"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, August 20, 2019

MATUMIZI YA DIVAI.


Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu

Kama inavyojulikana na wote kuwa Divai ina kilevi…Lakini swali linakuja kama ina kilevi kwanini Bwana Yesu aligeuza maji kuwa Divai, na kwanini Divai ilitumika katika kushiriki?..hata wakati wa kanisa la kwanza, ilitumika katika kushiriki meza ya Bwana?..Na je! Mpaka leo ni sahihi kuitumia kwa kushiriki?

Divai ni kinywaji ambacho kilikuwa na matumizi mengi zamani, Kwamfano Divai iliweza kutumika kama dawa…Ndio maana Mtume Paulo, alimwambia Timotheo asitumie maji peke yake bali atumie mvinyo…
1 Timotheo 3:23 “Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara”..
Unaona hapo? Aliambiwa atumie kwa ajili ya magonjwa yanayompata mara kwa mara, kumbuka Wakati ule, Mitume walisafiri umbali mrefu wakati mwingine wakiwa wamefunga kwenda kuhubiri injili, hivyo ile hali ya kukaa na njaa muda mrefu, utumbo ulikuwa unajisokota, kwahiyo suluhisho la hayo, ilikuwa mtu anakunywa kiasi kidogo cha Divai na ndipo ale chakula kingine…Zingatia hilo Neno ‘kidogo’…biblia inasema hapo kidogo sio sana!..ikiwa na maana kuwa ni kiwango ambacho hakiwezi kuleta madhara ya nje kama kulewa. Ingesema kunywa mvinyo wa kutosha kwa ajili ya tumbo, tungeelewa kuwa maandiko yamehalalisha ulevi. Na pia zingatia dhumuni la kunywa divai hapo sio kulewa, au kujiburudisha, au hamu…hapana! Bali kwaajili ya tumbo, ikiwa na maana kuwa kama afya yake itakuwa vizuri hana sababu ya kuinywa hata kidogo!!

Kadhalika Divai hiyo hiyo haikutumika tu kwa ajili ya matibabu ya magonjwa au madhaifu ya Tumbo, bali pia ilitumika kwa matibabu ya nje! Kama kutibu vidonda n.k..Tunaona jambo hilo katika ule mfano Bwana Yesu alioutuoa wa Msamaria mwema…
Luka 10:30 “Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.
31 Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.
32 Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.
33 Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,
34 akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia MAFUTA NA DIVAI; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza”.
Umeona hapo?..alimpaka Mafuta na kutia Divai katika majeraha ya yule mtu. Ikionesha kuwa Divai ilikuwa na kazi pia ya kutibu vidonda!..

Sasa tukirudi katika nyakati zetu, tuna dawa zinazotibu vidonda, hatuwezi kutumia tena divai…ingawa sio dhambi wala kosa kuitumia, lakini zipo dawa zinazofanya kazi nzuri Zaidi ya divai, kwamfano kuna dawa inayoitwa SPIRIT wengi wetu tunaijua, dawa hii ni maalumu kwa kusafishia vidonda na kuua vijidudu visivyoonekana kwa macho, dawa hii inakiwango kikubwa sana cha KILEVI kuliko hata DIVAI….kilevi kilichopo ndani ya dawa hiyo ambayo wengi wetu tunaitumia pasipo kufahamu, ni kiwango kikubwa kiasi kwamba mtu akiinywa kwa bahati mbaya anayo hatari ya kuwa kipofu…Hakuna pombe yoyote duniani inayonywewa na mwanadamu yenye kiwango cha kilevi kikubwa kama hicho kilichopo kwenye Spirit.

Kadhalika, zipo pia dawa zinazotumika na wengi zenye kiwango cha kilevi ndani yake, Kwamfano kuna dawa ya kuongeza vitamin kwa kwa Watoto na watu wazima, inayoitwa SSS TONIC Dawa hii ina kiwango cha kilevi asilimia 12, kiasi kwamba mtu anayeitumia akinywa nyingi pamoja na madhara mengine atakayopata lakini pia atalewa!..ndio maana inatumika kwa kiwango kidogo sana kilichothibitishwa na madaktari kwamba hakitaweza kuleta madhara, wala kumlewesha mtu, kijiko kimoja au viwili vya chai, inatosha….sasa kwa njia hiyo iyo ndio Mtume Paulo alimshauri Timotheo atumie Mvinyo (Divai) kidogo kwa ajili ya tumbo..

Pia zipo dawa nyingi za kutuliza maumivu zimetengenezwa na kiwango fulani cha kilevi, ambazo mtu akinywa analewa… na kuna dawa za kuoshea midomo zenye kiwango cha kilevi ndani yake…

Kadhalika dawa nyingi za maji maji zinazotumika kutibu matatizo ya kifua na kukohoa, zimetengenezwa kwa kiwango Fulani cha kilevi ndani yake, kwamfano dawa kama expectorant, Chlorintmeton n.k hizi ni dawa za kifua za chupa zina kiwango cha kilevi ndani yake... kilevi hicho kimewekwa ndani yake kusaidia kuihifadhi dawa hiyo ikae kwa muda mrefu…Hivyo kwa namna moja au nyingine, watu wote wameshakunywa au kutumia kilevi pasipo kujijua kwa malengo mbali mbali kama tiba ya ndani au ya nje…lakini si kwa lengo la kulewa, wala kujiburudisha..

Sasa Divai hiyo zamani ilitumika katika kushiriki meza ya Bwana, na si kwa kulewa.. ambayo inawakilisha damu ya Yesu Kristo, na wakristo wa kanisa la kwanza walikuwa wanaitumia kwa kiasi kidogo sana katika kushiriki meza ya Bwana, na si kwa kulewa…kama tu vile mtu anayetumia mojawapo ya dawa hizo hapo juu kwa kiwango kidogo sana cha tiba, na kisiwe na madhara ya kumlewesha…Kadhalika na katika meza ya Bwana Divai ilikuwa inatumika kwa kiwango kidogo sana, kisichoweza kumfanya mtu alewe kabisa, mtu alikuwa anakunywa kiwango kidogo sana hata robo glasi inaweza isifike, kama ishara tu ya kushiriki DAMU YA YESU…Ingawa walikuwepo watu wachache waliokuwa wanakunywa kwa kiwango kikubwa mpaka kulewa! Hao ni wale ambao walikuwa ni walafi na walevi ambao… hawawezi kuupambanua vyema Mwili wa Kristo na Damu yake, na Mtume Paulo aliwakeme vikali na kuwaonya….kasome (1 Wakorintho 11:21-34).

Kwahiyo Divai kama wakristo wa kanisa la kwanza walivyoitumia kwa lengo la kushiriki, na sisi tutafanya kama wao, kwa lengo hilo hilo,tunaitumia katika kushiriki meza ya Bwana katika kiwango kidogo sana kitakachotufanya tusilewe kama wao walivyofanya…na hatunywi divai hiyo kwa hamu, wala kwa kiu, wala kwa kujiburudisha, wala hatuitumii kwa matumizi mengine yoyote ya tamaa wala ulafi..tunatumia kama ishara ya Damu ya Yesu isiyoharibika, kama Damu ya Yesu yenye matumizi mengi, kutibu mambo yote ya rohoni na mwilini, ndivyo ilivyo divai.

Kinachotokea kwenye baadhi ya makanisa yasiyokuwa ya kiroho yanatumia mistari hii ya Biblia kuhalalisha unywaji wa pombe, hivyo mtu yeyote akijisikia tu hamu, au haja ana kwenda kunywa pasipo sababu yoyote, na kulewa kwasababu Mtume Paulo kasema..’usitumie maji peke yake bali mvinyo pia’…Ndugu hiyo sio kazi ya divai kwa Mkristo, na pia pombe nyingine zozote hazijatengenezwa kwa lengo la matibabu, pombe kama hizi zinazouzwa madukani, zimetengenezwa kwa lengo la mtu kulewa, na ulafi, na kujifurahisha, hazijashauriwa hata na daktari yoyote zitumike, na wala hakuna daktari yoyote anayemshauri mtu akanywe pombe…kwahiyo ulevi wa aina yoyote ule ni dhambi…Hakuna mkristo yeyote katika agano jipya aliyelewa kwa pombe hakuna! Na wala maandiko hayajahalalisha ulevi..(Kwa maelezo marefu juu ya ULEVI, Tutumie ujumbe inbox tutakutumia somo hilo).

Vile vile kuna watu wanaotumia juisi ya mzabibu katika kushiriki, lakini ukweli ni kwamba hakuna maandiko yoyote yanayoonyesha kilichokuwa kinatumika ni pombe, bali ni Divai kama divai yenye kilevi ndio iliyokuwa inatumika.

Bwana akubariki sana.

Maran atha!

No comments:

Post a Comment