"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, June 1, 2019

CHANZO CHA MAMBO.


Jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio taa iongozayo njia zetu. Biblia inasema “Mjue sana Mungu ili uwe na Amani (Ayubu 22:21)”..Siku zote ukijua sababu ya jambo Fulani basi unapata amani. Amani inakuja baada ya kujua sababu ya jambo Fulani.
Leo tutajifunza juu ya vyanzo vya matatizo, na namna ya kuyatatua. Kama tunavyojua wengi wetu vyanzo vya matatizo mengi ni shetani..huo ni ukweli usiopingika. Lakini je! Shetani analetaje matatizo?.

Tukijifunza Mfano wa Ayubu, tunaweza kupata majibu baadhi, tunaona shetani alimshambulia Ayubu baada ya kupata kibali maalumu kutoka kwa Mungu, hiyo ikifunua kwamba shetani hawezi kumgusa mtu yeyote wa Mungu pasipo ruhusa yeyote kwa Mungu..

Hivyo Mungu anaporuhusu mtu ajaribiwe…anachokifanya ni kutoa ulinzi wake juu ya Yule mtu, na akishatoa ulinzi wake maana yake shetani anapata nafasi ya kumwingia. Hivyo anamshambulia.
Na shetani huwa ana njia kuu mbili za kuwashambulia watu.

1) Anatumia mapepo…Katika njia hii mtu atajikuta tu ameingia matatizoni pasipo kujua chanzo ni nini. Kumbe ni majeshi ya mapepo wabaya yamemvamia.

2) Na njia ya pili anatumia watu..(Na watu atakaowatumia ni aidha watumishi wake wa uongo wanaovaa mavazi ya kondoo lakini ndani ni mbwa-mwitu wakali…au atatumia wachawi na waganga)….atatumia watumishi wa uongo kuwajaribu wale wanaomjua Mungu, na atatumia wachawi na waganga kuwajaribu wale wasiomjua Mungu…au wakati mwingine atatumia vyote viwili kuwajaribu wale watu wanaomjua Mungu.

Sasa tukirudi kwenye mfano wa Ayubu..baada ya ulinzi wa kiMungu kuondoka juu yake…shetani alimletea majaribu wengi… Kama haikuwa ni kazi ya mapepo moja kwa moja basi kuna uwezekano mkubwa sana shetani alitumia watu Fulani kumfanyia Ayubu yale mambo…Alichofanya shetani baada ya kuona ukingo wa kiMungu umeondoka juu ya Ayubu ni pengine aliwatupia roho ya wivu watu baadhi waliokuwa wanamzunguka…na ile roho ilipowaingia pengine ikawasukuma kumwendea hata kwa waganga… labda walikwenda kwa mganga fulani maarufu kwa kipindi hicho mwenye nguvu, wakaenda na picha yake na za watoto wake..na nyayo zake labda..Na wakiwa kule wakaona wanafanikiwa kumwona kwenye kioo chao cha kichawi, na pengine huyo mganga akafanya mambo yake na kutuma kimbunga cha kichawi juu ya watoto wake wakiwa karamuni, na kwasababu ulinzi wa kiMungu umeondoka juu ya Ayubu jambo lile likafanikiwa na Kuwaua watoto wake wote. Na magonjwa ni hivyo hivyo ni kikundi Fulani cha maadui zake Ayubu kilihusika kumletea yale magonjwa.

Sasa labda baada ya tukio hilo pengine Ayubu aliona tabia Fulani za watu wanaomzunguka kufurahi..na pengine walisema vimaneno Fulani kuonyesha kuwa wao ndio walifanya vile. Sasa kwa jicho la haraka haraka kama Ayubu angekuwa sio mtu wa rohoni…angesema maadui zake wamemfanyia visa..Lakini Bwana alimpa jicho la Mbali kujua mwanzo wa Matatizo yake hayakuwa ni wale watu..bali alijua yalikuwa ni Mungu mwenyewe…kutoa ulinzi juu yake. Ndio maana aliishia kusema “Bwana alitoa na Bwana alitwaa, jina lake libarikiwe”…Alijua maisha yake ni makamilifu isipokuwa ni Mungu tu katoa ulinzi juu yake kwa makusudi Fulani. Angalia jinsi alivyouamini uhusiano wake na Mungu, kiasi cha kwamba hakuweza kuyumbishwa ni kitu chochote, na sisi je! tunaweza tukawa hivyo?.
Na mambo hayo hayo yanaendelea leo hii, watu wanatumiwa na shetani kukuharibu, pengine ni wachawi au waganga…na kushindwa kuelewa chanzo cha mambo yote ni nini?...chanzo cha mambo yote sio watu kukuonea wivu, au wachawi kukuchukia hapana!..chanzo cha matatizo yote ni Ulinzi wa kiMungu kuondoka juu yako..Usianze kupambana na watu wanaokuchukia, anza kutafuta mzizi wa tatizo ni wapi..kama Ayubu.

Ayubu alijua chanzo cha matatizo yake, kuwa ni Bwana ndiye kayaruhusu hayo lakini njia zake ni kamilifu…alijua sio dhambi ndani yake iliyosababisha ulinzi wa kiMungu uondoke juu yake.
Kadhalika na sasa tunapaswa tujitathmini, kama kuna jambo Fulani limetokea ambalo halipo sawa…chanzo chake ni nini?..Je! ni kama Ayubu? (Njia zetu ni kamilifu isipokuwa ni Bwana anatujaribu tu) au ni kwasababu ya dhambi zetu, kwasababu kitu pekee kinachotoa ulinzi wa kiMungu juu ya mtu ni dhambi…

Ukiwa mwasherati magonjwa yatakusumbua na wachawi watakusumbua sana, mapepo yatakusumbua sana hakuna namna utaweza kuwashinda, hata uombewe kiasi gani hakuna namna utaweza kuchomoka mikononi mwao…ukiwa mtazamaji wa pornography na mfanyaji wa masturbation ni hivyo hivyo…ukiwa ni mzinzi, ni shoga ni msagaji ni hivyo hivyo, watakusumbua na hakuna namna utaweza kuwashinda…Usidanganywe kuwa kuna mchungaji yeyote duniani mwenye uwezo wa kukuombea wachawi au mapepo yasikufikie wala kukudhuru, wala usidanganyike kuwa kuna maji yoyote au mafuta yoyote ya upako yanayowazuia wachawi wasiweze kufika nyumbani kwako…Usidanganyike kabisa ndugu…

Kitu pekee kinachoweza kufukuza na kuzishinda nguvu za giza juu ya maisha yako ni MAISHA YA UTAKATIFU katika Kristo Yesu, Uhusiano wako na Mungu ni wa kiwango gani, hicho tu! Wala hakuna kingine….Maisha unayoishi ndio yanayoamua ulinzi wa kiMungu uwe juu yako au uondoke.

Fanya uamuzi sahihi leo, usitazame wachawi, wala waganga, kama ndio chanzo cha matatizo yako…wala usiende kutafuta suluhisho kwa kuombewa, wala kupakwa mafuta..Suluhisho lipo kwako ambalo ndio chanzo cha mambo yote…suluhisho ni KUBADILIKA na kuishi maisha ya utakatifu, ambayo hayo yanakuja kwa kutubu kwanza dhambi zako zote, na kudhamiria kuziacha kabisa kuanzia sasa na kuendelea na kwenda kubatizwa na kisha kupokea Kipawa cha Roho Mtakatifu ambaye atakusaidia kushinda dhambi.

Ukifanya hivyo, ulinzi wa kiMungu utakuwa juu yako, haihitaji wewe kwenda kuombewa wala kupakwa mafuta, wala kuwaogopa wachawi…Utaishi kwa Amani sana, na wala hakuna chochote kitakachokugusa. Kwasababu nguvu iliyopo ndani yako ni kubwa kuliko ya kwao..Bwana Yesu alisema..
  
Luka 6.17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio;...... watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa;..."

Bwana akubariki sana. 

No comments:

Post a Comment