"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, October 14, 2017

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?:


Karibu tuongeze maarifa katika Neno la Mungu,


Tukisoma kwenye biblia kitabu cha warumi 4 tunaona mtume Paulo anasisitiza kuwa mtu hahesabiwi haki mbele za Mungu kwa matendo yake bali kwa Imani, lakini tukisoma tena katika kitabu cha Yakobo 2, Yakobo anasisitiza kuwa mtu hahesabiwi haki kwa Imani tu, bali pia na kwa matendo. Tunaona sentensi hizi mbili zinaonekana kama kupingana, Lakini je! Biblia kweli inajipinga au ni sisi uelewa wetu ndio unaojipinga??..tuichambue mistari hii miwili kwa undani kidogo..


1) Warumi 4:1-6


"1 Basi, tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili?
2 KWA MAANA IKIWA IBRAHIMU ALIHESABIWA HAKI KWA AJILI YA MATENDO YAKE, ANALO LA KUJISIFIA, LAKINI SI MBELE ZA MUNGU.

3 Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki.
4 Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
6 Kama vile Daudi anenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,.

Ni dhahiri kuwa hapa mtume Paulo alipokuwa anazungumzia MATENDO, alikuwa analenga matendo yatokanayo na sheria  ya kwamba hakuna mwanadamu yoyote anaweza akasimama mbele za Mungu kwa matendo yake kuwa ni mema au amestahili kumkaribia Mungu. Kwa mfano mtu kusema nimestahili kwenda mbinguni kwa matendo yangu mazuri, mimi sio mwasherati, sio mwizi, sio mtukanaji, sio mlevi, sio mwongo, sio mwuuaji n.k. kwa kusimamia vigezo kama hivyo hakuonekana hata mmoja aliyeweza kumpendeza Mungu isipokuwa mmoja tu naye ni BWANA wetu YESU KRISTO! wengine wote kama biblia inavyotaja kuanzia Adamu mpaka mwanadamu wa mwisho atakayekuja duniani Mungu alishawaona wote tangu mwanzo kuwa wamepungukiwa na utukufu wake,

 Warumi 3:23" kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; " na ukisoma pia Zaburi 14:2-3 inasema " Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja." .Hivyo hii inadhihirisha kabisa hakuna hata mmoja atapata kibali mbele za Mungu kwa matendo yake mazuri.


 lakini swali ni je! kama sio kwa matendo, basi mtu atapata kibali mbele za Mungu kwa njia gani tena??..


Ukiendelea kusoma mbele tunasoma mtume Paulo anasema ni kwa njia moja tu tunaweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu nayo ni njia ya kumwamini BWANA YESU KRISTO tu!. Ndio njia pekee inayotupa sisi kupata kibali mbele za Mungu, kwa namna hiyo basi tunayo haki ya kuwa na uzima wa milele, kwenda mbinguni, kubarikiwa kwasababu tumemwamini mwana wa Mungu YESU KRISTO na sio kwa matendo mema tuyatendayo. Kumbuka zipo dini nyingi zenye watu ambao wanatenda matendo mema lakini je! wanao uzima wa milele ndani yao? utakuta ni wema kweli wanatoa zaka, wanasaidia maskini, sio waasherati, sio  walevi n.k. lakini bado Mungu hawatambui hao. Lakini sababu ni moja tu, hawajamwamini mwana wa Mungu ili aziondoe dhambi zao. Kwahiyo tunaona hapo jambo kuu Mungu analolitazama ni wewe kumwamini mwana wa Mungu, na ukishamwamini (yaani kumpa maisha yako) ndipo ROHO wake MTAKATIFU anakutakasa na kukufanya uishi maisha matakatifu ya kumpendeza.

2). Lakini tukirudi kusoma kitabu cha Yakobo 2:21-26 


"21 JE! BABA YETU IBRAHIMU HAKUHESABIWA KUWA ANA HAKI KWA MATENDO, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu?
22 Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale.
23 Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.
24 Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake.
25 Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine?
26 Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.

Katika kifungu kile cha kwanza ukiangalia kwa undani utaona kuwa mtume Paulo alikuwa anazungumzia juu ya MATENDO YATOKANAYO NA SHERIA. Lakini hapa Yakobo hazungumzii habari ya matendo yatokanayo na sheria bali ni MATENDO YATOKANAYO NA IMANI.. hivyo ni vitu viwili tofauti. MFANO WA MATENDO YATOKANAYO NA IMANI: 

Kwamfano: Mtu amepimwa na daktari na kuambiwa kuwa anaugonjwa wa kisukari, na hatakiwi kula vyakula vyenye asili ya sukari na wanga. lakini mtu yule akilishikilia lile Neno kwenye biblia Mathayo 8:17 linalosema " ....Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu. " Na kuliamini na kuamua kuchukua hatua na kusema mimi ni mzima na sio mgonjwa kwasababu yeye alishayatwaa madhaifu yetu, na kusimama na kutembea kama mtu mzima asiyeumwa na kula vyakula vyote hata vya sukari na wanga ingawa daktari alimkataza, akiamini kuwa amepona kwa NENO lile atapokea uponyaji wake. sasa  kitendo cha yeye kuchukua hatua ya kuishi kama mtu mzima ambaye haumwi japo ni mgonjwa na kula vile vyakula alivyoambiwa asile hicho ndicho kinachoitwa MATENDO YA IMANI Yakobo aliyoyazungumzia..


Unaona hapo haki ya huyo mtu kuponywa haikutokana na matendo ya sheria (yaani utakatifu, kutokuwa mwasherati, au mlevi au mwizi n.k.). bali ni matendo yaliyotakana na kumwamini YESU KRISTO katika NENO lake ndio yaliyomponya. Na ndio jambo hilo hilo lililomtokea Ibrahimu pale alipomwamini Mungu na kumtoa mwanae kuwa dhabihu, kwahiyo kile kitendo cha yeye kumtoa mwanawe hayo ndiyo MATENDO yanayozungumziwa na Yakobo YA IMANI kwasababu hiyo basi ikampelekea yeye kupata haki mbele za Mungu. Unaona hapo haikuwa sababu ya yeye kutokuwa mwongo, au mlevi, au muuaji n.k. ndio kulimpa haki yeye ya kubarikiwa hapana bali ni kumwamini Mungu na kuiweka ile imani katika matendo. Kwasababu kama ingekuwa kwa usafi wake Mtume Paulo asingesema Ibrahimu hana la kujisifu mbele za Mungu.

Vivyo hivyo kwa mambo mengine yote kwamfano haki ya kuzungumza na Mungu, haki ya kuponywa magonjwa,  haki ya kubarikiwa, haki  ya kwenda mbinguni, haki ya karama za rohoni, haki ya kuwa mrithi, n.k. havitokani na MATENDO YA SHERIA bali MATENDO YA IMANI. Kwa sisi kumwamini YESU KRISTO katika Neno lake ndipo tunapopata vyote. Kwahiyo matendo yote mema ya sheria yanakuja baada ya kuwa ndani ya Kristo na hayo ndiyo yanayokupa uhakika kama upo ndani ya Kristo, ni kweli huwezi ukawa ni mkristo halafu bado ni mlevi, mwasherati, mwongo, mwizi n.k.. lakini jua katika hayo mtu hahesabiwi haki mbele za Mungu kama tukitaka tuhesabiwe katika hayo hakuna mtu atakayesimama mbele za Mungu.


Kumbuka Ibilisi anawinda IMANI yetu kwa Bwana pale tunapoiweka katika matendo na sio kingine, tunasamehewa dhambi kwa imani, tunaponywa kwa imani, maombi yetu yanajibiwa kwa imani, kila jambo tunapokea kwa Mungu kwa IMANI IPATIKANAYO KATIKA NENO LAKE. Lakini shetani anaenda kinyume kukufanya udhani utasamehewa dhambi kwasababu unashika amri kumi, au  kwa kufunga na kuomba sana ndio utapata haki ya kuponywa, n.k. Bwana amesema waebrania 10:38 " Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. "


Wagalatia 2:16 " hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. "

Waefeso 2:8-9 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;  wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. "

Bwana akubariki.


4 comments:

 1. Mmmh bado sijaelewa kwakweli; roho mtakatifu anisaidie maana Neno linasema pasipo utakatifu hakuna atakayemwona Mungu; na utakatifu si nikuacha dhambi ambazo ndi matendo ya sharia?

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ikiwa tutahesabiwa haki kwa matendo ya sheria basi Kristo alikufa bure kama maandiko yanavyosema, kwasababu tungeendelea tu kubakia na torati tuishike tuishi kulingana na hiyo..

   Lakini Yesu alipokuja aliivunja laana ya torati ambayo kwa hiyo haikuwahi kutokea mtu aliyeweza kuiishi kwa utimilifu wote,Hivyo sasa kwa kumwamini yeye, tunahesabiwa haki bure pasipo yale matendo...ndio maana mtu akimwamini tu YESU kwa kutubu dhambi zake, tayari kashahesabiwa kuwa mmoja wa watoto wa Mungu bila hata kutenda tendo lolote jema mbele za Mungu,hata akifa atakwenda mbinguni..na atahesabiwa kuwa ni mtakatifu.

   Lakini sasa je! tuendelee kuishi katika dhambi kwasababu neema ipo?, jibu ni hapana, ni sawa tu na mtu anasema sasa sumu ya nyoka imepatikana ngoja nikacheze na kila nyoka porini waniume nitie dawa..kwani dawa si ipo??...Mtu kama huyu unaona atakuwa na upungufu wa akili...

   vivyo hivyo hatuwezi kuenenda tena katika maisha ya dhambi ya kale kwasababu neema ipo, badala yake kila siku tutamwishia Mungu, tukihakiki ni yapi mapenzi ya Mungu, huko ndio kutakaswa, kidogo kidogo, tunakuwa katika utakatifu wote mpaka sasa tunafikia kilele cha kimo cha mtu mkamilifu..Hapo ndipo viwango vya Utakatifu vinakuwa vimejikita mizizi ndani mtu.

   Na ndio maana tunaimbiwa katika wafilipi 2:2.12Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.2.13Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.

   Kwahiyo kwa kumalizia, ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyemwamini Yesu, asitembee katika utakatifu...Na Utakatifu halisi na thabiti unaletwa na YESU na sio torati....Yesu anaweka kinga ndani ya mtu, torati inatoa tiba tu,..mtu akiwa na kinga ugonjwa hauwezi ukawa na madhara ndani yake, wala hauwezi kumsumbua..lakini mtu akitegemea tiba, ni kweli anaweza kuwafanikiwa kupona kwa kitambo tu lakini baada ya muda kidogo ugonjwa utamrudia tena, na tena na tena...na ndio maana mtu anayeishi kwa kuitegemea torati na wala si Kristo kama vile waislamu, kamwe hawawezi kuwa kumpendeza Mungu, au kuwa watakatifu.

   Ubarikiwe ndugu.

   Delete
 2. Katika Injili ya LUKA. 18:18-30 Kuna jambo la kujifunza hapo
  "Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado;
  viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?
  Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu. Petro akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata. Akawaambia, Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu, asiyepokea zaidi mara nyingi katika zamani hizi, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele."
  Hapo tunaona kuna mtu mmoja mkubwa ambaye kibinadamu alitoa CV yake kwa YESU KRISTO ili ajue ni nini cha kuongeza kwenye iyo CV yake ili apate kuurithi ufalme wa MUNGU na akawa anajivunia kuwa amekuwa anazijua na kuzishika AMRI za Mungu tangu utoto wake kwa hiyo alidhani kuwa YESU KRISTO angemwambia wewe ni mtu mzuri sana na teyari kwa matendo yake yeye alidhani ameshapata nafasi kwenye Ufalme wa Mungu. lakini umeona jibu la YESU KRISTO?
  alimwambia WEWE UMEPUNGUKIWA NA NENO MOJA BADO, Lipi? Viuze ulivyo navyo VYOTE ukawagawanyie maskini nawe utakuwa na hazina mbinguni (kumbuka hazina ya mtu ilipo ndipo moyo wake ulipo mathayo 6:21). kwa maana nyingine wewe utakuwa umepata hakika ya kwenda Mbingu lakina umeona kilichomtokea mtu yule? neno la Mungu linasema
  "Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi"
  kwa maana nyingine kwa kila tendo la sheria tunalofanya ili kuonekana tuna UTAKATIFU mbele za MUNGU kuna jambo ambalo tutakuwa tumepunkiwa nalo.
  kwa mfano :unaweza kutoa milioni kumi kanisani kama mchango wa kujenga kanisa na moyo wako ukajihesabia haki kwa Mungu kwa sababu ya mchango wako kumbe Mungu anaweza kukuona tofauti sana kwa sababu kama umetoa milioni kumi pengine Mungu anaona ungeweza kutoa milioni mia moja na ukitoa milioni mia moja Mungu anaona ungefanya juhudi ungetoa bilioni moja.
  ki ukweli tunahesbiwa haki ya kuwa WANA wa MUNGU na Kuurithi Ufalme wa Mungu kwa kupitia imani yetu katika KRISTO YESU hakuna njia nyingine,
  Kumbuka yule Mwana sheria (aka mtu mkubwa) alisema kuwa kama ni amri amezishika sawasawa tena tangu utoto naye YESU KRISTO akamkamata hapo hapo kwenye amri. kumbuka
  amri ya kwanza inasema "MPENDE BWANA MUNGU WAKO KWA MOYO WAKO WOTE, NA KWA ROHO YAKO YOTE, NA KWA NGUVU ZAKO ZOTE, NA KWA AKILI ZAKO ZOTE, NA MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO:"
  Neno la Mungu linataafsiri jirani yako kama mtu mwenye UHITAJI AU MTU ALIYEPATWA NA TATIZO au kwa kifupi ni maskini wa mali au Afya (LUKA 10: 29-37).
  YESU KRISTO alimkamata yule aliyetaka kuhesabiwa haki kwa kushika amri kumi hapo kwenye kipengele cha "MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO"
  na kilichotokea ni kwamba yule aliyezishika amri kumi aliondoka mbele za YESU KRISTO kwa HUZUNI KUBWA.
  YESU KRISTO ASIFIWE SANA.

  ReplyDelete
 3. Amen, nmebarikiwa sana.

  ReplyDelete