"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, June 21, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 66

SWALI: Ninafahamu kwamba, watu waliokua wanakusanya vitabu/maandiko matakatifu kwa lengo la kuandaa BIBLIA, walikua wakiongozwa na ROHO MTAKATIFU Mwenyewe. Ili kitabu au maandishi yachaguliwe, waliangalia vigezo gani?-sababu na sikia, kuna baadhi ya vitabu havikuchukuliwa -Mfano Injili ya petro , na ya Tomaso.
JIBU: Hiyo ipo wazi kabisa kila kitabu cha biblia cha mwandishi yoyote tunayemsoma kimevuviwa na Roho Mtakatifu, hali kadhalika pia kuwepo kwa idadi ya vitabu 66 katika biblia hilo nalo ni tendo lililovuviwa na Roho Mtakatifu na wala sio wazo la kibinadamu kama wale ambao sio-wakristo wanavyofikiri. Ni mpango ambao Mungu alishaupanga kabla hata ya kuwekwa misingi ya dunia.
Lakini siku zote Mungu huwa anamtumia “mtu” kutenda kazi japo sio kwamba hawezi kutenda pasipo hao hapana bali huo ni utaratibu wake tu aliojiwekea yeye(ndivyo ilivyompedeza). Sasa tukirudi katika agano la kale, kukusanywa vitabu vile vyote 39, Mungu alitia hekima kwa wayahudi washindania Imani wakati ule,waliomcha Mungu, waliokuwa wasomi na wafuatiliaji wazuri wa unabii na historia ya taifa la Israeli kwa ujumla, hivyo kwao haikuwa kazi kubwa, kuvihakiki vitabu vya manabii waliowatangulia, Hivyo wale waliokubalika na habari zao zilithibitika kuja kutokea kweli,.Kwamfano vitabu vya torati ya Musa, ni vitabu ambavyo havikuwa na tashwishwi yoyote kwa wayahudi kwani ni vitabu vinavyoeleza chimbuko lao na vimepita kizazi hadi kizazi havijapotea tangu siku vilipoandikwa..
Vile vile Ukiangalia vitabu kama Esta,Ruthu,Wafalme, n.k. ni vitabu vya historia ambavyo vinaeleza habari zilizohalisi kabisa, vile vile vitabu vya manabii kama Isaya, Yeremia,Danieli vyote hivyo ni vitabu vilivyothibitika kuwa ni Vitabu vya wakati wote, na unabii wake ni thabiti ambao watu walikuwa wanawaona. Na kwa kuzingatia hayo ndio vikapatikana vile vitabu 39 vya Agano la kale. 
Lakini katika agano jipya, utaona kulikuwa pia kuna vitabu ambavyo vilishakubalika tangu kanisa la kwanza. Kwamfano nyaraka za mtume Paulo zilikuwa zinatumiwa tayari na watakatifu wa makanisa yote yaliyokuwa Asia wakati ule kabla hata yeye hajaondoka, nyaraka zake zilikuwa zinazungushwa toka kanisa hadi kanisa..tunasoma hilo katika Wakolosai 4:16 “Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi”…Kwahiyo haikuwa ngumu kuendeleza utaratibu huo mpaka kwa makanisa ya mbeleni.
Vile vile utaona mtume Paulo, pia akirejea baadhi ya vifungo ambavyo vilikuwa katika vitabu vya Injili mfano Injili ile ya Luka, soma (1Timotheo 5:18b,linganisha na Luka 10:7) utalibitisha hilo kuwa kumbe hata Paulo alishapokea vitabu vya Injili kama sehemu ya maandiko matakatifu ya kurejea hiyo ni kuonyesha kuwa vitabu vya Injili vilikuwa tayari vimeshapokewa kama sehemu ya maandiko matakatifu ya wakati wote tangu kanisa la kwanza.
Sasa baadaye watu kama wakina Klementi wa Rumi , Ignatusi wa Antiokia na Polikapi na wengine wakaja kutaja vitabu vingine. Na baadaye tena mabaraza kadhaa yaliitishwa ili kuthibitisha Uvuvio wa vitabu hivyo Na vigezo walivyokuwa wanatumia, ni kama vifuatavyo.. 
1) cha kwanza je! Mwandishi wa kitabu husika alikuwa ni mtume au alikuwa na uhusiano wa karibu na mitume.
2) Je! Kitabu husika kinakubalika na kanisa kwa ujumla.
3) Je! Kitabu kinabeba mafundisho halisi na ya msingi (kumtambua Yesu Kristo kama kiini cha Imani)?
4) Je! Kitabu hakivunji miiko na kanuni za rohoni ambazo zinathibitishwa na kazi ya Roho Mtakatifu mwenyewe?.
5) Kitabu lazima kiwe kwa sehemu Fulani kimenukuu vitabu vingine vya agano la kale..Kwamfano unaona nyaraka za Paulo nyingi zilinukuu vitabu vya Zaburi,Ayubu na Mwanzo..
Hivyo baraza la mwisho ambalo lilihitimisha kuwepo kwa vitabu 66 vya Biblia vilivyovuviwa, lilifanyika mwaka 397WK. Na ndio vitabu tulivyonavyo sasa.
Lakini kumbuka kama tulivyosema kazi ya vitabu vya biblia kuwa 66 sio mwanadamu alipanga, hata ingekuwaje, kwa namna yoyote ile, kwa kupitia hatua hizo au nyingine zozote biblia ingetufikia tu kwa ukamilifu wake wote. 
Ubarikiwe.

SWALI: Biblia inaposema "heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao" hawa maskini wa roho ndo watu gani? je hatuna ruhusa ya kuwa matajiri katika roho?.
JIBU: Maskini ni mtu ambaye yupo katika hali ya kutojitosheleza, Sasa Bwana aliposema “heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao”, hakumaanisha kuwa HERI wale wasio na maarifa yoyote au ufahamu wa mambo ya rohoni (yaani watu wasiomjua Mungu), hapana bali alimaanisha heri wale ambao kila siku wapo katika hali ya uhitaji wa kufahamu mambo ya ufalme wa mbinguni, watu ambao hawajajikinai, watu ambao kila siku wanatamani kuongeza kitu kipya katika maisha yao ya rohoni, watu wenye kiu na njaa ya kumjua Mungu kila siku…Hao ndio Mungu anawaona ni maskini wa roho ambao kila siku wanamlilia yeye BABA, tupe! Tupe! Chakula cha rohoni.. 
Lakini kuna wengine hawana haja tena ya kujua zaidi mambo ya rohoni, tayari wameshahitimu, pengine labda kwa kuwa walipitia vyuo vya biblia, au wameshasoma sana maandiko, hivyo wanajiona sasa wanajua kila kitu, hawana haja tena ya kujifunza, hata wakiletewa habari ya mpya wanadharau moyoni mwao wanaona kwamba hakuna chochote huyu mtu anaweza kuniongezea? Ndivyo ilivyokuwa kwa wale waandishi na mafarisayo. Hawakutaka kukaa chini kumsikiliza maneno ya YESU walimdharau na kumwona si kitu tofauti na yale makutano walimsikiliza kwasababu ndani yao kulikuwa na kiu na njaa na shauku ya kumjua Mungu zaidi na zaidi, na ndio maana Bwana Yesu akazungumza maneno yale.
Ikiwa wewe unajiona hapo katika dhehebu lako ndio umefika, na hivyo huna haja ya kuambiwa chochote hata kama kinatoka kwenye maandiko basi fahamu kabisa kuwa upo mbali sana na ufalme wa mbinguni.
Ufunuo 3:17 "Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona."
Mtume Paulo mpaka anafikia uzee wake, anakaribia kufa pamoja na kwamba Mungu alimfanya kuwa askofu wa mataifa yote, mwenye heshima duniani kote katikati ya waaminio, mtu ambaye Mungu alimpa mafunuo makubwa ambaye hata sasa nyaraka zake tunazitumia kama MUAMALA lakini mpaka dakika ya mwisho anamwagiza Timotheo kwamba siku akimfuata vifungoni mwake asiache kumpelekea vile vitabu vya ngozi ili azidi kujifunze zaidi,(2Timotheo 4:13) inatupasaje sisi?… Huo ni mfano mzuri wa mtu aliye maskini wa roho, haridhiki sehemu alipo, haridhiki na kile alichonacho au alichopewa katika dhehebu lake au dini yake, kila siku anataka zaidi na zaidi amjue Mungu…Sio ajabu mtume Paulo aliandika hivi:
1Wakorintho 8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.”
Hivyo tupende kila siku kutamani kupiga hatua moja zaidi rohoni, na hiyo inakuja kwa kutokukinai kujifunza Neno la Mungu kila siku.
Ubarikiwe sana.
 SWALI: Nina swali kuhusu alama ya mnyama, kulingana na baadhi ya injili zinazohubiriwa ni kuwa ..alama ya mnyama itapimwa kwa siku ya kuabudu, yani wale watakaokubali kusali jumapili wote watakuwa wamepokea 666, ikimaanisha kuwa Papa atatangaza siku moja tu ya kuabudu iwe jumapili dunia nzima, lengo likiwa kuvunja amri ya nne itunze siku ya saba, kwahyo amri ya papa itakapopita itapiga 666 kwa wote watakaokubaliana nayo, wana refer maandiko ya ufunuo sikumbuki ngapi KUWA ATABADILI MAJIRA NA SHERIA.

JIBU: Shalom ndugu, Ni kweli kabisa wapo wanaoamini kuwa Papa atageuza MAJIRA NA SHERIA kulingana na Danieli 7:25….Lakini ukijifunza biblia utagundua kuwa majira yanayozungumziwa hapo sio siku moja maalum itabadilika…hapana! Kwasababu majira ni Neno pana na la wingi ambalo linaweza kuwa kipindi Fulani cha muda…labda cha siku kadhaa, wiki, miezi au miaka kadhaa…kinachoambatana na tukio Fulani.

Ili tuelewe vizuri hebu tuchukue mifano kadhaa ya kwenye biblia..

Luka 21: 7 ‘’Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? 8 Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, MAJIRA YAMEKARIBIA. Basi msiwafuate hao’’.

Katika mstari huo unaona neno MAJIRA lilivyotumika hapo, sio kipindi cha SIKU MOJA MAALUM ambacho kitafika watu watakuja kwa jina lake na kusema wao ndio…Utaona sio tafsiri yake hiyo, bali majira ilivyotumika hapo ni kwamba ‘itafika kipindi Fulani cha muda’ ambacho hakijulikani kitadumu kwa muda gani ambapo watatokea manabii wa uongo wakija kwa jina la Yesu…Na hicho kipindi ndio hichi tunachoishi sasa,

Pia tunaweza kujifunza katika huu mfano mwingine Bwana alioutoa..

Luka 12: 54 ‘’Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.
55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua MAJIRA haya?’’
Unaona hapo tena?...Majira yanayozungumziwa hapo ni kipindi Bwana Yesu alichokuwepo duniani akihubiri na kufundisha njia za haki…ni majira ambayo makutano walishindwa kufahamu kuwa Masihi yupo ulimwenguni…Na majira hayo ni kipindi cha miaka mitatu na nusu Bwana aliyokuwa anahubiri..na sio siku Fulani moja maalum.

Pia mfano mwingine ni huu..Kutoka 21: 18 ‘’Watu wakigombana, na mmoja akimpiga mwenziwe kwa jiwe, au kwa konde, asife, lakini yualazwa kitandani mwake;atakapoinuka tena na kuenenda nje kwa kutegemea fimbo, ndipo hapo yule aliyempiga ataachwa; ila atamlipa kwa ajili ya hayo majira yake yaliyompotea, naye atamwuguza hata apone kabisa..’’..Hapo pia utaona ‘majira’ sio siku moja maalumu bali kipindi cha muda.

Kadhalika pia tunaweza kujifunza mfano huu wa mwisho maana ya majira..
Luka 21: 29 ‘’Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti mingine yote.
30 Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba MAJIRA YA MAVUNO yamekwisha kuwa karibu.
31 Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.’’

Unaona majira ya mavuno yanayozungumziwa katika maandiko sio siku moja MAALUMU, kama wasabato wanavyodhania, bali ni kipindi Fulani cha mavuno ambacho kinaweza kuwa ni siku kadhaa, au wiki kadhaa…Ipo mifano mingi unaweza ukapitia Pia (pitia Luka 21:54-55, Luka 21:23-25, Luka 19:41-44 utaelewa zaidi juu ya jambo hilo).

