Maombi yamegawanyika katika sehemu kuu tatu 1) kushukuru 2) kuwasilisha mahitaji kwa mungu 3) Kutangaza.
1) MAOMBI YA SHUKRANI; Maombi haya ya shukrani ni Dhahiri na yanajulika na Wengi, kwamfano maombi ya kushukuru ni muhimu sana, na ni wajibu wa kila mtu, kuyafanya…Na haya yanahusisha kumshukuru Mungu kwa Uzima anaotupa, kumshukuru Mungu kwa afya anayotupa, ukizingatia wakati unapumua kuna wengine wapo ICU, wengine Mochwari n.k, pia maombi haya yanahusisha kumshukuru Mungu kwa mambo yote mabaya aliyokukingia katika wiki yote iliyoisha, mwezi wote uliopita na miaka yote iliyopita nyuma yako, njiani umepishana na mapepo mengi, shetani alikuwa amepanga mauti na ajali nyingi juu yako lakini Mungu kakuepusha nazo zote pasipo hata kukuambia, uthibitisho ni wewe kuimaliza wiki salama, na pia yanahusisha kumshukuru Mungu kwa riziki zote za kiduni anazotupatia, katika shughuli zetu na mapato yetu yote,..Kwahiyo maombi haya kwa ujumla yanahusisha kumshukuru Mungu kwa mambo yote anayoyafanya tunayoyaona na tusiyoyaona. Ni maombi yanayoonesha unyenyekevu wetu mbele za Mungu na kumwonesha Mungu wetu kuwa tunathamini na kuutambua na kuujali ulinzi wake na Fadhili zake juu yetu. Kwahiyo ni sehemu ya maombi ambayo ni muhimu sana.
2) Sehemu ya pili ya maombi ni ile ya KUWASILISHA MAHITAJI YETU MBELE ZA MUNGU. Hii inahusisha kumwendea Mungu kwa unyenyekevu kumwomba atufanyie au atupatie jambo Fulani katika Maisha yetu, Tunamwendea tukiamini kuwa yeye ndiye mpaji wetu (YEHOVA-YIRE). Tunamwomba azidi kutupa riziki zetu, azidi kuzifanikisha kazi zetu za mikono, azidi kutupa afya, azidi kutuepusha na yule mwovu na mipango yake yote, azidi kutupa Neema ya kumjua yeye Zaidi popote tuendapo atukutanishe na injili yake na kuitii, azidi kutupa mioyo ya nyama na si ya jiwe katika kutenda mapenzi yake, azidi kutupa hekima, tunamwomba Bwana azidi kutupa furaha, amani, upendo pamoja na kibali kila tuendapo, na kutufanikisha katika mambo yote katika masaa ya siku yaliyobakia, wiki na katika mwezi huu na unaokuja. Hapa tunamwomba Mungu atuepushe na kila jaribu lililopangwa na shetani kinyume chetu mbele yetu..Kama Bwana alivyosema mahali Fulani “Ombeni kwamba msiingie majaribuni. (Luka 22:40)”.
Ikiwa na maana kuwa usipoomba ni lazima utaingia majaribuni tu!..Wakina Petro usiku ule Bwana aliwaambia waamke kusali ili wasiingie majaribuni wakapuuza, wakalemewa na usingizi wakalala, masaa machache baadaye Petro alipojaribiwa na Ibilisi amkiri Yesu, alishindwa mwisho wake akamkana mara 3 lakini endapo angeomba usiku ule kama Bwana alivyomwambia na kuifunika siku yake wakati Ibilisi anamjaribu angeshinda lile jaribu, saa ile nguvu fulani ya ujasiri ingemshukia pale pale na angemkiri Bwana badala ya kumkana, au Mungu angemuepusha kabisa na jaribu hilo. Lakini kutokana na kwamba alikuwa hana hazina ya maombi ya kutosha, nguvu za roho zilikuwa chin alishindwa. Na aina zote za majaribu zinaweza kuzuiwa au kuepukwa kwa maombi… unapopita mahali na watu kukuudhi mpaka kukasirika na kugombana mpaka kutoa maneno machafu hilo ni majaribu ambalo ungeweza kulizuia kwa kuomba usiku mmoja kabla hujalala, au asubuhi kabla ya kuanza shughuli zako.
Kadhalika unapojikuta unafanya kitu kisichofaa ambacho hukutarajia au hukupanga kukifanya hilo nalo ni jaribu ambalo lingeweza kuzuiliwa kwa kuomba kabla ya kuianza siku..Na dhambi nyingine zote za bahati mbaya zinasababishwa na upungufu wa maombi. Inapotokea safari ya ghafla ambayo ni ya hasara na si ya faida hilo nalo ni jaribu ambalo endapo ungeomba lisingekukuta.nk n.K.
