"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, December 13, 2016

MASWALI YALIYOULIZWA NA MAJIBU YAKE:SEHEMU YA 3

SWALI 1: Nami nina swali kuhusu watumishi wa Mungu swali ni kwamba ukiwa unaabudu kwa mtumishi ambaye unaamini ni mteule wa Mungu na kumbe ni nabii wa uongo akakufundisha neno kutoka kwenye biblia akakuongoza katika maombi akafanya miujiza wagonjwa wakapona viwete wakatembea kumbe anatumia nguvu za giza na wewe hujui ,je atakapokuja Yesu utanyakuliwa?
JIBU:  Kama anatumia nguvu za giza huyo ni mchawi, na wachawi hawawezi wakawa watumishi wa Mungu wanakupeleka jehanum..lakini kama hatumii uchawi na bado ni mwongo na miujiza inatendeka ndio unaweza ukaenda mbinguni, kwasababu Mungu anaweza kumtumia mtu huyu kama chombo cha kuazima na baada ya shughuli kuisha Mungu akawa hana kazi nae tena. Yesu alisema mathayo 7:21 wengi watakuja wakati ule wakisema Bwana hatukufanya miujiza mingi kwa jina lako n.k lakn Yesu atawaambia sijui mtokako ninyi mtendao maovu....andiko hili ndio linawahusu watu kama hao, ambao wanatumia upako wa Mungu kwa faida zao wenyewe angali mioyo yao iko mbali na Mungu.
Kuja jambo lingine la kujifunza. Mungu anaweza kumpa mtu upako akawa anaombea watu wanapona, anafufua wafu na kufanya miujiza mingi lakini Mungu asimtambue huyo mtu..na ni nguvu za Mungu anatumia sio uchawi...biblia imewaita makristo wa uwongo waliotabiriwa kuja siku za mwisho, biblia inasema utawatambua kwa matunda yao. Maana ya neno kristo ni mtiwa mafuta kwahiyo aliposema watatokea makristo wa uwongo maana yake ni watiwa mafuta wa uwongo..kwahiyo usishangae kuwaona wana upako lakini mienendo yao haifanani na ukristo jiepushe nao, kigezo cha mtumishi wa Mungu kuwa na upako sio sababu ya Mungu kuwa naye bali ni yule anayetenda mapenzi ya Mungu kwa kuliishi na kulifundisha Neno lake.

SWALI 2: Je! ni kweli dunia iliumbwa takribani miaka 6000 iliyopita? na je! shetani alikuwepo duniani wakati dunia inaumbwa?

JIBU: Tangu Edeni mpaka wakati wa Gharika, ni miaka elfu 2, na tangu wakati wa gharika mpaka kuzaliwa kwa Bwana Yesu ilipita miaka kama elfu 2 hivi, na tangu   kipindi cha Bwana wetu Yesu hata leo nacho pia ni kipindi cha miaka elfu 2 kimepita. Kwahiyo jumla yake tangu Edeni mpaka sasa ni miaka kama elfu 6 hivi, au imezidi kidogo au imepungua kidogo..Sasa kumbuka huo ulikuwa ni mwanzo wa Edeni, lakini haukuwa mwanzo wa Dunia..dunia ilikuwepo kabla ya Edeni..Tunasoma.

mwanzo 1:1 "hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi"...hapa hajasema huo mwanzo ulikuwa ni wa miaka mingapi iliyopita inaweza ikawa ni miaka elfu kumi,milioni kumi au vinginevyo...

lakini mstari wa pili unasema nayo nchi ilikuwa ukiwa na utupu inamaanisha kuwa kuna jambo lilitokea likaifanya hiyo nchi kuwa ukiwa baada ya Mungu kuziumba mbingu na nchi na hapa si mwingine zaidi ya shetani ndiye aliyeiharibu na kuifanya ukiwa (kama anavyoendelea kuiharibu sasa hivi) maana Mungu hakuiumba dunia iwe ukiwa bali ikaliwe na watu,

Isaya 48:18 inasema "

18 Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. ".

Lakini baada ya dunia kuharibiwa kwa viwango vya hali ya juu, ikapoteza umbo lake ikawa kama moja ya sayari nyingine, na ndio tunaona Mungu akaanza kufanya uumbaji upya baada ya nchi kukaa muda mrefu katika hali ya ukiwa, hapo mbingu na nchi zilikuwa tayari zimeshaumbwa muda mrefu nyuma. kwahiyo mwanadamu na viumbe vyote inakadiriwa viliumbwa miaka takribani 6000 iliyopita lakini dunia iliumbwa kabla ya hapo na shetani alikuwepo duniani kabla ya mwanadamu kuumbwa, kwasababu tunamuona alionekana katika bustani ya Edeni na biblia inamwita shetani kama lile joka la zamani ufunuo 20:2, kwahiyo inamaanisha alikuwepo toka zamani kabla hata ya mwanadamu kuumbwa, ambapo tunaona alitupwa huku duniani baada ya kuasi mbinguni pamoja na malaika zake.


 SWALI 3: Ipi tofauti kati ya dhehebu na Ukristo? je madhehebu yote yalitoka wapi?  je Mungu ni mwanzilishi wake?
JIBU: Madhehebu ni makanisa yalioacha uongozi wa Roho mtakatifu na kufungwa na mifumo fulani isiyoruhusu mafunuo mapya ambayo yangepelekea kanisa kusonga mbele katika kumjua Mungu,kiasi cha kwamba inafanya kanisa liwe la ubinafsi na kufa katika roho. sababu hiyo basi inamfungulia shetani mlango wa kuwadanganya wanadamu waone kama wanamwabudu Mungu kwa kulichanganya neno la Mungu na desturi za kibinadamu(au walizojitungia wao).Lakini ukweli wa mambo ni kwamba shetani anaabudiwa kwa siri. kama vile kujiteulia vyeo kama upapa,ukadinali, ubaba mtakatifu,ukasisi(kuwafanya watu wadhani pasipo wao hauwezi kumfikia Mungu),kuongeza vitabu kwenye neno la Mungu,ibada za sanamu, ibada za wafu, litrujia, ibada za miungu mitatu,ibada  zisizoruhusu uponyaji wa kiungu na karama za rohoni, kanisa linaloingiza siasa,michezo na mambo ya kijamii n.k kwaufupi makanisa yote yaliyotengeneza mifumo isiyoendana na neno la Mungu na kujifunga ni madhehebu mfano wa makanisa haya tunayo katoliki,lutherani,anglikana,sda,mashahidi wa Yehova,na sasa baadhi ya wabranamite, na makanisa ya kipentekoste nayo n.k lakini  biblia inasema tokeni kwake watu wangu msishiriki dhambi zake ufunuo 20:4. Na ukristo ni kuishi kama Kristo anavyotaka yaani kuishi na kuenenda katika Neno lake ambalo ni biblia pasipo kupindisha kushoto wala kulia au kuongeza wala kupunguza, na katika ukristo hakuna kujitenga wala kujifunga,tuanaishi kwa upendo katiba yetu ikiwa ni NENO la Mungu, hakuna mapokeo ya kibinadamu yanayopingana na Neno kujumuishwa katika imani, na kila jambo linahakikiwa na Neno la Mungu na wakristo wanaongozwa na Roho wa Mungu na wala sio mapokeo yoyote kutoka kwa viongozi wao au makanisa yao.Na hilo ndilo kanisa halisi Bibi-arusi wa Kristo.

SWALI 4: Kwanini mtu akiitwa na Mungu mtu huenda na kusajili huduma mfano t.a.g; e.a.g.t; anglican; menonite; pefa; fbg; efatha; ukombozi;  4square; p.a.g; kkkt; s.d.a; mmpt; fpct; winners; n.k mbona hatuoni katika biblia mitume kufanya jambo hilo?
JIBU: kusajili kanisa ni tofauti na kusajili dhehebu, kusajili kanisa sio vibaya pengine kulingana na sheria ya nchi fulani inataka makanisa yote yasajiliwe ili yajulikane na nchi kwa madhumuni ya kulipa kodi n.k na kanisa kuitwa  jina lolote sio vibaya, hilo ni jina tu la mahali pa kukutania, lakini point hapo ni maana ya dhehebu...dhehebu ni kanisa lililosajililwa lililoacha uongozi wa Roho Mtakatifu na kuongozwa na dogma za kibinadamu likiwa limejitenga na kufuata kanuni zake zenyewe lilizojiwekea mbali na NENO sasa kanisa la namna hiyo ndio linaitwa dhehebu kwasababu Mungu anakua ametupiliwa nje na linakuwa ni kama moja ya dini nyingine tu. Kanisa la dizaini hiyo linamfanya mtu kuwa mtumwa wa kanisa kuliko kuwa mtumwa wa Kristo, linamfanya mtu ajione kuwa pasipo dhehebu lake hawezi kwenda mbinguni, kwamba dhehebu lake ndio tiketi ya kwenda mbinguni, linasahau kuwafundisha watu kurudi katika utakatifu na kuishi kulingana na Neno la Mungu na sio kulingana na mapokeo ya kanisa, hivyo basi linamfanya mkristo kutokuliona Neno kuwa la muhimu zaidi ya kanisa lake kwahiyo mtu huyo anakuwa vuguvugu, inafika mahali mtu anahubiriwa aache mambo fulani ambayo biblia inakataza, atasema kanisa letu haliamini hayo, hii ni hatari sana kwa mtu yeyote anayejiita mkristo kukataa Neno la Mungu na kukubali mapokeo ya kibinadamu kwa kigezo cha kanisa lake kutokuamini hivyo, Mungu anaishi kwenye neno lake sio kwenye mifumo ya wanadamu..haiwezekani kanisa linaongozwa na askofu ambaye ni mwanasiasa au ameoa wake wengi au kiongozi wake ni shoga, au mlevi,au makanisa yanayojihusisha na mambo ya kidunia kama kumiliki timu za mipira,vyama vya kisiasa,lodges, n.k kiasi ambacho huwezi ukatofautisha kati ya kanisa na mashirika ya kijamii,na mshirika anajihisi kuwa yuko sehemu salama ya kiroho,haoni shida kuendelea kudumu na dhambi zake hiyo ni hatari.Jambo hili linapelekea mauti ya kiroho.

SWALI 5: kuna ufufuo wa aina ngapi?
JIBU: Biblia inasema kuna ufufuo wa aina mbili, Ufufuo wa kwanza, umejumuisha wale watakatifu waliofufuka na Yesu (mathayo 27:52),pamoja na watakao fufuka katika unyakuo, na watakao fufuliwa wakati wa kuingia kwenye utawala wa miaka 1000 (ufunuo 20:4) haya ni makundi matatu yanayotengeneza ule ufufuo wa kwanza ufunuo 20:6 "....Heri na mtakatifu ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza, juu ya hao mauti ya pili haina nguvu..."...na ufufuo wa pili utakuja mara tu baada ya utawala wa miaka 1000 kuisha..ambapo wafu wote ambao hawakuwepo katika ufufuo wa kwanza watafufuliwa na kuhukumiwa na Kristo katika hukumu ya kile kiti cheupe tukisoma ufunuo 20:11-15" ...Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.  Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.  Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto".

SWALI 6: wale manabii wawili ni akina nani?
JIBU: Ndugu justice manabii wawili unaweza ukawasoma katika kitabu cha ufunuo 11..baada ya unyakuo kupita Mungu atawanyanyua hawa kupeleka injili israel, kuwatia muhuri wale wayahudi 144,000 jumla yao, yaani watu 12,000 kwa kila kabila la Israeli.Hawa manabii wawili watahubiri injili kwa wayahudi muda wa miaka mitatu na nusu baada ya kumaliza ushuhuda wao mpinga kristo atawaua lakini baada ya siku tatu na nusu kama biblia inavyorekodi watafufuka na kunyakuliwa juu mbinguni, Roho ya Mungu itakaa juu yao kwa nguvu na uweza mwingi kama ilivyokuwa kwa Musa na Eliya walivyokuwa duniani


SWALI 7: nashukuru kwa jibu lakini hata hivyo bado nina swali jingine. je; hukumu sasa zitakuwepo za aina mbili au? Maana unasema watafufuliwa kisha wahumumiwe na watawale na Kristo miaka 1000 lakini kwa mujibu wa biblia utawala wa miaka 1000 ni kabla ya hukumu ya kile kiti cha enzi sasa inakuwaje hawa wahukumiwe kabla ya utawaka wa miaka 1000?

JIBU:Kuna Hukumu kuu tatu za Mungu mwenyezi..HUKUMU YA KWANZA:..Ni hukumu ya watakatifu watakaoenda mbinguni, hukumu hii siyo ya kulaumiwa wala ya adhabu, bali ni ya thawabu, kila mtakatifu atalipwa kulingana na kazi aliyoifanya ya injili akiwa hapa duniani, 2wakorintho 5:10 "Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya." pia warumi 14:12 "Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu." tunaona hapa paulo alikuwa hazungumzi na watu wasioamini bali na wakristo kwahiyo hiyo hukumu inawahusu watakatifu tu....

HUKUMU YA PILI: Hii itakuwa baada ya mwisho wa ile siku kuu ya Bwana baada ya ile dhiki kuu, itawahusisha wale wakristo walioachwa katika unyakuo, wasioipokea ile chapa ya mnyama, na kuuawa na mpinga kristo. kulingana na ufunuo 20:4..na mathayo 25:31-46, Kristo atakapowatenganisha kondoo na mbuzi....

HUKUMU YA TATU:..itakuwa baada ya mwisho wa ule utawala wa miaka 1000 pale Kristo atakapokaa katika kiti cha enzi cheupe kuwahukumu mataifa ukisoma ufunuo 20:11-15 "Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao." Hii itakuwa ni hukumu ya mataifa kwa wale wingine wote waliobaki watahukumiwa kulingana na matendo yao. Na wale wote walioipokea chapa ya mnyama watahukumiwa kuona sababu ya kuenda katika ziwa la moto.

No comments:

Post a Comment