"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, August 3, 2019

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?


Biblia inasema katika..
1 Wakorintho 14: 5 “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa”.
Wengi wanausimamia mstari huu kama msingi wa kuwa ni lazima watu wote wanene kwa Lugha kwasababu maandiko haya yanasema hivyo, Lakini leo hebu tuingie ndani Zaidi ili tusiwe wachanga kifikra na kujikuta tunashindwa kuyaelewa maandiko vyema…

Biblia inasema katika 2 Timotheo 2: 15 “ Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli”

….Hapo inasema ‘ukitumia kwa halali Neno la kweli’..ikiwa na maana kuwa kuna kutumia visivyo halali Neno la Kweli…Bwana atusaidie katika hilo, kutumia halali Neno la Kweli..
Sasa kwa mhutasari ni Kwamba kitabu hichi cha Wakorintho wa kwanza kimeandikwa na Mtume Paulo, aliandika waraka huu kwa wakristo walioko mahali panapoitwa Korintho, na kwasababu Neno la Mungu halina tarehe ya kumaliza matumizi, hata sasa sisi ni Wakorintho kwahiyo kila kilichoandikwa huko kinatuhusu sisi asilimia mia moja..Na Neno la Mungu ni kweli, na hakuna mahali popote limekosewa.

Sasa kabla ya kufika kujua ni kwanini Mtume Paulo aliliandikia kanisa kwamba…‘anataka watu wote wanene kwa lugha’ ni kwanini alisema vile?…Ni vizuri kwanza tukarudi nyuma kidogo kwenye wakara huo huo, mlango wa 12…ambao aliandika siku hiyo hiyo aliyoandika sura hiyo ya 14, na kwa kutumia kalamu hiyo hiyo moja… …aliandika hivi kwa uweza wa Roho.
1Wakorintho 12: 28 “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.
29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?.
30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? WOTE WANENA KWA LUGHA? WOTE WAFASIRI?”
Hizo ni sura mbili tu nyuma, yaani kurasa mbili tu nyuma, ambapo Mtume Paulo alitangulia kusema…JE! WOTE WANENA KWA LUGHA?

Sasa swali linakuja hapo? Mtume Paulo alikuwa anajichanganya hapa kwenye sura ya 12 aseme si wote waweza kunena kwa lugha…halafu mbele kidogo tu pengine hata haijachukua dakika 20 aandike ‘watu wote ni lazima wanene kwa lugha’?...Hilo linaingia akilini kweli?..Hebu chukua dakika chache kutafakari kama hilo linakuingia akilini…Mtu hawezi kuongea vitu viwili tofauti kwenye waraka huo huo mmoja afadhali hata ingekuwa ni nyaraka mbili tofauti..lakini ni huo huo mmoja.

Kwahiyo hapo pasipo hata kutumia nguvu nyingi ya kufikiri utagundua kuwa Mtume Paulo hawezi kujichanganya kwenye waraka huo huo mmoja tena kwenye sura zinazokaribiana kiasi hicho…kwamba hapa aseme hivi na huku hivi…Hivyo ni wazi kuwa Ni sisi wasomaji ndio hatujakielewa alichokiandika Paulo. Kama Mtume Petro alivyosema mahali Fulani…
2 Petro 3:15 “Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; 
16 vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni VIGUMU KUELEWA NAYO; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, HUYAPOTOA, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe”.
Unaona watu wasio na elimu, Biblia inasema wanayapotoa maandiko, hususani yaliyaondikwa na Paulo… na hiyo ni kutokana na kuchukua kipengele kimoja cha maandiko na kukishikilia hicho hicho pasipo kusoma habari yote mpaka mwisho na kuomba msaada kutoka kwa Roho Mtakatifu kuyaelewa maandiko.

Sasa ili tuelewa ni kwanini Mtume Paulo alisema hapo kwenye mstari wa 14 kwamba “nataka ninyi nyote mnene kwa lugha”..Hebu turejee tena kwenye hicho hicho kitabu cha 1Wakorintho mlango wa 7..Biblia inasema…
1 Wakorintho 7: 7 “Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.
8 Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.
9 Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”.
Hapo kwenye mstari wa 7 Mtume Paulo hajasema, “ninyi nyote mnatakiwa muwe kama mimi nilivyo”, bali anasema apendalo ni kwamba watu wote wawe kama alivyo….hiyo ni kuonesha kuwa ni tamanio lake binafsi kwamba watu wote wawe kama yeye alivyo katika hali yake ya kutokuoa pamoja na karama alizonazo.. na sio sheria au agizo la Mungu, ndio maana hapo mbele utaona anasema ‘WALAKINI KILA MTU ANA KARAMA YAKE’…Ikiwa na maana wengine wameitiwa kuoa, na wengine kutokuoa kwa ajili ya ufalme wa mbinguni…sio kila mtu ambaye hajaoa au hajaolewa anafanya mapenzi ya Mungu, wengine karama zao ni lazima waoe au waolewe…Lakini Paulo hapo juu anasema apendalo ni kwamba watu wote wawe kama yeye alivyo…sio mmoja bali wote wawe kama yeye!..sasa kwa sentensi hiyo hatuwezi kumhukumu Paulo kwamba katuagiza watu wote tusioe au tusiolewe!!

Sasa ukilinganisha sentensi hiyo utaelewa ni kwanini katika waraka huo huo alioundika siku moja, na kalamu moja, mbele kidogo kwenye sura ya 14 anasema maneno haya…’Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha’…utaona kuwa hapo ni yeye anataka (yaani matamanio yake binafsi) na sio kwamba ni agizo la Mungu, kwamba kila mtu anene kwa lugha… kwasababu kila mtu anayo karama yake kama alivyotangulia kusema katika mlango wa 12…..kwamba sio wote wanaweza kunena kwa lugha, wala si wote wanaweza kuwa waalimu,nk. huyu anaweza kuwa hivi yule vile kwa jinsi Roho apendavyo…
Kwahiyo ndugu, katika Waraka huu wa Paulo kwa wakorintho ni vizuri kuelewa matamanio ya Paulo na maagizo ya Mungu…ukichukua kipengele kimoja tu! Cha maandiko na kukishikilia hicho pasipo kulinganisha na sehemu nyingine za maandiko ni rahisi kutikiswa na kila aina ya upepo wa mafundisho. Wengi wamechukuliwa na uongo wa shetani kwa njia hiyo…

Mafundisho haya ya uongo kwamba kila mtu ni lazima anene kwa lugha ndiyo yaliyozagaa sasahivi kila mahali…watu hata wasio na hiyo karama utawasikia wanazungumza mambo yasiyoeleweka, na hiyo yote ni kwasababu hawajayaelewa maandiko…au wamefundishwa visivyopaswa…Mtu akimpa Kristo Maisha cha kwanza ataulizwa kama amenena kwa lugha au la!..akisema bado, basi ataambiwa bado hajampokea Roho Mtakatifu…Ndugu usidanganyike…karama hizi Mungu anagawa kama apendavyo yeye si kama apendavyo mtu Fulani, Vinginevyo utakuwa unafanya kwa akili, na sio kama Roho anavyokujalia.

Hata hivyo katika kanisa la watu 100 pengine waliopewa hiyo karama unaweza kuta ni mmoja au wawili, au watazidi hiyo idadi kidogo lakini si sana…wengine Roho Mtakatifu unakuta amewapa karama nyingine tofauti na hiyo..pengine wengine wawili watatu tena watakuwa manabii, wengine watano watakuwa wainjilisti, wengine watano watakuwa waalimu, wengine wachungaji, wengine masaidiano, wengine faraja, wengine Neno la Hekima, wengine miujiza, Imani n.k

Mwisho wa siku unakuta idadi yote ya mkusanyiko kila mtu anasehemu yake ya kuchangia ya kipekee tofauti na ya mwingine..lakini kulazimisha kwamba ni lazima wote wawe manabii, wote wawe wachungaji, wote wainjilisti,wote wanene kwa lugha ndio mwanzo wa kukaribisha roho ngeni…utasikia mtu hata sio nabii lakini anatoa unabii feki kwa akili zake na kusema Bwana asema hivi, kumbe ni akilli zake, na hiyo inasababisha kutatokea mashindano makubwa na kumzimisha Roho, mahali popote ambapo unaona kanisa zima lina nena kwa lugha, au kanisa zima wanatabiri, au kanisa zima ni wachungaji, au waalimu.. fahamu kuwa hapo kuna machafuko…hiyo ni kulingana na maandiko!..
1 Wakoritho 14:23 “Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je! Hawatasema ya kwamba mna wazimu?
24 Lakini wote wakihutubu, kisha akaingia mtu asiyeamini, au mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote;
25 siri za moyo wake huwa wazi; na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudifudi, na kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka”.
Hivyo kwa kuhitimisha ikiwa unanena maneno yasiyoeleweka kwa akili zako, ni heri uache, au umwombe Mungu akupe lakini usitoe matamshi ambayo unayafikiria kwenye akili zako mwenyewe..Lugha inaposhuka katika kinywa cha mtu kwa uweza wa Roho, akili yake haina matunda, kinywa chenyewe ndio kinanena..Kama hiyo haipo kwako, omba tu kawaida. Na Bwana atakusikia.

Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment