"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, June 21, 2019

MFALME ANAKUJA.


Watu wengi wanadhani makao ya watakatifu yatakuwa ni mbinguni milele, yani siku ile ya mwisho dunia itakunjwa kunjwa na kutupwa motoni, halafu sisi tutakwenda kuishi na Mungu mbinguni milele, Ni wazi kuwa jambo hilo sio la kimaandiko kabisa, Biblia inatufundisha kuwa tutakaa mbinguni miaka saba tu! Kisha tutarudi kutawala na KRISTO hapa duniani Milele.
Mungu alivyotuumba sisi wanadamu ni tofauti kabisa na alivyowaumba malaika, Utukufu Mungu aliouweka kwetu sisi, haufanani na ule wa malaika zake, Sisi tumeumbiwa miili, sisi tumeumbiwa kumiliki, sisi tumeumbiwa kutawala, na hivyo tutamwabudu Mungu katika njia hiyo hiyo. tofauti na malaika, Ndio maana Adamu mtu wa kwanza alishushwa hapa duniani, ili kutimiliza hayo makusudi. Alishushiwa mbingu yake hapa chini.

Lakini alipoasi ndipo alipofanya dunia ionekane kuwa sio sehemu ya kutamaniwa tena kuishi kwa watu, lakini ashukuriwe Mungu, vitu vyote vitakuja kurejeshwa katika uhalisia wake moja ya hizi siku.

Biblia inaposema Dunia inapita na tamaa zake zote (1Yohana 2:17), Haimaanishi kuwa Dunia itateketezwa na kuondolewa kabisa hapana bali Inaamisha kuwa Ulimwengu huu uliopo ndio unaopita na ndio utakaoteketezwa, mambo yote tunayoyaona, falme zote unazoziona, shughuli zote unazoziona na tunazozifanya, ustaarabu wote uliopo duniani leo hii, serikali zote na mamlaka yote hakuna hata mmoja kitakachosalia, vyote hivi vitaondoshwa kupisha majira mengine kuanza. Na ndio maana tunaambiwa tuishi kama wapitaji, kwasababu vitu tunavyovisumbukia havituwekei kumbukumbu la milele.

Leo hii unaipenda dunia, unapenda kuwa na maisha mazuri, unapenda kufanikiwa na kuwa tajiri na ndio maana unatafuta mali kwa nguvu zote, Unafanya hivyo ni ili uishi maisha mazuri na ya raha hapa duniani. Ni wazi kuwa hakuna mtu ambaye anaufurahia umaskini, kila mmoja anatamani awe na mafanikio makubwa, na hiyo ndiyo inayombidiisha afanye kazi kwa bidii. Lakini jifunze pia kukaa chini kutafakari nini kusudi la maisha, usiishi tu kama mnyama, hutaki kujua umetokea wapi na unakwenda wapi, badala yake unajitaabisha sana kujitashirisha.. mwisho wa siku unakuwa kama Yule mtu Bwana aliyemtolea mfano baada ya kufanikiwa sana kwa shughuli zake, sasa anatulia ili aiburudishe nafsi yake, lakini usiku ule ule waliitaka nafsi yake.

Ndipo Bwana akasema na zile mali alizozisumbukia zitakuwa za nani?(Luka 12:16) Unaona, ni muhimu kujua maisha unayopitia leo iwe ni katika vingi au katika vichache je! inafunua nini katika ulimwengu wa roho?.

Sasa Mungu karuhusu tuyaonje hayo, kama kivuli cha huo ufalme mwingine mkuu sana utakaokuja huko mbeleni. Kwamba watu hawatakuwa sawasawa kutakuwa na matajiri sana na vilevile kutakuwa na watu wa kawaida sana. Ufalme huo ambao utashuka hapa mara baada ya siku ile kuu ya Bwana kupita duniani, Yesu atakapotokea katika mawingu pamoja na watakatifu wake aliokuwa amewanyakua zamani, sasa wakati huo dunia itakuwa imeshasafishwa, na shetani ameshafungwa kwenye lile shimo la kuzimu kwa muda wa miaka 1000, dunia kuanzia huo wakati itakuwa Paradiso kama hapo mwanzo, Ustaarabu mpya wa kimbinguni utaanza kutenda kazi duniani, YESU KRISTO akiwa kama Mfalme wa wafalme, na Bwana wa Mabwana, ikimaanisha kuwa atakuwa na wafalme wengi sana chini yake na mabwana wengi sana chini yake, na makuhani wengi sana chini yake, ili kutumiza pamoja nao kazi ya ufalme wa Mungu Baba.(Ufunuo 1:6)

Nafasi hizo hazitakuwa za kila mtakatifu, hapana bali kila mmoja atalipiwa kulingana na matendo yake na taabu yake hapa duniani, kama wewe maisha yako yote yalikuwa ni ya ulevi, mpaka uzee wako ndio unamrudia Bwana, ukifika kule hutakuwa sawa na Mtume Paulo. Maisha tunayoishi sasa kwa Kristo ndio yanayotuleza kule tutakuwa nani.
Wakati huo ukifika kutakuwa na majuto mengi sio tu kwa watu waliokufa katika dhambi, hapana bali pia kwa watakatifu wakijutia kwanini hawakufanya zaidi kwa kujiwekea hazina katika huo ufalme wa milele wa Yesu Kristo utakaoshuka duniani.

Sasa kutakuwa na shughuli nyingi sana, na mambo mengi sana yatakayokuwa yanaendelea kule, na tunasoma baadaye hizi bahari zote zitakuja kuondolewa, leo hii ni 21% tu ya dunia inakaliwa na wanadamu sehemu nyingine zote ni maji na pamoja na hayo bado haijajazwa, sasa wakati huo habari hazitakuwepo Eneo la makazi ya watu litaongeza na haya mabara basi yatakuwa si chini ya 30, leo hii yapo 7 tu,na kote huko kutakuwa ni miji mikubwa, na makazi yaliyobuniwa mbinguni. kutakuwa hakuna magonjwa wala laana, wala wachawi, wala ajali, tutumwabudu Mungu katika makazi hayo milele na milele.

Kwa mambo makuu yote hayo utajisikiaje unakuwa mtu wa kawaida kule milele?, Ukitaka kufahamu vizuri utakuwa katika hali gani jijengee picha sasahivi, katika hali uliyopo, ujifananishe labda na Raisi, au Waziri, au mtu Fulani aliye na mali nyingi, uone tofauti yake na yako jinsi ilivyo kubwa, mambo mengi unavyoyakosa ndivyo itakavyokuwa kule, tofauti tu ya huku na kule, ni kwamba huku unaishi bado katikati ya hatari na shida na bado ni kwa kipindi kifupi tu, lakini kule Ukiwa umepewa mamlaka na YESU ni mamlaka ya milele na milele isiyokuwa na mwisho, hakutakuwa na kupandishwa cheo wala kushushwa cheo,Karama za Mungu hazina majuto…Ni afadhali tukose kila kitu hapa, lakini kule tukapate kila kitu.

Na ndio maana tunashauriwa tukiwa hapa duniani tuukomboe wakati, kwa kutafuta kujua mapenzi ya Mungu hasa ni nini kwetu. kwa jinsi ile ile tunavyohangaika kutafuta mambo ya ulimwengu huu, ni wakati sasa wa kupeleka nguvu zetu nyingi zaidi kutafuta mambo ya ufalme wa mbinguni unaokuja wa milele wa Yesu Kristo Bwana wetu …Kwasababu huko ndiko ndio kuna maisha. Haleluya.

Kumpa Yesu maisha yetu tu haitoshi, ni lazima tufanye na kitu cha ziada, safari ndio inaanza…tujiwekee hazina kule, kwa kufanya mapenzi ya Mungu na kuitenda kazi yake kwa uaminifu. Bwana anasema hivi.
Ufunuo 22:10 “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.
11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.
12 TAZAMA, NAJA UPESI, NA UJIRA WANGU U PAMOJA NAMI, KUMLIPA KILA MTU KAMA KAZI YAKE ILIVYO.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.”
Napenda umalizie kwa kusoma habari hii, kisha sasa uanze kuchukua hatua kuanzia leo….

Luka 19:12 “Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.
13 Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.
14 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.
15 Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.
16 Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.
17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.
18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.
19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.
20 Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.
21 Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.
22 Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;
23 basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?
24 Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.
25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.
26 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.”

Mfalme anakuja.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment