"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, July 27, 2019

MKATAE SHETANI NA MAWAZO YAKE YA KIBINADAMU.


Marko 8:31 “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.
32 Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea.
33 Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
 
Katika habari hiyo tunajifunza mambo mengi, jambo la kwanza tunaloweza kujifunza hapo ni jinsi ya kushughulika na roho ya uadui inayotutafuta kila kona, shetani ni adui yetu mkubwa.. na anapenda kutumia Zaidi watu kutushambulia, kutuumiza, hata wakati mwingine kutafuta kutuangamiza na kutuua.. na sisi tukikosa ufahamu na shabaha tunaweza kujikuta tunajibu mashambulizi isivyopasa…tunakipiga chombo cha muhusika badala ya mhusika mwenyewe….badala ya kumdhuru mrusha mkuki, unajikuta unatafuta kuidhuru mikuki.

Katika tukio hilo tunaona Bwana Yesu haraka sana alishajua ni shetani anazungumza ndani ya Petro, pasipo hata Petro kujijua kama anatumika na shetani, yeye alijua tu Bwana Yesu anahuzuni hivyo anahitaji faraja..kwahiyo wazo lilimjia kuwa anahitaji kumfariji Yesu…lakini hakujua kuwa hilo wazo ni kinyume na maandiko…Maandiko yanasema “ni lazima mwana wa Adamu asulibiwe na siku ya tatu afufuke”..

kwahiyo wazo lingine lolote litakaloibuka kinyume na hilo ni kutoka kwa yule Adui……….Kumbuka sio kwamba shetani alimvaa Petro kama nguo na kuanza kuzungumza ndani yake hapana!, aliyekuwa anazungumza pale ni Petro mwenyewe isipokuwa hilo wazo ndio lilitoka kwa shetani, na kumbuka shetani ana uwezo wa kumtupia mtu yeyote mawazo yake, awe mtumishi wa Mungu asiwe mtumishi wa Mungu..na mtu asiyekuwa na Neno vizuri ndani yake ni rahisi kukubali wazo la shetani pasipo kujua kuwa ni wazo la shetani. Ndicho kilichomtokea Petro hakuwa na Neno la kutosha ndani yake kuweza kuchambua wazo la Mungu ni lipi na la shetani ni lipi.

Na Bwana alipojua ni wazo la shetani hilo ndani ya Petro, hakuanza kushughulika na Petro bali na roho iliyopo ndani ya Petro,..na baada ya kuikemea ile roho au lile wazo la ibilisi, aliendelea kutembea na Petro kama kawaida kwani alikuwa bado ni mwanafunzi wake aliyempenda…Na ile ilimsaidia Petro kuwa makini na chochote anachokizungumza, kukilinganisha na maandiko.

Hivyo na sisi tunajifunza hapo namna ya kushughulika na roho ya uadui, hatupaswi kushughulika na yule mtu, bali na lile wazo au roho ndani ya yule mtu, hapo ndipo vita vyetu vilipo…sio kumchukia yule mtu.
Waefeso 6: 12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”.
Lakini jambo la mwisho la kujifunza ambalo ndio kiini cha somo letu leo ni “MAWAZO YA SHETANI”…

Tukirejea hapo juu mstari wa 33 unasema.. “Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.

Hapo Bwana Yesu anafunua ni kitu gani shetani anachowaza au kilichopo ndani ya kichwa chake siku zote…yeye siku zote anafikiria mambo ya duniani tu! (mambo ya wanadamu)...mambo ya kimwili, anawaza siku zote ni namna gani mwanadamu atakuwa anafikiri mambo ya hapa duniani tu!..hatataka mtu awe anafikiria mambo ya kimbinguni ya wakati ujao, yeye ni Maisha ya hapa tu!...hataki mtu afikiri ni nini kitamtokea baada ya kufa! Hataki mtu afikirie kwamba kuna kifo cha ghafla! Hataki mtu afikirie habari za Maisha baada ya haya, ndio maana hapa akamrushia Petro wazo haraka sana kumwambia Bwana hatakufa!. Ili amshawishi ajiwekee hazina hapa duniani na asifikiri mambo yajayo.

Ndugu kama ulishawahi kukaa pekee yako na kufikiri ni nini kitakukuta baada ya kufa, ni lazima utakuwa umeona Maisha hayana maana kabisa…hiyo ni hatua ya kwanza ya Mungu kukuvuta kwake, kama ulishawahi kuhudhuria msiba, ndio utajua kuwa Maisha haya hayana maana tunapita tu!..Usipende raha raha tu kila wakati! Kila siku kuhudhuria sherehe na party, hudhuria pia misiba, nenda mahospitini hata siku moja, pita tu! Ujifunze….. shetani hapendi! Wewe uende huko atakuambia aah unakwenda kujitoa kwenye mood tu!..atakurushia wazo la kwenda kujifariji na nyimbo Fulani za kidunia.

Hataki uhudhurie huko kwasababu anajua ukitoka pale utakuwa umepata funzo kubwa sana la Maisha, na hivyo atakukosa, na yeye hataki akukose…shetani anawaza yaliyo ya wanadamu tu! Hataki ufikirie mambo yajayo.

Siku moja jioni nilitoka nyumbani nikawa natembea mtaani tu, nikaenda mbali sana mitaa mipya kidogo, njiani nikawa natafakari Maisha yangu binafsi na mambo mengine ya kawaida..nilikuwa nina amani ya kawaida tu! Lakini nilipita sehemu nikakuta geti la nyumba moja limefunguliwa, na watu wanaingia ndani kwa huzuni, nilibahatika kumwona ndugu mmoja nafikiri atakuwa ni ndugu wa marehemu analia mpaka ameshikwa ndipo nikajua kuwa ulikuwa ni msiba, nami pia nilihuzunika kidogo…nikasema hiyo pia ingeweza kunitokea na mimi pia leo hii…

Kwa kitendo kile, kikanifanya nizidi kuingia kutafakari hatima ya Maisha haya zaidi, likanijia andiko kichwani kutoka katika kitabu cha Mhuhiri
Mhubiri 7:1 “Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.
2 Heri kuiendea nyumba ya matanga, Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake.
3 Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo.
4 Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha”.
Kujifunza juu ya hatima ya haya Maisha sio kukosa tumaini la Maisha hapana! Bali ni hekima..kwasababu hiyo inaonyesha unayapenda Maisha yako, leo utamwuliza mtu una mipango gani ya baadaye, atakupa mipango ya miaka mingi ya mbeleni sana, na ataanza kujiwekea hazina sasahivi…lakini hatakupa mipango ya misha baada ya kifo, sasa huyu huwezi kusema anaona mbele kwasababu anayeona mbele lazima avuke Maisha haya, azidi kuona mbele Maisha baada ya kufa, huyo ndio anayeona future yake…

Sasa Huyu ni Sulemani ambaye alikuwa na plani kubwa sana za Maisha yake na aliyekuwa ni Tajiri na mwenye hekima ambaye hakuna mfano wake ndiye anayesema haya maneno …”heri kuiendea nyumba ya matanga kuliko nyumba ya karamu”. Ni heri kusikia habari za misiba kuliko kila siku kusikia habari za shangwe tu na sherehe. Kwasababu kwa habari hizo zitakupa chachu ya kutafakari Maisha baada ya hapa.

Usisikilize mawazo ya shetani ambayo hayo ni kukupa wewe tumaini la mambo ya kiulimwengu tu kila siku, anakwambia hutakufa! Utaishi! Na huku upo bado kwenye Maisha ya dhambi, anakuambia utakuwa na heri na kufanikiwa, wakati unaishi na mke/mume wa Mtu. Na wakati maandiko yanasema wazi kabisa roho itendayo dhambi itakufa…shetani atatumia watu kukufariji kwa kila aina ya faraja, atatumia mpaka wanaojiita watumishi wa Mungu kukupa wewe faraja kwamba hutapatikana na mabaya...na wakati maandiko yanasema kinyume na hayo.

Atasema pia, wakristo hawapitiagi dhiki..ndicho alichomwambia Bwana Yesu, kuwa hatakufa..na wakati maandiko yanasema “ulimwenguni mnayo dhiki (Mathayo 16:33)” na “na tena mtakuwa watu wa kuchukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu”..lakini shetani atakwambia mtapendwa na watu wote…tangu lini mafisadi wakawapenda watu wasio mafisadi kama wao?...Danieli alikuwa ni mtu apendwaye mbinguni lakini duniani alikuwa anachukiwa, na watu waliokuwa wanakula rushwa…Na katika Ukristo ni hivyo hivyo zipo dhiki za hapa na pale, ambazo Bwana alituambia mapema kabisa tutakutana nazo ili tuwe na Amani…zitakapotokea tusihuzunike sana.

Hivyo tunajifunza kuyakataa mawazo ya shetani ambayo yanatusukuma kuyatazama mambo ya ulimwengu huu tu, mambo ya kitambo!mambo ya wanadamu Na kutuzuia kutafakari mambo yajayo. Na tunayakataa mawazo hayo kwa formula moja! Iliyorahisishwa katika Neno lake na hiyo ni kwa kutubu kwa kumaanisha kwanza kuacha dhambi na pili ubatizo sahihi wa kuzama mwili wote na kwa jina la Yesu na tatu Roho Mtakatifu..Roho Mtakatifu akishaingia ndani yako ni kama mlinzi wetu, atayaathiri Maisha yako na kuyapeleka anakotaka yeye,kama vile upepo uvumapo usipojua wewe…
atakukumbusha juu ya hatima ya maisha haya na kukupasha habari ya mambo yajayo…

Na baada ya hapo kilichosalia ni kudumu katika kujifunza Neno la Mungu siku zote za wakati wako zilizosalia hapa duniani…ili uwe na uwezo wa kuzipambanua roho, Petro alikuwa hana uwezo wa kuzipambanua roho kwasababu Neno halikuwa ndani yake, laiti angekuwa analifahamu Neno linalosema kuwa “Mwana wa Adamu ni lazima afe kwa ajili ya dhambi ya ulimwengu” yale mawazo yalipokuja kichwani mwake ya kumfariji Bwana angeyakataa…na yeye mwenyewe angesema moyoni mwake, shetani ondoka ndani mwangu na mawazo yako ya kibinadamu, kwasababu Neno linasema hivi na hivi. Na sisi tunapoyajua maandiko ni silaha tosha, biblia inasema Neno la Mungu ni Upanga wa Roho, linamkata kata shetani vipande vipande.

Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment