"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, July 14, 2019

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 4


Shalom! Karibu tujifunze Biblia, bado tupo katika mwendelezo wa kujifunza vitabu vya Biblia, tukiwa tayari tumeshavitazama vitabu tisa vya kwanza, na leo tutaendelea na kitabu kimoja kinachofuata kijulikanacho kama Samweli wa Pili,

Kumbuka huu ni uchambuzi tu! Ambao umechukua tu baadhi ya sehemu, sio ukamilifu wote, na biblia haina tafsiri moja maalumu, hapana! Mstari mmoja unaweza kuwa na mafunuo au mafunzo zaidi hata ya milioni moja, kwa jinsi tu Roho atakavyopenda kumfunulia mtu na mtu.

Kwahiyo ikiwa wewe ni mkristo mwenye Roho Mtakatifu ndani yako ni vizuri pia kuutumia muda wako binafsi kuisoma biblia yako, ukiwa peke yako, kwani Roho anaweza kukufulia jambo ambalo haujawahi kulisikia likuhubiriwa kwa mtu yoyote au mtumishi yoyote. Kwasababu Roho ya Mungu sio ya mwanadamu. Yeye hagawanywi kwa vipimo, hivyo mtu yoyote akiwa na NIA ya kujua, Roho Mtakatifu atamfunulia yote kama alivyoahidi katika neno lake.(Yohana 16:13)

Katika kitabu kilichopita cha Samweli wa kwanza (1Samweli), tulishaona kuwa kitabu hichi kiliandikwa na Nabii Samweli mwenyewe, isipokuwa katika sehemu za mwishoni mwa kitabu hicho, ambazo ziliandikwa na Nabii Nathani na Nabii Gadi, kwasababu Samweli asingeweza kuandika habari za kufa kwake mwenyewe katika kitabu hicho, hivyo ni wazi kuwa kuna wengine ndio waliondika sehemu hizo za mwisho..kama hujapitia bado hichi kitabu basi ni vizuri ukapitia kwanza uchambuzi wa vitabu vya mwanzo ili tuende pamoja huku mbeleni. BOFYA HAPA⏩ Vitabu vya biblia:Sehemu ya 3

Kitabu cha Samweli wa Pili, kiliandikwa na Nabii Nathani na sehemu baadhi kiliandikwa na Nabii Gadi..Nabii Nathani alikuwa ni Nabii wa Mungu, Wafalme hawakuwa manabii, ilikuwa ni ngumu wao kusikia Neno la moja kwa moja kutoka kwa Mungu, hivyo walihitaji watu maalumu waliopewa hiyo karama (ambao ndio manabii) kwahiyo kila mfalme alikuwa na manabii kadhaa ambao ndio walikuwa washauri wake wa karibu na ndio waliokuwa wanawaambia mambo yote Mungu aliyozungumza kuwahusu wao na ufalme wao. Kwahiyo Nathani alikuwa ni Nabii wa Mfalme Daudi, chochote Bwana alichokuwa anataka kuzungumza alikuwa anamwambia Nathani na kisha Nathani anakwenda kumwambia Daudi..kwahiyo Nathani kwasababu muda wote ndio alikuwa anakaa na Daudi yeye ndiye aliyekuwa anarekodi matukio yote ya utawala wake kwa kuongozwa na Mungu.

Sasa kitabu hichi kinaelezea maisha ya Daudi katika Ufalme wake, Kumbuka baada ya kufa mfalme wa Kwanza wa Israeli (yaani Sauli), Daudi ndio aliuchukua utawala mahali pake, kwasababu aliahidiwa na Mungu kuwa atatawala juu ya Israeli. Kwahiyo kitabu hichi kinamhusu Daudi mwanzo mwisho.

Unaweza kuipata historia ya Daudi kwa kusoma mwenyewe kitabu cha Samweli wa kwanza, lakini kwa ufupi ni kwamba Daudi hakuupata ufalme kama Sauli alivyoupata..Ukielewa vizuri jambo hili litakusaidia kujua kuwa wakati mwingine njia za Mungu si kama za mwanadamu,…utajifunza pia kutokujilinganisha na mtu mwingine na kumshukuru Mungu kwa kila kitu, katika mahali ulipowekwa… kwasababu njia hazifanani…Umewahi kusikia watu ambao Mungu kawabariki kwa mali za urithi na wale ambao Mungu kawabariki kwa kuhangaika kwao wenyewe?...Makundi yote haya mawili yanaweza yakawa yamepewa thawabu hiyo moja na Mungu mwenyewe isipokuwa katika njia mbili tofauti, mmoja kwa kurithi pasipo kuhangaika na mwingine kwa kuhangaika..Lakini kila moja ina faida zake na hasara zake.

Na kwa Daudi ilikuwa ni hivyo hivyo, Mfalme wa Kwanza Sauli, aliupata ufalme pasipo hata kuhangaika, baada ya kutiwa tu mafuta na Samweli, Bwana akamtengenezea njia akawa mfalme ndani ya usiku mmoja pasipo hata kuhangaika, lakini ilipofika zamu ya Daudi kuwa mfalme juu ya Israeli, shughuli ilikuwa ni nzito kidogo…hakuupata kama Sauli alivyoupata…Na hiyo ni kwasababu ilimpendeza Mungu iwe hivyo, ndio maana unaona Daudi alimpendeza Mungu zaidi ya Sauli.

Daudi baada ya kupakwa mafuta na nabii Samweli alidhani itakuwa ni rahisi tu kuingia kwenye ile enzi kama ilivyokuwa kwa Sauli, alijua utafika wakati tu, Israeli wote watautii unabii wa Samweli juu ya yeye kuwa mfalme na hivyo watakusanyika na kwenda kumwomba awe mfalme kwasababu amechaguliwa na Mungu, kama ilivyokuwa kwa Sauli hakutakuwa na upinzani wowote…lakini ukisoma biblia ndio utajua mambo Daudi aliyoyapitia mpaka alipokuja kuwa mfalme…Aliteseka nyikani kutwa kuchwa kuwindwa kama ndege kwa muda wa si chini ya miaka 15, baada tu ya kupakwa mafuta, aliongeza idadi ya maadui kwa kasi kubwa, mpaka mfalme alikuwa adui yake…Jaribu kujenga picha sasahivi unakuwa adui wa Raisi?..utakimbia wapi asijue? Maana anao wapelelezi wake kila kona, hata kitongoji wa kijiji atakuwa adui yako kwasababu akikuona ni kama kapata deal la fedha, au “kick” kwa mfalme…Inahitaji mkono wa Mungu tu! Kuepukana naye…ndio Daudi naye alikuwa hivyo hivyo, ilihitajika mkono wa Mungu tu kuepuka na mkono wa Mfalme Sauli aliyekuwa anamwinda usiku kucha.

Ilifika kipindi akawa hakai mjini tena, anakaa maporini na kwenye mapango kwa miaka ya kutosha, kwasababu akitokeza mjini tu, waandishi wa habari wapo wa kumpelekea mfalme taarifa, chakula kilikuwa ni cha kwenda kuomba! Omba! Unakula leo hujui kesho itakuwaje!..kuna wakati alikuwa anapungukiwa kabisa anapitia njaa kali pamoja na wale watu wachache aliokuwa nao…na mbaya zaidi alipata maadui ambao walikuwa wanamchochea kwa mfalme mambo ya uongo…

Ilifika kipindi wale mafilisti ambao alikuwa anawaita wamelaaniwa na wasiotahiriwa, wale ambao aliwaulia jemedari wao Goliathi, alikimbilia nchini kwao kuomba msaada (kuungana nao) [1Samweli 27:1], joto lilikuwa kali Israeli mpaka akaona akiendelea kukaa Israeli ana muda mchache sana wa kuishi…maana alikuwa anatafutwa kila kona, alikuwa na kesi za kutengenezewa si haba!.kiasi kwamba alikuwa anajua akishikwa tu na mfalme ni anakwenda kuchunwa ngozi mzima mzima. Ilifika kipindi hofu ya Mfalme ilikuwa kubwa hata kwa Israeli kiasi kwamba ukimwona Daudi halafu hujatoa taarifa na ikajulikana ulimwona hujatoa taarifa, ilikuwa ni KIFO!.

Sijui kama ulishawahi kupitia hali kama hivyo? Daudi hakuna chochote alichokuwa anafanya cha kujiendeleza kwa miaka zaidi ya 15.Wala alikuwa haishi maisha ya raha, Ni pori na yeye yeye na pori, Sio wewe unapitia kusemwa kidogo unasema una maadui!! Unapitia kutukanwa kidogo unasema unamaadui!..unatengwa kidogo unalalamika na kunung’unika unasema una maadui na bado unakula vizuri na unakunywa, na kesho unao uhakika wa kuishi… Daudi mpaka alihamia nchi jirani, kwenda kwa watu wasiotahiriwa ambao aliwatukana hapo kabla, angalau apate unafuu, kwa makubaliano kuwa hata ikitokea vita dhidi ya ndugu zake yupo tayari kuungana na wafilisti kwenda kunyume nao…

Taifa zima lilimgeuka, hata kama kulikuwa na wachache waliomkubali lakini itasaidia nini, kama Serikali nzima iko kinyume chako?..Wewe sasahivi Raisi atoe agizo la kukutafuta ili uuawe, ukizingatia kwenu ni wakulima na wafugaji, huna chochote…si utasema ni heri usingezaliwa…tena afadhali siku hizi mfumo wetu ni wa Uraisi ,zamani ilikuwa ni Ufalme, Mfalme alikuwa yupo juu ya sheria, tofauti na sasahivi ambapo Raisi hayupo juu ya sheria, na Mfalme alikuwa anatawala mpaka afe sio sasahivi baada ya miaka 10 tu amebadilika ameingia mwingine..

Kwahiyo hayo ndio mambo Daudi aliyokuwa anayapitia …Wengi wetu hatujui Kitabu cha Zaburi kiliandikwaje andikwaje! Sehemu kubwa ya kitabu cha Zaburi Daudi alikiandika akiwa nyikani, alipokuwa anawindwa…wakati anapitia shida! Ndipo akawa anasema….
Zaburi 13:1 “Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako?
2 Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?
3 Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti.
4 Adui yangu asije akasema, Nimemshinda; Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa.
5 Nami nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.
6 Naam, nimwimbie Bwana, Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu”.
Huo ni mfano wa Maombi ya Daudi akiwa katika tabu ya kuwindwa na majeshi ya Mfalme Sauli..na hakuomba leo yakajibiwa leo leo…yalichukua miaka ya kutosha…Kwahiyo hizo Zaburi hazikuandikwa na mtu aliyekuwa hajui nini anazungumza, hakumwandikia mtu hizo, alijiandikia yeye…kila maombi aliyokuwa anaomba alikuwa anayaandika…ndio sisi tunayasoma leo kama ZABURI.

Kila hatua aliyokuwa anapitia alipokuwa anatafutwa, alikuwa anamwomba Mungu na kumshukuru na kumwimbia..na kila nyimbo kila sala na kila shukrani alikuwa anaiiandika, siku baada ya siku..Kuna wakati Daudi alikuwa hatiani kufa kwa kushikwa na Sauli, alikuwa ameshazingirwa pande zote, lakini Bwana akamwokoa na mkono wa Sauli, hivyo akamwimbia Mungu nyimbo za kumshukuru na akaziandika zote…

Sehemu chache sana za Zaburi Daudi aliziandika akiwa tayari kashakuwa mfalme…na nyingi ya hizo aliziandika kwa lengo la kumshukuru Mungu jinsi alivyomwokoa na maadui zake alipokuwa taabuni...Sasa utauliza ni wapi penye uthibitisho kuwa Zaburi iliandikwa na Daudi wakati yupo matesoni au wakati yupo kwenye ufalme?...Ukisoma kitabu cha Zaburi 18:1-7 biblia inasema “
1 Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
2 Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
3 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu.
4 Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
5 Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili.
6 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.
7 Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu…...”
Ukisoma mistari hiyo ya mlango wa 18 wa Zaburi, unaweza usielewe mwandishi kwanini aliandika hivyo au ni nini kilichomsukuma mpaka akaandika hivyo…alikuwa katika mazingira gani?...sasa jibu la swali hilo tunalipata katika kitabu cha 2 Samweli 22…
2 Samweli 22:1 BASI DAUDI AKAMWAMBIA BWANA MANENO YA WIMBO HUU, SIKU ILE BWANA ALIPOMWOKOA MIKONONI MWA ADUI ZAKE ZOTE, NA MKONONI MWA SAULI;
2 akasema, Bwana ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu;
3 Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio yangu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri.
4 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu.
5 Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
6 Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili.
7 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu;
8 Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasuka-suka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu…”.
Umeona sababu za Daudi kuandika Zaburi?... Hivyo kitabu cha Samweli wa pili kinatufundisha jinsi Mungu anavyotenda kazi juu ya mtu na mtu…njia atakayotumia kukupa wewe, sio sawa na atakavyotumia kumpa mwingine, ni vizuri zaidi kupenda kupitishwa njia ngumu kwasababu hizo ndio zinazotufanya mara nyingi tuwe wakamilifu kuliko zile njia rahisi. Njia rahisi za kupata kitu zinatufanya tusikithamini kile kitu chenyewe,…kama Mfalme Sauli alipata ufalme kwa njia rahisi ndio maana hakuuthamini ufalme wake, akawa anafanya mambo ambayo Mungu hakumuagiza,…

lakini Daudi kwa miaka zaidi ya 15 alijaribiwa kwa mateso na hatari za vifo na kwa kurudia rudia kuomba pasipo majibu ya papo kwa hapo…..ndipo tunaona alipokuja kuupata ufalme aliuthamini sana, na aliishi kulingana na mapenzi ya Mungu..siku zote za ufalme wake, mpaka Mungu akamwahidia uzao wake utamtoa MASIHI (BWANA YESU KRISTO) ambaye sasa ndiye mkombozi wetu MWANA WA DAUDI. Katika ufalme wake alijifunza kunyenyekea na kuwathamini na kuwafariji pia walioko kwenye tabu..maana na yeye alishayapitia hayo..alikuwa hawaonei watu maana anajua uchungu wa kuonewa na kukimbizwa..

Pia kitabu hichi kinatufundisha njia kamili ya Mungu ni kutupa kidogo kidogo, mpaka kinakuwa kingi (Mithali 13:11)…usipende njia za haraka haraka, nyingi ya hizo sio mpango wa Mungu, utaona pamoja na Daudi kupitia taabu zote hizo hata ufalme hakupewa wote ndani ya siku moja…ukisoma biblia utakuja kuona kuwa alipewa na Mungu kwanza utawala juu ya Kabila moja kwa miaka 7, na baadaye ndipo akapewa utawala wa Israeli yote kwa miaka 33..Na aliishi kwa kumpendeza Mungu maisha yake yote, isipokuwa kwa kasoro ndogo ndogo alizokuwa nazo, lakini kwa ujumla alimpendeza Mungu sana..hiyo ni kutokana na kunolewa vyema kabla ya kuipokea ahadi aliyopewa na Mungu.

Na pia tunajifunza katika kitabu hichi kutokukata tamaa…Daudi alipitia tabu, mpaka dakika ya mwisho aliyokuwa amekata tamaa ndio kipindi hicho hicho Mungu alimpa ufalme, kipindi ambacho yupo nchi nyingine..kipindi ambacho asingetarajia, wala kulikuwa hakuna dalili yoyote ya yeye kumiliki ufalme ndio kipindi alichopokea ufalme tofauti na mategemeo yake, pengine alidhani wakati anamuua mfilisti wakati Israeli wote wanamshangalia ndio angeupata ufalme lakini badala yake, mahali ambapo yupo katika shida nchi ya ugenini ndipo Mungu anamnyanyua..kadhalika, njia za Mungu hazichunguziki, kipindi ambacho mtu anaweza kusema hapa haiwezekani tena, afadhali ingekuwa jana au juzi au mwaka juzi, lakini hajui kuwa kumbe huo ndio wakati uliofaa wa Mungu, kwahiyo ni kujifunza kuishi maisha ya kutokukata tamaa na kutokunung’unika siku zote na kumwamini Mungu.

Na mwisho maisha ya Daudi yamebeba siri ya Maisha ya Yesu Kristo, jinsi alivyopitia na kuishi ni Ufunuo wa Yesu Kristo jinsi alivyoishi hapa duniani..Naye pia alikuwa ni mfalme aliyekataliwa kama Daudi, na hata zaidi ya Daudi..tangu kuzaliwa kwake. Biblia inatuambia hivyo katika..
Isaya 53:1 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?
2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
Tunaona Herode alitamani kumwua, hata Israeli hawakumwamini ingawa yeye ndiye aliyeteuliwa na kupakwa mafuta na Mungu kuwa mfalme juu ya Israeli..lakini alipofika miaka 30 kama Daudi ndipo ulimwengu kidogo kidogo ukaanza kumsikia, ile ahadi ya ufalme ikaanza kutimia…akaanza kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa…Na alipokuja na kufufuka ikatimia, sasahivi hatumtambui tu kama mfalme bali ni MFALME MKUU,MUNGU MWENYE NGUVU..Tutakuja kuulewa vizuri ufalme wake wakati wa Utawala wa miaka 1000 hapa duniani, sasahivi bado.

Hivyo kama hujayakabidhi maisha yako kwake ni vyema ukafanya hivyo leo usikawie kawie kwasababu haya maisha hatujapewa guarantee ya kufika kesho, na hakuna mwingine utakayeweza kupata tumaini kwake kama sio KRISTO…Yeye ndiye mpakwa mafuta pekee wa Mungu, tubu leo kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, kama hujafanya hivyo…ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa jina lake upate ondoleo la dhambi zako, na kisha upokee kipawa cha Roho wake Mtakatifu, kabla mlango wa Neema haujafungwa.

Bwana akubariki sana

Usikose mwendelezo wa vitabu vinavyofuata..
Unaweza pia kutembelea webiste yetu hii kwa mtiririko mzuri wa masomo yetu ⏩www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment