wao kuja kuwa na Mfalme, haikuwa mpango wa Mungu kabisa wana wa Israeli waje kuwa na Mfalme, kwani mfalme wao ni mmoja tu yaani YEHOVA, lakini kwasababu Mungu aliona Mbele kwamba watakuja kukengeuka na kutaka kuwa na mfalme kama mataifa mengine walivyokuwa nao ndio hapo akamwambia Musa awape maagizo ya mfalme atakavyopaswa kuja kuwa..Kwahiyo kile kitendo chao cha kuwa na tamaa ya kutaka mfalme ilikuwa ni dhambi kubwa sana, na Mungu hakupendezwa nacho. Tunasoma hayo katika…

1 Samweli 8: 4 “Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;
5 wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; BASI, TUFANYIE MFALME ATUAMUE, MFANO WA MATAIFA YOTE.
6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana.
7 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; KWA MAANA HAWAKUKUKATAA WEWE, BALI WAMENIKATAA MIMI, ILI NISIWE MFALME JUU YAO.
8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe”.

Umeona hapo kitu Mungu anachomwambia Nabii samweli?…
“hawakukukataa wewe bali wamenikataa mimi nisiwe mfalme juu yao”….Sasa ingekuwa Mungu amehalalisha wana wa Israeli kuwa na Mfalme kule kwenye nyuma kwenye Kumbukumbu la Torati 17 …asingekasirika hapa kuona wana wa Israeli wanataka mfalme…asingelaumu, lakini badala yake unaona Mungu anachukizwa sana na kitendo hicho cha wana wa Israeli kutaka mfalme.

Umeona? Kwahiyo ni wazi kuwa kule kwenye kumbukumbu 17, Mungu alipotoa maagizo ya namna mfalme atakavyopaswa kuwa sio kwamba ndio alitoa ruhusa wana wa Israeli wawe na mfalme, badala yake ni maagizo yatakayotumika baada ya wao kukengeuka akili na kutaka mfalme..(Kwasababu ya mioyo yao kuwa migumu)

Kadhalika na katika suala la ndoa. Mungu alitoa maagizo katika agano la kale namna watakavyoishi endapo watajiongezea wake…lakini sio kwamba alitoa amri ya watu kuoa mke zaidi ya mmoja! Au kutoa talaka…Mungu hakuwahi kumwagiza mtu kufanya hivyo vitu, wala kumpa hayo maagizo…alizungumzia namna ya kuishi na mke zaidi ya mmoja ndio, na maagizo ya talaka kwasababu aliona tayari wana wa Israeli walishakengeuka na watazidi kuja kukengeuka na kuweka mioyo yao migumu na kuwa na shingo ngumu, kwa kutaka kila mtu kuwa na mke zaidi ya mmoja, na kila mtu kutaka kumwacha mkewe….na kwasababu walishamkataa Mungu katika fahamu Mungu naye akawaacha wafuate akili zao…Kama vile tu walivyomkataa Mungu asiwatawale na kujichagulia mfalme wao wenyewe, Mungu aliwaacha katika akili zao hizo. Lakini haukuwa mpango kamili wa Mungu tangu awali.
ndio maana Bwana Yesu alikuja kusema mambo hayo hayakuwa hivyo tangu mwanzo.…

Mathayo 19: 3 “Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?
4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,
5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?
6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
7 Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
8 Akawaambia, Musa, KWA SABABU YA UGUMU WA MIOYO YENU, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi”.

Kwahiyo kwa maandiko hayo yanatufundisha kuwa mke ni mmoja tu na mume ni mmoja tu! Na hairuhusiwi kumwacha mwanamke, kwasababu yoyote ile isipokuwa ya uasherati tu!..Mtu anayeoa wake wengi na bado anajiita ni mkristo, azini, asitumie kisingizio cha kuwa agano la kale liliruhusu, YESU ni mkuu kuliko nabii yoyote maandiko yanasema kuwa “katika yeye utimilifu wote wa Mungu unakaa kwa jinsi ya kimwili (Wakolosai 2:9)”.

2 Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.”

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine..

No comments:

Post a Comment