1Wakorintho10:11 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.”
Shalom ndugu, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe milele. Nakukaribisha tuyatafakari kwa pamoja maneno ya uzima, maadamu rehema zake ni mpya kila siku asubuhi(Maombolezo 3:22-23). Leo tutajifunza hii miisho ya zamani inayozungumziwa kwenye mistari hiyo ni ipi na tutaitambuaje kama tumeifikia au kuikaribia..
Kama ukisoma mistari kadhaa ya juu kabla ya huo, utaona kuwa biblia imeandika mambo maovu na makosa waliyoyafanya wana wa Israeli walipokuwa kule jangwani mpaka ikawapelekea wengi wao wa waliotoka Misri kutokuiona nchi ya Ahadi Mungu aliyowaahidia, kama tunavyofahamu ni watu 2 tu kati ya mamilioni waliotoka Misri ndio walioiona nchi ya ahadi, na mambo yaliyotajwa hapo kuwa yaliwakosesha ni pamoja na ibada za sanamu, uasherati, manung’uniko, na kumjaribu Mungu.
Lakini mfano Mungu angeyaacha tu hivyo hivyo bila kuyaandika kwa ajili ya vizazi vya mbeleni, ni wazi kuwa na sisi pia tungeyarudia yale yale na hiyo ingetupelekea watu wachache sana kuirithi mbingu mfano wa Yoshua na Kalebu.. Lakini Mungu aliyaandika sio tu kwa vizazi vya mbeleni bali pia kwa vile vya mbali zaidi vitakavyofikiwa na miisho ya zamani.
Neno “Miisho ya zamani”, kwa lugha rahisi ni sawa na kusema mwishoni wa nyakati, au majira,..Au ni sawa na kusema pia utimilifu wa nyakati…..au kilele/ukingoni mwa nyakati….Sasa ukisikia mahali popote katika biblia inasema tunaishi katika siku za mwisho,/wakati mwa mwisho , Huo wakati kibiblia haujaanza leo wala jana bali ulianza rasmi takribani miaka 2000 iliyopita,..
1Yohana 2:18 “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho.”
Na Mambo hayo kwa mara ya kwanza yalianza kuhubiriwa na Yohana Mbatizaji pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo wakisema, TUBUNI kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia…Kwasababu walijua tayari wameshaingia katika majira ya siku za mwisho.
Lakini swali unaweza ukajiuliza kama ni hivyo, kwanini basi Bwana Yesu akiwa katika mlima wa Mizeituni alianza kuwaeleza tena dalili za siku za mwisho ikiwa tayari anafahamu kuwa yupo katika siku za mwisho, dalili nyingine za nini tena?
Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa Bwana Yesu alikuwa hazungumzii habari za SIKU za mwisho kwani tayari wakati ule ilishajulikana kuwa zile ni siku za mwisho…Bali alikuwa anazungumzia habari ya SIKU ya mwisho jinsi itakavyokuwa…dalili zitakazoonesha kuwa ule mwisho wa yote utavyokuja ..
Ni sawa tu na kusema mwaka 2020 ni mwaka wa uchaguzi, lakini uchaguzi wenyewe utafanyika mwezi wa 10, hivyo kwa namna ya kawaida mwaka wa uchaguzi unapoanza, kunakuwa na vuguvugu la kampeni, vyama vinajiweka tayari, vinaanza kufanya kampeni za nyuma ya mgongo, dalili ndogo ndogo zitaonekana kwa tabia zao, sera zao n.k. lakini kampeni rasmi hazijafunguliwa bado.. hivyo ule wakati ukifika miezi 2 kabla ya uchaguzi wenyewe kufika, ndipo Kampeni rasmi zinafunguliwa na hapo ndipo utaona mambo yanavyofanyika kwa kasi na kwa nguvu ambazo hujawahi kuziona ni kwasababu wanajua muda waliopewa na waliobakiwa nao ni mchache sana kabla ya siku yenyewe kufika..
Na ndivyo Bwana Yesu alivyokuwa anafanya, ni kueleza dalili rasmi za kukaribia kwa “siku” ile ya mwisho na sio kukaribia kwa “siku za mwisho”...akasema mtakapoona wimbi kubwa na manabii wa uongo limejitokeza, wanafanya kampeni ili kukusanya magugu matita matita basi mjue ule mwisho ule umekaribia….hayo mambo hayakuwahi kuonekana katika wakati wowote katika historia tangu kipindi cha mitume hadi kizazi hichi cha karne ya 21, kutokea kwa wimbi kubwa la manabii wa uongo namna hii, yaani kuanzia mwaka 2005 kupanda juu mambo haya ndio yameanza kujitokeza kwa kasi….hii inaonyesha kuwa tunaishi ukiongoni kabisa mwa wakati,.. kipindi cha utimilifu wa wakati.
Alisema watakuja wengi kwa jina langu wakisema mimi ni Kristo,.yote hayo tunayaona kila kukicha.. Hizi ni dalili za kukaribia kwa siku ile kuu ya kuitisha,
Alisema kutaongeza maasi, na upendo wa wengi kupoa,..Leo hii tunaona jinsi teknolojia ya simu na mitandao jinsi ilivyoleta maovu karibu na watu kuliko kipindi chochote cha nyuma, ndani ya simu ndogo tu mtu anaweza akapata mambo yote maovu yanayoendelea ulimwenguni kote, mpaka watoto wadogo sasa hauna jambo lolote la siri kwao. Mambo hayo yameanza kukolea kuanzia kipindi cha mwaka 2005 kupanda juu wala hata sio siku nyingi….Ulimwengu umeshajua kuwa siku zake zimebaki chache hivyo unafanya kampeni kwa nguvu kuielekea ile siku yake kuu ya kuangamizwa.
Na dalili nyingine kubwa Bwana Yesu aliyoizungumzia katika (Mathayo 24:32)ni kuchipuka kwa “mtini” ambao huo unawakilisha taifa la Israeli..Alisema jambo hilo likishaanza kuonekana basi tujue kuwa kizazi hicho hakitapita mpaka hayo yote yatakapotimia…
Kwa upana wa somo hili bofya link hili la kuchipuka kwa Israeli bofya hapa ⏩ Amin! Amin! nawaambia.
Hivyo unaweza kuona hapo kuwa sisi ndio watu tuliofikiliwa na miisho ya zamani.. ndio watu ambao sio tu tunaishi katika siku za mwisho, bali pia ni watu tunaoishi katika ukingo kabisa wa siku hizo…
Je! Bado mambo ya ulimwengu yanakusonga?. Bado upo njia panda? Bado unazini na mke ambaye si wako au mume ambaye si wako?, bado ni mlevi, bado ni mfanyaji mustarbation, bado ni mtazamaji pornography? Bado ni mfanyaji anasa?,bado ni mtoaji mimba, bado mla rushwa? bado tu upo buzy huna muda na injili za wokovu?... Hizi ni nyakati mbaya..Kama bado upo nje ya Kristo jitahidi uingie kabla mlango haujafungwa.
Anasema..
“20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”(Ufunuo 3:20-22)
Shalom.
No comments:
Post a Comment