3) Sehemu ya tatu na ya mwisho ya maombi ni maombi ya KUTANGAZA. Hii ni sehemu ya mwisho na ya muhimu sana kwa kila Mkristo kuifanya. Na faida yake kuu ya haya maombi ni ile ile ya KUTUEPUSHA NA MAJARIBU, Maombi haya ni maombi ya kimamlaka…Maombi haya na yale ya KUPELEKA MAHITAJI yanakazi moja tu nayo ni KUTUEPUSHA NA MAJARIBU.
Sasa kabla ya kuingia kujifunza juu ya jambo hili hebu kwanza tujifunze ulinzi wa kiMungu juu ya mtu aliyezaliwa mara ya pili.
Mtu anapozaliwa mara ya pili, na kuishi Maisha yanayompendeza Mungu asilimia zote, kunakuwa kuna ulinzi Fulani wa kiujumla ambao Mungu anauachilia juu yake, kiasi kwamba huyo mtu hata iweje hawezi kupotea, shetani hawezi kumtoa mkononi mwa Mungu, labda tu huyo mtu kwa hiyari yake mwenyewe aamue kujiuza kwa shetani, lakini kwa namna nyingine yoyote hawezi kutoka mikononi mwa Mungu, anakuwa analindwa kuanzia unywele wake mpaka unyayo wako, na anakuwa amevuka kutoka mautini kuingia uzimani, …Lakini pamoja na huo ulinzi wa kiujumla kuna sehemu ndogo sana ambayo Mungu kamwachia shetani aimiliki..na hiyo ni kutokana na kwamba bado tupo katika miili hii ya dhambi, sehemu yote ya ulinzi wa kiMungu tutakuja kuipata baada ya ukombozi wa miili yetu pale tutakapovaa miili mipya ya utukufu.
Ndio maana unaona sasa japokuwa umeokoka na unaishi Maisha ya kumpendeza Mungu kwa asilimia zote lakini bado utapitia wakati mwingine wa viudhaifu vya hapa na pale, utaumwa kichwa, utajisikia kichefuchefu, mafua yatakusumbua, wakati mwingine itakubidi umeze Panadol kupunguza maumivu au uende hospitali n.k. Sasa hiyo yote ni kuonesha kuwa Mungu hajaipa miili yetu hii asilimia 100 ulinzi…ingawa hivi viudhaifu haviwezi kutuathiri kiasi cha kututoa kwenye Imani, kwasababu Mungu hawezi kuruhusu tujaribiwe kupita tuwezavyo, alisema hivyo katika Neno lake.
1Wakoritho 10: 13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili”.
Kwahiyo haya majaribu madogo madogo ni lazima yaje! Na ni wazi kuwa yanaletwa na shetani kututesa tu! Na kutuhangaisha…Kwahiyo shetani anachokifanya ni kutumia hii nafasi aliyopewa ya sehemu ndogo ambayo Mungu kaiacha, kutujaribu…Na kwasababu anajua hawezi kumjaribu mwamini kwa asilimia zote, atahakikisha kuwa hiyo sehemu ndogo aliyopewa anaitumia ipasavyo.
Sasa swali? Anaitumiaje?
Anaitumia kwa KUTANGAZA, Anawatumia watu kutamka maneno Fulani Fulani juu yako, ambayo hayo yanaweza kutokea kama walivyozungumza, kwasababu Mungu alivyomuumba mwanadamu akizungumza kitu kwa Imani ni lazima kitokee hata kama mtu huyo sio mchawi. Ndio maana wazazi hata kama ni waabudu sanamu wanao uwezo wa kumbariki mtoto au kumlaani, na hizo baraka au laana zikampata huyo mtoto hivyo hivyo kama alivyozisema. Kwasababu hiyo basi shetani anaweza kutumia watu au wachawi au mapepo yake KUTANGAZA mambo Fulani mabaya juu ya mtu.
Kumbuka tena kwa msisitizo..kama umezaliwa mara ya pili na kuishi Maisha yampendezayo, haijalishi ni mambo gani makubwa watayatangaza juu yako, hayatatimia yote kwasababu kuna asilimia kubwa ya ulinzi wa kiMungu kwenye Maisha yako, lakini pia yapo baadhi madogo madogo yanayoweza kutimia na hiyo ni kwasababu hatujapewa dhamana wa ulinzi wa miili hii asilimia zote kama tulivyotangulia kusema..(huu ni msingi mkubwa ambao unahitaji kuelewa) Na sio kwamba Mungu kashindwa kutufunika asilimia zote, hapana ni kwasababu tu ndivyo imempendeza iwe hivyo…kwamba tujue kwamba bado tupo duniani?, tujue kuwa sisi bado ni wadhaifu mbele zake, na tujifunze kumtegemea yeye na kumwomba ulinzi…na pia tujue kuwa vita bado vinaendelea…mpaka siku tutakapovaa ile ya utukufu, ndipo vita vitaisha.
