Tukisoma biblia kwa utulivu tutagundua kuwa maandiko yamegawanyika katika sehemu kuu tatu, sehemu ya kwanza ni maandiko ambayo yamefunuliwa moja kwa moja kwa wakati wote, na ya pili ni maandiko ambayo yalikuwa yamefungwa lakini yakaja kufunguliwa baadaye. Na sehemu ya Tatu ni maandiko ambayo yalionekena tu kwa sehemu lakini yakaja kufungwa tena.
Ni vizuri tukalielewa hilo ili tusiichukulie biblia kirahisi rahisi tu au kama kitabu kingine chochote cha kawaida ambacho hakina habari mpya ndani yake.
Sasa Maandiko yaliyofunguliwa moja kwa moja kwa wakati wote ndio yapi?, ndio haya ambayo kwa sehemu kubwa mimi na wewe tunayafahamu, ni maandiko ambayo yapo wazi,yalinakiliwa katika vitabu mtu yeyote anaweza akasoma na kwa kupitia hayo akamwomba Mungu na Mungu akamfunulia hekima iliyopo ndani yake, kwamfano unaposema vitabu vya Torati vyote, unaposoma vitabu vya wafalme, Ayubu,Esta,Zaburi, Yeremia, Isaya, Ezekieli, unaposoma vitabu vya Injili ya Yesu Kristo na Injili ya Mitume, n.k. vyote hivyo ni vitabu vilivyofunuliwa kwetu kwa wakati wote havina masharti Fulani au makomeo au mipaka. Yaani kwa lugha rahisi ni vitabu vinavyotufaa kwa wakati wote, kufundishia, kuonya na kufariji, kujenga n.k..sawasawa wakolosai 3:16
Lakini pia kuna aina nyingine ya maandiko ambayo hayo yalikuwepo tangu zamani, yalikuwa yamefungwa mpaka ulipofika wakati Fulani wa kufunuliwa..Na mfano wa haya tunaona ni kile kitabu cha Mihuri 7 katika kitabu cha Ufunuo mlango wa 6 ambacho kilikuwa kimetiwa muhuri ndani na nje, siri zilizokuwa ndani yake, hazikuwahi kujulikana na mtu yeyote mpaka wakati wa kufunuliwa kwake ulipofika, na tunasoma ni Yesu peke yake ndiye aliyestahili kuivunja mihuri ya kile kitabu na kwa kupitia ufunuo ule mkubwa ndipo tulipofahamu sisi ni akina nani, ndipo tulipofahamu tulipotoka na tunapokwenda, ndipo tulipofahamu mwenenendo wa yule mpinga-kristo, Yule Asi, jinsi atakavyoanza mpaka atakapomaliza na mahali kiti chake cha enzi kilipo, atakapotokea na atakapoishi. Mambo hayo hayakujulikana hapo kabla..Isipokuwa kwa wakati husika..
Vile vile yapo maandiko mengine ambayo, yaliyoonekana kwa sehemu tu na baadhi ya watu lakini yalifungwa mpaka wakati husika uliowekwa Na ndio maana utasoma Danieli aliambiwa..
Danieli 12:3 “Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.
4 Lakini wewe, Ee Danieli, YAFUNGE MANENO HAYA, UKAKITIE MUHURI KITABU, HATA WAKATI WA MWISHO; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka”.
Sasa tunaona watu hawa walipotaka kuyarekodi katika biblia walikatazwa wakaambiwa wasiyaandike kwanza, kwani hayo yametengwa mahususi kwa wakati Fulani wa mwisho. Ndugu nataka nikuambie, Mungu anayo Agenda yake kama vile ibilisi alivyo na Agenda yake, Sio kila siri ya ufalme wa mbinguni imerekodiwa katika kitabu hichi cha biblia, mambo mengine Mungu karuhusu makusudi yafichwe kwasasa, ili shetani asielewe chochote Mungu alichokipanga, Embu fikiria maneno yale Bwana Yesu aliyoyasema, msitupe Lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua.. Ikiwa Mungu ameruhusu sio kila jambo la ufalme wa mbinguni tutalifichua kwa kila mtu tu, kwanini na yeye asitenge fungu lake kwa ajili ya familia yake tu?.
NGURUMO SABA ZIPO MBIONI KUTOA SAUTI ZAO.
Tunaona Yohana alipokuwa Patmo, alionyeshwa maono mengi sana na Bwana Yesu Kristo, na mengi ya hayo aliambiwa ayaandike, ikiwemo ufunuo wa yale makanisa 7 na jumbe zao, ikiwemo baragumu saba, na vitasa saba, Lakini alipofika kwa Yule malaika mwenye nguvu sana aliyeshika kile kitabu kidogo, alipolia na ngurumo saba kutoa sauti zake alipotaka kuandika, alikatazwa asiandike. .Tunasoma hayo katika Ufunuo mlango wa kumi:
Ufunuo 10: 1 “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.2 Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wakushoto juu ya nchi.3 Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. NA ALIPOLIA, ZILE NGURUMO SABA ZIKATOA SAUTI ZAO.4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, YATIE MUHURI MANENO HAYO YALIYONENWA NA HIZO NGURUMO SABA, USIYAANDIKE”.
Ni mambo nyeti sana na ya kutisha vile vile, kwasababu siku zote ngurumo mara nyingi kwenye biblia inaashiria hukumu ya Mungu, sasa hizi ngurumo 7 (ambazo ni Huduma 7/watu 7) zitapoanza kutoa sauti zao, kwa kupitia maubiri hayo ambayo yatasikika ulimwenguni kote, Nguvu ya Mungu itashuka kwa namna ya ajabu juu ya watu wengi wanaume kwa wanawake waliochaguliwa…. ndugu yangu, masikio ya wengi yatawasha, kwasababu mambo yatakayosikiwa yatakuwa ni mpya yatakayoambatana na hukumu na mapigo. Wanaoichezea madhabahu ya Mungu sasahivi na wakiona hakuna chochote kinachotokea siku hiyo ndio watayapojiona kuwa wao kumbe walikuwa ni takataka mbele za Mungu, watajihukumu wenyewe kabla hata ya kufika kwa Mungu, wao wenyewe watakiri kuwa hawakuwa watumishi wa Mungu kwa jinsi mambo yatakayokuwa yanasemwa na hiyo nguvu ya uamsho wa ajabu itakayokuwa inatembea katikati ya Kristo na Bibi-arusi wake duniani.
Zekaria 13:3 “Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la Bwana; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii.4 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; WALA HAWATAVAA JOHO YA NYWELE ILI KUDANGANYA WATU;5 bali atasema, MIMI SI NABII KAMWE; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nalifanywa mtumwa tokea ujana wangu”.
Huu ni unabii Zekaria aliopewa wa kipindi hicho kinachokuja, kutakuwa na utiisho mkubwa katika kanisa la Mungu ambao haujawahi kuwepo, zaidi hata ule wa Petro alipokutana na Anania na Safira, walipoanguka na kufa baada ya kumwambia uongo Roho Mtakatifu, utakuwa ni mkubwa kuliko huo.
Kutakuwa na ishara na miujiza ya ajabu ambayo haijawahi kurekodiwa katika historia yoyote ya kanisa, Mungu atafanya mambo ambayo kila jicho litashangaa, na Mungu atafanya hivyo kumpa Bibi-Arusi wake imani ya kunyakuliwa, hapo ndipo sehemu ya pili ya ule unabii wa Yoeli wa mambo yatakayotokea siku za mwisho utatimia.
Matendo 2:19 “Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi20 Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri21 Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa”.
Hayo yote yatatimia katika wakati huo, na hiyo itafanyika ndani ya kipindi kifupi sana, na ghafla utanyakuo utapita.
Dunia itabakia imeduwaa ikijiuliza ni nini hiki.. Na ndio maana mambo hayo yalihifadhiwa yasijulikane kwanza, na pia kumbuka kutatamkwa mambo mapya kabisa ambayo hutaweza kuyapata katika biblia,lakini hiyo haimaanishi kuwa yatapingana na Biblia hapana, bali yatakuwa mapya na sio wote watakayo yapokea isipokuwa wale wanawali werevu tu, ambao Mungu mwenyewe atawapa hekima ya kuyapokea. Huo ndio wakati Danieli aliosema Maarifa yataongeza, watu wote wa Mungu wataongezewa maarifa ya kumjua Mungu kwa kiwango cha ajabu.
Mjumbe wa Kanisa hili la mwisho la Laodikia WILLIAM BRANHAM, ambaye Mungu alimtumia kwa ishara nyingi na miujiza mingi Mungu naye pia alionyeshwa maono ya siku hizo zitapofika, kumbuka hapo kabla Bwana alimpa Maono mengi sana yaliyokuja kutokea yakathibitishwa kimataifa, mojawapo ndio lile la vita kuu vya pili vya dunia alionyeshwa jinsi Hitler atakavyonyanyuka na kuipeleka dunia katika vita na mpaka mwisho wake utakavyo kuwa wa kutokueleweka, aliliandika hilo (akamtaja mpaka jina) likisubiriwa litokee, na likaja kutokea vilevile,..na mengine mengi ukitaka kujifunza masomo yake utaniambia inbox niwe nakutumia.
Alionyeshwa kwa sehemu uamsho huo utakavyoja kuwa akasema alitamane na yeye awe mmojawapo wa uamsho huo kwa jinsi alivyoona miujiza ya ajabu iliyokuwa inafanyika. Halikadhalika na wahubiri wengi wengi maarufu walithibitishiwa juu ya hilo na Mungu mwenyewe.
Hivyo ndugu, ikiwa bado haupo ndani ya wokovu, unasubiria nini wakati huu wa neema sasa?. Kumbuka Jambo hilo litakapotokea halitamuhusu kila mtu duniani bali watu ambao tayari walishaanza kutembea na Mungu tayari huko nyuma, watu waliopokea ubatizo wa Roho Mtakatifu,Watu wanaotambua majira wanayoishi, Wengine wote hawataelewa chochote wala hawatasaidiki kwasababu Yule ROHO anayewavuta watu kumwamini yeye atakuwa hayupo ndani yao.
Ukiyajua haya, ufanye uteule wako imara sasa, tubu anza kutembea na Mungu katika muda huu mfupi uliobaki, kabla ya siku za hatari hazijaanza. Kwani kwa jinsi mambo yanavyoonekana tusitazamie sana vizazi vingine mbele yetu, hichi kizazi tunachoishi mimi na wewe kinaweza kushuhudia hayo yote.
Ubarikiwe.
No comments:
Post a Comment