Mhubiri 11:3b “…… Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.”
Maisha yetu yanafananishwa na mti, na tunajua siku mti unapoanguka aidha kwa uzee, au kwa kukatwa, kuanguka kwake kunategemea sana jinsi ulivyokuwa. Hata kama ni mnazi unaoonekana umenyooka kama rula, bado unayo sehemu Fulani umelemea upande mwingine, utajua hilo siku ile unapokatwa wakati unadondoka..Kamwe haiwezekani ukawa sawasawa pande zote, na pia ukishalala pale chini, ndivyo utakavyolala hapo hapo milele, kwasababu mti sio kama viumbe hai vingine vinavyoweza kujongea, hata vikianguka vitasimama..Lakini Mti hautembei wala hausogei, hivyo anguko lake ni la milele.
Vivyo hivyo na sisi tunavyoishi, hapa duniani kama unyakuo hautatukuta, basi tufahamu kuwa kifo tutakutana nacho siku moja..Wengi wanasema nikikaribia hicho kipindi nitatubu, nataka nikumbie unapolemea maisha yako yote leo hii ndipo utakapolalia milele siku ile ya kukatwa kwako, huwezi ghafla ghafla tu, ukageukia upande wa pili ingekuwa ni rahisi hivyo Bwana asingekuwa anawahubiria watu injili tangu utoto wao mpaka wanakuwa watu wazima wamgeukie yeye. Si angesubiri tu siku ile wanakufa awahubirie injili waende mbinguni..Haipo hivyo wokovu ni tendo linalogharimu maisha na sio tukio Fulani tu.
Na kama tulivyoona mti unapoanguka unalala hapo daima,iwe ni kaskazini, iwe ni kusini, ndivyo itakavyokuwa baada ya kifo, umeangukia katika uzima utakuwa katika uzima milele, umeangukia katika mauti, utakaa katika mauti daima..Hakuna nafasi ya pili, Wala hakuna nafasi ya katikati.
Hivyo pima maisha yako leo uangalie ni wapi yamelemea kwa sehemu kubwa, na uanze kuyatengeneza upya ili kusudi kwamba hata ikitokea kifo kimekukuta kwa ghafla basi unakuwa na uhakika wa kuangukia mahali salama. Kama bado hujampa Bwana maisha yako, nafasi bado unayo sasa, hapo ulipo tubu na kusema kuanzia leo Bwana ninataka kuegemea kwako, na yeye atakusamehe, kisha kama hujabatizwa nenda kabatizwe,katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji kwa jina la YESU KRISTO, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako. Na Bwana atakupa Roho wake Mtakatifu kukulinda na kukuongoza sikuzote.
Ubarikiwe sana.
No comments:
Post a Comment