"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, June 24, 2019

UMEITIKIA WITO INAVYOPASWA?

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu, Taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu.

Moja ya masomo mapana sana ni ‘Namna ya kusikia sauti ya Mungu na kuielewa’..Mungu huwa anazungumza na sisi kila siku, lakini ugumu unakuwa ni namna ya kuielewa sauti ya Mungu..Ni kweli sio kila kitu Mungu atakachozungumza na sisi tutakielewa..sio kila kitu kwasababu tuna mipaka Fulani ya kiufahamu kutokana na hii miili tuliyonayo ya kidunia…lakini tutakapoivaa ile miili mipya ya utukufu basi tutamsikia na kumwelewa Mungu kwa mapana Zaidi. Lakini ni muhimu kutafuta kuisikia na kuielewa sauti ya Mungu kwa kadri tuwezavyo sasa, kwasababu Mungu kila siku anazungumza na sisi.

Zipo sababu nyingi zinazofanya tusisikie sauti ya Mungu kabisa..mojawapo ni maovu yetu (Isaya 59:1-2) na kingine ni kusongwa na mambo mengi…masumbufu ya Maisha haya…hizo ni kama kelele masikioni mwetu zinazozuia tusisikie sauti ya Mungu…Unapokuwa unasongwa na sauti nyingi nyingi za mambo ya ulimwengu huu inakuwa ni ngumu sana kuisikia sauti ya Mungu, mtu anayejihusisha na utazamaji wa movies muda mrefu, anakuwa anajisikilizisha sauti nyingine ambazo zinazuia masikio yake kusikia sauti ya Mungu…ni sawa na Mtu aliyeweka earphones kwenye masikio yake…hawezi kusikia sauti ya mtu anayezungumza naye akiwa nje…au kama ataisikia ataisikia kwa mbali sana…au anaweza akasikia isivyopaswa.

Kadhalika mtu anayekuwa katika shughuli nyingi za utafutaji wa mali kuanzia asubuhi, mpaka jioni anafanya hivyo siku saba katika wiki na miezi 12 katika mwaka..ni ngumu sana kuisikia sauti ya Mungu ikizungumza naye..purukushani za huku na kule za Maisha, anakutana na watu hawa, wale..anakumbana na tatizo hili au lile, watu hawa wanamweleza hivi au vile n.k hiyo inazuia sana kuisikia sauti ya Mungu.

Lakini leo hatutaingia sana huko. Leo tutajifunza ni kwa namna gani tunaweza tukaitikia vyema wito wa Mungu..yaani wakati Mungu anapotuita.

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa, Mungu anapozungumza sio kama wengi wetu tunavyotazamia..kwamba atazungumza nasi kwa radi mbinguni au mingurumo, au tutasikia sauti Fulani ya kipekee ya ajabu ikitunong’oneza masikioni. Inaweza ikatokea hivyo lakini hiyo sio njia ambayo Mungu anaitumia kusema na watu siku zote…wengi wanaitafuta hiyo njia lakini Mungu hatumii njia hiyo, sauti ya Mungu inapokuja ni kama ‘’mawazo Fulani yanaingia ndani yako ambayo yanakuwa yanakupa ufunuo fulani’’..Mawazo Fulani yanayokufumbua macho ya kuelewa jambo Fulani ambalo ulikuwa hulielewi au ulikuwa hulijui. Na hayo mawazo yanakuwa ni kama vile wewe umeyatengeneza…unaweza ukadhani ni wewe unajiambia mambo hayo, lakini sio wewe ni Bwana anazungumza na wewe…Sauti yake wakati mwingine inafanana na sauti yako kabisa, isipokuwa ya Mungu inakuja na ufunuo Fulani wa kimaandiko, ambao huo ukiupata unasikia kusisimka katika roho, unajisikia furaha kulijua hilo jambo, unajisikia amani, unajisikia kumgeukia Mungu Zaidi na kumpenda…unajisikia kutolewa sehemu moja hadi nyingine kiimani…Hiyo ni sauti ya Mungu imezungumza na wewe. Na mara nyingi hii inakuja ukiwa sehemu ya utulivu sana ukimtafakari Mungu, au ukiwa katika kulisoma Neno lake. Kwa jinsi unavyokuwa mtulivu zaidi na kulitafakari Neno la Mungu zaidi ndivyo wigo mpana wa kuisikia sauti ya Mungu unavyokuja.

Pia licha ya sauti ya Mungu kufanana sana na sauti yako, lakini pia inafanana na sauti ya Mtu mwingine ambaye yupo karibu na wewe kiimani..Mtu anaweza kuzungumza na wewe Neno Fulani la kiMungu ukaona limekupa msisimko fulani ndani yako ya kutaka kumjua Mungu Zaidi, au kumpenda Mungu, au kumtafuta..Huyo ni Mungu anazungumza na wewe, ingawa unaweza kudhani ni yule mtu kazungumza na wewe, lakini kiuhalisia si Yule mtu bali ni Mungu.

Unaweza pia kuwa katika utulivu..Bwana akaanza kuzungumza na wewe kupitia mahubiri ambayo ulishawahi kuyasikia huko nyuma, ukasikia kabisa kama vile yule mtu anakuhubiria masikioni mwako saa hiyo…ukapata kufunguliwa macho na kuona kitu kipya ambacho ulikuwa hukijui…Sasa huyo ni Mungu anazungumza ndani yako kupitia sauti ya yule Mtumishi uliyemsikia. Na kwasababu bado hujaijua sauti ya Mungu wewe utadhani ni yule mtumishi anazungumza na wewe na hivyo utatafuta njia yoyote ya kwenda kukutana naye au kujiunga katika dhehebu lake au kanisa lake..

Lakini nataka nikuambie hapo utakuwa hujaitikia vyema wito wa Mungu. Ingawa uliisikia kweli sauti ya Mungu. Lakini huko uendako unakwenda kupotea….Hebu tujifunze kidogo katika maandiko juu ya jambo hilo.

1 Samweli 3: 1 ‘Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.
2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),
3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;
4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.
5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.
6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.
7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.
8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.
9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.
10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.
11 Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.
12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho.
13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.
14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.’’
Katika habari hiyo tunamwona kijana Samweli…Na siku moja Mungu alipotaka kujifunua kwake, hakuzungumza naye na sauti mpya ya ajabu ya kipekee…bali alizungumza naye moyoni mwake na sauti inayofanana kabisa na ile ya Eli…’yaani kwa ufupi aliisikia sauti ya Eli ikimwita’..Na yeye kwasababu alijua Eli ni Mtumishi mteule wa Mungu, aliyechaguliwa na Mungu atumike katika nyumba ya Mungu…aliitikia wito isivyopaswa akamfuata Eli kwasababu tu ile sauti aliyoisikia ilikuwa kama ya Eli..akaenda kwa Eli lakini hakukipata kile alichokuwa anakitafuta kwa maana alitegemea aambiwe sababu ya kuitwa kwake lakini hakuambiwa..Akarudi kulala tena…akaisikia ile ile sauti kama ya Eli ikimwita mara tatu, bado akarudia kosa lile lile la kwenda kumfuata Eli mpaka Eli alipomsaidia kupata ufahamu kuwa Sauti aliyoisikia sio ya Eli ni ya Mungu, japokuwa inafanana na ya Eli mtumishi wa Mungu.