Jina la
Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha
Ufunuo, leo kwa Neema za Bwana tutajifunza sura hii ya 8.
Ufunuo 8:1 ‘Hata alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama muda wa nusu saa’.
Katika
mstari huu wa kwanza, Tunaona Yohana anaanza kwa kuonyeshwa ono la kufunguliwa
kwa Muhuri wa saba. Kwenye mlango wa sita wa kitabu hichi tulishaona ni
nini maana ya mihuri, na ilipofunguliwa ni nini kilitokea,kwahiyo kama
hujapitia Mlango wa 6, ni vizuri ikaipitia ili tuweze kwenda pamoja katika sura
hizi zinazofuata…Lakini kwa ufupi tuliona Muhuri huu wa saba umebeba siri ya
Ujio wa Yesu Kristo mara ya pili…Na utatimizwa kipindi kifupi sana kabla ya
unyakuo, ambapo ndani ya muhuri huo wa saba tuliona ndio umebeba siri ya zile
ngurumo saba zilizozungumziwa katika Ufunuo 10:3 ambazo Yohana
aliambiwa asiziandike. Kwa kupitia siri hizo kanisa la Kristo (linalojulikana
kama bibi-arusi safi) litapata Imani ya kwenda kwenye unyakuo.
Tukiendelea ni mistari inayofuata biblia inasema…
Ufunuo 8:2 ‘Nami nikawaona wale malaika saba wasimamao mbele za Mungu, nao wakapewa baragumu saba.3 Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu,akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu yadhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi.4 Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika’’.
Hapa
tunaona Yohana akioneshwa maono mengine..Aliona Malaika saba wanaosimama
mbele
za Mungu..wakipewa baragumu saba…Sasa hawa malaika Yohana aliowaona sio malaika
wa sifa au makerubi hapana! Bali ni malaika wa hukumu. Na utaona wanapewa
baragumu saba…kila mmoja baragumu moja..Maana ya Baragumu ni ‘Mbiu’ kwa
lugha ya sasa hivi..Kwahiyo kila mmoja alipewa mbiu yake…Sasa kazi za hizi mbiu
ni kutoa sauti ya tukio Fulani la ghafla kuanza au kutokea…Zamani vita ilikuwa
Ikisikika baragumu (au mbiu) vitani ni ishara ya kuwa vita
vimeanza..au mapambano yameanza, au kuna kitu cha hatari kinakuja…Kwahiyo na
hawa malaika wanaonekana hapa wakiwa na baragumu kufunua kuwa watakapopuliza tu
basi kuna kitu cha hatari kinafuata.
Lakini
katika mstari wa tatu, tunaona Yohana anakatishwa yale maono ya wale malaika
saba, anapelekwa
kwenye maono mengine anaonyweshwa madhabahu na malaika mwingine tofauti na wale
saba, anakuja na chetezo pamoja na uvumba ili autie pamoja na maombi ya
watakatifu wote juu ya madhabahu iliyokuwa mbele ya kiti cha enzi.
Sasa
uvumba unaashiria maombi ya watakatifu, watakatifu tunapoomba maombi yetu
yanaenda kama harufu ya uvumba mzuri mbele za Mungu, Daudi alisema
katika Zaburi 141:1-2 ‘’Ee
Bwana,
nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. Sala yangu ipae mbele
zako KAMA UVUMBA,
Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.’’..ukisoma
pia Ufu.5:8 utaona jambo hilo, kuwa uvumba siku zote unawakilisha
maombi ya watakatifu.
Kwahiyo
Malaika huyu kazi yake ilikuwa ni kuchukua maombi ya watakatifu wote..kuanzia
agano la kale hadi mwisho wa dunia na kuyapeleka mbele za Mungu, na yote
yalikuwa yanajibiwa kwa wakati..Lakini sasa hapa mwisho utaona kazi yake ya
kupeleka maombi ya watakatifu mbele za Mungu inaisha, na inaishia kwa kukichukua
kile ‘chetezo’ na kukiweka makaa ya moto yatokayo madhabahuni na kuyatupa juu
ya nchi (yaani duniani). Ikiashiria kuwa hakuna tena huduma ya kupeleka
maombi ya watakatifu mbele za Mungu, kwani watakatifu wote wameshaondolewa
duniani(katika Unyakuo)…kilichosalia ni hukumu tu.
Yule
malaika mara baada ya kumaliza kuvukiza uvumba ule mwingi alichokua moto
uliokuwa kwenye madhabahu na kuuweka kwenye chetezo chake na kuumwaga juu ya
nchi…chetezo ni kifaa kidogo kilichokuwa kinatumika kuwekea ubani
(uvumba)..ambacho ndani yake kinawekwa mkaa
wa moto
na ubani na kilikuwa na mkono wa Kamba au mnyororo hivi ambacho kuhani mkuu
alikuwa ana uwezo wa kutembea nacho ndani ya hekalu wakati wa kufanya
upatanisho, na kinakuwa kinatoa moshi wa ule ubani unaochomeka mule
ndani(Kutoka 30:5-9) …Hivyo kuhani alipochoma ubani moshi unatoka kwenye kile
chetezo na kukijaza chumba chote moshi wa manukato.
Ufunuo 8:5 ‘Na huyo malaika akakitwaa kile chetezo, akakijaza moto wa madhabahu, akautupa juu ya nchi, KUKAWA RADI NA SAUTI NA UMEME NA TETEMEKO LA NCHI.6 Na walemalaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari ili wazipige.’’
Hivyo
huyu malaika alipotupa ule moto katika roho duniani kukawa na radi na sauti ya
umeme na tetemeko la nchi. Sasa hivyo vitu vitatu, radi, sauti na
tetemeko la nchi..Tafsiri yake ndio ipo katika wale Malaika 7 waliopewa
baragumu wazipige…, hawa malaika saba ndio walioleta hizo radi, sauti na
matetemeko ya nchi, kila mmoja kwa sehemu yake mpaka saba wote walipokwisha
kupiga/kupuliza hizo baragumu.
Ufunuo 8:7 inasema:..‘Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea’.
Sasa
kabla ya kuingia kwenye baragumu ni muhimu kujua kuwa Baragumu hizo zitaanza
Kupigwa
baada ya unyakuo kupita, yaani baada ya kanisa kunyakuliwa na kwenda mbinguni..wakati
ambapo Mpinga-Kristo atanyanyuka duniani, na kwenda kuketi katika Hekalu la
Mungu, katika nchi ya Israeli na kutaka kuabudiwa yeye kama Mungu (ukisoma 2Wathesalonike
2:1-10 utaona jambo hilo).
Kumbuka
sasa wayahudi/waisraeli wengi leo hii hawamwamini Yesu kama ndiye Masihi, hivyo
wengi hawajawa wakristo bado wanashika desturi za Torati ya Musa, huku
wakimsubiria Masihi mwingine aje kuwaokoa, Kumbuka ni Mungu mwenyewe ndio
kawafumba macho wasimtambue Bwana Yesu kuwa ndiye Masia wa kweli, hivyo mpaka
unyakuo unapita watabakia katika hali hiyo hiyo ya upofu, hivyo wataikosa
mbingu…
Lakini
Mungu atawahurumia wao tu na kuwafumbua macho baada ya unyakuo kupita Sasa
Wakati huo ndio Israeli watagundua kuwa Yesu Kristo waliyemkataa Zaidi ya miaka
2000 iliyopita ndiye Masihi wao waliokuwa wanamtazamia, watatubu ndipo Bwana
atawafungua macho..(saa hiyo watu wamataifa walioachwa kwenye unyakuo
wataendelea kudanganyika na kupotea) kwasababu kutakuwa hakuna tena mlango wa
Neema kwa watu wa mataifa, Zaidi ya kusubiria kuipokea ile chapa ya mnyama na
kuingia katika siku ya ghadhabu ya Bwana..na watu wa mataifa kumbuka ni watu
wote tofauti na Taifa la Israeli (yaani waafrika, wahindi, wazungu, wachina na
wengine wote).
