Shalom.Karibu katika mwendelezo wa
kitabu cha Ufunuo, ni vizuri ukakisoma kitabu hichi peke yako kwanza kwa
utulivu, na katika uwepo wa Bwana, na kufuatilia mfululizo huu tangu mwanzo ili
tunapoendelea katika sura hizi zinazofuata usibakie nyuma twende pamoja.
Katika sura iliyopita tuliona jinsi
wale malaika 7 walivyopewa baragumu zao na pindi walipozipuliza/kuzipiga ni nini
kilitokea, Na tulishaona baragumu nne za mwanzo…kama hujapitia pia ni vizuri
ukapitia au bofya hapa⏩ Ufunuo:Mlango wa 8. Na tuliona kuwa baragumu hizo ni kama mwanzo wa utungu tu! Wa vile
vitasa saba vitakavyokuja kuachiwa huko mbeleni katika siku ile kuu ya Bwana.…Ni
sawa na mtu anayenawa uso kwa muda tu! Lakini baadaye atakuja kuoga mwili
mzima.
Vile vile tuliona pia hizi baragumu zitaanza kupigwa mara baada ya
unyakuo kupita tu! Na zile tatu za kwanza Zitawaathiri sana wayahudi walioopo
Israeli (na watu wanaoishi mashariki ya kati), isipokuwa lile la 4 ambalo
litaathiri dunia nzima, kwasababu jua likipigwa ni dunia nzima itaathirika na
sio sehemu tu!..na mapigo hayo yatatekelezwa kupitia wale mashahidi wawili
waliozungumziwa katika ufunuo 11.
Ufunuo 11:3 “Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia.
4 Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi.
5 Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa.
6 Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo”.
Unaona Mashahidi hawa wawili wataleta
mapigo hayo kwa amri ya Bwana kama vile Musa alivyoleta mapigo juu ya Farao kwa
Amri ya Bwana.
Na mwishoni mwa sura ya 8, tuliona
pia kulikuwa na malaika (Tai) aliyeruka katika anga na kutangaza ole kwa wote
wanaokaa juu ya nchi kwasababu ya sauti ya zile baragumu 3 zilizosalia, yaani
baragumu la 5,6 na la 7.
Hivyo leo tunaendelea na sura ya 9
kwa Neema za Bwana..ambayo inaelezea juu ya baragumu zilizosalia isipokuwa ile
ya saba tu.
Ufunuo 9: 1 “Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu.
2 Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni.
3 Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi.
4 Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wo wote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.
5 Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu.
6 Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.
7 Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama taji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu.
8 Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.
9 Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani.
10 Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao.
11 Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni”.
Kama tulivyotangulia kujifunza,
Nyota iliyoanguka kutoka mbinguni si kimondo bali ni ‘shetani’ na Ufunuo 12:12
inasema.. “hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. OLE WA NCHI NA
BAHARI! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya
kuwa ana wakati mchache tu.”
Na pia sehemu nyingine Bwana Yesu
anasema: Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama
umeme. (Luka10:18)
Ikiwa na maana kuwa kuanguka kwa
shetani, na kutupwa chini duniani ni LAANA! Sio kitu kizuri..viumbe vyote
vikaavyo baharini vitaathirika na kadhalika vikaavyo juu ya nchi…sasa wanadamu
ndio wanaokaa juu ya nchi, hao ndio waathirika wakuu!.
Katika baragumu hili tunaona shetani
kama nyota iliyoanguka kutoka juu…akipewa funguo za kuzimu…sasa kumbuka kuzimu
zimegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni sehemu ambapo roho za
watu waliokufa katika dhambi zipo, ni sehemu ya mateso sana, roho za watu hawa
zipo zikiwa katika hali ya vifungo, zikiteseka zikingoja ufufuo wa hukumu.
Na sehemu ya pili ya kuzimu, ni
sehemu ambayo roho za baadhi ya malaika walioasi mbinguni zimefungiwa…Kumbuka
sio mapepo yote yaliyoasi yanatenda kazi leo duniani, hapana, yapo mengine
mabaya kuliko haya yaliyopo sasa, ambayo yalifungwa katika hii kuzimu ya pili,
kwa makosa yaliyofanywa na hata kuna mengine yanaweza kutupwa huko hata leo, ndio maana utaona kuna
yale yaliyomsihi Bwana Yesu asiyapeleke shimoni..Huko shimoni kunakozungumziwa
ni “kuzimu ya malaika walioasi’’ ni sehemu ya vifungo vya giza na mateso ambapo
roho hizo zimefungwa huko mpaka siku zitakapotupwa katika ziwa la moto…ambapo
tutakuja kuona katika ufunuo 20 shetani naye atakuja kutupwa huko na kufungwa
kwa miaka 1000.
Sasa pia kumbuka shetani
alinyanganywa funguo za mauti na kuzimu na Bwana Yesu mwenyewe, kwasababu hapo
kwanza alikuwa nazo alikuwa na uwezo wa kuzileta juu roho za watu waliopo
kuzimu na baadhi ya mapepo,! Ndio maana maana unaona aliweza hata kumleta Nabii
Samweli juu aliyekuwa amekufa kuzungumza naye. Lakini Baada ya Bwana Yesu kuja,
mamlaka yote ya wafu yakawa chini ya Yesu Kristo, hakuna kiumbe chochote hata
shetani chenye mamlaka juu ya wafu au roho zilizopo kuzimu au peponi. Lakini
tunaona hapa! Shetani anapewa ufunguo za kuzimu…na kama unavyoona ni ANAPEWA!!
Ikiwa na maana kuwa hakuwa nazo hapo kabla…alikuwa amenyanganywa lakini hapa
anapewa tena kwa muda.. sasa hapewi funguo za kuzimu mahali wanadamu walioasi
walipo hapana bali anapewa funguo za kuzimu mahali malaika walioasi
walipo?..hizo ni sehemu mbili tofauti.
Na kwasababu ana ghadhabu nyingi na
lengo lake ni kuiharibu dunia kwasababu anajua muda wake umeisha….funguo
atakazopewa atafungua kuzimu na kuyafungulia mapepo ambayo Bwana Yesu
aliyafunga yasifanye kazi duniani kwa kipindi Fulani kwasababu yangeleta
uharibifu mkubwa sana ambao haujawahi kuwepo!!..Ndio maana kuna umuhimu mkubwa
sana wa kumshukuru Mungu kwaajili ya Yesu Kristo, maana kama si yeye sijui
tungekuwa wapi leo. Shetani angetupepeta vya kutosha.
Kwahiyo shetani atapewa funguo na
atayafungua hayo mapepo yaliyokuwa kifungoni, ambayo ni mabaya kuliko haya
yaliyopo huru sasa duniani..Sasa biblia imeyafananisha hayo mapepo na hao nzige
tunaowasoma kwenye sura hii…Kumbuka sio nzige kama nzige hawa wadudu tunaowajua
watakaotoka kuzimu hapana! Bali ni maroho! Biblia imefananisha mara nyingi roho
chafu na roho za wanyama au wadudu..(Kwamfano Ufunuo 16:13 unaweza ukaona jambo
hilo….Inasema: “Nikaona roho tatu za
uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika
kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo Hizo ndizo
roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu
wote…”).
Maumivu yao ni kama ya ng’e..roho
hizi zitaleta madhara makubwa katikati ya watu..pigo hili litakuwa ni kwa watu
wa dunia nzima…Unajua sasahivi kila uovu Fulani unaasisiwa na roho Fulani (au
pepo fulani)..Kwamfano ushoga ni mapepo Fulani ya aina hiyo yanawaingia watu na
kuwapeleka kwenye ushoga…yasingekuwepo hayo watu kwa hali ya kawaida
wasingeweza kuwa mashoga..kadhalika na usagaji, utafanyaji masturbation, uuaji,
wizi, usengenyaji, n.k yote hayo ni mapepo.
Ili kuelewa vizuri kama wewe ni
mdadisi wa kifaa kinachoitwa computer au simu, utagundua kuwa unaponunua
computer au simu inakuwa na mambo machache sana…ili kuiongezea uwezo inakubidi
kudownload baadhi ya programs au softwares ili iweze kwenda kama unavyotaka
wewe..utagundua kuwa ili sauti iweze kusikika vizuri, au ili uweze kuongeza
milio ya simu, au uweze kuwasiliana na watu kisasa n.k inakubidi udownload
applications au software kwenye simu yako au computer yako..sasa hizo
applications au softwares unazoziongeza kwenye simu yako ndio mfano wa mapepo
ambayo shetani anayaongeza ndani ya watu ili waweze kuwa mashoga, wauaji,
wazinzi, walawiti n.k
Sasa katika siku hizo
yatakapofunguliwa, zitazalika tabia duniani ambazo hazipo duniani leo…pengine
utaanza kuona watu wanaanza kula nyama za watu, au utaanza kuona watu wanaanza
kuwa na uwezo wa ajabu wa kipepo, ukatili wa ajabu utaongezeka ambao haujawahi
kuonekana hapo kabla, pengine utaona watu wanafanya uzinzi mabarabarani bila
aibu,..na kuzuka baadhi ya magonjwa ambayo ni mapya, ya mateso kushinda
saratani au ukimwi,..pengine utaanza kuona na wanyama pia wanabadilika tabia,
hawafugiki tena, nk n.K, siku hizo ndizo watu watatamani kufa lakini biblia inasema
mauti itawakimbia. Kila mtu ataona hakuna maana ya maisha tena, duniani
hakukaliki hofu ya kila kitu.
Na kwenye ule mstari wa mwisho
biblia inasema wanaye mfalme naye ni malaika wa kuzimu..jina lake kwa kiebrania
ni Abadoni na kwa kiyunani ni Apolioni…Abadoni maana yake ni “MAHALI PA
UHARIBIFU”. …na Apolioni maana yake ni “MUHARIBIFU”…Majina yote haya mawili
yanamzungumzia ‘shetani’ ambaye ndiye mwaribifu na kila aina ya uharibifu
unatoka kwake. Yeye ndiye mfalme wa kuzimu na mfalme wa hawa malaika
walioachiwa kutoka kuzimu.
