"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, July 14, 2019

USIWE SABABU YA WATU KUMKUFURU MUNGU.


2 Samweli 12:9 “Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.
10 Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.
11 Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.
12 Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua.
13 Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.
14 Lakini, KWA KUWA KWA TENDO HILI UMEWAPA ADUI ZA BWANA NAFASI KUBWA YA KUKUFURU, MTOTO ATAKAYEZALIWA KWAKO HAKIKA YAKE ATAKUFA”.
Shalom! Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.
Leo tutajifunza, madhara ya kuruhusu dhambi katika maisha yetu!..Tukijifunza kwa Daudi, ambaye Mungu alimpaka mafuta awe Mfalme juu ya Israeli, kama wengi wetu tunavyojua, alikwenda katika njia za Mungu kwa ukamilifu wote isipokuwa katika habari za Mke wa Uria.
1 Wafalme 15:5 “kwa sababu Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana, wala hakukosa katika yote aliyomwamuru, siku zote za maisha yake, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti”.
Kosa la Daudi kumchukua mke wa Uria na kumwua Uria mwenyewe, ndio lililotia doa haki yake…Lilikuwa ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu, mpaka Daudi alikuwa hatiani kufa…kwasababu alistahili kufa…Lakini kwasababu pia alikuwa ni mwepese wa kujirudi na kukimbilia kutubu, Bwana alimhurumia na akaghairi kumwua, lakini hakumwacha bila adhabu.