Ipo dhambi ya Mauti, Hiyo mtu aliye mkristo akiitenda kama Bado Neema ya Mungu ipo juu yake, atakufa lakini ataokolewa siku ya kiyama. Mfano Musa!, alimkosea Mungu, akasamehewa kosa lile lakini adhabu ya kifo haikuondolewa juu yake, Bwana alimwambia kwa kosa lile hataiona nchi ya ahadi na kufa atakufa…lakini baada ya kufa, alikwenda mahali pa watakatifu.Ndio maana utamwona akitokea tena na kuzungumza na Bwana Yesu, yeye pamoja na Eliya katika ule mlima Mrefu.
(Mathayo 17:1-9), Sasa hiyo ni dhambi ya mauti ambayo, unaadhibiwa mwili ili roho ipone (1 Wakoritho 5:5)..Kwa maelezo marefu juu ya dhambi hii ya Mauti, tutumie ujumbe inbox tutakutumia.
Lakini ipo dhambi ya isiyo na msamaha kabisa hapa duniani wala huko katika dunia inayokuja…Hiyo ni dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Dhambi hii watu wanaitenda na kadhalika mtu asipoielewa dhambi hii ni rahisi kupelekeshwa na shetani sana…Kwasababu shetani anamjua mwanadamu sana kwa miaka mingi, tangu Edeni, hivyo mojawapo ya njia anazotumia kumkandamiza mwanadamu asiye na ufahamu wa kutosha ni kumletea mawazo kwamba ana dhambi isiyosameheka mbele za Mungu, Tutakuja kuona hapo mbeleni kidogo, namna ya kukabiliana na hilo jaribu Kongwe la shetani!
Lakini sasa hebu tujifunze ni namna gani mtu anamkufuru Roho Mtakatifu.
Biblia inasema katika
Mathayo 12:31 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.
32 Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao”.
Hapo Neno limewekwa moja kwa moja kuwa yeye atakayenena Neno juu ya Roho Mtakatifu na wala si mwana wa Adamu, haimaanishi kuwa Kuna Miungu watatu, hapana! Mungu ni mmoja tu…Ila Roho Mtakatifu ni Utendaji kazi wa Bwana Yesu Kristo mwenyewe katika mfumo wa Roho, kwasababu Roho Mtakatifu ndiye roho wa Yesu mwenyewe (Matendo 16:7) ndio maana ilimpasa yeye aondoke kwanza katika mwili ili arudi tena katika roho ( soma Yohana 16:16), kwasababu mtu anayefanya kazi katika roho, anakuwa na matunda Zaidi kuliko anayefanya kazi katika mwili, mchawi anayekwenda mahali katika roho anauwezo wa kuathiri kikundi kikubwa cha watu kuliko angekuwa mahali pale katika mwili…Kwahiyo utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ndio utendaji kazi wa Mungu, ulio karibu Zaidi na wenye matunda Zaidi kuliko Mungu alivyokuwa katika mwili…ndio maana kuna hatari kubwa sana ukimkufuru….kwasababu nguvu ya kumshawishi mtu kuja kwa Mungu inatokana na Roho Mtakatifu.
Sasa endapo mtu ambaye hajawa mkristo kabisa, na ndani ya moyo wake anasikia kabisa kuna kitu kinamshuhudia kuwa Yesu ndiye njia, na kinampa uthibitisho wa kila aina kuwa hakuna njia nyingine nje ya Yesu Kristo, huyo ni Roho Mtakatifu ndani ya huyo mtu anayemlilia ageuke atubu na kumwamini Yesu, lakini mtu huyo pamoja na msukumo wote huo wa kiMungu ndani yake, na wenye kila aina ya uthibitisho, akaamua kwa idhini yake mwenyewe kuikataa na kutamka maneno ya kufuru wazi kwa kinywa chake dhidi ya ule ushawishi au dhidi ya mtu anayemletea injili ile, Roho Mtakatifu ndani yake anaondoka milele, kamwe mtu huyo hataisikia tena ile sauti ikimshawishi kuwa Yesu ni njia. Kamwe hatasikia tena kitu kikimvuta kutubu, atabakia kupinga injili Maisha yake yote…Hapo Mtu huyo anakuwa na dhambi ya Milele (amemkufuru Roho Mtakatifu)…haiwezekani tena yeye kutubu!...Kumbuka sio kwamba itafika kipindi atatamani kutubu na Mungu amkatae! Hapana! Hatasikia sababu wala hamu ya kutubu mpaka anakufa!..kwasababu anayeleta moyo wa Toba ndani ya mtu ni Roho Mtakatifu mwenyewe, kama mtu anahukumiwa dhambi zake na kutamani kutubu ina maana bado Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yake, lakini asiyetaka kabisa kutubu ni wazi kuwa Roho Mtakatibu hayupo kabisa juu ya Maisha yake.
Kadhalika kama mtu tayari ni Mkristo, na ameshawishika kabisa kumfuata Kristo, na kuonja mema yote na vipawa vyote vya kiMungu na kutambua kabisa ya kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zake na ameshajua utendaji kazi wa Roho Mtakatifu upoje, na kuamua kugeuka kuacha wokovu, na kugeukia shetani moja kwa moja, na kunena maneno ya kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu au dhidi ya mtu anayehubiria wengine Injili ya wokovu kwa uweza wa Roho, hapo mtu huyo Roho Mtakatifu anaondoka moja kwa moja juu yake, na harudi tena! Kamwe moyoni ile sauti iliyokuwa inamhukumu atendapo mabaya au iliyokuwa inamwongoza inakuwa haipo tena, huko alikokwenda ndio anakuwa wa huko huko moja kwa moja….hawezi wala hatakuwa na hana hamu ya kutubu tena, wala hatasikia kuupenda wokovu tena, kwasababu anayetupa sisi hamu ya kuendelea kuupenda wokovu ni Roho Mtakatifu.
Waebrania 6:4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,5 na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.7 Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu;8 bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.”
Sasa kuna kitu kinaitwa kurudi nyuma, au kupoa! Hii inatokea pale, mkristo alikuwa moto sana, alikuwa anaomba na kusali lakini kapunguza kufanya hivyo, alikuwa anafanya kitu Fulani cha kiMungu lakini kakipunguza, alikuwa anahubiria wengine lakini kapunguza, …Kumbuka anakuwana anapoa sio anakuwa baridi!, Mtu anayekuwa baridi maana yake ametoka kwenye wokovu kabisa! Hivyo ni ngumu kurudi tena, yupo hatiani kupata dhambi ya mauti au dhambi isiyosameheka..Lakini aliyerudi nyuma, maana yake anaweza kurudi pale alipokuwepo akitubu na ndani yake, bado kuna kitu kinachomshuhudia kuwa anahitaji kumgeukia Mungu, na hofu ya kwenda kwenye ziwa la moto sasa huyo ni Roho Mtakatifu bado anafanya kazi ndani yake.
Lakini sasa, shetani akishajua kuwa mtu karudi nyuma, jambo la kwanza analokwenda kulifanya ni kwenda kumwekea ukingo asirudi alipokuwepo, na hiyo anaifanya kwa kumletea sauti inayomwambia UNA DHAMBI ISIYOSAMEHEKA! Au UMEMKUFURU TAYARI ROHO MTAKATIFU.
Mwamini yule akisikia sauti ile ndani yake ikimwambia vile basi anavunjika moyo, na kuingia kwenye dimbwi kubwa la mawazo yasiyoisha. Hata hamu ya kuendelea mbele yote inaisha!..Sasa mtu wa namna hiyo hajamkufuru Roho Mtakatifu kwasababu bado anahitaji kurudi kwa Mungu, bado anataka kutubu, hiyo hamu au hitaji la kutubu linaletwa na Roho Mtakatifu, hivyo Roho Mtakatifu bado hajaondoka juu yake, ingawa shetani atamletea mawazo ya kwamba ana dhambi ya milele.
Kwamfano kuna mtu mmoja mwenye tatizo kama hilo alinitumia ujumbe inbox, akiwa na mashaka hayo na hajui afanyaje…Hebu fuatilia kidogo mazungumzo haya…
Shalom! swali langu ni kwamba je mtu akiokoka halafu akakengeuka ila akarudi tena kuomba toba madhabahuni, je mtu huyu anakuwa kasamehewa au atakuwa hajasamehewa? na jina lake litaendelea kuwepo kwenye kitabu cha uzima?
Nikamjibu swali hilo, nikamtumia na somo linalohusu swali hilo…na kisha akaendelea kuniambia…
“Asante sana Mtumishi wa Mungu…Yani mimi nimeokoka sasa kuna kipindi nikaanguka nikazaa kabla ya ndoa halafu pindi naishi na mwanaume wangu nlikuwa nashika mimba mwenzangu ananiambia nitoe nami nilikuwa nikifanya hivyo lakini badae nikaona amani ikawa inaisha kila kukicha kwa kitendo nlichofanya nikaamua kwenda kwa mchungaji nikamwelezea akanikemea na akanitenga kihuduma kwa muda na akanambia nisirudie tena kutenda dhambi Mungu ataniacha vibaya sana sasa wakati nahudhuria ibada kanisani kuna mpendwa akauliza nililokuuliza mchungaji akajibu akasema mtu huyu hasamehewi tena basi tu tunaendelea kufarijiana ila hakuna msamaha tena hapo basi toka siku hiyo mimi linaniumiza sana neno hilo sijui nifanyeje ili niweze kurudisha amani yangu katika kumwabudu Mungu”.
Baada ya kunitumia ujumbe huo, nikamwambia ni sahihi kabisa alichofanya mchungaji wako kukutenga kwasababu umestahili kutengwa kulingana na maandiko kwa kitendo ulichokifanya,(1 Wakorintho 5:9-13)..Na alikujibu pia sawa, kwamba usirudie tena kufanya hivyo akimaanisha ukatubu!...lakini siku nyingine alipojibu swali kama hilo kwa mwingine akasema mtu kama huyo hana msamaha,….Nikamwambia mchungaji wako sijui Ni kwanini alimjibu vile huyo mtu wa pili lakini naamini hakumjibu huyo mtu wa pili kwa kulinganisha na tatizo ulilonalo wewe, yeye alimjibu yule pengine akimaanisha mtu aliyeacha kabisa wokovu na kukengeuka na kuiacha njia ya msalaba, na kukufuru huyo ndiye mtu ambaye Roho Mtakatifu anaondoka ndani yake kabisa kabisa!…na hatuwezi kumfariji kwasababu hata hatatamani kufarijiwa wala kutamani kanisa..ataendelea kudanganyika na kutamani mambo maovu…
2 Timotheo 3: 13 “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika”..
lakini sio wewe! Wewe bado kuna nguvu ya kutaka kutubu ipo ndani yako, kitu fulani kinachokusukuma kumrudia Mungu, ambacho ni Roho Mtakatifu…
Sasa hicho kitu cha kumsukuma kutubu endapo kisingekuwepo ndani ya huyu dada, na akawa anafurahia kuendelea na tabia hiyo, hapo ndio angekuwa pengine na hiyo dhambi isiyosameheka…kwasababu Roho Mtakatifu anayehusika katika kumvuta kutubu hayupo…(Yohana 6:44).
Tatizo hili limekuwa ni la watu wengi, hususani waliofanya dhambi za mauaji, ubakaji na utoaji mimba, mizaha iliyopitiliza katika madhabahu za Mungu…Unakuta mtu aliitenda dhambi hii sasa kasikia sauti ndani ikimshawishi kutubu lakini akikumbuka kwamba alishaua kuna kitu kinamwambia huwezi kusamehewa, hivyo anavunjika moyo moja kwa moja, mwingine alitoa mimba kadhaa, mwingine alifanya kitendo kibaya kiasi kwamba hawezi kukisema hata mbele za watu…Sasa mawazo kama hayo yanapokujia, wakati unapotaka kumgeukia Mungu, unapaswa UYAKATAE! Kwa nguvu na kuendelea kusonga mbele, kwasababu ni mawazo ya shetani!
Na pia jiepushe na kutenda dhambi hizo kwasababu madhara yake ndio kama hayo ya kuletewa mawazo ya mkandamizo kutoka kwa shetani!, usipotenda mambo hayo, shetani hawezi kukupata kwa mawazo yake. Na pia dhambi hizo ukizitenda baada ya kuamini, na kumkataa kabisa Roho Mtakatifu. kuna uwezekano mkubwa wa Roho Mtakatifu kuondoka kabisa ndani yake..usisikie tena hamu ya kumpenda Mungu na hivyo kuishia kuipinga injili na wokovu milele.
Bwana akubariki.
Maran atha!
No comments:
Post a Comment