"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, May 10, 2019

SWALI LA KUJIULIZA!

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe! Karibu tujifunze Biblia. Leo kwa Neema za Bwana tutajifunza juu ya “swali kuu la kujiuliza katika maisha yetu”.

Hebu jaribu kutengeneza picha labda kuna mtu, kakukamata halafu kakufunga macho na kisha akakusafirisha na kukupeleka labda tuseme nchi ya India, na ulipofika pale hakukwambia kama upo India, badala yake akakutelekeza kwenye moja ya mitaa ya India na kukimbia, na baadaye ulipofanikiwa kufungua kile kitambaa mbele yako ukaona mazingira ambayo hujawahi kuyaona, mitaa ambayo ni mipya kwako, watu ambao huwajui, lugha inayozungumzwa ni ngeni kwako, ulipotazama kulia ukaona kuna watu wanacheza mpira kiwanjani, ulipotazama kushoto ukaona kuna mgahawa wa chakula, watu wanakwenda pale kula, ulipotazama nyuma ukaona kuna watu wanakimbilia kupanda gari la usafiri, na pembeni mwa barabara ukaona kuna kama soko Fulani la mboga mboga na matunda na wafanyabiashara wengi, mbele yake kidogo unaona nyumba nzuri za kifahari na bustani nzuri za kumpumzika..

Jiweke katika hiyo nafasi halafu uniambie..ungekuwa ni wewe ungekimbilia kipi cha kwanza?..inawezekana ukasema ningekimbilia kucheza mpira, au kwenye mgahawa wa kula, au sokoni kula matunda. Lakini kama umefikiria mojawapo ya hivyo basi ni wazi kuwa utakuwa umefikiria jambo la kipumbavu la mtu asiyefikiri.

Kwanini ni jambo la kijinga?...Ni kwasababu baada ya kujikuta tu pale, swali la kwanza ambalo ungetakiwa kujiuliza HAPA NI WAPI? Na NI KWANINI NIPO HAPA?..Hilo ndio jambo la kwanza kabisa la kujiuliza kabla ya kufanya jambo lolote au kujiunga na kitu chochote kule..Utajiuliza kwa makini sana HAPA NI WAPI?..Niko wapi hapa?..na baada ya hilo swali kujiuliza litakalofuata ni NI KWANINI NIPO HAPA?.
 
 
Sasa majibu ya maswali haya utayapata kutoka kwenye vyanzo viwili tofauti…Swali la kwanza linalouliza HAPA NI WAPI au NIKO WAPI HAPA…Jibu laek utalipata kwa kwenda kuwauliza watu wanaokuzunguka, labda utaenda pale mgahawani na kumwuliza mtu mmoja na kuwambia “samahani eti hapa ni wapi?”…Pengine Yule mtu anaweza akashangaa kidogo kuulizwa swali kama lile anaweza akafikiri wewe ni kichaa lakini mwisho wa siku atakwambia hapa ni INDIA.

Na baada ya kujua kuwa upo INDIA, swali litakalofuata ni NANI aliyenileta hapa, na ni kwa dhumuni gani yeye kunileta hapa?..sasa jibu la hili swali huwezi kulipata kwa wale watu tena wanaokuzunguka, kwasababu ukienda kuwauliza watakuona umerukwa na akili…Hivyo itakugharimu kufanya uchunguzi wako kumjua aliyekupeleka pale na dhumuni lake, hapo ndipo itakugharimu uchunguzi kidogo Kumtafuta Na kama Yule aliyekuleta atapenda kujidhihirisha kwako, ili kukueleza sababu ya yeye kukuweka pale basi atakupa sababu zote, na dhumuni lake lote, kisha ukishatimiza mapenzi yake, yeye ndiye atakayekuonyesha njia ya kurudi katika nchi uliyotoka. Huo ni mfano tu!.

Sasa katika maisha tunayoishi ndio hivyo hivyo….Sisi wanadamu wote tumezaliwa katika hii dunia, TUMEJIKUTA TU! TUMETOKEA HAPA ULIMWENGUNI. Hatukukaa katika kikao cha makubaliano na yeye aliyetuleta hapa ulimwenguni. Tumejikuta tu! Tupo tayari ulimwenguni ni kama tumetekwa mateka na kuletwa mahali tusipopajua. Na wote tulipozaliwa tayari tumekuta kuna mambo yanaendelea duniani, tumekuta kuna michezo, kuna burudani, kuna shughuli hizi na zile, kuna kumbi za starehe na mambo mengi, kuna fursa nyingi kila mahali…Lakini swala ni lile lile litakuwa ni jambo la kipumbavu kujiunga na hayo mambo kabla ya kujiuliza baadhi ya maswali..KWAMBA MIMI NI NANI? NIMETOKA WAPI? NIPO WAPI? NA NI NANI ALIYENILETA HAPA? NA KWA DHUMUNI GANI?...Hayo ndiyo maswali ya kwanza ya muhimu ya kujiuliza ya mtu mwenye akili kabla ya kujiunga na taasisi yoyote ile, kabla ya kujiunga na chuo Fulani, kabla ya kujiunga na biashara Fulani, kabla ya kuanza kupanga mipango fulani ya maisha…hayo ndio maswali ya msingi ya kujiuliza.

Na baadhi ya majibu ya hayo maswali unaweza kuyapata kwa wanadamu wenzako lakini kuna ambayo huwezi kuyapata kutoka kwa wanadamu, kwamfano ukienda kumwuliza mtu hapa ni wapi? Atakuona mwendawazimu lakini mwisho wa siku atakupa jibu hapa ni duniani, na atakupa mpaka historia ya dunia ilipotokea n.k.

