"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, June 10, 2019

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.


Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu.
Kama wengi wetu tunavyojua kuwa hakuna wokovu nje ya Yesu Kristo, wala hakuna Maisha nje ya Yesu Kristo. Kama Mtume Paulo alivyoandika kwa uweza wa Roho kwamba ‘Mauti ilikuja kwa njia ya mtu mmoja(Adamu)…kadhalika uzima utaletwa kwa njia hiyo hiyo ya mtu mmoja (ambaye ni Kristo)’.

Kwahiyo yeye peke yake ndio njia iliyo sahihi na iliyothibitishwa ya kumfikia Mungu..njia nyingine zote tofauti na yeye ni za upotevu, haijalishi zina wafuasi wengi kiasi gani.

Bwana Yesu alipokuwa hapa duniani, alizungumza kwa mifano mingi, yote ni kwa lengo la kumfanya mwanadamu aelewe mpango wa Mungu juu ya Maisha yake…Alitumia mifano ya miti, mashamba, wafanyabiashara, wakulima,familia, wageni, wafalme na mingine mingi ambayo hata haijaandikwa kwenye biblia, kwasababu kama yangeandikwa mambo yote aliyoyafanya moja moja…biblia inasema hata dunia isingetosha kwa jinsi vitabu vingekuwa ni vingi (Yohana 21:25)..

Lakini tunaona baada ya kuondoka alikuja tena kuzungumza na Mtume Yohana katika maono , alipokuwa katika kisiwa kile cha Patmo na kumpa mfano namna ambayo huwa anavyowajilia watu wake alimwambia…
Ufunuo 3: 20 ‘’Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami’’.
 
Mfano huo Bwana Yesu aliutoa kuonyesha ujio wake kwa mtu ni kama wa mgeni…Ujio huu sio wa kulichukua kanisa…kwasababu ujio wa kuja kulichukua kanisa alisema utakuwa kama ujio wa mwizi…hata kuja kwa kugonga na kusihi, bali atakuja usiku watu wakiwa wamelala na atachukua walio wake na kuondoka….ndio maana unyakuo ukipita sio watu wote watajua…Kwahiyo kuna kipindi Bwana Yesu atakuja kama mgeni na kuna kipindi atakuja kama mwivi.

Sasa katika mfano huu..anasema tazama nasimama mlangoni nabisha! Kubisha maana yake ni kugonga mlango huku unatoa sauti Fulani kama hodii hodii!! Hiyo ndiyo maana ya kubisha!..Kwahiyo hapa Bwana anasema nasimama nabisha, halafu anasema mtu akiisikia sauti yake na kuufungua mlango ataingia…hii ikiwa na maana kuwa mtu anaweza akaisikia sauti yake na asifungue…au mtu anaweza asiisikie kabisa sauti yake…labda kutokana na kwamba amelala au kutokana na usumbufu uliopo ndani ya nyumba kuwa mkubwa (labda kelele za miziki au watu).

Na baada ya kuingia utaona anasema…’nitakula pamoja naye na yeye pamoja nami’…sasa tafakari hapo kwa makini, hasemi tutakula pamoja hapana!...bali anasema nitakula pamoja naye…na yeye pamoja nami…ikiwa na maana kuwa alipokuwa anangonga alikuja na chakula chake, hakuja mikono mitupu…kadhalika na yule mtu aliyemfungulia atamkuta na chakula chake…na hivyo kila mmoja atashiriki na mwenzake kile alichokiandaa.

Sasa ukiingia ndani Zaidi kuutafakari mfano huu utaona kuwa unahusu wakati wa jioni…lugha yetu ya Kiswahili haijajitosheleza katika maneno mengi…lakini kama ukisoma tafsiri nyingine kama zile za kiingereza au kigiriki utaelewa vizuri kuwa ni wakati wa jioni ndio Bwana alikwenda kugonga mlango.. ni wakati wa chakula cha jioni (evening supper).

Kwahiyo katika mfano huo Bwana anakuja kugonga mlango wakati wa jioni…akiwa na chakula chake, hajaja kudoea wala kula vya watu bure!…Inaashiria kuwa Kristo anapotaka kuja kuingia katika Maisha yetu sio kwa lengo la kutaka vya kwetu, au kutuharibia Maisha hapana! Bali ni kwa lengo la kutupa sisi faida. Na atakuja jioni, hizi ni nyakati za jioni, wakati wa kumalizia wa mwisho wa dunia ndugu.

Na kama tunavyojua tabia ya mgeni anapogonga, huwa hagongi mfululuzo kama vile analazimisha mlango ufunguliwe…bali utaona anagonga kidogo kwa utaratibu kisha anatulia kidogo, akiona hasikiwi atarudia tena kwa sauti kidogo baada ya muda Fulani kupita..atafanya vile kwa kipindi Fulani, akiona hakuna kabisa majibu labda yule mtu amelala usingizi mzito hawezi kusikia hatavunja mlango ataondoka arudi tena baadaye au arudi wakati mwingine…Lakini akigundua yule mtu kule ndani anamsikia lakini hataki kumfungulia makusudi tu! Basi ataondoka asirudi tena…kwasababu anajua hahitajiki mahali pale.

Na Ndivyo hivyo Kristo anavyogonga mioyoni mwetu leo hii, atakutumia wahubiri pale mahali ulipo, kwa kukusihi umfungulie moyoni mwako aingie…akiona bado humsikii ataongeza watumishi kila mahali utakapokwenda hata kwenye mitandao utakutana na Neno lake, sauti yake utaisikia kila mahali ikikuita, utakapoitii ataingia, na vitu alivyokuja navyo kukuletea hutaamini macho yako kuvioona..Lakini endapo unajua kabisa huyu ni Kristo ananiita kupitia mahubiri, na kuwa hii ni sauti yake kabisa na unafanya makusudi kutokumfungulia…basi ataondoka na Neema hiyo itakwenda kwa wengine..

Ndugu usidanganyike kuwa utatubu uzeeni, Sauti ya Mungu itarudia kuita kwa wale watu ambao wakati Bwana amegonga wapo usingizini…wale watu ambao nguvu za giza zimewafunga kiasi kwamba hawawezi kuisikia injili…hao ndio Bwana ataendelea kuwaita kila wanapokwenda, mpaka watakapoamka usingizini, na kundi hili mara nyingi ni lile kundi ambalo halijawahi kabisa kupata nafasi ya kuujua msingi wa Imani ya kikristo, wale watu ambao wamezaliwa katika familia za kipagani, au familia za watu wasio wa dini, na hawamjui Kabisa Kristo…hawa ni sawa wapo usingizini au wapo kwenye makelele ya ulimwengu kiasi kwamba hawawezi kuisikia sauti ya Bwana Yesu..Hivyo Bwana ataiongeza sauti yake mpaka wasikie.Watapata Neema kubwa Zaidi.

Lakini kwa wengine ambao wamezaliwa katika Ukristo tangu udogoni, wamehubiriwa vya kutosha kuhusu msalaba, na wanaielewa kabisa sauti ya Yesu inapoita, na wengine mpaka wamemwona Bwana katika maono, na wamepewa ishara kadha wa kadha, Bwana akiwaita na hawataki kusikia…Kristo ataondoka kwao na asirudi tena kamwe. Wengi hawapendi kusikia hivi lakini huu ndio ukweli maandiko yanasema hivyo..Wana wa Israeli Taifa la Mungu yaliwatokea hayo, si Zaidi watu wa mataifa.. Bwana Yesu aliwaambia waisraeli maneno haya, baada ya kuwaonya mara nyingi na kushupaza shingo zao haya ndio aliyowaambia:
Mathayo 23:37 ‘’Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!
38 Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa.
39 Kwa maana nawaambia, HAMTANIONA KAMWE TANGU SASA, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana’’.
Aliwaambia ‘’hamtaniona kamwe tangu sasa’’..Hili Neno ni kali sana na linaumiza…’’kutengwa na Mungu milele’’..Si ni afadhali tutengwe na wanadamu kuliko Mungu…Ni heri wanadamu wote wanichukie na kunitenga lakini sio Mungu, ni heri nichokwe na wanadamu wote lakini sio Mungu.

Hebu tafakari leo hii Kristo anakwambia haya maneno ‘HUTANIONA TENA KAMWE TANGU SASA’!!!...Yaani wewe na Kristo ndio Basii!!...

Leo hii usikiapo maneno haya kwenye mtandao, na bado hutaki kuacha dhambi na ulimwengu, kumbuka haukuwa mpango wa Mungu usikie injili yake kwa njia hii ya mitandao..Mpango wake ulikuwa siku ile ile ulipoisikia injili kwa mara ya kwanza ulipohubiriwa na mtu aliyeshika biblia mkononi ungeamini, kulikuwa hakuna sababu ya wewe kuja kusikia tena injili hapa……lakini kwasababu Moyo wako ulikuwa mgumu, ndio maana amekufuata kwa njia nyingine hii ya mtandao..ili awe na uhakika kabisa unaisikia sauti yake. Lakini unaidharau..pengine hii ndio sauti yake ya mwisho kwako, isikie ufungue, asije akakwambia kama alivyowaambia wayahudi ‘HUTANIONA TENA KAMWE TANGU SASA’….Maneno haya yalizungumzwa na Kristo yule yule aliyesema ‘njooni kwangu nyinyi nyote’….hapa anasema ‘hamtaniona tena kamwe’…sehemu nyingine anasema ‘tokeni kwangu’.

Pale ulipo mwambie Bwana natubu dhambi zangu zote, na kukusudia kutokuzifanya tena, tubu kabisa kwa kudhamiria kabisa kuacha kuzifanya.Mfungulie mlango na yeye ataingia ndani yako haraka kukugeuza, hataanza kukulaumu kwanini nimegonga muda wote huo ukufungua, yeye si kama sisi, moja kwa moja atazungumza na wewe na muda wa kula ukifika atakufungulia hazina zake alizokuletea mshiriki pamoja, atakupa baraka zote za mwilini na rohoni, na kukufundisha maneno yake ya uzima. Utakuwa na tumaini la uzima wa sasa na ule wa baadaye.

Lakini usipotaka ataondoka, na siku moja atakuja kama mwivi, siku hiyo atakuja kwako tu bali atakuja kwa ulimwengu mzima, atavunja atavunja mlango na kuwaiba waliowake ndani, na kwenda nao mbinguni, huku nyuma moto utawaka. Usitamani uwepo hicho kipindi cha dhiki kuu. FIKIA TOBA LEO!

Ni maombi yangu kuwa utakitendea kazi ulichokisikia.
Bwana akubariki, pia washirikishe wengine hichi kitu ili nao pia wapone kama wewe.

No comments:

Post a Comment