Na ndio maana ni vizuri kutengeneza
mambo yako sasa, angali neema ya Kristo ipo, huko mbeleni ni vilio na
maombolezo kwa watakaokosa unyakuo.
Tukiendelea na mistari inayofuata
biblia inasema…
Ufunuo 9: 12 “Ole wa kwanza umekwisha pita. Tazama, bado ziko ole mbili, zinakuja baadaye.
13 Malaika wa sita akapiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu,
14 ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue nao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati.
15 Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu.
16 Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi; nilisikia hesabu yao.
17 Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti.
18 Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao.
19 Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwa hivyo.
20 Na wanadamu waliosalia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda.
21 Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao”.
Katika mstari wa 14 tunaona
ikitolewa amri ya kufunguliwa kwa wale malaika wanne waliokuwa wamefungwa
katika Mto Frati. Na hawa lengo la kuzuiwa katika Mto Frati ni ili wasilete
madhara waliomriwa kuleta kabla ya wakati kufika, kwamba wakati ukifika waue
theluthi ya wanadamu wanaoishi juu ya nchi…Ili tujue hawa malaika ni
wapi…turudi nyuma kidogo kwenye ufunuo Mlango wa 7.
Ufunuo 7: 1 “Baada ya hayo nikaona
malaika wanne wamesimama katika pembe nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi,
upepo usivume juu ya nchi, wala juu ya bahari, wala juu ya mti wo wote.
2 Nikaona malaika mwingine, akipanda
kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa
sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari,
3 akisema, Msiidhuru nchi, wala
bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu
ya vipaji vya nyuso zao”.
Malaika hao wanne waliokuwa
wamezuiwa kwenye mto Frati ndio hawa hawa ambao walionekana wamesimama kwenye
pepo nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi, Na pepo hizi nne ni upepo wa KI-SIASA,
upepo wa KI-DINI, KI-UCHUMI na KI-JESHI. Hizo ndio pepo 4 za nchi.
Malaika hawa waliwekwa kuzuia vita
vikuu vya Harmagedoni visitokee juu ya nchi.. Kwahiyo walikuwa wanazuia shughuli
zozote za kipepo zisifanye kazi juu ya siasa ya dunia, uchumi wadunia, dini ya
dunia wala jeshi la dunia, lakini sasa wakati huu, wataruhusu shetani aingie
kuvuruga siasa ya dunia, uchumi, dini pamoja na jeshi…Yale mapepo yaliyotoka
kuzimu yatawaingia wanasiasa wa dunia, sasa kuanzia wakati huu kutakuwa hakuna
kuelewana duniani, kutakuwa hakuna kuvumiliana tena…mipango ya vita itawekwa,
na amani itavurugika kwa kiwango kikubwa sana…Na ndio maana unajiuliza kwanini
Leo mataifa makubwa yanagombana lakini hayapigani, nikwasababu malaika hawa
wameamuriwa wazuie machafuko, lakini wakati utafika hakutakuwa na kuzuiwa tena,
vitendo vitafuata.
Biblia inasema zaidi ya wanajeshi
milioni 200 (elfu ishirini mara elfu kumi), watahusika katika mapambano ya vita
hiyo ya Harmagedoni… “na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na
katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti.” Mstari huu unazungumzia
aina za silaha zitakazotumika wakati huo, farasi anawakilisha silaha za kijeshi
kama ndege za vita, vifaru, helicopter za mabomu ya atomiki n.k na kama hapo
inavyosema katika midomo yao inatoka moto, moshi na kiberiti…inazungumzia mabomu, na makombora
yatokayo kwenye vifaru hivyo, ndege hizo, nk na walikuwa na vichwa kama vya
simba, kama vile simba angurumapo atafutapo wawindo na silaha hizi zitakuwa na
mingurumo zitumiwapo.
Kwahiyo katika baragumu hili la sita
ndio utakuwa mwanzo wa maandalizi ya vita ya tatu ya dunia…Vita ya Mungu
mwenyezi, (Harmagedoni). Ambayo tutakuja kuisoma vizuri katika Kile kitasa cha
sita katika Ufunuo ule mlango wa 16. Wakati huu machafuko ya mataifa yatakuwa
mengi sana duniani.
Kristo yupo mlangoni, umefanya
uteule wako na wito wako Imara sawasawa na 2 Petro 1:10?. Kama sivyo jitazame
mara mbili, kisha chagua mwisho mwema, mambo haya sio hadithi tu za zale ni
mambo ambayo yatakuja kutokea dhahiri mbele ya macho ya watu wengi.
Bwana akubariki.
Usikose kufuatilia sura zinazofuata,
pia usiache kuwashirikisha wengine habari njema baada ya kuujua ukweli huu.
Kwa mfululizo mzuri wa uchambuzi wa kitabu hichi cha Ufunuo tembelea website yetu hii ⏩ www.wingulamashahidi.org
No comments:
Post a Comment