Na swali la kwamba ni nani aliyekuleta hapa duniani, unaweza ukajibiwa tu kirahisi kuwa ni MUNGU..Lakini dhumuni la yeye kukuleta hapa ni lipi? Hakuna atakayekujibu!..hapo itakugharimu wewe utafute, hakuna mtu anayeweza kukupa jibu la dhumuni la Mungu kukuleta hapa duniani?..Kwasababu kila mtu anakusudi lake la kutimiza hapa duniani tofauti na mwingine.

Sasa utajuaje kusudi la aliyekuleta hapa duniani (Yaani kusudi la Mungu)..juu yako?

1) Kwanza Ni lazima umpate huyo aliyekuleta duniani, na namna ya kumpata huyo ni kwa kupitia kitu kimoja kinachoitwa MSALABA..Kwa kupitia YESU KRISTO, Hakuna namna nyingine yoyote utakayoweza kumjua Mungu nje ya huyu YESU KRISTO, Huo ndio ukweli ndugu yangu, na huyu unampata tu kwa kumwamini na kwa kutubu dhambi zako na kumgeukia yeye kikweli kweli, na kwa kubatizwa na kwa kupokea Roho Mtakatifu. Hapo utakuwa umempata huyu aliyekuleta ulimwenguni.
2) Baada ya kumpata kwa kubatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, sasa moja kwa moja ataanza kuongea na wewe na kukuongoza katika lile kusudi alilokuitia duniani, hajakuleta hapa duniani bure bure tu! Wala hajakuleta hapa ili uwe mfanyabiashara, au uwe maarufu, au uwe milionea, hapana lipo kusudi lingine ambalo ndilo alilokuletea hapa, na hilo kusudi linafanya kazi kwa silaha alizoziweka ndani yako tayari (yaani karama aliyoiweka ndani yako), kwa kupitia huyu Roho wake Mtakatifu atakufunulia hilo kusudi, na ukishalijua hilo kusudi ndipo amani ya ajabu ya kuishi duniani itakujia, kwasababu umeshajua dhumuni la wewe kuletwa duniani. Na kusudi hilo ndilo litakalokufanya uishi kama mpitaji tu katika hii dunia, ukijua kuwa hapa duniani, sio kwako, ni kama umetekwa tu na umeletwa ili utimize kusudi Fulani, na huku ukijua kabisa aliyekuleta sio mjinga kwamba akulete humu duniani na kisha ashindwe kukuhudumia mahitaji yako ya mwilini, kwahiyo utakuwa unaishi kwa bajeti ya aliyekuleta, sio bajeti yako wewe, huku ukiangalia na kulitazama kusudi lake. Na lolote utakalolifanya ndani yake utafanikiwa.
Ndugu unayesoma ujumbe huu, swali ni lile lile? UNAJUA UPO WAPI?...UNAJUA SABABU YA WEWE KUWEPO HAPA?...Ni jambo la kuhuzunisha kama unaishi katika hii dunia na unafanya anasa, unaendelea na shughuli zako za kiuchumi…lakini hujui sababu ya wewe kuishi duniani, ni sawa na Yule mtu aliyetweka na kufumbuliwa macho na pasipo hekima yoyote akaanza kukimbilia mgahawani kula chakula, pasipo hata kujiuliza yupo wapi…Hivyo ndiyo unavyoonekana mbele za Muumba wako wewe usiyetaka kuyatafakari msingi wa maisha yako?..unaonekana mpumbavu mbele zake kwa kutokutambua kusudi lako na uwepo wake na wako..wewe na mtu asiyeamini kuwa Mungu yupo hamna tofauti.

Zaburi 14: 1 “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu….”;

Kama leo hii umeamua kufumbua macho yako na kutafuta kujua kusudi la Mungu juu ya maisha yako, hatua ni nyepesi za kufuata, ndio hizo hapo juu…kwanza tubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kutokuzitenda tena, kusudia moyoni kuacha uasherati, uzinzi, utazamaji wa pornography, masturbation, usengenyaji, ulevi, uvutaji wa sigara, rushwa,utoaji mimba, ulawiti,wizi, utukanaji na mengineyo..kisha ukishadhamiria kuacha hayo mambo…hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa, kumbuka ubatizo sahihi ni wa muhimu sana na ni wa kuzamishwa mwili wote katika maji tele na kwa JINA LA YESU KRISTO, Ubatizo wa udogoni sio sahihi kulingana na maandiko, kama ulibatizwa hivyo, hukufanya dhambi kwasababu ulikuwa hujui, ulifanyiwa pasipo kujua lakini sasa umejua ukweli,nenda kabatizwe tena upya kwa Imani, kwasababu ni maagizo ya Bwana YESU mwenyewe. Kulingana na Matendo 2:38. Na baada ya kumaliza hatua hizo muhimu..Nguvu ya Ajabu ya Roho Mtakatifu itaingia ndani yako, hiyo itakuongoza katika kuijua kweli yote ya biblia na kukufunulia kusudi la Mungu juu ya maisha yako, na jinsi ya kulitimiza hilo kusudi hatua kwa hatua..Na huyo huyo Roho atakusaidia kulitimiliza mpaka mwisho wa siku zako.

Wafilipi 1: 6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu”;

Anza leo kazi njema, Timiza kusudi la aliyekuleta hapa ulimwenguni, na siku ile upokee Taji ya Uzima.

Bwana akubariki sana.Tafadhali “share” na wengine ujumbe huu.

(www wingulamashahidi org)

No comments:

Post a Comment