"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, June 10, 2019

JIPE MOYO.


Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo, lisifiwe daima. Nakukaribisha tushiriki pamoja Baraka za rohoni. Leo tutaitazama kauli hii moja ambayo Bwana Yesu aliitoa siku ile kwa wanafunzi wake baada ya kuwaagiza mambo yote ya kufanya na kuwaaga, alimalizia na kusema..  

Mathayo 28:20 “….. na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”.
Kauli ni nyepesi kuisikia ni ya faraja kuisikia lakini imebeba tafsiri kubwa sana nyuma yake…Kwa lugha rahisi ni hii kama mbeleni Bwana Yesu asingeona kuwa watahitaji msaada wake asingewaambia maneno hayo, asingeona kama mbeleni kuna shida, asingewaambia maneno hayo, kama asingeona mbeleni kuna milima na mabonde bado asingewaambia kauli hiyo, kwani wangekuwa na uwezo wa wenyewe kutembea katika raha mpaka siku atakapokuja kuwachukua tena.
Lakini aliona kuna vifungo vingi mbeleni vinawasubiria watu wake, na hivyo watahitaji mtu wa kuwatia moyo, aliona kuna magonjwa mengi mbeleni hivyo watahitaji mtu wa kuwaponya, aliona kuna kuchukiwa na kutengwa kwa ajili ya jina lake hivyo watahitaji mtu wa kuwafariji na kuwa nao karibu, aliona kuna wakati watu wake watashindwa kujua jambo la kufanya na hivyo watahitaji mshauri wa karibu, aliona wataonewa na wenye dhambi na hivyo watahitaji mtetezi, aliona watapita katika bonde la uvuli wa mauti hivyo watahitaji mchungaji wa kuwaongoza, aliona kuwa wakati watazungukwa na maadui pande zote hivyo watahitaji mlinzi,..n.k. Yote hayo Bwana aliyaona mbeleni na ndio iliyokuwa sababu ya yeye kuitoa kauli kama ile kwa wanafunzi wake.. “NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE, HATA UKAMILIFU WA DAHARI.” Dahari maana yake ni “nyakati au muda”..kwahiyo hapo Bwana alimaanisha atakuwa pamoja nao mpaka mwisho wa nyakati au muda, au kwa lugha nyepesi zaidi tunaweza kusema mpaka mwisho wa dunia.

Sasa utaona huko nyuma alishakwisha kuwaambia..katika Yohana 16.33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni MNAYO DHIKI; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu..”

Hii inatufundisha watakatifu wanaomngojea Bwana, kuwa wavumilivu…Ndugu usikatishwe tamaa na dhiki hizi za kitambo kifupi. Wakati mwingine katika safari yako utakapokutana na misukosuko kwa ajili ya YESU, wala usidhani unayo bahati mbaya, badala yake JIPE MOYO, kwani ni mambo yaliyokwisha tabiriwa yatawakuta waaminio wote, hivyo uwe na uhakika kuwa unapopitia hayo Bwana YESU yupo pembeni yako kukuhudumia kwa namna usiyoijua wewe, anakuwazia mawazo yaliyo mema siku zote, hatauacha mguu wako ujikwae kamwe, haijalishi mawimbi yamekuwa mazito kiasi gani Hutakufa UTAISHI! Nawe utayasimulia matendo ya Bwana (Zab 118:17) ikiwa bado unamshikilia tu huiachi imani, atakupa nguvu ya ajabu ya kuendelea mbele, ulimwengu utashangaa inakuwaje huyu mtu anapitia hali hii mbaya lakini hatetereki katika Imani, hiyo yote hawajui kuwa ni kwasababu ile Ahadi ya Kristo inatimia juu yako kuwa atakuwa pamoja nawe siku zote mpaka utimilifu wa dahari. Hivyo nataka nikuambie JIPE MOYO, mtazame Yesu songa mbele.

Lakini kumbuka ndugu ahadi hii ni kwa wale wanafunzi wa Kristo tu, sio kila mtu, swali Je! Wewe ni mwanafunzi wa Kristo?. ikiwa bado upo kwenye dhambi, ukweli ni kwamba huna mfariji, wala mwombezi, wala mtetezi, wala mshauri. Wewe ni yatima haijalishi una ndugu wengi wa mwilini kiasi gani… una utajiri wa nje mwingi kiasi gani bado ni maskini, au unayo afya kiasi gani, wewe ni bado ni mgonjwa tu!..huna ulinzi wowote ndani yako, ni nyumba isiyokuwa na msingi, ambayo siku yoyote inaweza kudondoka, Na ndio maana unashindwa kustahimili mawimbi yote ya ibilisi yanayokuja juu yako ni kwasababu hujajengwa juu ya MWAMBA.

Zaburi 1: 4 “Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo”.
Ufunuo 3: 17 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja name”.
Lakini leo hii habari njema ni kuwa Yesu bado anagonga kwenye milango ya mioyo ya watu, mkaribishe sasa, ayageuze maisha yako, atembee na wewe , afanyike kuwa mchungaji wako mpaka siku ya ukombozi wako,ili utembee kwa ujasiri hata ukifa leo ujue unapokwenda.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment