"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, May 7, 2019

UBATILI.

Mhubiri 1:1 “Maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi,mfalme katika Yerusalemu.
2 Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili.
3 Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?
4 Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima.
5 Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake.
6 Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.
7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena.
8 Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia.
9 Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua.
10 Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi”.

Shalom karibu tujifunze Neno la Mungu, Sulemani alipewa na Bwana hekima kuliko watu wote wakati huo, alichunguza mambo mengi na kupata jawabu moja ya mambo hayo na kusema yote ni UBATILI.

Ubatili maana yake ni “kitu kisichokuwa na maana”…au “kitu ambacho kwa nje kinaonekana kina thamani kubwa lakini ndani yake hakina maana”..hiyo ndio maana ya Neno UBATILI.

Umewahi kujiuliza kwanini Sulemani aliishia kusema mambo yote ni Ubatili??...Hebu tujifunze kidogo ni kwanini alisema hivyo..

Ukisoma mstari wa 4, 5,6 na wa 7 hapo juu utapata picha ni kwanini Sulemani anasema mambo yote ni Ubatili. Utaona kuwa aliyajaribu kutafiti mambo kadhaa akidhani kuwa atapata jambo jipya ndani yake lakini kinyume chake akagundua kuwa mambo yote yanamrudisha kwenye jambo lile lile la kwanza, akachukia na kuhuzunika akasema sasa inafaida gani kujitaabisha na kitu ambacho hatma yake ni kule nilikotokea.

Alilitafakari jua, alilichunguza linapozama huwa linaenda wapi…pengine akatafakari labda linapotea na kutokea jua jingine jipya…lakini alipozidi kuchunguza akagundua jua ni lile lile moja, hakuna jua jipya, ni lile lile lipo kwenye mzunguko wake..

Akatafakari tena ni wapi maji masafi yanatengenezwa, akachunguza milimani ni sehemu gani hiyo inayoyatengeneza safi kila siku malita ya maji mapya yanayotiririka chini ya milima na kuishia baharini, alipochunguza sana akitazamia agundue jambo jipya, akaishia kugundua kuwa hata hakuna mahali maji mapya yanapotengenezwa, maji ni yale yale yanajisafisha na yapo kwenye mzunguko wake..yanaingia kwenye bahari yanarudi milimani na kutiririka tena,akaona tabu yote aliyoipata kuchunguza inamrudishia jibu lile lile kuwa hakuna jipya.

Hakuishia hapo, akaanza kuutafakari tena na upepo, akitafuta upepo, baada ya kumpuliza mtu unaenda wapi, akitazamia kugundua kuwa kuna mahali upepo mpya unajitengeneza kila siku na ule wa zamani kuna mahali unakwenda kuishia…Lakini Mwisho wa siku akagundua kuwa hakuna upepo mpya, upepo ni ule ule upo kwenye mzunguko wake. Ukachukia kwasababu alitumia muda mwingi kuchunguza akitegemea kuvumbua kitu kipya ndani yake, kinyume chake alipata majibu madogo.

Ili kuuelewa vizuri uchungu wa kupoteza muda Hebu tafakari mfano huu: mtu mmoja asiyeijua Jeografia ya dunia aliamua kuanza safari ya kwenda mbali na makazi yake ili kuutafuta mwisho wa dunia, akitumiani kuwa pale upeo wa macho yake unapoishia ndio kutakuwa ni mwisho wa dunia, kwahiyo akaanza kufunga safari na kusafiri mamia ya maili huku kila siku anaongeza mamia ya maili katika safari yake, akajifariji kuwa kashafika mbali sana, hivyo akazidi kusafiri miezi na miezi na hatimaye miaka, akisema akilini mwake kuwa nataka nifike mwisho wa dunia, nitasafiri maisha yangu yote mpaka nifike mwisho wa dunia mahali atakapokuta kuna ukomo wa ardhi. Akavuka bahari na mito, na ghafla pengine baada ya miaka 50 ya safari yake anakuja kujikuta katokea tena pale pale alipoanzia safari yake….

Baadaye sana ndio anakuja kugundua kuwa dunia ni duara..utakapoanzia ndipo utakapomalizia..Unafikiri mtu huyo atajisikiaje?? Ni wazi kuwa atakasirika na kuchukia, kwasababu kapoteza miaka mingi kutafuta kitu kisichokuwa na maana, na pengine atajiona mjinga na kapoteza muda wake mwingi kwasababu alifikiri anavyozidi kusafiri ndipo anapokwenda mbali zaidi kumbe ndivyo anavyozidi kuukaribia mwanzo wake.

Ndio maana unaona katika kitabu hichi Mfalme Sulemani haanzi na salamu, wala maneno ya hekima kama alivyoanza katika mithali..badala yake anaanza kama mtu aliyeonja kitu na kukitema haraka na kusema hakifai!! hakifai!! Kimeoza!! Kimeoza kimeoza!!...na ndio tunaona anasema hapa ubatili!! Ubatili!! kila kitu ni ubatili!!...Hiyo ni sentensi ya kuwaonya wale watu ambao bado hawajaonja!! Kwamba wasijaribu kuonja! Kwasababu watakuta kitu ambacho hawajakitegemea, na mwisho wa siku watapata hasara.
Mhubiri 1: 12 “Mimi, Mhubiri, nalikuwa Mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.
13 Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu, na kuyavumbua kwa hekima; ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.
14 Nimeziona kazi zote zifanywazo chini ya jua; na, tazama, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo”.
Anatuonya sisi tulio watoto, ndugu tusisubiri tufike mwisho ndio tugundue kuwa tulikuwa tunapoteza muda. Mfalme Sulemani anatosha kutufanyia utafiti na sisi tusiurudie tena huo utafiti ambao hauna matumaini yoyote mwisho wake.

Ndugu Mwanzo wa Mwanadamu ndio Mwisho wa mwanadamu. UMETOKA KWA MUUMBA WAKO UTARUDI KWA MUUMBA WAKO. Watu wengi ambao wapo katika dhambi hawalijui hilo…hawajui maisha ni DUARA kama vile DUNIA ilivyo duara..unapoanzia ndipo utakapoishia..haijalishi utajiona umepiga hatua kiasi gani kutoka katika mwanzo wako..lakini siku moja utaparudia tu pale ulipokuwa penda usipende, Na siku hiyo utajichukia na kujiona mjinga na umepoteza muda mwingi.

Ndio maana Sulemani huyu huyu sura za mbeleni anasema “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako Mhubiri 12” ..
kwasababu siku za uzee wako ndio siku za kuurudia mwanzo wako..Usiku unavyozidi sana ndipo asubuhi inavyokaribia…

Utajiona umefanikiwa katika mambo yako, kwahiyo huna haja ya kutubu wala kumkumbuka muumba wako, utajiona umekuwa na majukumu mengi hivyo huna haja ya kulisoma Neno lake na kulitafakari, utajiona umekwenda mbali sana kiteknolojia na kisayansi hivyo mambo madogo madogo yanayohusu Imani, na wokovu hayana maana tena kwako, utajiona una afya nyingi na ulinzi mkubwa hivyo hakuna haja ya kutafuta ulinzi wa maisha yangu ya milele…Siku zinazidi tu kwenda unajishughulisha na mambo tu yasiyokuwa na maana, Lakini nataka nikuambie HAKUNA JIPYA CHINI YA JUA..ULIPOANZIA NDIPO UTAKAPOMALIZIA. Hujui kuwa Unakaribia kumaliza duara la maisha yako, kurejea mwanzoni, pasipo wewe kujijua na siku hiyo ndio utakayofahamu kuwa yote uliyokuwa unajitaabisha nayo hayana maana.

Sulemani anasema..Mkumbuke Muumba wako kabla roho yako haijamrudia yeye aliyoitoa..

Mhubiri 12: 6 “Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; ……… 7 Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, NAYO ROHO KUMRUDIA MUNGU ALIYEITOA”.

⏩Anamalizia kwa kusema maneno haya..
Mhubiri 12: 8 “Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!
9 Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.
10 Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, YAANI, MANENO YA KWELI.
11 Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja.
12 Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.
13 Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, MAANA KWA JUMLA NDIYO IMPASAYO MTU.
14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.
Jumla ya mambo yote ndio hiyo MCHE Mungu uzishike amri zake, je! Swali linakuja unazishika amri?, je wewe ni mlevi? Mwasherati? Mshirikina? Mtazamaji pornography?, mwizi? Msengenyaji? Je ni mfanyaji masturbation?..je ni mtukanaji? Je ni mtoaji mimba? Ni msagaji au shoga?..au ni mfanyaji wa dhambi kwa siri? Watu nje wanakuona uko sawa lakini ndani yako hakufai kumeoza?.

Usisubiri mwisho wako ufike, kwasababu wengi siku ile watatazamia wafike sehemu mpya, wengine watafikiri baada ya kufa kutakuwa hakuna maisha, lakini watajikuta wamerudi pale pale kwa mwokozi wao waliomkimbia mwanzo, leo wewe usiwe mmoja wao. Kristo yupo hai , na anawapokea wenye dhambi na wote wanaomkimbilia, unachopaswa kufanya hapo ulipo ni kutenga dakika chache kutubu dhambi zako zote kwa kudhamiria kuziacha sasa angali muda upo..unadhamiria kwa vitendo kuacha ulevi, sigara, pornography, utukanaji, usengenyaji, wizi n.k, na ndipo Mungu atakapo kupa NGUVU ya kuvishinda ……hapo ulipo yeye yupo haihitaji mtu akuombee, kwa Imani amini yupo hapo anakusikia..Mwambie akuoshe dhambi zako zote na yeye ni mwaminifu na si mwongo atakupokea na kukufanya mpya na kukusamehe..

Kisha baada ya kutubu nenda katafute ubatizo sahihi kama hujafanya hivyo, mahali popote karibu na wewe kumbuka ubatizo ni wa kuzamishwa mwili wote katika maji mengi na kwa Jina la YESU, na baada ya kubatizwa, Roho atafanya kazi ndani yako kwa namna isiyo ya kawaida na uwezo wa ajabu wa kushinda dhambi utashuka ndani yako, na uwezo mkubwa wa kuyaelewa maandiko utaingia ndani yako..Hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili na kuwa na uhakika wa kuiona mbingu.

Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment