"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, June 1, 2019

WATAMTAZAMA YEYE AMBAYE WALIMCHOMA;

Jina Bwana wetuYesu libarikiwe. Ni siku nyingine tena Bwana ametupa neema kuiona hivyo nakukaribisha ndugu popote pale ulipo tushiriki pamoja Baraka Bwana alizotuandalia leo.

Tukisoma Zekaria 12:9-14, inasema. 
9 Hata itakuwa siku hiyo, ya kwamba nitatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu. 
10 Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.
11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.
12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;
13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.
14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao”.
Watu wanaozungumziwa hapo ni wayahudi (yaani Waisraeli) , Embu leo jiulize tu Israeli ni Taifa dogo sana kama mkoa wa njombe, ni taifa ambalo huwezi hata ukaenda na kukutana na vitu vya kuvutia huko au vya kushangaza kama mataifa mengine makubwa, lakini ni kwanini leo hii imekuwa ni JICHO LA DUNIA?. Wapo mbali na Mungu lakini ni watu wenye akili na wenye mafanikio makubwa duniani, jiulize siku wakiwa karibu na Mungu itakuwaje?
Hayo maandiko hapo juu ni lazima yatime, utafika wakati biblia inasema Roho ya neema itaachiliwa juu yao na watamwamini huyu Yesu ambaye sasa hawamwamini, Siku hiyo Watalia na kuomboleza baada ya kugundua makosa yao kuwa Yule waliyemsulibisha na KUMCHOMA MKUKI miaka 2000 iliyopita kumbe ndiye Masiya waliokuwa wanamsubiria kwa miaka mingi..Ile roho ya ufarisayo na usadukayo itaondoka juu yao.

Kama vile biblia inavyotabiri kutakuwa na maombolezo makubwa sana huko Yerusalemu wakitubu makosa yao.

Sasa hicho ndio kile kipindi ambacho mtume Paulo alikiandika katika
 Warumi 11:25 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili [anasema na sisi watu wa mataifa]; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.
26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.
27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao”.
Unaona hapo unabii huo utatimia katika hiyo siku?, Huo wakati wa Israeli kurudiwa na kutengwa na maovu yao upo karibuni sana, na utakapoanza tu basi ujue utimilifu wetu sisi mataifa utakuwa umeshawasili yaani kwa lugha nyingine neema kwetu itakuwa imeshaondoka na kurudi tena Israeli, na hiyo itaambatana na tendo KUU la UNYAKUO.

Sasa wayahudi ambao leo hii utawaona wanalia usiku na mchana pale kwenye ule Ukuta wa maombolezo (wailing wall). wakimwomba Mungu wa Ibrahimu baba yao aje kuwaokoa na maadui zao na kuleta utawala wa masihi duniani, ipo siku hayo maombolezo yatakoma, na ndipo Mungu atawarudia kwa kuwafumbua macho na kumwona YESU, Kumbuka Mungu aliwapofusha kwa makusudi kabisa wasimwamini Kristo ili sisi mataifa tuipate neema vinginevyo huyu Yesu wa thamani ambaye leo hii tunaifurahia neema yake, tungemsikilizia tu kwa wayahudi, sisi tungeendelea kuwa waabudu miti,vinyago, na wachawi. Na hata hivyo dunia ungekuta imeshakwisha siku nyingi, wakati ule ule tu Yesu aliokuwa ndio ungepaswa uwe ni wakati wa wao kurejeshewa ufalme wa dunia na Yesu.

Unakumbuka mitume walimuuliza Yesu baada ya kufufuka je! Huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme? Yesu akawaambia, sio kazi yenu kujua nyakati wala majira.(Matendo 1:6), Hii ikiwa na maana kuna wakati utafika watarudishiwa na huyu huyu masihi Yesu Kristo.

Hivyo huo wakati unafika, Pale Mungu atakaposimama tena upande wa Israeli na kuwashindania kwa nguvu nyingi kama alivyokuwa anafanya zamani, pale mataifa yote ulimwenguni yatakapoungana ili yaje kujaribu kuisambaratisha Israeli katika ile vita ya Harmagedoni ndipo hapo Kristo atakawapigania toka juu kwa nguvu na uweza mwingi…damu nyingi itamwagika sana, maadui wote wa Israeli watakufa kama kuku waliochinjwa wakaachwa, wakati huo Bwana atakapolipigania Taifa lake…. Tunalisoma hilo katika..
Zekaria 14:1 “Tazama, siku moja ya Bwana inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako.
2 Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali.
3 Hapo ndipo ATAKAPOTOKEA BWANA, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita.
4 Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.
5 Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku zaUzia, mfalme wa Yuda; na Bwana, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye.
Kwahiyo tusifurahie tu kuona leo hii Israeli inazidi kufanikiwa lakini badala yake tuogope na tujiulize maswali je! Wewe tumejiandaaje sasa?, neema ndio hivyo inaondoka kwetu, tazama hata hali ya ukristo sasa hivi duniani sio kama ile ya zamani, tazama mataifa ya ulaya ambayo ndio yalikuwa ya kwanza kutuleta injili lakini sasa jinsi yanavyozidi kujitenga na ukristo kwa kasi, hiyo ni dalili kuwa neema inaondoka kwa mataifa, inakimbilia Israeli..Itafika wakati mataifa yote yataenda kinyume na taifa teule la Mungu hata hili taifa letu vilevile litaungana na yule mpinga-Kristo ili kuiangamiza Israeli.
Zekaria 12: 3 “Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake”.
Ndugu wakati huo sio wa kuutamani kwanini tusubirie mpaka hayo yote yatukute kwa ghafla wakati tunayo nafasi sasa? Neema inamalizikia AFRIKA, usiiche ikupite, chukua hatua ya kumwamini Yesu ayasafishe maisha yako, ili uwe tayari kwa unyakuo ulio karibuni kutokea.

Bwana akubariki.
www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment