"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, July 14, 2019

LAANA YA YERIKO.


Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze maneno ya uzima. Wana wa Israeli walipokuwa wanavuka Yordani kuingia Kaanani kama tunavyosoma habari walikutana na kizuizi kikubwa sana, nacho si kingine zaidi ya Mji wa Yeriko pamoja na watu wake ambao walikuwa hodari sana, majitu makubwa yenye nguvu, hayo ndiyo yaliyowasababishia mpaka Mungu achukizwe nao, kwa vile walivyojiona mbele zao kama mapanzi na hivyo Mungu akakasirishwa nao na kuwafanya wazunguke jangwani kwa muda wa miaka 40.
Hivyo mji huu wenye kuta kubwa, ulikuwa ni kama kikwazo kikubwa cha wana wa Israeli kumiliki nchi yao tangu zamani, hata hakukuwa na mji uliokuwa mkubwa zaidi ya ule, mfano Yeriko usingekuwepo, wana wa Israeli tangu zamani wangeshakuwa wamewasili katika nchi yao ya Kaanani Mungu aliyowaahidia.

Sasa ndio baadaye tunaona Yoshua baada ya kupewa maagizo ya kuushambulia ule, mji, kwa kuuzunguka mara 7, kisha waingie ndani waue kila kitu, na walipomaliza vita, na kuuchoma mji tunaona Yoshua anasimama na kuzungumza maneno haya ya Laana:
Yoshua 6:26 “Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za Bwana mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.
27 Basi Bwana alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote”.
Tunaona Laana hii Yoshua aliitamka tu kwa mji huu, wa Yeriko hakutamka maneno kama hayo kwenye miji mingine ya Kaanani waliyoishambulia, ni kwasababu gani? Ni kwasababu Yeriko ndio mji pekee uliowatesa, na ndio uliowagharimu muda mwingi kuuweka chini. Yoshua ndio anayejua vizuri shida waliyoipata wakati ule walipokuwa na wale wapepelezi wenzake miaka 40 iliyopita jinsi mji huo ulivyokuwa kikwazo kikubwa kwao mbele za Mungu, Mpaka Yoshua akaona kujengwa tena mji huo ni sawa na kukumbushwa machungu yote ya kule jangwani..Ndio maana akazungumza Laana ile.

Hivyo wale watu waliokuwa na Yoshua, waliyashika maneno yale, hata wakati wamemaliza kuiteka miji yote na kuanza kujenga na kupanda, kama Bwana alivyowaagiza kuwa watakapoingia nchi ya ahadi wajenge na kupanda maaana atawabikia kwa vingu…lakini ule mji wa Yeriko ulibakia vile vile bila kuguswa kama makumbusho ya Taifa, hakuna aliyedhubutu kwenda kuuendeleza kwa namna yoyote ile, na hiyo iliendelea kwa miaka mingi mbeleni.

Lakini baada ya miaka kama 530 hivi kupita, wakati wa utawala wa mfalme Ahabu, alitokea mtu mmoja, aliyeitwa Hieli mbetheli, yeye kwa kutokujua, au kwa kupuuzia, au kwa uzembe wake wa kutofuatilia msingi ipoje, na torati inasema nini juu ya mji huo, hakujiuliza ni kwanini mji huo umeachwa ukiwa muda mwingi angali mingine inaendelezwa yeye akanyanyuka na kwenda kuanza kuujenga Yeriko,..Na Laana ile ikampata sawasawa na maneno ya Yoshua.
1Wafalme16:34 “Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.”
Hii inatufundisha nini?, …kutokujua sheria hakukufanyi wewe usihukumiwe kwa sheria..Mungu akitamka laana zake halikadhalika na Baraka zake haijalishi unafahamu au haufahamu zitakupata tu. Hapa tunaona jambo hili lilitimia miaka 530 baadaye, nataka nikuambie hata na Leo eneo la Israeli ambalo mji wa Yeriko ulikuwepo, mtu aliyehusika au atakayehusika kuliendeleza eneo hilo jambo hili lilimpata au litampata haijalishi anafahamu au afahamu.

Sasa hiyo ni laana inayowahusu waisraeli, na agano la Kale, lakini vilevile katika agano jipya ipo laana ya namna hiyo hiyo imetolewa na Mtume Paulo..Tena hii ndio mbaya zaidi kwasababu inahusisha na mambo ya rohoni moja kwa moja.
Wakati ule, Mitume walipokuwa wanateseka, kuuhubiri injili ya ufalme wa mbinguni unaopatikana kwa Imani ya YESU KRISTO tu, wakiwa wanazunguka huku na huko, wakipitia hatari nyingi za kupigwa, na kufungwa na kuuawa, Na mwisho wa siku wanafanikiwa kuifikisha injili duniani kote..Mataifa yanaokoka, watu wanamtazama Yesu Kristo, wanaufurahia wokovu wake, wamestarehe.

Lakini huku nyuma kukaanza kutokea jopo lingine la wayahudi wa uongo, mitume wa uongo, waalimu wa uongo na manabii wa uongo, wakaanza kuwafundisha wale watu ambao walishamwamini Kristo injili ya namna nyingine ambayo mitume hawakuipeleka kwao. Jambo hili liliwahuzunisha sana mitume mpaka ikafikia hatua mtume Paulo anatoa laana hii kwa uweza wa Roho:
Wagalatia1:6 “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia INJILI YA NAMNA NYINGINE.
7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.
8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, NA ALAANIWE.
9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, NA ALAANIWE.
10 Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.”
Umeona, laana hii ilitoka karibia miaka 2000 iliyopita, na inayo nguvu ile ile hadi sasa, kama kipindi kile kulikuwa kumeshaanza kuonekana mitume wa uongo, sasahivi tusemeje.Hakuna mtu asiyejua hilo, Kila mahali tunasikia injili ambazo ukizilinganisha na injili za mitume hazina uhalisia wowote.. Na hatujui kuwa laana hii inaendelea kufanya kazi hadi sasa. Tusijidanganye na kusema hatujui, ni vizuri kabla ya kutaka kuwa waalimu, au wahubiri wa Neno la Mungu, tufahamu biblia inatufundisha nini au inataka nini. Vinginevyo tunaweza kujikuta tunadondokea katika laana mbaya ya Mungu pasipo hata sisi kujua.

Bwana Yesu alifunga vitabu vya agano jipya kwa maneno haya:
Ufunuo 22:17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.

18 Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”
Tufundishe Injili ya mitume ili tuwe katika Upande salama. Bwana atusaidie katika hilo.

Pia usiache kutembelea website yetu hii, kwa mfundisho zaidi.(www wingulamashahidi org)

1 comment:

  1. Powerful message, be blessed you man of God

    ReplyDelete