Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia”,10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.12 Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?13 Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya”.
Hata ilipotimia siku ya Pentekoste!!...Sentensi hiyo inaonyesha ni kama vile siku hiyo tayari ilikuwa imepangwa…na hivyo ni kama vile ilikuwa inangojewa ifike…ni sawa na mtu aseme… “hata ilipotimia siku ya kufikishwa kizimbani” au “hata ilipotimia siku ya kufanya kufanya mtihani”…sentensi hizo zinaonesha kuwa kuna tarehe Fulani zilizokuwa zimepangwa kwa tukio Fulani…Biblia inazidi kusema kuwa “walikuwako wote mahali pamoja”..kuashiria kuwa walishaambiwa wasisambaratike bali wakae pamoja mpaka hiyo siku ifike.
Mstari wa pili unasema 2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi”.
Uvumi uliotokea hapo sio uvumi wa upepo huu wa asili tunaoujua, ambapo ukitokea miti inapepesuka, mapazi yanapeperuka n.k bali ni uvumi wa upepo wa roho, ambao ili kuulezea vizuri biblia imefananisha na kama uvumi wa upepo wa kawaida wa asili…ndio maana hapo biblia inasema UVUMI KAMA, Zingatia hilo neno ‘kama’ ikiwa na maana sio upepo wa kawaida bali ni mwingine wa Roho
Sasa huu ni upepo wa Roho ambao hauwezi kuonekana kwa macho, kazi yake ni kumpeleka mtu mahali ambapo hajataka kwenda kwa nguvu zake mwenyewe, au hajataka kufanya kwa nguvu zake mwenyewe au kutamka kwa akili zake mwenyewe…Huu ndio Bwana Yesu aliosema mahali Fulani kuwa mtu aliyezaliwa mara ya pili anakuwa nao..
Yohana 3:8 “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho”.
Unaona kila mtu aliyezaliwa kwa Roho Mtakatifu kuna upepo Fulani wa Roho unaompeleka mahali asipopachagua yeye…Kwa upana zaidi wa somo hili la upepo wa Roho, nitumie ujumbe inbox nikutumie maelezo yake..
Sasa uvumi huu wa Upepo wa Roho ulipowashukia hawa watu siku ile ya Pentekoste ni nini kiliwatokea?..Tusome
Mstari unaofuata unasema….. “3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.
Ni wazi kuwa upepo ule ungewasukuma kuzungumza kitu ambacho hawajataka kuzungumza kwa akili zao, kingewafanya waende mahali ambapo hawajataka kwenda kwa akili zao, kama tu vile upepo wa kawaida unapovuma mahali unaweza hata kuezua mabati na kuwahamisha watu kuwatupa mahali ambapo hawajataka kwenda..
Na ndicho kilichotokea hapa, wote wakajikuta wanaanza kuzungumza lugha ambazo kwa akili zao hawajataka kuzizingumza bali wamesukumwa kuzizungumza.
Na biblia inasema kukawatokea “ndimi”…ndimi ni wingi wa neno “ULIMI”..Na ulimi tafsiri yake iliyotumika hapo sio ulimi tunaotumia kula, bali “LUGHA”…Kwahiyo hapo ziliwashukia ‘lugha’…Sasa swali ni je! Ni lugha moja? Au ngapi?...Jibu lipo hapo hapo..’ ‘zikawatokea ndimi zilizogawanyikana’….yaani ziliwatokea lugha zilizogawanyikana…sio lugha moja…bali nyingi, na kila mtu iliyomshukia ilikuwa na tofauti na ya mwenzake…Ni kama tu kilichotokea pale Babeli, kila mtu alijikuta anaongea lugha yake…
Na biblia inasema wote wakaanza kuzungumza kwa lugha mpya, kila mmoja ya kwake tofauti na mwingine, kwa jinsi Roho alivyowajalia..ikiwa na maana kuwa si kwa jinsi ya akili zao bali kwa jinsi Roho alivyowajalia.
Na pia kumbuka Ndimi zilizowatokea zilikuwa ni ndimi za Moto, yaani lugha za moto!..Lugha za moto ni tofauti na lugha za kawaida.
Lugha za moto au ndimi za moto ni lugha ambazo mtu aliyejawa na Roho Mtakatifu anazizungumza ambazo zimejaa Neno la Mungu linalochoma nafsi ya Mtu anayesikia na kumfanya atubu au aache uovu anaoufanya…Na lugha hizi za moto/ndimi za moto hazipo tu kwa wahubiri wanaozungumza kwa njia ya maneno, bali hata kwa waimbaji wanaoimba nyimbo zinazowabadilisha watu wanaosikia na zinazomtukuza Mungu, hizo ndio lugha za moto au ndimi za Moto ambazo pia ziliwatokea hawa watu siku ya Pentekoste.
Kama walikuwa watu 120, pale walipokusanyika, upepo wa Roho uliposhuka, lugha 120 zilitokea pale pale, labda ingekuwa ni nyakati hizi, zingesikika lugha 120 tofauti tofauti watu wale wakizizungumza, kama ni kiingereza, kichina, kimasai, Kiswahili, kimakonde, kifaransa n.k
Na maneno waliyokuwa wanazungumza yalikuwa ni maneno ya kumtukuza Mungu katika hizo lugha walizokuwa wanazungumza, labda mmoja alikuwa anasema…’ ‘wewe Bwana unaweza kwa lugha ya kichina’…mwingine ‘tubuni ufalme wa Mungu umekaribia kwa lugha ya kifaransa’…labda mwingine tena akasikika akisema ‘utukufu una wewe ee Mungu wa miungu kwa lugha ya kiswahili’ n.k
Sasa Yerusalemu kipindi hicho kulikuwa na watu kutoka duniani kote waliokuwa wanakuja kuabudu, kila mmoja akasikia watu wanazungumza kwa lugha ya walikotokea, wakashangaa sana…Ni sawa leo uende kijiji cha china huko katikati kabisa halafu usikie mtu mchina anamsifu Mungu kwa lugha ya kwenu ya kihaya? Lazima utashangaa huyo mtu kajuaje hiyo lugha na hali yeye ni mchina na hajawahi kufika Tanzania na wala hawajui watanzania…Ndicho kilichotokea pale siku ya Pentekoste…watu kutoka kila kona walisikia lugha zao zikizungumzwa Yerusalemu na watu waliojazwa Roho….Na watu kuona hiyo ishara ikawaogopesha sana! Wakawaendea na kuwauliza maana ya mambo hayo ni nini? Ndipo wale waliojazwa na Roho na kusukumwa na upepo wa Roho na kuanza kusema kwa ndimi za moto wakawaambia…
Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi’’.
Unaona maana ya kunena kwa lugha mpya?..sio haya machafuko ambayo tunayaona sasahivi, watu wanazungumza maneno yasiyojulikana na hakuna mtu wa kutafsiri, Roho Mtakatifu hayupo hivyo! Mmoja anaponena lazima wawepo wafasiri anayesikia kile kilichonenwa,kama hapa siku ya pentekoste watu waliokuwa nje walisikia lugha zao za asili hao tayari walikuwa ni wafasiri…sasa endapo wangesikia watu wanazungumza lugha zisizoeleweka na kisha hakuna mtu wa kuwafasiria wangevutwaje kwa Kristo?
Ndugu, ndimi hizi za moto..bado zinapita sasa..Unaposikia injili na unaona unakuchoma ndani ya moyo wako na kukuvuta utubu! Fahamu kuwa ni Roho Mtakatifu anakuvuta kwake…anataka ugeuke uache dhambi na anasa, na mabaya yako yote, akuoshe kwa damu yake.
Biblia inasema hao watu baada ya kuchomwa mioyo yao? Wakawauliza mitume wafanyaje?!...Pengine na wewe una swali hilo hilo leo?...Nifanyaje?..Jibu lipo hapo hapo kwenye biblia mstari unaofuata..
“Tubu ukabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi”..
Hivyo hapo ulipo tenga dakika chache peke yako, tubia dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa…unakusudia kuacha uasherati kama ulikuwa unaufanya, rushwa, utukanaji, ukahaba, wizi, ulevi, anasa, ushoga, ulawiti, uuaji, usagaji, utazamaji pornograph, ufanyaji masturbation, n.k na kisha katafute ubatizo sahihi, wa kimaandiko kama ulivyoyasoma hapo juu, ubatizo sahihi ni wa kuzama mwili wote kwenye maji na kwa jina la BWANA YESU huo utakufanya umpe Roho Mtakatifu kibali cha kufanya kazi ndani yako..kwa kufanya hivyo utakuwa umetimiza matakwa yote ya Mungu anayotaka juu ya maisha yako..na kujiweka katika mstari mzuri wa kwenda mbinguni.
Bwana akubariki sana.
www.wingulamashahidi.org
No comments:
Post a Comment