"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, December 12, 2016

MASWALI YALIYOULIZWA NA MAJIBU YAKE : SEHEMU YA PILI


SWALI 1; Hekalu la Sulemani lilikuwa limejengwa kwa dhahabu na madini mengi; ni akina nani waliolibomoa na hayo madini yalienda wapi?
JIBU:hekalu la sulemani lilibomolewa kwa mara ya kwanza na nebukadreza mfalme wa babeli, baada ya kuteketezwa na vyombo vya hekaluni kupelekwa babeli  ukisoma 2wafalme 25:8-9" Hata mwezi wa tano, siku ya saba ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na kenda wa mfalme Nebukadreza, mfalme wa Babeli, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, mtumishi wa mfalme wa Babeli, akaingia Yerusalemu.Akaiteketeza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto."historia hairekodi sanduku la agano.lilienda wapi na mpaka leo hii haijulikani lilipoishia. Miaka 70 baadaye Hekalu lilipojengwa kwa mara ya pili baada ya wana wa israeli kurejea kutoka babeli halikuwa na sanduku la agano ndani yake kama ilivyokuwa katika hekalu la kwanza lililojengwa na mfalme sulemani. lakini vile vyombo vya dhahabu vilivyokuwa vinatumika hekaluni kwa kazi za kikuhani vilivyochukuliwa mpaka babeli na mfalme nebukadneza vilirudishwa tena Yerusalemu baada ya ile miaka 70 iliyotabiriwa na nabii Yeremia kuisha.

 SWALI 2:JE historia ya mama wa Yesu ilikuwaje, baada ya Yesu kupaa? , Je! aliendelea kuishi na Yusufu au waliachana?
JIBU: Baada ya Yesu kuondoka Mariamu aliendelea kuishi na Yusufu kama mume wake, kama tu alivyokuwa anaishi nae hapo mwanzo kabla ya Yesu kupaa na pia Mariamu alizaa watoto wengine kama biblia inavyorekodi. mathayo 13:55-56"Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda?  Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? " Kwahiyo tunaona hapa kuwa Mariamu alikuwa na familia yenye watoto wa kike na wakiume na mumewe alikuwa ni Yusufu kwahiyo wasingeweza kuachana kwakuwa tayari ni familia hiyo. na Mariamu alikufa kama watu wengine hakupaa kama baadhi ya dini zinavyofundisha kwasababu hakuna sehemu yoyote katika maandiko inaonyesha kuwa Mariamu alipaa.

SWALI 3; je; kwa wale watakaotupwa jehanamu ya moto, wataungua maisha yote au itakuwa ni kipindi fulani kisha wataungua na kuteketea kabisa?
JIBU: Kwa wale watakaotupwa kwenye ziwa la moto hawatachomwa milele...itafika wakati roho zao zitakufa hiyo ndiyo mauti ya pili biblia inayoizungumzia katika ufunuo 20:14..na pia biblia inasema kwenye ezekieli 18:20 roho itendayo dhambi itakufa. Tukisema mtu atachomwa milele inamaanisha kuwa huyo mtu atakuwa na uzima wa milele katika ziwa la moto jambo ambalo haliwezekani, uzima wa milele upo katika Yesu Kristo tu.2wathesalonike 1:8-9 "8 katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake; " Tunaona hapa kwenye huu mstari Paulo anasema watu hawa wataadhibiwa kwa maangamizi ya milele yaani kuangamizwa kwao ni kwa milele na sio wataadhibiwa miele..kwahiyo waovu wote watachomwa ila hatujui ni kwa muda gani kama ni miaka 10, au 20 au 1000 au miaka bilioni moja hatujui lakini mwisho wa yote roho zote zilizoasi zitakufa pamoja na shetani na malaika zake na huko ndiko kutengwa na Mungu milele. mathayo 10:28 "Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. " kwahiyo tunaona hapo pia roho ya mtu aliyeasi itateketezwa katika jehanam ya moto na kufa.

SWALI 4: Kule mbinguni tukifika tutavalishwa mataji, je! hayo mataji ni kitu gani na yatatumika wapi?
JIBU: Taji linawakilisha mamlaka utakayopewa ukifika huko kulingana na uaminifu wako na kazi uliyoifanya hapa duniani kwa ajili ya injili..naamini taji mtu analipokea akiwa hapahapa duniani, tukifika kule ni kuvikwa tu....biblia inasema  katka ufunuo 3:11 "naja upesi shika sana ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako'' kwahiyo kila mmoja wetu analo taji lake mkononi maisha unayoishi na machango wako katika kuieneza injili itaelezea nafasi utakayokuwa nayo huko, hauwezi ukaishi maisha ya kutokujali ya uvuguvugu haijulikani wewe ni mkristo au la, halafu ukawe sawa na mtume Paulo kule..haiwezekani. Kwahiyo kumbuka maisha yako ndio taji lako.

SWALI 5; Mizimu huwa ni kitu gani hasa? Na je mpaka leo mizimu ipo?
JIBU:Mzimu ni roho ya mtu aliyekufa. Zamani katika agano la kale shetani alikuwa anazo funguo za kuzimu alikuwa ana uwezo wa kuwasiliana na roho za watu waliokufa ikiwemo watakatifu, tunaweza kuona katka kitabu cha 1samweli 28, mzimu wa samweli ulipandishwa juu na yule mwanamke mchawi na kumfanya Sauli aweze kuwasiliana na mzimu wa samweli lakini baada ya Bwana Yesu Kristo kuchukua funguo za mauti na kuzimu shetani akawa hana uwezo tena wa kuzileta juu roho za wafu kama alivyofanya kwa samweli..kwahiyo leo hii hilo jambo haliwezekaniki tena, ukiona mzimu au mtu aliyekufa ukamwona tena ujue huyo ni shetani amevaa kinyago cha mtu aliyekufa..na sasa hivi shetani anawadanganya watu wengi sana kwa njia hiyo kwa wale wasiomjua  Mungu. Kwahiyo mwenye mamlaka na wafu wote ni Yesu Kristo mwenyewe shetani hana mamlaka tena na mtu anapokufa isipokuwa ni Bwana Yesu mwenyewe kakuonyesha katika maono, nje ya hapo ni shetani amina.
jambo ambalo shetani anaweza akalifanya ni kuiteka roho ya mtu, na kuificha kwa uchawi wake anamfanya mtu huyo aonekane kama amekufa lakini anakuwa hajafa bali ametekwa na ibilisi vifungoni watu wanatumia lugha (msukule) isaya 42:22 lakini Mungu anaweza akamrudisha mtu huyo katika maisha yake ya kawaida, kule anakuwa hajafa. kwahiyo roho ya mtu ikishakufa tu shetani hana mamlaka nayo tena kufanya lolote ila Mungu tu kwahiyo tunapaswa tuwe waangalifu tusishirikiane na mashetani shetani hana uwezo wa kukuonyesha ndugu yako aliyekufa.

SWALI 6: kuna tofauti gani kati kufa na kulala? je! kuna tofauti gani kati ya kulala kwetu kwa kila siku na kulala kwa watu kama "Lazaro na huyo kijana" ambaye Yesu alipokuwa anaenda kuwafufua alisema kwamba 'wamelala'
JIBU:  Kufa na kulala ni kitu kimoja...lakini kifo cha kulala kipo mara mbili kimoja ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ambacho mtu anafufuka hapa hapa duniani tunaona mfano lazaro, na yule kijana n.k..na kulala kwa pili kunawahusisha watakatifu wote waliokufa wenye tumaini la kufufuka katika kiama cha mwisho kuingia katika utukufu wa milele. Lakini wale waliokufa katika dhambi wanahesabika kama wamekufa sio wamelala kwasababu wanaisubiria mauti ya roho zao (ambako huko ndo kufa kwa pili katika ziwa la moto). Na kulala kwetu siku zote kama kawaida kitandani na kuota ndoto kisha baadaye kuamka tunakujua, ni kwa ajili ya kutimiza matakwa ya mwili(mapumziko).

 SWALI 7: Kwanini Mungu hakumuua nyoka, akamwacha Hawa ajaribiwe katika bustani ya edeni? kwanini aliachilia tuanguke katika dhambi?
JIBU: Mungu ameruhusu sisi wanadamu tujaribiwe, maana hakuna ushindi kama hakuna vita, ameruhusu haya yote ili tuujue uweza wake na tumjue yeye zaidi, tungejuaje kama yeye ni mwokozi kama tusingepotea, kama yeye ni mponyaji kama tusingeumwa, tungejuaje yeye ni wa rehema kama tusingeanguka, yeye ni wa neema kama tusingekuwa hatuna haki, yeye ni mwenye msamaha kama tusingekuwa na kosa n.k...dhahabu ili ing'ae lazima ipitishwe kwenye moto ijaribiwe na sisi kama watoto wa Mungu lazima tujaribiwe na ndio maana Mungu hakumuua shetani. Kwahiyo Mungu anamakusudi yake chini ya jua kutupitisha njia hiyo. Tunafahamu kuwa siku zote Mungu anatuwazia mawazo yaliyo mema ili kutupa tumaini siku zetu za mwisho. yeremia 29:11. Yote haya Mungu kayaruhusu ili kutuwekea msingi mzuri wa maisha yajayo matamu ya umilele.

No comments:

Post a Comment