"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, August 3, 2019

MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.


Tukisoma kitabu cha Waamuzi ile sura ya 19, tunaona habari ya mtu mmoja Mlawi ambaye alikuwa na suria wake mzinifu, Hiyo pekee haikutosha yule suria aliondoka na kurudi nyumbani kwa baba yake, Lakini kwa jinsi Yule mtu alivyokuwa anampenda Suria wake miezi minne ilipoisha alifunga safari kutoka mjini kwake na kwenda kumfuata nyumbani kwa baba yake ili kumsihi arudi nyumbani.

Lakini alipokuwa njiani kurudi nyumbani na giza limeshaingia alikutana na mzee mmoja aliyetoka shamba ambaye alimwona amesimama barabarani hana pa kulala, hivyo alimkaribisha nyumbani kwake alale usiku ule ili kesho yake aendelee na safari yake, lakini kumbe huku nyuma wenyeji wa ule mji walikuwa wanawafuatilia, na usiku ule ule wakamfuata Yule mzee nyumbani wakigonga mlango wake kwake wakisema tutolee huyo mtu tulale naye, mambo yale yale yaliyotendekea sodoma yanajirudia tena Israeli, lakini Yule mzee alikuwa mkarimu sana, akawasihi awape binti yake ambaye ni bikira wamfanyie ouvu wao, wamuache Yule mgeni aliyeingia nyumbani kwake akae katika hali ya usalama, lakini walikataa, nusu wamuue Yule mzee, ndipo Yule mtu akaamua kutoka akawapa suria wake wamfanye wanachotaka kumfanya..
 
Kwa ukatili mkubwa sana wale watu walimbaka Yule mwanamke usiku kucha, tengeneza picha pengine wanaume zaidi ya 100 walikuwa pale nje, mpaka kunapambazuka bado wanaendelea kumfanyia uovu ule, hadi walipoona mwanga unakaribia kutoka ndipo wakamwacha wakaondoka, Yule mwanamke kufika tu mlangoni mwa ile nyumba hali ikawa mbaya zaidi akafa pale pale, Asubuhi mume wake anafungua mlango amwambie amka tuondoke zetu, anakutana na maiti mlangoni..

Kama tunavyosoma habari akamchukua Yule mwanamke akaenda kujifungia nyumbani mwake mwenyewe, akamkata kiungo baada ya kiungo akavigawa mafungu 12, kisha akavichukua na kwenda kuviweka katika mipaka yote ya Israeli kwa idadi ya makabila yao, ndipo watu kuona kitendo kile walishtuka sana, wakijiuliza jambo hili maana yake ni nini? Kwani halijawahi kutokea katika Israeli tangu walipotoka Misri, Ndipo Yule mtu akaanza kuwaelezea jinsi tukio lilivyokuwa.
Watu wote wakasema haiwezekani ni lazima hao watu ambao wamefanya hivi huko Benyamini watolewe wauawe ili kuondoa ouvu Israeli, lakini Benyamini walipoambiwa wawatoe watu hao waligoma..Kwao halikuwa kama jambo la kushtusha sana, kuonesha ni jinsi gani walivyokuwa wameoza kwa uovu kama wa Sodoma na Gomora..Ndipo makabila yote 11 ya Israeli yaliyosalia yakaapa hawatakaa wawape binti zao, na zaidi ya yote wakakusanyika kwenda kuisambaratisha Benyamini juu ya uso wa Israeli.

Siku ile ile watu mashujaa wakahesabiwa, Ndipo wakamuuliza Mungu juu ya kabila lipi lianze kwenda kupigana nao, ndipo Mungu akawajibu na kuwaambia lianze kwenda kabila la Yuda. Lakini walipokwenda mambo yalikuwa tofauti na walivyotazamia, badala ya kuwaangamiza Benyamini wale waovu wao ndio walioangamizwa, walipigwa kwa mapigo makuu, watu 22,000 wa Israeli waliuliwa siku ile.

Lakini Israeli hawakukata tamaa tena, walijipanga upya kwa mara ya pili, tunasoma.
Waamuzi 20:22 “Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza.
23 Wana wa Israeli WAKAKWEA JUU NA KULIA MBELE ZA BWANA HATA JIONI; wakamwuliza Bwana, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? Bwana akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye.
24 Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili.
25 Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga.
Tunaona hapo japo Mungu aliwaambia wakwee kupigana nao lakini bado hawakufua dafu, watu wengine 18,000 wa Israeli waliuliwa vibaya na jeshi dogo la Wabenyamini.
Ni rahisi kusema, mbona Mungu si mwaminifu kwetu, mbona tumelia mbele zake siku nzima na ametupa majibu kabisa tukwee lakini matokeo yanakuja tofauti?, mbona tuna lengo zuri la kumwondolea uovu Israeli, lakini waovu ndio wanazidi kufanikiwa na kututukana.

Lakini tunasoma, mara ya Tatu walipokwenda mbele za Bwana, hawakwenda na vilio na kufunga tu peke yake, lakini pia wanamtolea Bwana Sadaka za Amani na za kuteketezwa.Tusome..
Waamuzi 20:26 “Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za Bwana, wakafunga siku hiyo hata jioni; NAO WAKASONGEZA SADAKA ZA KUTEKETEZWA NA SADAKA ZA AMANI MBELE ZA BWANA.
27 Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa Bwana (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo,
28 na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? Bwana akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako.
29 Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote.”
Tunasoma safari hii Mungu hakuwaambia wakwee tu, bali aliongezea na kuwaambia “Kesho nitawatoa na kuwatia mikononi mwenu”. Na baada ya hapo ukiendelea kusoma utaona jinsi Benyamini ilivyoshambuliwa na kuangamizwa vibaya mno, kwa nafasi yako pekee soma habari yote ilivyoishia utaona jinsi maangamizi yale yalivyokuwa makubwa…Ilikuwa bado kidogo tu lile kabila lingefutika lote, watu wa Benyamini walibakia wachache kama faru tulionao mbugani, Na kama sio Israeli kughairi mashambulizi yao na kuwaruhusu wale waliosalia wakaibe wake huko leo hii tungekuwa tunayafahamu na kuyaosoma makabila 11 tu ya Israeli.

Lakini kiini cha somo tunachojifunza hapo ni nini?. Haijalishi unachokwenda kuomba mbele za Mungu ni chema kiasi gani, haijalishi unalia mbele za Mungu kiasi gani, haijalishi unafunga wiki, miezi au miaka kiasi gana, kuna mambo mengine hayawezi kutoka hivi hivi bila ya kuhusisha SADAKA. Kama vile hao walivyotoa sadaka za aina mbili za kuteketezwa na za amani, vivyo hivyo na sisi katika agano jipya tunazo sadaka za aina mbili, Ya kwanza ni ya kuteketezwa ambayo ni Yesu Kristo, aliyeteketezwa kwa ajili yetu,alichinjwa kwa ajili yetu, Hivyo Kama upo nje ya Yesu Kristo ndugu halafu unamwendea Mungu na kumwomba akupiganie katika vita vyako, nataka nikuambie utaishia pabaya na kuvunjika moyo, na kuona kama Mungu hayupo. Vile vile na wewe uliye ndani ya Kristo, unamwomba Bwana akupiganie katika majaribu yako, halafu unakwenda mbele zake mikono mitupu, kuna uwezekano mkubwa wa tatizo lako kutokuondoka… Kwasababu wapo wakristo ambao ni Hodari wa kuomba kweli kweli na kulia na kufunga mfano wa hawa wana wa Israeli, lakini kwenye suala la kumtolea Mungu, wanadharau, wanaona kama Mungu hatazami hilo, wanasema yeye sikuzote huwa anatazama moyo. Nataka nikuambie, Mungu anapendezwa na moyo wa shukrani, pale unapomtolea Mungu mfuko wako anaona huyu mtu ananithamini, sio kwamba anayo haja ya fedha yako, lakini ni utaratibu wake, anapendezwa zaidi ya wenye moyo wa utoaji. unapomwendea Mungu na kumwomba akufanikishe katika jambo lako zito au jepesi jifunze kuambatanisha na sadaka ipeleke madhabahuni pake ndugu.
Unaweza kusema ooh! Mungu ameniambia yupo pamoja na mimi, Mungu kanionyesha maono, Mungu kanipa unabii, lakini utashangaa kwanini bado unashindwa pamoja na maono yako yote, Ni kwasababu unakuwa kama hawa Waisraeli, Mungu kila wakati alikuwa anawaambia Kweeni, ni yeye kabisa alikuwa anawasapoti katika walichokuwa wanakifanya lakini tunaona japo walikuwa na jeshi la watu LAKI NNE, walipigwa na jeshi dogo la watu ELFU 26 tu la Wabenyamini. Na wewe vilevile usishangae kushindwa na mambo madogo, ukilinganisha na nguvu iliyoiwekeza katika hilo mbele za Mungu, Tatizo linaweza kuwepo hapo.

Anza kujifunza kumtolewa Bwana, naye atazifanya njia zako kuwa nyepesi.

Bwana akabariki. Tafadhali “Share ” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.

No comments:

Post a Comment