Hivyo
baada ya unyakuo kupita Bwana atawatumia mashahidi wake wawili kwa Roho ya Musa
na Eliya, kuwarejesha Israeli kwenye mstari na kuihukumu dunia kwa sehemu
Fulani…Kwa uelewa Zaidi juu ya urejesho wa Israeli na huduma ya hawa mashahidi
wawili…(fungua mfululizo huu katika sura ya 7 na ya 11 au bofya hapa⏩Ufunuo
7&11…soma yote vizuri kisha ndipo uendelee na
hapa)…Kwasababu sehemu kubwa ya baragumu hizi saba zinahusu huduma ya hawa
mashahidi wawili. Na baragumu hizi saba zitakuwa ni mwanzo wa UTUNGU, wa
siku ile kuu ya BWANA..
Sasa tukirudi kwenye zile baragumu biblia inasema…
Ufunuo 8:7 ‘Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea’.
Kipindi
kifupi sana baada ya unyakuo kupita Bwana atawanyanyua Mashahidi wawili na
atawapa amri ya kuipiga dunia kama watakavyo ukisoma katika Ufu.11,utaona
hilo, mambo haya yatatekelezwa na mashahidi hawa wawili, kutatokea na mtikisiko
katika anga, kutakuwa
na matukio ya mvua za mawe, ingawa pia katika roho mvua ya mawe inaashiria kitu kingine..Lakini
kutakuwa na vipindi vibaya sana vya mvua ya mawe, kama ile ilivyotokea wakati wa wana
wa Israeli walipokuwa Misri, ambayo iliharibu mimea yote na mazao yote ya
chakula katika nchi ya Misri, na tunasoma ni Musa ndiye
aliyeleta pigo lile kwa amri ya Mungu, na kadhalika katika
baragumu la kwanza litakapopigwa wale mashahidi wawili ndio watakaoleta mapigo
hayo..
Ufunuo 8:8 ‘Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto,kikatupwa katika bahari; theluthi ya bahari ikawa damu.9 Wakafa theluthi ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya merikebu zikaharibiwa’’.
Katika
pigo hili bado litatekelezwa na hao hao mashahidi wawili, kama vile Musa
alivyogeuza maji kuwa damu mbele ya Farao, ndivyo mashahidi hawa wawili
watageuza maji kuwa damu mbele ya yule mnyama (Ufu.11:6)..na
theluthi ya bahari itakuwa damu…theluthi inayozungumziwa hapo..ni sehemu ndogo ya
bahari yaani eneo la mashariki ya kati pale! (Bahari ya Mediterenia na maziwa
yaliyo kando kando) Eneo la mashariki ya kati Ndio litakaloathirika na mapigo
hayo kwa sehemu kubwa…mahali ambapo yule mnyama atakuwepo, kama vile kipindi
cha Farao sio maji yote ya dunia nzima yaligeuzwa kuwa damu hapana isipokuwa ni
yale tu ya Misri, ndivyo itakavyokuwa siku hizo,watu wote waliopo mashariki ya
kati, maji yatageuka kuwa damu.Na samaki watakufa na shughuli za usafirishaji
zitasimama…Huo ni mwanzo wa utungu tu wa hukumu ya Mungu itakayoijilia dunia
nzima,
Katika
siku za mwisho mara baada ya baragumu kuisha vitakuja vitasa saba, ambavyo
hivyo ndio vinabeba hukumu ya Mungu katika utimilifu wote, ndani ya hivyo
vitasa sana, maji yote ya dunia nzima yatageuzwakuwa damu, na chemichemi
haitakuwa theluthi tena kama tunavyoona hapa katika baragumu hizi.
Tuendelee..
Ufunuo 8:10 ‘Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji.11 Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalitiwa uchungu’.
Nyota
inayozungumziwa hapa sio kimondo..kwasababu haiwezekani kimondo kimoja
kiangukie mito yote na chemchemi zote za maji…Nyota inayozungumziwa
hapo ni ‘shetani’ yeye ndiye nyota iliyoanguka kutoka mbinguni..Na
kwasababu yake yeye mito na bahari na nchi vimepigwa na
vinapigwa kwa laana ya Mungu…Ndio maana ukisoma kwenye kitabu cha ufunuo 12:12, utaona inasema… ‘ Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole
wa nchi na
bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu
nyingi, akijua ya kuwa ana
wakati mchache tu’.
Unaona
hapo anasema ole wa nchi na bahari, ikimaanisha kuwa kuanguka kwa
shetani duniani, bahari itaathirika pia, itageuka kuwa damu, na maji kuwa
machungu na
katika
pigo hili…la Baragumu ya tatu…Bwana ataipiga mito na chemichemi za maji..Maji
yatatiwa
uchungu..kama yale wana wa Israeli waliyokutana nayo mahali palipoitwa ‘mara’
Kutoka 15: 22 ‘’Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa,wakisema, Tunywe nini?’’
Watu
wengi wanaokaa katika mashariki ya kati na baadhi ya maeneo
duniani..watateseka, lakini pigo hili halitauwa la dunia nzima.
Ufunuo 8: 12 ‘’Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, wala usiku vivyo hivyo’’.
Unazidi
kuona, bado ni theluthi inayopigwa sio kitu kizima…Ikifunua kuwa ni mwanzo tu
wa Utungu! Itafika wakati sio theluthi tena itakayopigwa bali yote…Malaika huyu
wanne alipopuliza baragumu lake, Jua theluthi ya jua ikapigwa…na mwezi, na kama
tunavyofahamu jua likipungua nguvu kitu gani kitatokea…ni wazi kuwa kutakuwa na
baridi isiyokuwa ya kawaida na baadhi ya shughuli zitasimama…Ndicho
kitakachotokea siku hiyo, watu wataona jua limepungua nguvu sasa hapa dunia
nzima itaathirika na pigo hili…Na hiyo Itatangaza kuwa kipindi kifupi sana
baadaye jua lote litazima..kama tutakavyojifunza tutakapofika kwenye vitasa
saba katika Ufunuo mlango wa 16.
Ufunuo 8:13 “Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwa sababu ya sauti zisaliazo za baragumu za malaika watatu, walio tayari kupiga”.
Hapa
Yohana anaoneshwa Tai akiruka katikati ya mbingu, sasa huyu Tai sio ndege tai,
bali ni mmoja wa malaika anayebeba tabia kama za Tai katika roho, ukisoma
kwenye tafsiri nyingine utaona ni ‘’angel’’ yaani
malaika ndio maana utaona hata Katikati ya wale wenye uhai wanne kulikuwa na
mmoja mwenye uso kama wa Tai.
Sasa
Malaika huyu Yohana alimwona katika roho akisema…ole wao wakaao juu ya nchi!
Kwasababu ya sauti za baragumu za malaika watatu waliobakia..Ikifunua kuwa
madhara yatakayoletwa kwa baragumu za hao malaika watatu waliosalia yatakuwa
mabaya zaidi ya hao wanne waliotangulia.
Na kama
tunavyosoma hapo, inasema ole wakaao juu ya nchi!!...Ikifunua kuwa ni madhara
yatakayosababishwa na kuanguka kwa shetani, yatakuwa juu ya hao wakaao juu ya
nchi kulingana na ufunuo 12:12 “Ole
wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu
nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu’’…Madhara juu ya bahari
yameshapita…theluthi ya bahari, chemichemi na mito kuwa damu, na viumbe vya
majini kufa…sasa yanayofuata ni kwa wale wakaao juu ya nchi..Tutayaona hayo
zaidi katika sura inayofuata..
Swali
ni je! Umempa Kristo maisha yako?..Una uhakika akija leo utakwenda naye
mbinguni?, kama hauna uhakika basi ni wazi kuwa utaachwa akija, kwahiyo utii
ushauri wake leo unaosema…
Ufunuo 3:18 “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”.
Mfungulie
mlango wa moyo wako leo kwa kutubu na kumaanisha kuziacha dhambi zako na yeye
atakupokea…Toka kwenye kamba za madhehebu ambazo zinakufungia mlango wa maarifa
na kukufanya usimjue Mungu kama anavyotakiwa kumjua.
Bwana
akubariki sana..
➔Usikose mwendelezo huu wa sura inayofuata ya 9.
Hii tafsiri haina mashiko braza. Kusema kweli ina makosa mengi ya kilokole. Hivi Shetani leo yuko mbinguni? Atatupwa chini baada ya unyakuo wa siri? Hamna kitu cha unyakuo ktk Biblia bro! Nenda kwa Wasabato watakusaidia tafsiri iliyo sahihi ya baragumu.
ReplyDelete