"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, May 10, 2019

MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.


1 Timotheo 4 :1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;”

Mwanzoni nilipokuwa ninausoma huu mstari nilidhani kuwa itafikia kipindi watu wataucha ukristo na kugeukia imani nyingine,labda uislamu au kama sio hivyo basi watageuka na kuwa wapagani moja kwa moja, lakini nilipokuja kuuchunguza tena kwa makini Bwana akanipa kujua kuwa kumbe sio hivyo, badala yake ni kwamba watu wataendelea kubakia katika Ukristo lakini kumbe Imani zao siku nyingi tayari zilishabadilishwa na kuwa kitu kingine,..

Ni sawa na wanafunzi waliosajiliwa shuleni Tanzania lakini mwalimu wao anawafundisha sylabus ya Kenya, unaona haijalishi wataelimika kiasi gani, haijalishi watafahamu mambo mengi kiasi gani, siku ikifa ya mtihani wa mwisho wa taifa wanafunzi wale wote wanauwezekano mkubwa wa kufeli, kwani watakutana na mambo ambayo hawajawahi kufundishwa. Na mwisho wa siku itageuka na kuwa hasara kwao na sio hasara ya mwalimu.

Na ndivyo ilivyo katika siku hizi za mwisho, Biblia inasema wengine watajitenga na Imani, hii ikiwa na maana kuwa watakosa shabaha ya Imani halisi ya kikristo, wakidhani kuwa wapo katika njia sahihi kumbe walishapotea au walishapotezwa siku nyingi. Wameifuata Imani feki isiyotambulika mbinguni.

Ndugu jambo hili sio la kulichukulia juu juu tu, naomba usome mpaka mwisho inawezekana na wewe ulichukuliwa katika wimbi hilo pasipo kujijua, kwani shetani ni mjanja sana, usijione unafahamu kila kitu, wala tusijione kuwa tunafahamu mambo yote, tunakuwa na kujifunza kila siku.

Leo tutaona mambo mawili makuu yatakayopelekea wewe kujitenga na Imani ya kweli mwenyewe. Sasa tukirudi kwenye huo mstari hapo juu, tunaona unasema.. Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, WAKISIKILIZA ROHO ZIDANGANYAZO, na MAFUNDISHO YA MASHETANI;
 
Umeona sababu zenyewe hapo?, kitakachowasababishia kujitenga na Imani kwanza, ni kusikiliza roho zidanganyazo, na pili ni Kusikiliza mafundisho ya mashetani.

1) KUSIKILIZA ROHO ZIDANGANYAZO: Hizi roho zidanganyazo ni zipi,? biblia imeweka wazi kama tukindelea kusoma vifungu vinavyofuata tutapata picha yote ilivyo…Na roho hizi pia zimetajwa kugawanyika katika mafungu makuu mawili, moja ni Kuzuiwa kuoa, na pili ni kulazimishwa ujiepushe na vyakula…Tusome.

Timotheo 4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; 
2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;
3 wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli”.
4 Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani;
5 kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba”.
Angalia maneno hayo ndugu ukishaona unafika mahali unaambiwa ili ukubaliwe na Mungu au ili uwe mtumishi wa Mungu, ni lazima usioe kama Mtume Paulo alivyokuwa vinginevyo haustahili kuwa askofu, au mchungaji au mtumishi wa kanisa, basi fahamu kuwa hizo ni roho zidanganyazo na zinakutenga na Imani halisi inayotajwa kwenye biblia ya mitume..

Hali kadhalika ukiona, umefika mahali unaanza kuambiwa chakula hichi ule au hichi usile, hiki ni najisi hakifai, ukila hichi ni dhambi, kama vile wafanyanvyo baadhi ya dini kama sabato, Ndugu fahamu kuwa upo katikati ya roho zidanganyazo, zitakazokupeleka mbali na Imani, Ni kwanini hayo mambo ni mabaya?...Ni kwasababu yanakutoa katika kuhesabiwa haki kwa Imani na kukuleta katika kuhesabiwa haki kwa vitu vya mwilini kama vyakula, na kuutiisha mwili kwa nguvu.. …Haihitaji ufunuo kuelewa hilo, na ndio maana hapo juu biblia inasema Roho ananewa wazi wazi, unaona ni mambo yaliyowazi kabisa,

Jitenge nazo haraka sana, kwasababu zilishatabiriwa katika siku za mwisho hizo ndizo zitakazowaongoza watu waikose mbingu, watu watakuwa wanakazana kuangalia namna ya kula kama ndio kitu kinachompendeza Mungu, na wanasahau mambo muhimu ya Imani kama upendo, utakatifu, amani n.k
Wakolosai 2:20 “Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani,
21 Msishike, msionje, msiguse;
22 (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu?
23 Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili”.
2) MAFUNDISHO YA MASHETANI: Haya mafundisho ya mashetani ni yapi?, Biblia nayo imeendelea kuweka wazi katika vifungu vinavyofuata..

(4:7 Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa..)

Unaona biblia inazitaja hadithi za kizee, ambazo hizo hata hazina vimelea vya dini ndani yake, haya ndio mafundisho ya mashetani yaliyobuniwa kuzimu ili kuwafanya watu wasiliamini tena Neno la Mungu hata kidogo na uweza ulio katika Kristo Yesu badala yake kuhamishia imani zao katika vitu visivyo na uhai. Na hapa ndipo wakristo wengi walipokamatiwa hususani wa makanisa ya kiroho,.Hizi zinaitwa hadithi za kizee, ni hadithi ambazo zimetungwa lakini zinahusishwa na imani, kwamfano utafika mahali unafundishwa usipande mti Fulani nyumbani kwako, unasababisha baba wa nyumba kufa, unasababisha mikosi kwenye nyumba, na magombano yasiyoisha, na wewe kama mkristo unakwenda kuung’oa huo mti, wewe hujui kuwa Imani yako imehamishwa kutoka katika kweli ya Mungu na kuamia katika ibada za sanamu, mambo ambayo hayana tofauti na yale yanayofanywa na waganga wa kienyeji.

Utakuta mwingine anakuambia, lipande ua hili au mti huu au fuga mnyama ndani ni viumbe rafiki vinaleta Baraka katika nyumba na kuondoa mikosi, na wewe kama mkristo unamsikiliza mtu huyo ambaye anajiita ni mtumishi wa Mungu bila kuhakiki jambo hilo linatoka wapi katika maandiko wewe unakwenda kufanya hivyo, hujuwi unamtia Mungu wivu kiasi gani unasahau kuwa Baraka za Mungu zinatoka katika chemchemi ya maji ya Uzima ndaniYesu Kristo peke yake,..unasahau kuwa utakatifu ndio nyenzo ya kuishi maisha ya amani hapa duniani lakini wewe unakwenda kutafuta njia mbadala kutoka katika viumbe na mimea, na mchanga, na vyakula, unasikiliza hadithi za kizee sizizo na dini, unajitenga na Imani ya Kristo Yesu wewe mwenyewe bila ya wewe kujijua, unamtia Mungu wivu kwa mambo hayo yasiyotokana na Imani ya Kristo Yesu.

Kaka/ndugu, Hizi ni siku za mwisho Roho amekwisha kunena wazi wazi tena leo hii bila kutuficha, Biblia Inaposema wengi watajitenga na Imani, haimaanishi watahama ukristo na kugeukia dini nyingine, hapana watabaki huku huku lakini kumbe siku nyingi walishahamishwa..Na ndio lengo la shetani hilo…Kudanganya, siku zote kudanganya..Maana ya kudanganya ni kudhani umeambiwa/unafanya kweli kumbe ni uongo.