Kwahiyo tukirudi pale kwenye danieli 7:25…Kwamba Mpinga kristo atabadili ‘’majira na sheria’’ biblia haikumaanisha kuwa mpinga kristo atakuja kubadilisha siku moja ya kuabudu Jumamosi na kuwa jumapili…Hapana bali MAJIRA yatakayobadilika hapo ni MAJIRA YA mafumo mzima wa maisha, kutoka kuwa ya amani na kuwa ya dhiki, huwezi kununua wala kuuza bila ile chapa…wakati huo Majira ya Neema yatakuwa yameisha na sasa ni majira ya dhiki kuu….yatakuwa ni majira ya mavuno..na hayo hayatakuwa siku moja hapana ni kipindi fulani cha muda ambacho kitadumu miaka mitatu na nusu…Kwahiyo mfumo wake mpya wa umoja wa dini na madhehebu yote ndio utakaobadili majira ya ulimwengu mzima..

Kama vile ujio wa Kristo ulivyobadili majira kutoka majira ya utumwa wa dhambi na sheria na kutuingiza katika majira ya Neema na uhuru wa roho, kadhalika baada ya unyakuo wa kanisa kupita Mpinga Kristo ataiingiza dunia katika majira mapya ya dhiki kuu na ghadhabu ya Mungu.

Kumbuka sasahivi tunaishi kipindi cha majira ya Neema ya Kristo, ambacho kinajulikana kama kipindi cha MAJIRA YA MATAIFA.(ukisoma Luka 21:24 utaona jambo hilo) Na kipindi hichi kitaishia na unyakuo.

Hivyo fundisho la wasabato linalosema kutotunza sabato, ndio kupokea alama ya mnyama, ni fundisho potofu na linapaswa liepukwe kwasababu halina msingi wowote wa kimaandiko.

Bwana akubariki sana.

SWALI: Bwana alimaanisha nini kusema JIKANE mwenyewe?.

JIBU: Neno kujikana linamaana kuwa, ‘kukataa matamanio yako binafsi au malengo yako kwa sababu fulani’. Hivyo kujikana kunakozungumziwa katika biblia ni kujikana kwa Kristo. Hii ikiwa na maana kuwa unapoamua kumfuata Kristo unakuwa tayari kuyakataa matamainio yako hata kama ni mazuri kiasi gani, hata kama yanatia maanani kiasi gani, unayaweka chini na kukubali kuyafuata yale ya Bwana Yesu tu.

Na ndio maana mtume Paulo aliweka wazi na kusema hivi:

“..Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.
8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;(Wafilipi 3:7-8)”.

Unaona hii ni nguzo kuu na ya muhimu sana, inayomtambulisha mtu kama amemfuata Kristo. Wanaotubu dhambi zao ni wengi lakini wanaodhamiria kumfuata Kristo ni wachache sana.

Unapoamua kuwa binti wa kikristo, uwe tayari kuukana uzui wako, na kuacha kuvaa vimini na suruali, nguo za kikahaba, na mapambo ya kiulimwengu…ili ufanyike mwanafunzi wa Yesu vinginevyo bado hujawa mkristo hata kama utasema umeokoka. Vile vile kijana unapokuja kwa Kristo uwe tayari kukataa tamaa zote za ujanani, disco, miziki ya kidunina, pombe na sigara, uasherati, unavipiga vita unaamua kumwangalia Kristo kuanzia huo wakati na kuendelea. Ni mambo ambayo ungeweza kuyafanya kama vijana wengine katika ujana wako lakini unajikana kwa ajili ya kuujua uzuri ulio katika Kristo. Na Bwana Yesu akishaona huo moyo wako hapo ndipo na yeye anapochukua nafasi ya kukufanya kuwa mtu mwingine wa tofauti kabisa katika viwango vya rohoni. Unafanyika kuwa mwanafunzi wake kweli kweli kama mitume wake.

Na hili ni tendo endelevu ambalo linapaswa liwe kila siku, hata katika kuifanya kazi ya Mungu unapaswa ujikane mwenyewe, muda ambao ungetakiwa kufanyabiashara kama watu wengine wewe unaifanya kazi ya Mungu, Vilevile tumeagizwa tudumu katika sala, wakati ambao ungepaswa ulale usiku kama watu wengine wewe unaamka kuomba, huko ni kujikana nafsi. Bwana anakokuzungumzia.

Lakini pamoja na hayo katika kujikana huko, na kupoteza matamanio yako au vitu vyako kwa ajili ya Kristo yeye mwenyewe anatuambia, kwa kufanya hivyo ndivyo tunavyozipata. Kwa Mungu hakuna matujo kwani sikuzote mawazo anayotuwazia sisi na ya amani wala sio mabaya ili kutupa sisi tumaini zuri katika siku zetu za mwisho(Yeremia 29:11). Na ndio maana hatuoni shida hata anapotuambia tuache kila kitu kwa ajili yake. Faida yake tutaiona kama sio katika ulimwengu huu basi katika ulimwengu unaokuja. Kwasababu anatuwazia kusudi jema siku zote.


Hivyo, Ni heri uonekane unapoteza kila kitu sasa kwasababu tu umeamua kumfuata Kristo, kuliko kupata kila kitu cha ulimwengu huu na mwisho wa siku unaishi katika ziwa la moto, itakufaidia nini?.

Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na AJIKANE MWENYEWE, ajitwike msalaba wake, anifuate.
25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. 26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?”.

Ubarikiwe.

SWALI: Kuna jambo linanichanganya naomba msaada pale Biblia inaposema “Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.(Matendo 10:15)”.Je kauli hii inatupa uhalali wa kula kila kitu?.

JIBU: Kauli hiyo ilitoka kwa Mungu mara baada ya Petro kupewa maono yale ya lile shuka kubwa lililoshuka kutoka mbinguni likiwa limebeba viumbe vya kila aina najisi na safi akaambiwa avichinje ale,.Lakini Petro saa hiyo hiyo akamjibu Mungu akamwambia Mungu sijawahi kula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi katika maisha yangu yote..Ndipo Mungu akamwambia “Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi”. Ufunuo huo japo Petro alipewa kumaanisha sisi watu wa mataifa ambao hapo kwanza tulikuwa tunaonekana najisi mbele ya waisraeli, lakini Bwana alipokuja alitutakasa wote kwa damu yake hivyo sisi watu wa mataifa sio najisi tena….na hivyo Mungu hawezi kuwatakasa wanadamu walio chanzo cha uovu wote asiwatakase Wanyama ambao sio wao waliofanya makosa, kwahivyo Wanyama nao wametakaswa hakuna kilicho najisi tena…. Kwahiyo ono lile Petro aliloonyeshwa ni Ufunuo mkubwa sana unaoonyesha wazi wazi kuwa mbele za Mungu hakuna kiumbe chochote kilichonajisi msalaba umefumbua hilo fumbo….Ikimaanisha kuwa viumbe vile ambavyo hapo mwanzo vilikuwa haviliwi sasa vyote vinaweza kuliwa, na sisi watu wa mataifa ambapo hapo kwanza tulikuwa hatustahili kumjua Mungu wa Israeli(tulikuwa najisi) sasa ni Taifa teule la Mungu.

Utaona jambo hilo hilo Mtume Paulo akilirudia sehemu fulani na kusema amehakikishiwa na Mungu kabisa hakuna kitu chochote kilichonajisi kwa asili yake Ukisoma Warumi 14:14 “Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.”

Lakini kumbuka pia kauli hiyo haijatupa ruhusa ya sisi kuwa walafi, biblia hiyo hiyo inasema japo vitu vyote ni halali lakini si vyote vifaavyo kwa mtu,(1Wakoritho 6:12), Kumbuka hata wanyama wale au vyakula vile vinavyokubalika na wengi na vinavyoonekana kuwa ni safi, bado vinaweza visimfae mtu mmoja mahali Fulani, Sio wote wanapenda nyama ya samaki, si wote nyama ya ng’ombe inawakubali, si wote nyama ya kuku inawakubali, si wote maziwa yanamanufaa mwilini mwao, sasa mtu kama huyo akila na kusema kuku imekubaliwa kwenye maandiko ngoja niishambulie, baadaye ikishamsumbua anaanza kulalamika, lakini ameshindwa tu kutumia hekima kufahamu neno hili “vyote ni halali lakini si vyote vifaavyo”..

Vilevile ukila nyoka, au panya, au mjusi, au mende, kama hicho ni chakula kinachokubalika na jamii yenu na wewe pia unakipenda na hakikuletei madhara yoyote mwilini mwako,
Hakuna shida yoyote kula tu hata vipepeo, na kinyonga ilimradi uvipokee kwa shukrani [yaani kwa kumaanisha](1Timotheo 4:3), Na sio kwa ulafi, kisa tu vimehalalisha vyote.

Bwana akubariki

No comments:

Post a Comment