2Wakorintho 1:8 “Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi.9 Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu,10 aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa;”
Sasa ili kupunguza nguvu za shetani kwa majaribu yake anayoyatumia kwa NJIA YA KUTANGAZA…Na sisi tulioamini tuna wajibu huo huo, wa kuingia kwenye maombi ya kuzipunguza hizo nguvu ndogo ndogo za shetani zinazofanya kazi kwenye Maisha yetu…Na maombi hayo hatuyafanyi kwa kupeleka mahitaji mbele za Mungu, bali kwa KUTANGAZA kama yeye anavyotangaza..Ndio hapo sasa Kila siku kabla ya kuianza siku unatamka baraka katika siku hiyo, unalaani na kufuta kila kazi zote za Adui zilizopangwa katika siku hiyo kwa jina la YESU, Unalaani vidhiki na vijaribu vidogo vidogo vilivyopangwa na shetani…Na unatamka kwa maneno yanayosikika kabisa, kwasababu maneno yanaumba, kwa Mungu aliiumba dunia kwa Neno, Unatamka kwa kutangaza kuziharibu nguvu zote na kufuta maneno yote yaliyozungumzwa na watu, wachawi, au mapepo katika siku nzima…unalaani nguvu zote za giza zilizoachiwa siku hiyo zitakazokufanya uikane Imani, au upate hasara ya jambo Fulani, au zitakazokufanya ulumbane au ugombane na watu, unalaani kwa kinywa chako kila nguvu zote za giza zilizoachiwa na yule adui kukufanya usipate muda wa kusoma Neno,na kila ratiba isiyoeleweka iliyopangwa kuzimu kinyume chako na ndugu zako…Unahikikisha unagusa kila kipengele katika Maisha yako, afya yako,familia yako, kazi yako na Imani yako. Usiache kitu!, kwasababu na yule adui anajua anaomlango mdogo juu ya Maisha yako hivyo anakaza kuutumia vizuri.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”
Kwa kufanya hivyo utakuwa umeharibu mipango yote midogo midogo ambayo shetani alikuwa amepanga kukusumbua katika siku hiyo na wiki hiyo. Na hivyo utakuwa umejiongezea Ulinzi wa kiMungu kwa asilimia nyingine kadhaa mbele. Kama alikuwa akuletee viugomvi, viugonjwa, unashangaa siku inaisha bila hivyo vitu, kama alikuwa amekusudia kukuletea vitabu vya hapa na pale visivyoeleweka vinatoweka.
Nakumbuka mwanzoni mwanzoni nampa Bwana Maisha, nilikuwa napitia changamoto nyingi sana na nilikuwa sijui chanzo chake ni nini?..lakini baada ya kujifunza somo la maombi, niliona mabadiliko makubwa sana…
Kwa hiyo ni maombi ya Muhimu sana na kila Mwamini anatakiwa aombe. Na ni moja ya silaha 6 tulizopewa katika biblia..
Waefeso 6: 11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;18 KWA SALA ZOTE NA MAOMBI MKISALI KILA WAKATI KATIKA ROHO, MKIKESHA KWA JAMBO HILO NA KUDUMU KATIKA KUWAOMBEA WATAKATIFU WOTE;19 pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;20 ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo;hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.”Kwa kumalizia kumbuka kuwa muda wa chini Bwana Yesu aliotuamuru tusali kwa siku ni LISAA LIMOJA.
Mathayo 26: 40 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
Umeona hapo, roho zetu zipo tayari kuomba lakini miili ndio inayokataa, hivyo mambo mengine ni unalazimisha, kama Bwana asiyekuwa na dhambi aliomba Zaidi ya lisaa limoja, unafikiri inatupasaje sisi wenye dhambi?..unakataa usingizi na uvivu wa kuomba, unalazimisha mambo, utashangaa dakika za kwanza unapata shinda lakini baaada ya dakika 10-15 mbeleni unashangaa kuna nguvu Fulani inakuvaa unajikuta unazama kwenye maombi…Na kwa vipengele hivyo vitatu ukianza na kushukuru, kisha kupeleka maombi na kutangaza baraka..huwezi kuacha kumaliza lisaa na Zaidi..
Na pia kumbuka kuwaombea na wengine, katika vipengele vyote hivyo vitatu, hata hichi unachokisoma hakijapewa guarantee ya ulinzi asilimia 100, kinahitaji maombi kiweze kuendelea kuwepo, kwahiyo uombapo ukumbuke kugusia kila eneo, pamoja na sisi tunaoandika hizi habari, Ili injili ya Mungu izidi kwenda mbele, kwa Neema za Mungu.
Bwana akubariki sana.
No comments:
Post a Comment