"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, July 6, 2019

AGIZO LA UTUME.


Utukufu na heshima una Bwana wetu Yesu Kristo, milele na milele…
Karibu tutafakari pamoja Neno la Mungu, naamini kuna kitu cha kipekee Bwana alichotuandalia mezani pake siku ya leo.

Kwa ufupi sana leo tutajifunza juu ya “Agizo la Utume, Paulo alilopewa na Bwana Yesu Kristo mwenyewe”.
Kama wengi wetu tunavyojua kuwa sehemu ya kwanza ambayo inamwelezea Paulo jinsi alivyotokewa na Bwana njiani haikueleza kwa mapana na marefu ni maneno gani aliyoambiwa na Bwana Yesu, inaishia kusema tu! Simama uingie mjini utaambiwa yakupasayo kufanya…tusome.
Matendo 9:3 “Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.
4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?
5 Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.
6 Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.
7 Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.
8 Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.
9 Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi”.
 
Kama tunavyosoma haielezei kwa mapana, Bwana alimwambia nini Paulo kuhusu kusudi la kumtokea…lakini tukizidi kukisoma kitabu hichi cha Matendo ya mitume, karibia na sura za mwisho mwisho tunaweza kuona ujumbe Bwana aliompa Paulo siku ile alipomtokea njiani…
Matendo 26:13 “….ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.
14 Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.
15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.
16 Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako;
17 nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao;
18 uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi”.
Unaona katika habari hiyo Mungu alimwambia Paulo mambo makuu manne.

1) Uwafumbue watu macho yao.
2) Awageuze waiache giza na kuielekea nuru.
3) Waziache na nguvu za shetani na kumwelekea Mungu.
4) Kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.

Hakuna sehemu hapo Bwana anamwagiza Paulo, akawafanye watu wawe washirika wa kanisa lake..au akawafanye watu wawe wa kuombewa tu! Au awahubirie Utajiri na mafanikio..bali unaona anaambiwa akawafumbue watu macho…Kufumbuliwa macho maana yake kuonyeshwa ni kitu gani kipo mbele yako huko unakokwenda usichokijua! Na kitu gani kilikuwepo huko unakotoka usichokijua, Na ni kitu gani kipo hapo ulipo usichokijua….Ndio maana alizungumza maneno haya katika moja ya nyaraka zake.

Pili aliambiwa awafundishe watu waiache giza waigeukie Nuru, kuacha giza maana yake ni kuacha matendo yote ya giza, kama uasherati, ulevi, wizi, uongo,uchawi, n.k. Alisema maneno haya mahali Fulani…
Waefeso 5:6 “Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi.
7 Basi msishirikiane nao.
8 Kwa maana zamani ninyi MLIKUWA GIZA, BALI SASA MMEKUWA NURU KATIKA BWANA; enendeni kama watoto wa nuru,
9 kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli;
10 mkihakiki ni nini impendezayo Bwana.
11 Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;”
Tatu aliagizwa awageuze watu waziache nguvu za shetani na kumgeukia Mungu: zingatia hilo Neno ‘waziache’ sio wakaombewe! Wengi sasahivi wanatafuta kwenda kuombewa waache uasherati, au uchawi, au wizi, utasikia mtu anakuambia niombee niacha uasherati!…Ndugu hivyo vitu haviwezi kuondoka kwa kuombewa peke yake kama wewe mwenyewe kutoka moyoni mwako hujakusudia kuviacha…hata uombeweje haviwezi kuondoka kama hujakata shauri..Maana ya kutubu ni kuacha kile ulichokuwa unakifanya hapo kabla…sio tu kuomba msamaha peke yake! Hapana msamaha lazima uambatane na vitendo. Unapotubia uasherati maana yake unaachana na huyo mtu unayetembea naye sasa ambaye si mke wako au mume wako, unaachana na utazamaji wa pornography, na ufanyaji wa masturbation, unakwenda kuchoma nguo zote zi kiasherati, na mambo yote yanayohusiana na uasherati, kadhalika na uchawi ni hivyo hivyo unachoma nyenzo zote za kichawi na unaacha kabisa na hayo mambo…hiyo ndio maana ya kutubu!
Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye NA KUZIACHA atapata rehema”.
Na mwisho anaambiwa kisha wapate msamaha wa dhambi na kuwa urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa Imani iliyo kwake yeye Yesu Kristo..Msamaha wa dhambi ni matokea ya mambo yote hayo hapo juu, kufumbuliwa macho, kutubu na kuachana na dhambi pamoja na nguvu za giza.

Katika Nyaraka zote Mtume Paulo alizoandika utaona zote zimetimiza hivyo vipengele muhimu hapo juu…Ndio maana Bwana akazitukuza nyaraka za Mtume Paulo Zaidi ya za wengi, na kuzifanya kuwa msingi kwa vizazi vyote, kwasababu zimehubiri lile lile kusudi Bwana alilolitaka lifike kwa watu wake, na ndio maana zinatufaa mpaka sisi sasahivi.

Hivyo ndugu…Kristo anataka kuyaona hayo hayo mambo yakijidhihirisha katika Maisha yetu..kwamba macho yetu yafumbuke, tuone tuliko toka, tulipo sasa na tunakokwenda…2) tuigeukie Nuru 3) Tuziache nguvu za shetani tumgeukie yeye na 4) Tupate msamaha wa dhambi na kuwa miongoni mwa waliotakaswa kwa Imani. Hayo mambo ndiyo anayohitaji kutaka kwetu!.
Swali ni Je! Umeyapata hayo ndani yako? Je umeigeukia nuru? Je! Umeziacha nguvu za shetani? Je! Umepata msamaha wa dhambi zako kwa kutubu na kubatizwa ubatizo sahihi?. Kama sivyo, wakati ndio huu wa kurekebisha kile ambacho hakijakaa sawa ndani yako, katika wakati huu mchache uliobaki kabla ya unyakuo.

Bwana akubariki. 

No comments:

Post a Comment