"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, July 27, 2019

DAMU YA ZAKARI BIN BARAKIA.


Mathayo 23:29 “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki,
30 na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii.
31 Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii.
32 Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.
33 Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?
34 Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji;
35 hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu.
36 Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.”
 
Bwana Yesu aligusia vifo vya hawa watu wawili kama mfano alipokuwa anazungumza juu ya hukumu itakayowapata waandishi na mafarisayo na wote walio wanafki, (Ambao kwa sasa inawalenga viongozi wote wa kidini walio wanafki katika kazi ya Mungu). Kama alivyosema Damu za wenye haki wote zitachanganywa na kuletwa juu yao. Ikianzia kwa Habili, mpaka kwa Zakaria bin Barakia. Wengi wetu tunafahamu habari ya Habili Jinsi ndugu yake alivyomuua kwa jambo moja tu ambalo ni wivu. Kaini baada ya kuona sadaka ya ndugu yake imekubaliwa na ya kwake imekataliwa, moja kwa moja akaamua kumuua ndugu yake, “tukose wote”. Hivyo kwa kuwa Habili alikuwa ni mwenye haki na damu yake imemwagika pasipo kuwa na sababu ya msingi au hatia yoyote, biblia inatuambia…japo alikufa lakini bado anaendelea kunena, kwa namna nyingine ni kuwa damu yake bado inalia katika ardhi…
Waebrania 11:4 “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, IJAPOKUWA AMEKUFA, ANGALI AKINENA.’
Soma pia Waebrania 12:24,..utathibitisha unenaji wa damu ya Habili. Yeye alikuwa ni mfano mmojawapo aliowakilisha watu wenye haki, waliouawa tangu kuweka misingi ya ulimwengu hadi mwisho wa dunia, na wote hao damu zao zinanena mfano huo huo kama ya Habili mahali Fulani.

Sasa mtu mwingine ambaye tunaona Bwana akimgusia tena katika habari hiyo ya mapatilizo ya damu, ni ZEKARIA, wengi wanamchanganya na Yule Zekaria mwana wa Berekia, aliyeandika kitabu cha Zekaria, lakini tukichunguza kwa undani habari Bwana Yesu aliyokuwa anaizungumzia hapa, haikumuhusu yeye bali ilimuhusu Zekaria aliyekuwa kuhani wa kipindi cha mfalme Yoashi wa Yuda , mwana wa Yehoyada enzi za wafalme. Huyu Yehoyada Mungu alimpa umri mrefu kwa jinsi alivyoijali nyumba ya Mungu na uzao wa Daudi na kuwaongoza watu katika njia za kweli, aliishi miaka 130, Hivyo Zekaria inawezekana alikuwa ni mjukuu wake, ikumbukwe kuwa biblia sehemu nyingi haielezi “Babu na mjukuu”, bali wote wanaitwa “watoto wa”. Hivyo Zekaria bin Barakia Bwana Yesu aliyekuwa anazungumzia hapo ni ndiyo huyu Zekaria mwana wa Yehoyada.
Sasa huyu Yehoyada ambaye alikuwa ni kuhani aliyemcha Mungu sana,kabla ya kufa kwake watu walimcha Mungu, lakini siku alipokufa tu, mfalme na watu wote wakakengeuka waakanza kuabudu masanamu, hata nyumba ya Mungu iliyokuwa inaendelea katika ukarabati ikasitishwa..Wakaanza kufanya maovu, ndipo Zekaria sasa mtoto wake akatumwa na Mungu kwenda kuwaonya, tusome:
2 Nyakati 24:17 “Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao.
18 Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.
19 Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.
20 Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.
21 Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Bwana.
22 Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, BWANA NA AYAANGALIE HAYA, AKAYATAKIE KISASI.”
Kama tunavyosoma hapo wakati Zekaria anakufa kwa kupigwa mawe, alisema maneno hayo “BWANA NA AYAANGALIE HAYA, AKAYATAKIE KISASI.”. Jambo hili hawakufahamu ni jinsi gani lilimuudhi Mungu. Ingekuwa ni heri waashie kuwaua tu wenye haki, lakini wanafika mpaka hatua ya kuwaua makuhani wake na kibaya zaidi wanawaua katika nyumba ya Mungu, mbele ya macho ya Mungu.

Na ndio maana tunaona mamia ya miaka mbeleni Bwana Yesu anawakumbushia wale mafarisayo habari ile ile wasidhani kuwa imesahauliwa, hakuna kilichosahaulika. Aliigusia hii mifano miwili iliyohai kuwakilisha na wengine wote waliotendewa na watakaokuja kutendewa huko mbeleni mambo kama hayo:
Tukisoma katika 
Ufunuo,6:9 “Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.
10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?
11 Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao”.
Ndugu, Kumbuka kuwa wayahudi wakati wa Dikteta Adolf Hitler waliuliwa kikatili bila hatia yoyote, waliuliwa kwasababu wao ni wayahudi tu, kwasababu Mungu aliwachagua hao basi, hakuna kosa lolote walilolifanya ni WIVU tu kama ilivyokuwa kwa Habili, sasa hawa leo hii roho zao zinalia chini ya madhabahu, zikitaka kisasi kilipizwe..Na sio juu ya waliokufa, hapana bali juu ya hao waliojuu ya nchi, yaani wale waovu waliopo sasa.

Vilevile, tangu kipindi cha mitume hadi kipindi cha matengenezo ya kanisa, historia inarekodi, zaidi ya watakatifu wa Mungu milioni 68 waliuliwa kikatili, na kibaya zaidi asilimia kubwa waliotekeleza shughuli hiyo walikuwa ni viongozi wa kidini ya kikatoliki..Maneno yale yale ya Bwana yanatimia hapo..

Ndugu, tutawezaje kupona kama leo hii hatutauthamini wokovu, kumbuka, mtu yoyote asiye wa Kristo tayari huyo ni adui wake. Anatekeleza ilani ya ufalme wa giza, unashirikiana na matendo ya giza, hata kama hajui…hivyo na wewe pia ikiwa upo nje ya wokovu damu hizi nyingi za watakatifu zitatakwa juu yako. Tubu leo Bwana Yesu akufanye kuwa askari wa ufalme wa mbinguni. Shetani hakupendi, leo hii unayopumzi ni kwasababu Mungu amekuhurumia pengine utubu leo. Lakini wale wasiotaka kutubu tukiachilia ziwa la moto kuna wakati utafika wakiwa hapa hapa duniani watazinywa hizo damu za wenye haki.
Ufunuo 16:4 “Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu.
5 Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi;
6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.
7 Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.”
Bwana akubariki. Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

No comments:

Post a Comment