Kama vile wema na fadhili zake hazikomi kutufuata siku zote za maisha yetu basi na Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lizidi kubarikiwa daima, Milele na milele.Amina. Karibu tujifunze maneno ya uzima.
Kama wanavyosema ni heri mtu ufe kwa kupigwa rasasi kichwani ambapo ndani ya sekunde chache tu unajua utakuwa umeshaondoka kuliko kufa kwa njaa, kufa kwa kukosa maji au chakula, kwani kifo cha namna hiyo huwa ni cha taratibu na cha mateso ya muda mrefu,.
Biblia yenyewe inakubaliana na hayo maneno tukisoma katika Maombolezo 4:9 “Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba.’’
Unaona na hiyo sio katika mwili tu, bali pia ipo katika Roho ni heri wale watu ambao Mungu alishawauwa kiroho siku nyingi, kuliko wale watu ambao bado wapo hai, wana hangaika huku na huko kutafuta chakula cha rohoni lakini hawakipati, watu wa namna hiyo kifo chao cha kiroho kinakuwa ni kibaya sana na cha mateso mengi..
Mwanzoni mwa mwaka wa 2007 nikiwa mimi pamoja na ndugu wengine 5,Mungu alituambia waziwazi kwa unabii kuwa kuna kipindi cha ukame kinapita duniani kote, Kwa wakati huo sikujua ni kwa namna gani njaa itakuja nilidhani Neno la Mungu litakuwa halihubiriwi kabisa, Kumbe sivyo.
Sikuzote ili kujipima kama upo katika njaa au haupo, ni uwezo wa kutambua ubora wa chakula unachokula, jaribu kufanya uchunguzi kaa siku moja bila kula kuanzia asubuhi mpaka jioni halafu uletewe maharage ya juzi uambiwe ule, nakuambia utauona ni mtamu kweli, lakini subiri njaa ile iwe imeshapoa halafu uletewe maharage yale yale ule, moja kwa moja utaanza kuona kasoro nyingi zilizopo katika yale maharage ambazo hapo mwanzo hukuziona, pengine utasema maharage gani haya hayana ladha, hajaungwa vizuri kwanza yamechacha, na yamezidi chumvi hayafai kuliwa yataniletea kiungulia..
Husemi hivyo kwasababu ya dharau ya shibe hapana lakini unazungumza ukweli wake kuwa sio bora, Sasa hapo ni kwasababu ile Njaa mwanzoni ilikudanganya hata kwa vitu visivyokuwa na manufaa kwa mwili wako kuviona vinafaa. Biblia inasema:
Mithali 27:7 “Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.”Ndivyo ilivyo katika hizi siku ambazo kila mtu anajua kuwa ni za mwisho, Mungu alisema ataleta njaa duniani kote, si njaa ya kukosa chakula cha kimwili, bali njaa ya watu kukosa kuyasikia maneno yake..
Amosi 9:11 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.
12 Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.
13 Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu.
14 Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.”
Sababu hiyo basi njaa hiyo inawatafuna watu leo hii kiasi cha kufikia hatua ya kuoana hata yale mafundisho manyonge kuwa ni yenye nguvu..yale mafundisho ya uongo kuwa ni ya kweli.
Kila ufunuo, kila unabii unaokuja hata kama haumjengi mtu, basi utapokelewa tu kwa moyo wote,na watu wanashukuru Mungu kwa huo, hiyo yote ni kwasababu ya njaa. Hata mtu akisema mimi ni YESU au Mungu, huku akitoa maandiko yake machache yanayothibitisha anachokisimamia bado watu wataona ni Neno la Mungu lililo hai …Kusingekuwa na njaa, manabii wa uongo na waalimu wa uongo wasingepata sehemu ya kupelekea mafundisho yao manyonge, lakini kwasababu uhitaji upo mkubwa hata vile feki navyo vinapata soko..kama tu vile simu za kichina.
Ndugu, janga hili la rohoni, linanihusu mimi na wewe, tusipotaka kumwendea na kukaa chini ya Yusufu wetu wa sasa ambaye ni YESU KRISTO, atupaye chakula sahihi cha roho kwa wakati husika..Hakika tutakufa kwa kiu na kwa njaa. Tutazunguka huko na huko, tutakwenda Nigeria, china mpaka ulaya, tukidhani kule ndipo chakula kipo, lakini mwisho wake baada ya mahangaiko hayo na mateso hayo yote tunakufa kwa njaa na kwenda kuzimu. Embu jiulize taabu zako zote, unaishia kwenda kukutana na mlevi kuzimu ambaye hajawahi hata kuwa na shughuli na Mungu.
Ashukuriwe Mungu, Ni Bwana Yesu pekee aliyeahidi atatupa msaidizi ambaye atatufundisha na kuturejesha katika kweli yote..Na msaidizi huyu ni Roho Mtakatifu, mtu yoyote atakayempokea huyu hakika hata potea, wala hatakufa kwa njaa kwani kama alivyoahidi atahakikisha anakaa mahali ambapo chakula halisi cha kweli kipo kwa maana palipo mzoga ndipo watakapokusanyika TAI(Mathayo 24:28)
Unachopaswa kufanya ni kumtii Kristo kwa kumkaribisha aje ndani ya maisha yako akubadilishe uwe kiumbe kipya. Na hiyo inakuja kwa kutubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, na kwenda kubatizwa katika ubatizo wa maji mengi kwa jina lake, kama ishara ya ondoleo la dhambi zako. Kisha ukishafanya hivyo yeye mwenyewe atakuwa na jukumu la kukupa Roho wake Mtakatifu akuongoze na kukutia katika kweli yote(Yohana 16:13). Huyo ndiye atakayekupa wewe nguvu ya kuendelea mbele, wakati wa kipindi hichi kikali cha njaa..
Usijaribu kujitafutia mwenyewe chakula kwa kanuni zako, utakufa kwa njaa..Ndio utafananishwa na hao biblia inayosema “watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione (Amosi 9:12)”…Ni kwasababu gani? Ni kwasababu hawakutaka kufuata uongozi wa Roho Mtakatifu,
Ndugu Roho Mtakatifu ndio salama yetu katika haya majira ya siku za mwisho za njaa tunazoishi. Bila Roho Mtakatifu, Hakuna mbingu wala hakuna kumjua Mungu, bali ni kukisubiria kifo..Mtafute yeye angali yupo, kwa maana ahadi hiyo ni ya kila mtu amwombaye Baba..
“…je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”(Luka 11:13)
Ubarikiwe sana.
Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.
No comments:
Post a Comment