Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo litukuzwe daima, Natumaini Mungu amekupa neema ya kuiona siku ya leo, hata mimi pia, hivyo ni vizuri wote tukashiriki neema hizi pia tukamshukuru kwa kujifunza Neno lake.
Watu wengi sana hususani kwa wakati huu tunaoishi wanafahamu au wanafundishwa kuwa Ukija kwa Kristo ni lazima uwe tajiri, Ibrahimu alibarikiwa, Isaka alibarikiwa, Yakobo alibarikiwa, Daudi alibarikiwa Sulemani alibarikiwa kwanini na wewe usibarikiwe ikiwa ni mzao wa Ibrahimu kweli kweli. Hivyo hiyo imekuwa chachu ya kuwavuta watu wengi sana waujaribu ukristo,, lakini kwa bahati mbaya pengine kinapopita kipindi Fulani kirefu, na hawaona mabadaliko waliyokuwa wanayatazamia kwa Mungu pengine baada ya kuombewa sana, na kufarijiwa sana, wanaanza kurudi nyuma au wengine wanaishia kuuacha wokovu moja kwa moja..Wengine wanaanza kumnung’unikia Mungu, mbona hivi, mbona vile, mbona hujibu maombi yangu?,
Wengine wanaanza kuwanyooshea watu vidole Yule kachukua nyota yangu, Yule kaniloga, Yule ananiendea kila siku kwa waganga n.k..Utagundua pia maombi ya mtu wa namna hiyo sikuzote yanakuwa ni ya vita kupigana na watu asiowajua, wokovu wake unakua ni mgumu sana, kila siku anaangalia chanzo cha tatizo ni wapi, leo hii atasema pengine ni huu mti niliopanda hapa nyumbani kwangu ndio unaozuia Baraka zangu,ataenda kuukata na asipoona mabadiliko kesho yake atasema labda ni hili jina nililopewa na mababu zangu ndio chanzo cha matatizo yangu yote, ataenda kufanyiwa maombi ya deliverance, akiona tatizo bado lipo, kesho kutwa atasikia mahali Fulani wanasema watu waliozaliwa usiku huwa wanavita kubwa sana ya rohoni, akiangalia yeye alizaliwa saa 7 usiku, hivyo ataenda kujaribu na huko aombewe, akiona bado tatizo linaendelea, atasikia tena mahali pengine wanasema hupati pesa kwasababu huinenei sadaka yako, ataanza kuzinenea sadaka zake zote, atakaa muda Fulani aone kama kuna mabadiliko akiona hakuna chochote atakimbilia pengine ataambiwa toa sadaka ya ukombozi, ni kwasababu hujakomboa kiwanja chako na biashara yako na ndio maana hupati wateja wengi, atafanya hivyo tena, huko kote haoni matokeo yoyote..ataaenda pengine ataambiwa weka chumvi hii na maji haya ya upako kwenye biashara yako…na kadhalika na kadhalika, maisha yake ya ukristo yanakuwa ndio hayo kila siku, ukihesabu nguvu na fedha aliyoitaabikia kutafuta msaada wa mafanikio yake hailingani na kile alichokipata.
Kaka/dada tumekuwa tukiuona ukristo kuwa ni mgumu namna hii kwasababu wakati tunauingia hatujujua ukristo hasaa msingi wake umejengwa wapi na unamuhitaji mtu awe ni wa namna gani..Tumejikuta tunauingia tu ili tukatimiziwe matakwa yetu, na ndio huko tunakutana na ugumu mwingi ambao huo umekuja kwa kukosa kwetu maarifa. Tukumbuke kuwa Agano la kale ni tofauti na Agano jipya, agano lile lilikuwa ni kivuli cha mambo yatakayoendelea rohoni katika agano jipya, Mungu alimwahidia Ibrahimu na uzao wake Urithi huu wa hapa duniani, atambarikia hapa, Agano la Ibrahimu na Mungu lilikuwa ni la hapa hapa duniani, hivyo hatushangai kuona Mungu akiwabariki Waisraeli kwa vitu vyote vya kidunia, lakini sisi tulio wakristo, hatujapewa nchi ya kurithi hapa duniani, Urithi wetu na wenyeji wetu upo mbinguni(Wafilipi 3:20), hivyo Baraka zetu hasaa ni Baraka za kimbinguni, kwasababu huko ndio utajiri wetu wote ulipo na ndio mahali ambapo hata Bwana Yesu mwenyewe alituambia tujiwekee hazina huko mahali ambapo wezi hawawezi kufika wala kuharibiwa na kutu.(Luka 12:33-34).
Hiyo yote ni kuonyesha kuwa ukristo unaoletwa na Bwana wetu YESU KRISTO, hautoi kipaumbele cha utajiri wa ulimwengu huu.. (sisemi kuwa anataka tuwe maskini hapana), lakini hiyo ni kuonyesha kuwa kiwango chako cha utajiri au umaskini hakihusiani kwa vyovyote na ufalme wa mbinguni. Na hivyo kila mtu aliye mkristo anapaswa ajifunze kuridhika katika hali ile aliyopo maadamu maisha yake kila siku yanaimarika kwa Kristo, Biblia imesema hivyo. Tukiwa na Chakula na nguo, tu basi hiyo inatutosha kusonga mbele na ukristo wetu, na kusitawi kabisa mbele za Kristo Yesu.
(1Timotheo 6:8 ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.).
Lakini watu wakristo wanaomfuata Kristo kwa namna moja au nyingine kwa lengo la kutajirika au kupata mali tazama wengi wao wanaishia katika upotevu, na hawadumu katika wokovu kwanza wanakuwa hawapendi kusikia habari za ufalme wa mbinguni, hata watu wanaohubiri hizo habari huwa wanawachukia, na saa nyingine kuwabeza, kwasababu hazina zao tayari walishaziweka katika mambo ya ulimwengu huu. Na bado wanajiita wakristo, wanajifunza kukipenda kiganja cha Bwana Zaidi ya kumpenda Bwana mwenyewe.
Hata wakimwona mkristo Fulani ni maskini wanaujarisi kabisa kusema Yule hana Mungu, wanasahau kuwa kulikuwa na kanisa lenye wakristo maskini sana kupindukia, wala Mungu hakulipa utajiri wowote zaidi Mungu aliwaambia wawe waaminifu hata kufa nao watapewa taji la uzima.Lakini pamoja na umaskini wao mbele za Mungu walionekana matajiri, (Soma Ufunuo 2:8-11 “ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai. 9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.”) .
Vile vile kulikuwa na kanisa lililojiona kuwa ni tajiri sana halihitaji kitu chochote lakini mbele za Mungu lilionekana kuwa ni maskini kupindukia, tena ule umaskini wa kuwa uchi, na unyonge na upofu na kanisa hilo ndio hili tunaloishi mimi na wewe linaloitwa Laodikia(Soma Ufunuo 3:14-22 “… Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi….”).
Biblia inaweka wazi pia ni ngumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni..
Marko 10:23 “Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!24 Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu!25 Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
Hivyo ikiwa wewe ni mkristo Mungu kakubariki kwa vingi au kwa vichache, jambo la msingi ni kujifunza kuridhika ukifahamu kuwa wenyeji wako upo mbinguni na kwamba utumie muda wako mwingi zaidi kujiwekea hazina kule mbinguni, kuliko hapa, Tukijizoesha hivyo hatutajikwaa mahali popote na huo ndio Ukristo wa kweli. Kiasi kwamba ifikie kipindi tuseme Bwana akitupa vingi ni sawa na asipotupa vingi pia ni sawa! Maadamu kasema hatatupungukia kabisa hiyo inatosha!
Waebrania 13:5 “ Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”
Ubarikiwe sana.
No comments:
Post a Comment