Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo
libarikiwe…Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Ufunuo, ambapo leo
tutaitazama ile sura ya 16, ya kitabu hichi, Ni vizuri kama hujapita sura za
nyuma ungeanza kwanza kuzipita hizo ili uweke msingi mzuri wa kuzielewa sura zinazofuata.
Katika sura hii ya 16, habari kuu
tunayoina ni juu ya vitasa 7, “Vitasa ni VIBAKULI kwa lugha ya sasa”..Na hasira
ya Mungu sehemu nyingine imefananishwa na mfano wa kimiminika fulani kinachojaa
katika chombo, ambacho kwa jinsi hasira ya Mungu inavyozidi kuongezeka juu ya
mtu au watu ndivyo kimiminika kile kinavyozidi kujaa ndani ya hicho kikombe au
kibakuli…Na kikiisha kujaa kukaribia kumiminika, ndipo mtu au watu wanapewa
wakinywe..na kunywa kunaashiria “kuipokea ghadhabu ya hasira ya Mungu (yaani
kuadhibiwa)”.
Ndio maana ukisoma kwenye biblia
wakati wana wa Israeli walipomkosa Mungu hata Mungu akadhamiria kuwapeleka
Babeli, Nabii Yeremia alipewa maono ya kuwanywesha wana wa Yuda kikombe cha
ghadhabu ya Mungu…Na wakati ulipofika wa Neno hilo kutimia Mfalme wa Babeli
alishuka juu yao akawachinja chinja wanawake na watoto, na wale waliosalia akawachukua mpaka Babeli
utumwani..Na utaona kikombe hicho cha ghadhabu ya Mungu hawakunywesha tu wana
wa Yuda bali mataifa mengi duniani pia walinyweshwa.
Yeremia 25: 15 “Maana Bwana, Mungu wa Israeli, aniambia hivi, Pokea kikombe cha divai ya ghadhabu hii mkononi mwangu, ukawanyweshe mataifa yote, ambao nitakupeleka kwao;
16 nao watakunywa, na kulewalewa, na kufanya wazimu, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yao.
17 Ndipo nikakipokea kikombe kile mkononi mwa Bwana, nikawanywesha mataifa yote, ambao Bwana alinipeleka kwao;
18 yaani, Yerusalemu, na miji ya Yuda, na wafalme wake, na wakuu wake, ili kuwafanya kuwa ukiwa, na ajabu, na mazomeo, na laana; vile vile kama ilivyo leo;
19 Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote;
20 na watu wote waliochanganyika pamoja, na wafalme wote wa nchi ya Uzi, na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, na Ashkeloni, na Gaza, na Ekroni, na mabaki ya Ashdodi;
21 Edomu, na Moabu, na wana wa Amoni;
22 na wafalme wote wa Tiro, na wafalme wote wa Sidoni, na wafalme wote wa kisiwa kilicho ng'ambo ya pili ya bahari; 23 Dedani, na Tema, na Buzi, na watu wote wakatao denge;”
Na pia tutakuja kumwona jinsi Yule mwanamke(Babeli
mkuu,Mama wa makahaba) akipewa kikombe hiki cha ghadhabu ya Mungu katika ufu.
16:19.
Lakini katika sura hii, tunaona
Malaika saba wakiwa na VIBAKULI saba. Hivi sasa ni vibakuli vya ghadhabu ya
Mungu juu ya dunia nzima sio tena juu ya mataifa Fulani baadhi au watu Fulani
wachache, ghadhabu ya Mungu juu ya watu wachache haihitaji kibakuli, kikombe tu
kingeweza kutosha..lakni hapa ni maovu ya dunia nzima..Maovu ya wanadamu ndio
yamevijaza vibakuli hivyo..Kimoja baada ya kingine kimejaa..Bwana hakukiweka
kimoja kwa sababu yeye ni wa rehema bali aliviweka saba ingekuwa ni kimoja
tayari siku nyingi sana tungeshaangamizwa kwasababu kingekuwa
kimeshajaa..lakini wanadamu wamevijaza vyote saba…Na hivyo vitakwenda kumiminwa
juu ya dunia nzima, kumbuka hawatanyweshwa watu bali watamiminiwa..hiyo ni
hatari sana.
➹➹Lakini kabla ya kuviangalia hivi
vitasa kuna vitu vichache vya utangulizi vya kufahamu..
Hii neema tulionayo leo itafika
mwisho, kuna baadhi ya misemo imekuwa ikisemwa kuwa Mungu wa agano la kale leo
hii hayupo, kama yupo zile ishara alizokuwa anatenda agano la kale ziko wapi
leo?. Lakini SIKU YA BWANA inakuja ndugu usitamani uwepo! USITAMANI UWEPO! ni
mambo ya kuogopesha ambayo usingetamani hata adui yako yampate, Mungu kuzuia
ghadhabu yake ni kwa ajili yetu sisi ili tutubu lakini tusipotubu hukumu
itatukuta wakati tusioutazamia.
Kuna vitu vitatu vya kutisha ambavyo
vipo mbele yetu sasa,
1) DHIKI KUU,
2) SIKU YA BWANA,
3) ZIWA LA MOTO.
Leo tutaitazama hii SIKU YA BWANA ni ipi,
itakuja lini na itakuwa inamuhusu nani.
Kwa ufupi ndugu, DHIKI KUU itakuja
na tunafahamu itakuwa kwa wakristo watakaokataa kuipokea ile alama/chapa ya
mnyama. Hii itamuhusu mpinga-kristo akiwatesa wakristo wale waliokataa kuipokea
ile chapa ya mnyama, Ambapo mwishoni mpinga-kristo atafanikiwa kuwaua kikatili
wote wasioipokea chapa. Na hii dhiki itadumu kwa muda wa miaka mitatu na nusu,
ni wakati wa kutisha sana unakuja mbeleni. Kwahiyo wakati wakristo wachache
wanapitia dhiki kuu, wengine wote waliosalia watakuwa wanaendelea kujifurahisha
na mambo yao ya dunia wakimfurahia mpinga kristo na utawala wake.
Sasa SIKU YA BWANA itaanza mara tu baada
ya DHIKI KUU kuisha ambapo watakatifu wote wakati huo watakuwa
wameshaondoka,(wameuliwa na mpingakristo) na unyakuo utakuwa umeshapita wakati
huo, lakini hao waliobakia walioipokea chapa ya mnyama itawapasa waingie kwenye
adhabu kali sana ya Mungu mwenyewe, Kwasababu wameshirikiana na mpinga kristo
kuwaua watu wa Mungu na kwasababu wamekataa kumcha Mungu na kuzishika amri
zake, ndugu Hii SIKU YA BWANA usitamani uwepo. Kumbuka haitakuwa jehanamu ya
moto, bali itakuwa ni adhabu ya hapa hapa duniani.
maandiko yanasema:
Amosi 5:18 "Ole wenu! Ninyi mnaoitamani SIKU YA BWANA; kwani kuitamani siku ya Bwana? Ni giza, wala si nuru. 19 Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. 20 Je! Siku ya Bwana haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.
Pia tukisoma...
Isaya 13:6" Pigeni kelele za hofu; maana SIKU YA BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu.
7 Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka.
8 Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto.
9 Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.
10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.
11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;
12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri."
Maandiko yanaposema SIKU YA BWANA
hayamanishi ni siku kama siku moja, bali inamaanisha ni kipindi fulani cha
WAKATI ambacho Bwana amekitenga kwa kusudi fulani. Kama maandiko yanavyotueleza
ni kipindi ambacho kimetengwa cha GHADHABU NA HASIRA ya Mungu kulipiza kisasi
kwa wanadamu wote wasiomcha Mungu. Kipindi Hichi cha SIKU YA BWANA kitadumu kwa
muda wa siku 75, Hizi zimepatikana kutoka katika kitabu cha Nabii Danieli
12:12, ambapo tunaona kipindi cha ile dhiki kuu kitadumu kwa muda wa siku 1260(sawa
na miaka 3 na nusu), na hapo zimeongezeka siku nyingine kutoka siku 1260 mpaka
kufikia siku 1335, kwahiyo ukichukua hizo siku 1335-1260=75. Kwahiyo hizi siku
75 zilizoongezwa ni mahususi kwa ajili ya BWANA kujilipizia kisasi kwa wanadamu
wote waliosalia juu ya uso wa nchi.
Kabla ya SIKU hiyo ya BWANA kuanza
Kutakuwa na baragumu saba zitakazopigwa kuitangulia , Hizi Zitabeba hukumu kwa
watu wote, kama onyo watu watubu kumgeukia Mungu, Dunia itapigwa kwa mapigo
mengi ya ajabu ukisoma Ufunuo 8 ikiwemo, theluthi moja ya maji kuwa damu,
theluthi ya maji duniani kutiwa uchungu,theluthi ya mwezi na jua na nyota
kupigwa,hebu tafakari kutakuwaje duniani wakati huo mchana kutakuwa kama jioni,
giza litakuwa nene usiku na baridi kali sana, nzige wa ajabu watapandishwa kutoka
kuzimu, maumivu yao ni kama ya kung'wata na nge, na meno yao ni kama meno ya
simba, n.k. Biblia inasema watu watakitamani kifo lakini hawatakiona, kumbuka
hapo bado SIKU YA BWANA haijaanza huo ni mwanzo wa utungu tu, unatangaza hukumu
KUU ya Bwana inayokuja mbeleni kwa urefu soma ufunuo sura ya 8 na ya 9.
inaelezea haya mapigo ya baragumu saba za Mungu.
Lakini pamoja na mapigo yote hayo ya
baragumu biblia inasema watu watakaokuwa juu ya uso wa nchi hawatatubu maovu
yao kwasababu roho ya uovu imeshakaa juu yao kwa kuwa wote wamekwisha ipokea
ile chapa ya mnyama neema ya Mungu imeondoka juu yao hawawezi kutubu tena.
Kwahiyo mara baada ya dhiki kuu
kuisha wakristo kuuliwa na unyakuo kupita, Sasa Hawa wanadamu waliobaki ndio
watakaoingia katika SIKU YA BWANA inayotisha, ile inayowaka kama moto yenye
vile vitasa saba ambayo ndiyo yale mapigo saba ya mwisho ya Mungu, katika hayo
ghadhabu ya Mungu imetimia : Hebu tutazame vitasa hivi kimoja baada ya kingine.
KITASA CHA KWANZA:
Ufunuo 16:1 " Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.
2 Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na JIPU BAYA, BOVU, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake."
Sasa adhabu hizi zitakuwa ni kwa
Dunia nzima na sio theluthi tena ya dunia kama ilivyokuwa kwa zile baragumu
saba. Majipu haya tunaona ni mfano wa yale yale waliopigwa wamisri, Kutakuwa na
majipu ya ajabu usidhani ni haya ya kuwaida uliyoyazoea, biblia imeyaita ni
MAJIPU MABOVU bado hajatokea kabisa duniani, huo ugonjwa bado haujazuka, Tuna
magonjwa mengi ya hatari duniani lakini biblia haijayataja yote hayo, lakini ni
huu ugonjwa wa MAJIPU tena jipu bovu ndio umetabiriwa utakuja, homa yake
itakuwa sio kama hizi za kawaida tulizozizoea, na utakuwa na vidonda vikubwa
sana, utampata kila mtu aliyekaa juu ya nchi, pamoja na wanyama Ndugu usitamani
kuwepo huko wewe unayesema Mungu wa agano la kale haishi, siku hiyo utayaona
haya wazi wazi.
KITASA CHA PILI:
Ufunuo 16:3 "Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa."
Duniani kutakuwa na harufu kama ya
damu ya mtu aliyekwisha kufa, damu ya mtu aliyekufa ni tofauti na ya aliye hai,
damu ya mtu aliyekufa inakuwa kama mgando Fulani mweusi hivi…ndivyo bahari
itakavyokuwa.. hakutakuwa na kiumbe chochote baharini chakula kitapungua
duniani, maji yataisha, shughuli za usafirishaji baharini vitakwama, mvua
zitaacha kunyesha duniani kutakuwa sio sehemu ya kuishi tena mwanadamu, taabu
itaongezeka duniani, hofu kuu itawaingia watu wakitazama ni mambo gani haya
yameipata dunia?..nini kinaendelea?.. lakini bado mapigo yatakuwa yanaendelea,
KITASA CHA TATU:
Ufunuo 16:4 " Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu.5 Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi;6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.7 Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako".
Baada ya bahari kugeuzwa kuwa damu
ya mizoga, watu wote tunajua wangekimbilia kutafuta maji katika mito na kwenye
chemchemi za maji, kutokana na kiu kali, lakini Bwana atayapiga pia maji ya
mitoni na kwenye chemchemi, wakati huo fedha itakuwa haifanyi kazi tena, Mtu
tajiri atakuwa ni mwenye kikombe cha maji safi mkononi mwake na sio fedha,
Kwahiyo Bwana atawalazimisha kuyanywa hayo maji ya DAMU kwasababu
walishirikiana na yule mnyama kumwaga damu ya watakatifu wa Mungu, hivyo nao
Bwana amewapa wainywe. Na kwasababu ya kiu kali watakunywa hiyo damu, na
wanadamu wengi wataangamia na kufa kwa pigo hilo.
KITASA CHA NNE:
Ufunuo 16:8 "Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.9 Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu."
Baada ya pigo la maji kuwa damu, jua
litashushwa chini, maunguzo yatakuwa ni makubwa sana, joto litaongezeka duniani
kwa nyuzi joto kubwa kuliko kiwango cha kawaida. Mimea yote itakauka ghafla,
dunia itafanana na jangwa ndani ya muda mfupi sana, jaribu kutafakari majipu ya
ajabu yanawapata watu wakati huo huo maji yote damu..na bado jua kali linapiga
na hakuna maji hata kidogo ya kujipooza,ni dhiki kiasi gani? ni mambo ambayo
huwezi dhania yatatokea lakini yapo mbioni kutokea. Lakini pamoja na hayo
mapigo yote biblia inasema watu watamtukana Mungu hawatatubu…watalia kwa
uchungu wa maumivu hayo watasema kama Mungu yupo kwanini anatufanyia hivi…na
kwasababu hawataona majibu yoyote wakati wanateseka watakasirika na kuishia
kumtukana Mungu.. Mfano tu wa kizazi chetu hichi watu wanapopatwa na majanga
badala wageuke na kumuuliza Mungu ni kwanini na kutubu, wao wanalaani na kutoa
maneno ya makufuru.
KITASA CHA TANO:
Ufunuo 16:10 "Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu,11 wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. "
Sasa pigo hili linamuhusu sana sana
yule mnyama aliyewakosesha wanadamu wote kuipokea ile chapa, mahali kiti chake
cha enzi kilipo ambapo ni VATICAN, Roma, Mungu ataachilia laana kwa mataifa ya
ulaya ambayo ndio zile pembe kumi, zitamchukia na kumwangamiza yule mwanamke
kahaba (Kanisa Katoliki) ambalo makao yake makuu ni VATICAN. Hii ni kutokana na
kwamba yale mataifa ambayo yalimtumaini mpinga kristo ayaletee amani duniani,
hayajaletewa zaidi ya yote mpingakristo (PAPA) ameiongezea dunia matatizo hivyo
basi watamchukia na kumwangamiza, tangu wakati huo utawala wa Roma, pamoja na
mpinga kristo (PAPA) na Vatican yake hawatakuwepo tena ufalme wao umekwishatiwa
giza. Wakati huo bado wataona bahari ipo vile vile damu, hakuna maji wala
umande, jua limegeuka kuwa moto, na majipu yanazidi kuwaharibu…wataona hakuna
sababu ya kuwepo na kiongozi mwongo kama asiyekuwa na msaada na mwongo.. hivyo
wakiwa katikati ya huo msiba mkubwa ulioikumba dunia watamgeuka Papa na kumwangamiza.
Soma ufunuo 17:16" Na zile
pembe kumi ulizoziona, na huyo mnyama, hao watamchukia yule kahaba, nao
watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa
moto. "
KITASA CHA SITA:
Ufunuo 16:12 "Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua.
13 Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.
14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.
15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)
Kitasa hichi kunazungumzia ile vita kuu ya HAR MAGEDONI ambayo itakuwa ni vita kati ya Mungu mwenyezi akilipigania taifa la Izraeli dhidi ya wafalme wote wa dunia. karibu kila taifa litaunga mkono vita hii wakiongozwa na mataifa kutoka mawio ya jua. Haya mataifa ya mawio ya jua ni mataifa ya mashariki, nayo ni CHINA,JAPAN, KOREA na machaache baadhi. Wakati huo Vatican itakuwa haipo, Marekani itakuwa haipo, Urusi itakuwa haipo yatatoweshwa katika vita vilivyoelezwa katika Ezekieli 38 & 39, Kwahiyo zile roho chafu ambazo zilikuwa zinaendesha Vatican na Marekani zitahamia kwenye haya mataifa ya mashariki yaliyosalia kwa ajili ya vita dhidi ya Izraeli. Wakati huo ndio Bwana YESU atakapotokea kuwapigania watu wake Izraeli. Ndugu wakati huo dunia itakuwa mfano wa sayari ya Zebaki, hakutakuwa na maji, chakula, magonjwa, joto litakuwa juu sana,maji yote damu, machafuko pamoja na vita, itakuwa ni vilio na kusaga meno, siku hiyo watu watatamani siku hizi za neema tulizonazo leo hawataziona.16 Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni."
KITASA CHA SABA:
Ufunuo 16:17 " Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa.
18 Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.
19 Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake.
20 Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.
21 Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno."
Hili ni pigo la mwisho, na katika
hili ghadhabu ya Mungu imetimia tukisoma pale muhuri wa sita ulipofunguliwa
ulitoa picha halisi jinsi hii siku itakavyokuwa soma Mathayo 24:30-31 na pia
Ufunuo 6:12-17
Ufunuo 6:12-17 " Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu,13 na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi.14 Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake.15 Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,16 wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo.17 Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?"
Pigo la saba la mwisho kama
tunavyosoma ni baya kuliko yote yaliyotangulia maana jua linaondolewa, mwezi
utakuwa damu, nyota zitatoweka, unaweza kuona kutakuwa na giza kiasi gani
duniani, na baridi kiasi gani (wakati huu sasa jua litakuwa limeondolewa),kutakuwaa
ni giza zito sana, hakutakuwa na chanzo chochote cha umeme, wala
nishati…shughuli zote za kimaendeleo zilishamalizwa katika mapigo
yaliyotanguliwa, hadi kufikia hapa watu wachache sana watakuwa wamesalia
duniani, kumbuka hapo bado ziwa la moto linasubiri watu, Hichi ni kisasi tu cha
hapa hapa duniani.
Mvua ya mawe kubwa sana itanyesha,
mawe kama talanta,(Talanta 1 ni kama kg 34), Huwezi kujificha kwenye nyumba
yako ya bati au ya kigae, kg 34 ni uzani mkubwa sana ambayo yatashuka kwa kasi
kubwa sana kutoka juu…itaambana na tetemeko ambalo halijawahi kutokea, kiasi
cha kwamba visiwa vitahama, kisiwa cha zanzibar kitapotea siku hizo, Milima
itatapika volkano, kumbuka hayo yote yatafanyika katikati ya giza nene, hakuna
mawasiliano, kutakuwa hakuna kuonana wala kupigiana simu.. hapo hakuna mfalme
wala mtumwa, raisi wala mwananchi wote waliosalia watatamani wafe kuliko
kuishi, watatamani milima iwaangukie waikwepe ghadhabu ya Mungu, Hapo ndipo
itakapoonekana ishara ya mwana wa Adamu mawinguni.
Soma Mathayo 24:29 "Lakini
mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga
wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;
30 ndipo
itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya
ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu
ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. "
Rafiki haya mambo ni kweli
yatatokea, ndivyo yatakavyokuja kuupata ulimwengu na dalili zote zinaonyesha
kuwa yatatokea katika kizazi chetu tunachoishi mimi na wewe, Bwana amekwisha
kutuonya mbele, Nia yake ni sisi tuiepuke hiyo ghadhabu na ndio maana kuna
mahali alisema alipokuwa katikati ya kitasa cha sita (Tazama, naja kama mwivi.
Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu
yake). Kwahiyo ametuonya tukeshe na kuyatunza mavazi yetu, maana hii siku ya
ghadhabu itakuja ghafla.
Ndugu kimbia injili ambazo
zinakufanya usifikiri hatma ya maisha yako ya milele badala yake inakupeleka
kutazama mambo ya ulimwengu huu tu!. Hii ni roho ya shetani inayowapumbaza
wengi wafikiri mambo hayo yatakuja kutokea baada ya miaka 2,000 mbele,
usidanganyike ni uongo wa shetani, ndugu dalili zote zinaonyesha, unabii wote
umetimia kwamba tunaishi katika kizazi cha hatari sana. Chunguza maisha yako na
maandiko angali neema ipo, mambo hayatakuwa hivi siku zote, pale mlango wa
neema utakapofungwa kutakuwa hakuna kurudi nyuma itakuwa ni vilio na
maombolezo, kimbilia kalvari sasa tubu dhambi zako, uoshwe kwa damu ya Yesu, na
Upokee Roho Mtakatifu kabla ya huo wakati kufika. Kumbuka adhabu ya hii SIKU YA
BWANA, sio jehanamu ya moto, baada ya mapigo hayo ndipo ziwa la moto ziwa la
moto litafuata, wote waliokufa katika hii siku ya Bwana ambao ndio wale wote
walioipokea chapa ya mnyama...baada ya ule utawala wa miaka 1000 watafufuliwa
na kuhukumiwa katika kiti cheupe cha hukumu na kisha watatupwa katika lile ziwa
la moto.
Ikiwa unataka kumpa Bwana Yesu
maisha yako na kugeuka leo tubu mwenyewe moyoni mwako au fuatiliza sala hii kwa
imani:
⏩SEMA: "Bwana Yesu, Leo hii nasogea mbele zako nikiwa mwenye dhambi, natubu makosa yangu yote niliyokukosea, naomba unisamehe, nimeamua kugeuka leo, nisaidie Bwana Yesu, neema yako iwe juu yangu, nikuishie wewe, siku zote za maisha yangu, asante Bwana Yesu kwa kunisikia na kunisamehe. AMEN! ".
Baada ya kutubu na kudhamiria
kutokufanya tena dhambi unahitaji kubatizwa, Hivyo basi tafuta kanisa
linalobatiza ubatizo sahihi nao ni kwa kuzamishwa kwenye maji mengi na ni kwa
jina la YESU KRISTO, Kwa kufanya hivyo Bwana atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu
na utakuwa umekamilisha wokovu wako.
MUNGU AKUBARIKI.
🔜Usikose mwendelezo huu wa kitabu cha Ufunuo..
🔜Usikose mwendelezo huu wa kitabu cha Ufunuo..
No comments:
Post a Comment