Na ndio maana Paulo kwa uweza wa Roho alimsisitiza sana Timotheo kwenye vifungu hivyo vya maandiko na kumwambia.

4:6 “Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na MZOEVU WA MANENO YA IMANI, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata..”

Unaona, kama mtumishi wa Mungu alionywa kuwakumbusha watu mambo hayo na kufanya vile naye atakuwa “mzoefu wa maneno ya Imani”, hii ikiwa na maana kuwa asipokuwa makini kama mahubiri atakengeuka na kufundisha maneno mengine ambayo sio ya Imani.

Nasi tunakukumbusha leo hii na kukwambia, ONDOKA! Mahali unapozuiwa kuwa mchungaji kisa umeoa mke, kama kanisa Katoliki lifanyavyo, Vile vile mahali ambapo pia wanakuzuia kuwa mhudumu wa Kristo kisa hujaona, ondoka hilo eneo kwasababu katika maandiko hakuna mahali popote pameagiza hivyo.

Ondoka, mahali ambapo unaambiwa ili Mungu akukubali au ili uwe kwenye njia sahihi ni lazima usile kitu Fulani, ni lazima, ushishe siku Fulani, ya jumamosi au jumapili, ni lazima ushike sabato, wanasisitiza mambo ya mwilini tu siku zote lakini Utakatifu wa ROHONI haugusiwi ondoka haraka eneo hilo kabla tatizo hilo halijawa donda ndugu kwako lisiloweza kupona tena, usije ukabakia kuwa mfuasi wa dini kushindana na kulumbana na watu kila mahali kama walivyokuwa wanafanya mafasayo na waandishi. Na uthibitisho wa roho hii, huwe inawapeleka watu kwenye malumbano na mashindano ya dini, ambayo biblia imetuonya tukae mbali nayo.

Ondoka pia mahali ambapo wanapenda njia mbadala za kutatua matatizo yako kwa kutegemea vitu vingine nje ya Neno la Mungu na uweza wa damu ya Yesu Kristo. Unaambiwa suluhisho la matatizo yako ni maji Fulani yaliyoombewa, au mafuta, au chumvi au udongo, na huambiwi kwasababu hapana tofauti na kwa mganga wa kienyeji, kwasababu huwezi kwenda kwa mganga wa kienyeji hata siku moja ukakemewa tabia yako, yeye ukifika pale atakupa dawa ya matatizo yako kwa njia nyingine anayoijua yeye, lakini sio kwa kukutathmini tabia yako, hata siku moja hawezi kukwambia wewe ndio mbaya, atakwambia mtu Fulani ambaye ni adui yako ndio mbaya, kwahiyo hata kama wewe ndio mwenye makosa atakupa dawa ya kumshambulia Yule asiye na kosa, vivyo hiyo na mahali popote unapofika ambapo unatabiriwa tu kupigwa kwa maadui zako lakini hujawahi kuambiwa kuwa ile tabia yako ya uasherati ndio adui mkubwa wa maisha yako, ondoka hilo eneo kwa usalama wa maisha yako. Unafika tu na kuambiwa nunua maji haya yaliyoombewa baada ya siku kadhaa matatizo yako yote yataondoka..Ujue hizo ni hadithi za kizee za kujitenga nazo.

Hivyo Kwa kuzingatia vipengele hivyo vikubwa viwili basi utakuwa umenusuruka pakubwa na undanganyifu ulipo duniani katika siku hizi za mwisho.

Ni jukumu la Kila mkristo kuilinda Imani yake na kuishindania, biblia inatuagiza hivyo.

Yuda 1:3 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba MWISHINDANIE IMANI WALIYOKABIDHIWA WATAKATIFU MARA MOJA TU.

Ikiwa wewe ni mmoja wa waliokombolewa na Yesu basi Nikutakia heri na mafanikio yote katika safari yako njema ya kwenda mbinguni. Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share’ ujumbe huu kwa wengine.

No comments:

Post a Comment