"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, May 31, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 64


SWALI: Je! Mbinguni Kutakuwa na kula na kunywa?.
JIBU: Biblia haijaeleza kwa mapana na marefu mambo yatakayokuwa yanaendelea mbinguni baada ya unyakuo kupita, na ndio maana mtume Paulo anasema katika 1Wakorintho 13:9 “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;..” Hivyo kuhusu kama watakatifu watakula au hawatakula na kunywa biblia haijatoa jibu la moja kwa moja lakini tunaweza kutazama baadhi ya mistari inaweza kutusaidia kupata picha fulani.

Tukisoma:
Marko 14.23 “Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.
24 Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.
25 Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.
26 Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni”.

Tunaona katika habari hiyo hapo, Yesu akiwaagiza mitume wake kwa habari ya kunywa katika ufalme wa mbinguni, Lakini pia tukimtazama Bwana baada ya kufufuka kwake alikuwa na mwili wa umilele wa utukufu usioweza kufa tena, wala kuugua, mwili ambao uliweza kufanya mambo makubwa zaidi yasiyoweza kufanywa na mwili wowote wa asili, ule mwili uliweza kupotea na kutokea mahali popote, uliweza kuchukua sura tofauti tofauti, uliweza kupaa, na mpaka sasa unaishi n.k. Na kumbuka pia biblia inatuambia “siku atakapodhihirishwa tutafanana naye (1Yohana 3:2)”..Sasa jambo ambalo utaliona pale alipowatokea mitume wake baada ya kufufuka kwake aliwaambia wampe chakula chochote ale.

Luka 24.41 “Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula cho chote hapa? 42 Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.43 Akakitwaa, akala mbele yao”.

Hiyo inatupa picha kwa sehemu jinsi miili hii ya utukufu itakavyokuwa, haitakuwa na mipaka Fulani kwamba kwasababu ni ya umilele haitaweza kula wala kunywa. Ni kweli kabisa uzima wa hiyo miili hautakuwa tena katika vyakula, inaweza kuendelea kuishi bila ya njaa wala chakula wala kutegemea chochote kile,kwasababu asili yake ni ya kimbinguni lakini hiyo haimaanishi kuwa haitaweza kunywa wala kula.

Pia kumbuka Adamu kwa asili kabla ya kuasi alikuwa mtu wa umilele, asiyeweza kufa, wala kuugua, wala kuzeeka, lakini pamoja na ukamilifu wake Mungu bado alimuumbia ndani yake kula na kunywa katika ile bustani ya Edeni.

Hivyo tusubiri tuone, tukifika huko tutajua zaidi, kikubwa tu tunachopaswa kufanya sasahivi ni kujitahidi kuishi maisha ya ushindi yampendezayo Mungu ili siku ile itakapofika tusikose kuyaonja hayo mambo mazuri Mungu aliyotuandalia ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.

Ubarikiwe.


SWALI: Bwana Yesu asifiwe watu wa MUNGU naomba kuuliza kuchora tattoo ni dhambi?

JIBU: Biblia inasema katika kitabu cha Mambo ya Walawi 19: 28 “Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala MSIANDIKE ALAMA MIILINI MWENU; mimi ndimi Bwana”.

Bwana alikataza watu kuchanjwa chale kwasababu chale zote zinahusiana na ibada za wafu, au ushirikina, Bwana hajawahi kuwaagiza wana wa Israeli wanapopatwa na matatizo fulani au wanapohitaji kinga ya jambo Fulani wachanjwe chale..Hizo zilikuwa ni ibada za kipagani ambazo tunaona hapa Bwana anawaagiza wana wa Israeli wasizifuate hizo desturi…Bwana aliwaagiza kuwa tiba ya magonjwa yao ni kuzishika sheria zake basi na sio kwenda kujichanja mwilini.

Lakini pia aliwaagiza wasiandike alama zozote katika miili yao (tattoo). Sasa wengi hawajui asili ya tattoo…watu wa zamani walikuwa hawachori tattoo kwa lengo la urembo kama sasahivi, watu wa zamani walikuwa wanachora tattoo kwenye miili yao kwa lengo hilo hilo kama la kuchanja chale, (kwa lengo la ibada) ilikuwa ni ibada za miungu, na walikuwa wanafanya hivyo kufuata maagizo ya miungu yao kuwa wanapotaka wapate jambo Fulani, au wajikinge na hatari Fulani, ni lazima wachore alama hizo katika miili yao..

Hivyo zinaweza kuwa ni michoro ya aina Fulani ya wanyama kama vile nyoka, ndege, au wakati mwingine majina Fulani ya lugha zisizoeleweka, au alama za jua, au mwezi n.k. Na kwasababu shetani ndiye aliyekuwa nyuma ya mambo hayo basi kila aliyefanya hivyo alikuwa ananufaika kwa sehemu Fulani kwa masuala ya kishetani..ni kama tu mtu aliyechanjwa chale au anayetembea na hirizi leo, anakuwa anatembea na pepo Fulani linalomkinga dhidi ya mambo Fulani yanayohusiana na anachokiamini.

Lakini miaka ilipokwenda mbele watu waliwaona watu wanaojichora tattoo kuwa wanapendeza, hivyo pasipo kuchunguza asili la lile jambo ni ipi nao pia wakaenda kuiga mioyoni mwao wakidhani kuwa wanaweka urembo tu kwenye miili yao kumbe wanaweka uchawi na mapepo kwenye miili yao pasipo wao kujijua..wanajiongezea roho Fulani za yule adui katika maisha yao.

Kwahiyo mwili wowote wenye tattoo tayari una pepo fulani ndani yake, kwasababu asili ya tattoo au chale sio urembo bali kinga Fulani za kichawi..Na Biblia imetuonya kuwa miili yetu inapaswa iwe hekalu la Roho Mtakatifu.

1 Wakorintho 6: 19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;
20 maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu”.

Kumbuka hapo biblia haijasema miili yetu sisi tuliomwamini Bwana YESU kuwa ni NYUMBA YA KAWAIDA, bali ni HEKALU, hekalu ni tofauti na nyumba za kawaida, kuna nyumba za aina nyingi, zipo za kulala wageni(guest house), nyumba za kuhifandhia mizigo, nyumba za kiofisi nk lakini HEKALU ni nyumba maalumu kwa ajili ya Ibada tu!!..sasa nyumba yenye chale au yenye tattoo itakuwaje hekalu la Mungu,?..Unaona? kwahiyo kuchora tattoo ya aina yoyote ile sio sahihi.

Kama ulijichora tattoo huko zamani, au ulichanjwa chale udogoni na sasa umempa Bwana maisha yako hiyo ni vizuri sana, ile roho nyuma ya hiyo tattoo imeondoka lakini shetani bado atakuwa na visababu vichache vichache vya kukushitaki mbele za Mungu, hivyo chukua uamuzi wa kwenda kuvifuta hivyo vitu ili shetani asipate sababu yoyote ya kukushitaki..na pia mwili wako usitumike kuitangaza kazi za shetani, kwasababu usipofuta ni sawa na kampuni fulani la matangazo..

Hivyo futa tattoo zote mwilini mwako, uuwekwe mwili wako wakfu kwa Mungu sasa ili autumie..

Ubarikiwe.


SWALI: Naomba kuuliza, Je! Ni dhambi kuvaa suruali za kubana (model), kunyoa mitindo (mfano kiduku), kwa kijana wa kiume aliye okoka..?

JIBU: Kumbuka mavazi tangu zamani licha tu ya kuwa na matumizi ya kujisitiri yalitumika pia kueleza hali ya mtu rohoni jinsi ilivyo. Kwamfano kwenye biblia utaona kulikuwa na mavazi ya kifalme (2Nyakati 18:9, Esta 6:8), Ni mavazi yaliyoweza kumtofautisha mfalme na watu wengine wa kawaida.Kulikuwa na nguo za magunia, tunalithibitisha hilo sehemu nyingi katika biblia, mtu akionekana amevaa mavazi ya magunia iliashiria kuwa yupo katika majonzi na maombolezo makubwa ya rohoni, pengine kwa kufiwa au kuomba toba mbele za Mungu …Pia biblia inataja kuwa kuna mavazi ya kikahaba, (Mwanzo 38:14 ) ukisoma Mithali 7:10 inasema “Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo;…mtu yeyote aliyekuwa ameonekana ameyavaa hayo”

Kulikuwa na mavazi ya kikuhani pia ambayo yakivaliwa, yanamjulisha Yule ni Kuhani nk. yote hayo mtu alipokuwa akivaa yalikuwa yaashiria kitu Fulani rohoni.Vivyo hivyo hata sasa, mavazi yanabeba tafsiri Fulani ya mtu rohoni.

Kama binti wa kike anatembea barabarani kava kimini, au suruali, au top, au nguo nyepesi inayoonyesha maungo yake ya ndani, huyo tayari ni kahaba, kwasababu mavazi hayo yanavaliwa na wale makahaba wa KASINO na DISCO, ndio kitambulisho chao kule., mfano leo hii ukikutana na gari linye kibao juu kimeandikwa TAXI, huhitaji mpaka lisimame na kuliuliza kama kweli ni TAXI, moja kwa moja tokea likuwa kule mbali utalipunga mkono, lisimame kisha utapanda, kwani kibao chenyewe kinajieleza juu kwa gari lile ni la umma, halidhadhalika ukimwona binti anatembea na nguo hizo hauhitaji kumthibitisha kama yeye ni kahaba tayari mbinguni na duniani anaonekana kama ni kahaba.

Sasa kwa kijana wa kiume, suruali za milegezo, suruali za kubana (zinazojulikana kama utumbo wa kuku), hizo zinajulikana ni za wasanii wa kidunia na wanamtindo wa ulimwengu huu ambao hata habari na Mungu hawana…Lengo lao kubwa ni kuitangaza miili yao na mitindo yao.. Sasa Jiulize wewe kijana wa kikristo unayesema umeokoka unavaa milegezo,na suruali za kubana n.k. mbinguni na ulimwenguni unadhani unaonekanaje?, wewe na wanamuziki wa ulimwengu huu ni kitu kimoja hata kama utakana, ndivyo ulivyo..Halidhadhalika unanyoa viduku, na kusuka, na kufuga rasta mtu akipita barabarani akakuita kama mmoja wapo wa wasanii wa ulimwengu wanaofanya hivyo au akikuita Bob Marley mvuta bangi utakwazika?.

Biblia inasema. Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.
2 Wala msiifuatishe NAMNA YA DUNIA HII; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu”. 
Hilo neno hapo juu NAMNA YA DUNIA HII, linamana ya FASHION. Kabla haujafikiria kuvaa suruali ya kubana, embu mvishe kwanza Yesu, kabla hujafikiria kunyoa kiduku mnyoe kwanza Yesu, ukiona hizo nguo hawezi hata kuzitazama mara mbili , inakupasaje wewe kama hayo mambo hayamstahili Mungu, wewe unayavaa ya nini?. Hivyo ni DHAMBI kwako..

Ubarikiwe.
www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment