"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, June 5, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 65

SWALI: Mtumishi nina swali linanitiza kidogo hapa nataka kujua Adamu aliwasiliana na Mungu kwa lugha ipi pale Bustanini?.

JIBU: Biblia haijataja lugha gani ilikuwa inatumika pale Edeni, Lakini ni wazi kuwa kulikuwa na lugha Fulani iliyotumika, kwasababu Mungu ametuumba sisi wanadamu tuwe tunawasiliana kwa njia ya kuzungumza, na hatuwezi kuzungumza bila lugha.

Sasa Mwanadamu wa kwanza Adamu alivyoumbwa ni tofauti na wengine tuliofuata..sisi wengine safari yetu ilianzia katika matumbo ya mama zetu lakini sio Adamu. Adamu Mungu alimwumba mkamilifu, maana ya mkamilifu ni kwamba hajazaliwa wala hajarithi, wala hajafundishwa, yaani ameumbwa tayari ana maarifa kichwani mwake. Tofauti na sisi, tunapozaliwa itatuchukua muda mrefu sana maarifa yaingie kichwani mwetu, mpaka tuweze kuelewa hichi na kile…inachukua miaka mingi….Ndio maana Mungu alipomtengeneza Adamu alimletea wanyama aangalie atawaitaje..Adamu akawapa majina wote pale pale…hakuhitaji kujifunza kwanza herufi na matamshi..pale pale alianza kuzungumza…Huo ni uwezo wa kipekee sana.

Kwahiyo Adamu aliumbwa na lugha tayari kichwani ambayo kwa kupitia hiyo angeweza kuwasiliana na mkewe, wanawe pamoja na Mungu..(Ingawa Mungu ana uwezo wa kuzungumza na sisi pasipo lugha na tukamwelewa).

Na lugha hiyo Adamu aliyoumbwa nayo ni wazi kuwa iliendelea kutumika kwa vizazi na vizazi mpaka wakati wa Babeli..ambapo lugha nyingi ndipo zilipozaliwa..(Mwanzo 11). Kwahiyo kuitambua lugha yenyewe hasaa ni ipi, ni ngumu inawezekana ni moja ya lugha tunazotumia sasahivi, au ilishamezwa ndani ya lugha nyingine na kupotea kabisa..

Ubarikiwe.

SWALI: Je! Kushiriki au kujihusisha kwenye michezo ni dhambi?...Kwa mfano kutazama mpira, au kucheza tennis n.k?
JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa vimtokavyo mtu ndani ya moyo ndivyo vinavyomfanya kuwa najisi..Chochote mtu anachokifanya, au anachojihusisha nacho kinachomsababishia moyoni mwake kutoke ugomvi, ubishi, mashindano, hasira,matusi kitu hicho tayari ni najisi kwake…Biblia inasema. 
Wafilipi 2: 3 ‘’Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake’’.
Swali je! Kuna mchezo wowote ambao ukiufuatilia haukupeleki kwenye mashindano(malumbano)?...kushindana mpaka wakati mwingine kutukana na kufanyiana mizaha. Kama upo basi huo sio najisi kwako.

Biblia pia inasema…

Wafilipi 2: 14 ‘’Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, 15 mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu’’.

Jiulize kuna mchezo wowote ambao ukishaisha haukupeleki kwenye manung’uniko?..yaani kuwanung’unikia wahusika wa huo mchezo, au kumnung’unikia mwenzako? 
Neno linasema hapo, ‘’ambao kati yao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu’’…sasa ni mwanga gani utakaoonesha endapo ukiwa ni mshabiki, au mtu wa manung’uniko, au mtu wa mizaha, au mbishi, na mtu wa mashindano? Ni kitu gani hapo kitakachomfanya mtu asiyeamini avutiwe na Imani yako?...Jiulize tangu uanze kuwa mshabiki wa mpira kuna mtu yeyote alishawahi kuokoka alipokutazama wewe wakati unaangalia mpira, au wakati wa wewe kumaliza kuangalia mpira? Au wakati magoli yanapofungwa?..kama ulishawahi kumbadilisha mtu kwa njia hiyo, basi kwako michezo sio najisi…Lakini kama bado ujue kuwa ni dhambi kujihusisha nayo. Hebu fikiria endapo Bwana Yesu yupo duniani angekuwa ni mshabiki wa mchezo Fulani, akishamaliza kuhubiria makutano anakwenda viwanjani kutazama michezo na akitoka hapo anashindana na wanafunzi wake kuhusu ule mchezo, tungewezaje kumwelewa?..angekuwa anatuchanganya…Na sisi hatupaswi kuwachanganya watu walio nje ya Imani yetu. Wanapaswa wavutiwe na mienendo yetu ili watoke huko na kuja huku tuliko(2 Timotheo 2:24).

Swali la mwisho kabisa la kujiuliza, ni juu ya muda unaotumia katika kushabikia au kuangalia hiyo michezo, jitathimini muda unaotumia kutazama hiyo michezo, ulinganishe na muda unaotumia kusali au kuomba au kusoma Neno. Kama unatumia dakika 10 kuangalia michezo na unatumia masaa matano au Zaidi kusoma Neno, basi ni wazi kuwa Michezo sio kitu kilichochukua nafasi moyoni mwako, na kinaweza kisiwe na madhara kwako, lakini kama unatumia masaa mawili kutazama michezo na Neno la Mungu au sala unatumia dakika tano au husali kabisa Hiyo ni Ashera ndani ya moyo wako, hivyo unaishi Maisha ya dhambi. Kama kwenye ibada unasinzia halafu kwenye michezo unachangamka hilo Ashera kwako, Kama kwenye michezo unaouwezo wa kupiga kelele kwa nguvu kwa ujasiri wote, mpaka mtaa wa pili wanasikia halafu, ibadani kumsifu Mungu unaona aibu unanong'ona kwa sauti ya chini, ni machukizo mbele za Mungu.

Kwahiyo kwa ujumbla michezo yote inayozaa magomvi, chuki, matusi, hasira, uchungu,mizaha,mafarakano, utani mbaya, vinyongo, manung’uniko, mashindano,visasi, vita, makwazo, tamaa, ulevi,wizi n.k..Yote ni kutoka kwa yule Adui kwahiyo ni dhambi kujihusisha nayo.

Ubarikiwe.

SWALI: Naomba kufahamu mstari huu Bwana alimaanisha nini kuusema “waache wafu wazike wafu wao.(Mathayo 8:21)?

JIBU: Ili kufahamu vizuri hii habari turudi kidogo kwenye historia ya Wayahudi katika shughuli zao za mazishi, Kumbuka Waisraeli walivyozika zamani sio kama wanavyozika leo, leo hii mtu akifa wanamvisha sanda,(katika baadhi ya tamaduni) kisha wanamfukia chini bila jeneza, na shughuli inakuwa imeisha, lakini zamani, haikuwa hivyo katika tamaduni zao, kwanza makaburi yalikuwa sio ya kuchimbwa chini futi 6 kama yanayotumika sasa hivi hapana, bali yalikuwa yanachongwa kwenye mwamba, au pango lililotokea lenyewe asilia, na yalikuwa sio ya kuzikia mtu mmoja mmoja hapana bali yalikuwa ni ya familia, na kulikuwa kuna kuzikwa “kwa kwanza” na “kuzikwa kwa pili”, tofauti na tamaduni karibu zote tulizonazo sasahivi.

Kwa mfano imetokea mshirika wa familia amekufa, mwili wake ukishaoshwa na kuvishwa sanda, ulikuwa unapelekwa kwenye kaburi hilo la familia, wakifika huko wanamweka sehemu yake maalumu peke yake,kwenye shelfu ambalo litakuwa limechongwa ndani ya kaburi hilo na huko wanaoruhusiwa kuingia ni wanafamilia tu, Hivyo wakishamlaza jambo linalofuata wanalifunga kaburi kwa jiwe kubwa kisha wanalisakafia, kisha wanarudi nyumbani kuendelea na maombolezo ambayo hayo yanadumu kwa muda wa siku kadhaa ikiwa aliyefariki ni mtoto katika familia, lakini kama ni mzazi iwe ni baba au mama siku za kuomboleza zinaendelea kwa muda wa mwaka mzima..Kisha baadaye mwaka ukishaisha wanafamilia wote na ndugu wanakusanyika tena kwa ajili ya maziko ya pili.

Hapa ndipo mifupa ya Yule marehemu inatolewa, pale alipolazwa mara ya kwanza na kupelekwa kwenye shelfu lingine lenye mifupa ya wanafamilia wote waliokufa kabla yake, na mifupa yake inalazwa pamoja na ya kwao, kisha habari ya mazishi inakuwa imeisha rasmi, na ndio maana kama ulishawahi kusikia, pale biblia “inaposema akafa akakusanywa pamoja na watu wake”, hilo lilikuwa ni tendo la mwilini ambalo lilifunua tendo la rohoni, (Soma Mwanzo 49:29-33, Hesabu 20:24, Waamuzi 2:10 n.k.)…Kuna kukusanywa katika mwili na katika roho pia. Lakini hatutaenda huko sana.

Sasa turudi kwenye swali, kwanini Bwana alimwambia Yule mtu vile..tusome: 
Mathayo 8:21 ‘Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu.

22 Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao’.

Tumekwisha kuona jambo la kumzika Baba, halikuwa jambo jepesi la kwenda na kurudi kuchukua siku mbili au tatu, ni jambo linalochukua mwaka..Lisingekuwa jambo kubwa kwa Bwana kumwambia nenda urudi, Kama ni hivyo hata Bwana Yesu asingekaa kuhudhuria msiba wowote lakini tuona aliposikia habari za msiba wa Lazaro pamoja na umbali wote ule na hatari zote zile za kutaka kuuliwa.(Yohana 11),lakini alifunga safari kwenda kumponya.

Lakini utaona huyu mtu alikuwa anajaribu kutafuta njia za kuikwepa kazi ya Kristo.

Ndugu fahamu kuwa ili uwe mwanafunzi wa Yesu, ipo gharama ya kuingia, yeye mwenyewe alisema apendaye Baba au Mama kuliko mimi hanistahili. Pale Mungu anapokuambia sasa ni wakati wa wewe kunitumikia, usiwe ni wakati wa wewe kusema ngoja kwanza nikamalizie kufanya biashara zangu msimu huu ukiisha nitakutumikia, Mungu hataki udhuru.

Na ndio maana akamwambia Yule mtu waache wafu wawazike wafu wao, ikimaanisha kuwa mtu yeyote aliye mbali na Kristo, ni mfu tayari katika roho japo atakuwa anatembea, lakini mauti ipo ndani yake na siku akifa wafu wenzake ambao bado hawajafa ndio watakaokwenda kumzika, Mauti inaanzia tukiwa tunapumua kadhalika wokovu unaanzia tukiwa bado tunapumua hapa hapa duniani..ndio maana hatuokoki tukishafika kule, wokovu unaanzia hapa hapa duniani, tunaokoka hapa, kule ni hitimisho la wokovu wetu.

hivyo sisi tunaonywa pia tusitoe udhuru kwa vitu tuvipendavyo pale Yesu anapotuchagua tumfuate.

Bwana akikuita umtumikie, na amekuambia acha kitu Fulani, usianze kutazama ni jinsi gani utawaachia wengine hiyo fursa wewe waachie wanaokifanya hicho kitu waendelee kukifanya wewe nenda kamtumikie Mungu, ikiwa leo hii amekuambie acha biashara haramu nifuate, usianze kumwambia Mungu ngoja kwanza nimalizie kuuza hizi zilizopo kisha nitaanza kufanya biashara halali. Mungu hapendi kuwekwa wa mwisho.

Na ndio maana YESU akawaambia wanafunzi wake. ‘’Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu’’.(Luka 9:62). Ukristo unayo gharama. Ni kujikana na kupiga gharama kweli kweli.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment