Luka 14:12 “Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.
13 Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu,14 nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki”.
Katika
habari hii, tunaona Bwana Yesu alialikwa na mtu mmoja mkuu sana
miongoni mwa Mafarisayo ale chakula cha mchana nyumbani kwake, na bila
shaka mtu huyu alikuwa ni tajiri, na katika karamu yake alialika watu
wakuu, watu wa maana, na si watu wa kawaida kawaida tu, Lakini kuna kitu
ambacho Bwana Yesu alikiona kimepunguka katika ukarimu wake mwema wa
kuwaalika watu na wageni katika shughuli zake, kwani si wote wenye moyo
kama huo.Wengine wanaweza wakawa ni matajiri na wakuu, lakini wakala
vitu vyao peke yao, lakini huyu alikuwa watofauti kidogo.
Lakini
pamoja na hayo, Bwana Yesu aligundua watu aliowaalika walikuwa ni
matajiri tu, watu wenye uwezo kama yeye, Hivyo Bwana Yesu kwa kuliona
hilo ili kumsidia kuifanya taabu yake isiwe bure, ndipo akamwambia kwa
kumshauri wakati mwingine, kuwa atakapofanya sherehe awaalike watu
wasiokuwa na uwezo wa kumlipa mfano wa hicho alichokifanya..Kwasababu
akiwaalika watu wenye uwezo, wale watu nao watarudisha mapigo siku moja,
watamwalika na yeye kwenye karamu zao na thawabu yake itakuwa
imeshalipwa na wao, lakini mbinguni hatakuwa na kitu, hivyo ili taabu
yake na wema wake uwe na nguvu idumuyo, siku nyingine akifanya karamu
kubwa kama hiyo, asiiachie thawabu yake ilipizwe na wanadamu bali ije
ilipizwe na Mungu katika siku ya ufufuo wa wenye haki, hivyo awaalike
watu wasiokuwa na uwezo wa kumfanyia kama kile alichowafanyia.
Hata
leo hii, yapo mambo mengi tunayafanya tukidhani tutalipwa tutakapofika
mbinguni kwa ukarimu tunaoufanya..Kwa mfano leo hii labda kutokee
mchango wa sherehe fulani ni rahisi kuchangia harusi ya boss wako, au
mfanyakazi mwenzako kwasababu unajua kuna siku moja na wewe utahitaji
wakuchangie kwenye sherehe yako, au ya ndugu yako. Lakini ukisikia yupo
jirani yako ambaye ni maskini hana mbele wala nyuma kipato chake ni
kidogo hata hakimtoshelezi yeye mwenyewe, halafu mwanawe anataka kuoa,
hivyo anahitaji sapoti yako kidogo, Ukweli ni kwamba wengi wetu tutakuwa
tayari kuingia mitini, ni kwasababu gani?, Ni kwasababu tunaona mbeleni
huyu anaweza asiwe na msaada kwangu siku shughuli yangu, hivyo hata
nisipomsaidia hainiathiri chochote.
Kiuhalisia
Mungu hatakulaumu ulipochangia sherehe ya Yule boss wako na kuiacha hii
ya huyu maskini, zaidi Mungu atakulipa, na kukulipa kwake kutakuwa ni
kwa kupitia wao, na habari thawabu yako itakuwa imeishaipata hapa hapa
duniani, juu mbinguni utakuwa huna kitu chochote. Ukinunua zawadi si
zote uzipeleke kwa marafiki na ndugu, nyingine tenga wapelekee wasio na
uwezo wa kukulipa,watu wasio na faida yoyote kwako. Unapokopesha
usikopeshe wale tu ambao watakupa na Riba juu yake..Kopesha hata na Yule
ambaye hawezi kukulipa na Riba juu yake mwenye uwezo wa kukurudishia
kiwango kile kile ulichompa.
Luka 6:35 “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, NA THAWABU YENU ITAKUWA NYINGI; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu”.
Na
ndio sababu ambayo Bwana alimshauri huyu mtu aliyemwalika, nasi tupokee
ushauri huo, tutafute thawabu zinazodumu milele. Ni kweli wakati
mwingine unaweza kuona ni mzigo kuwa msaada kwa wasiokunufaisha Lakini
thawabu yake, utaiona siku ile utakapofika mbinguni. Maana kiwango cha
hazina yako ndicho kitakachofunua utajiri utakaokuwa nao mbinguni.
“Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. (Wagalatia 6:9)”
Bwana akubariki.
No comments:
Post a Comment